Index

Back Top Print

[BE - CS - DE - EN - ES - FR - IT - HU - LA - LV - PT - SW - ZH]

 

Dikrii juu ya
huduma na maisha ya mapadre

 Paulo Askofu
Mtumishi wa Watumishi wa Mungu
pamoja na Mababa wa Mtaguso Mkuu
ataka haya yakumbukwe daima

 

UTANGULIZI

1. Zaidi ya mara moja Mtaguso Mkuu huu umewakumbusha watu wote heshima kuu ya DARAJA YA MAPADRE (Presbyterorum Ordinis)[1]. Lakini, maadamu mapadre hushika kazi iliyo muhimu sana na inayozidi kuwa ngumu katika harakati ya kulitengeneza upya Kanisa, basi imeonekana kuwa inafaa sana kujadili juu yao kwa ukamilifu na kina zaidi. Na yale yatakayoelezwa hapa hayana budi kuelekezwa kwa mapadre wote – hasa kwa wale wanaojishughulisha katika kuchunga roho za watu – ila yalinganishwe ipasavyo na hali ya mapadre ya kitawa. Mapadre, kwa ajili ya Daraja takatifu na ya utume wanaopewa na Maaskofu, wanapokelewa kumtumikia Kristo aliye Mwalimu, Kuhani na Mfalme; nao wanashiriki huduma yake, ambayo kwayo hapa duniani Kanisa hujengwa bila kukoma kuwa Taifa la Mungu, Mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Kwa sababu hiyo, Sinodi hii takatifu inatangaza na kuamua haya yafuatayo kusudi huduma ya mapadre iweze kupata tegemeo lililo imara zaidi katika mazingira ya kichungaji na ya kibinadamu ya siku hizi, ambayo mara nyingi ni mapya kabisa; tena ili kusudi maisha yao yashughulikiwe ifaavyo zaidi.

Sura ya Kwanza

UPADRE KATIKA UTUME WA KANISA

Maumbile ya upadre

2. Bwana wetu Yesu Kristo, “ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni” (Yn 10:36), huushirikisha Mwili wake wote wa fumbo ule mpako wa Roho ambao kwao alipakwa mwenyewe [2]: maana katika mpako huu waamini wote waunda ukuhani mtakatifu na wa kifalme, wamtolea Mungu hostia za kiroho kwa njia ya Yesu Kristo, na kuzitangaza fadhili zake Yeye aliyewaita ili kuwatoa katika giza na kuwapokea katika nuru yake ya ajabu [3]. Hivyo hakuna hata kiungo kimoja kisichoshiriki katika utume wa Mwili mzima, lakini kila kimoja miongoni mwake hakina budi kumtukuza Yesu moyoni mwake [4] na kumshuhudia Yesu kwa roho ya unabii [5].

Lakini Bwana mwenyewe, ili waamini waunganike katika mwili mmoja ambao “viungo vyake vyote havitendi kazi ileile” (Rum 12:4), aliwaweka baadhi yao kuwa wahudumu, hivi kwamba katika shirika la waamini wawe na mamlaka takatifu ya Daraja ili kutoa dhabihu na kusamehe dhambi[6], na vilevile watekeleze rasmi kazi ya kikuhani kwa ajili ya wanadamu. Hivyo, akiisha kuwatuma Mitume kama Yeye mwenyewe alivyotumwa na Baba[7], Kristo, kwa njia ya Mitume wenyewe, aliwashirikisha uwakfu wake na utume wake waandamizi wao, yaani Maaskofu[8], ambao tena dhima yao katika huduma ilifikilizwa kwa Mapadre[9] kwa Daraja ya chini zaidi. Nao, wakiwekwa katika Daraja ya Upadre, ni washiriki wa Daraja ya Maaskofu[10] ili utumishi wa kitume uliokabidhiwa na Kristo utekelezwe kwa utaratibu.

Kazi ya Mapadre, maadam imeunganika kiundani na Daraja ya Maaskofu, inashiriki mamlaka ya Kristo ambayo kwayo mwenyewe hukuza, hutakasa na kuongoza Mwili wake. Ndiyo sababu ukuhani wa mapadre, ijapo hudai kwanza sakramenti zinazoingiza katika ukristo, lakini hutolewa kwa njia ya ile sakramenti maalum ambayo kwa ajili yake mapadre, kwa mpako wa Roho Mtakatifu, hutiliwa muhuri wa pekee unaowafanya kuwa mfano wa Kristo Kuhani; hivi kwamba wawezeshwe kutenda kwa jina la Kristo na katika nafsi yake aliye kiongozi[11].

Aidha, mapadre wanalishiriki, kwa kadiri yao, jukumu la Mitume; ndiyo maana wanapewa kutoka kwa Mungu neema inayowawezesha kuwa wahudumu wa Yesu Kristo kati ya mataifa kwa njia ya huduma takatifu ya Injili, ili sadaka ya mataifa iwe ya kupendeza, na iliyotakaswa katika Roho Mtakatifu[12]. Maana kwa njia ya tangazo la kitume la Injili kweli Taifa la Mungu linaalikwa na kukusanywa, hivi kwamba wote wanaoshiriki katika Taifa hili, madhali wanatakaswa kwa Roho Mtakatifu, waweze kujitoa wenyewe wawe “hostia iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu” (Rum 12:1). Tena kwa njia ya huduma ya mapadre dhabihu ya kiroho ya waamini kweli inakamilishwa, kwa kuwa inaunganishwa na dhabihu ya Kristo aliye Mshenga pekee; maana kwa mikono ya mapadre na kwa jina la Kanisa zima dhabihu hii hutolewa katika Ekaristi pasipo kumwaga damu na kwa mtindo wa kisakramenti, hadi Bwana mwenyewe atakapofika[13]. Napo ndipo inapolenga huduma ya mapadre na kupewa kipeo chake. Maana utumishi wao unaoanza kwa tangazo la Injili, hupewa nguvu yake na matunda yake kutoka katika dhabihu ya Kristo; na madhumuni yake ndiyo kwamba “mji mzima uliokombolewa, yaani kusanyiko na jamii ya watakatifu, ujitoe kwa Mungu uwe dhabihu ya kilimwengu (universale sacrificium) kwa njia ya Kuhani Mkuu, ambaye pia alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu katika mateso yake, ili kutufanyiza tuwe mwili wa Kichwa kitukufu namna hii”[14].

Hivyo, shabaha wanayolenga mapadre kwa huduma na maisha yao ndiyo utukufu wa Mungu Baba wanaopaswa kuutafuta katika Kristo. Nao utukufu u kwamba wanadamu wapokee kwa utambuzi, kwa hiari na kwa moyo wa shukrani kazi timilifu ya Mungu iliyotendeka katika Kristo na kuidhihirisha katika maisha yao yote. Kwa sababu hiyo, mapadre, wawe wanajitolea katika sala na maabudu, wawe wanalihubiri neno [la Mungu], wawe tena wanatoa dhabihu ya Ekaristi na kutoa sakramenti nyingine, ama wanatekeleza huduma nyingine kwa kuwatumikia watu, basi wanachangia katika kuukuza utukufu wa Mungu na wakati huohuo kuwaendeleza watu katika uzima wa kimungu. Na mambo hayo yote – ambayo hububujika katika Pasaka ya Kristo – yatapata utimilifu kamili katika ujio mtukufu wa Bwana mwenyewe, pindi atakapompa Mungu Baba Ufalme wake[15].

Hali ya mapadre katika ulimwengu

3. Mapadre wanatwaliwa katika wanadamu na kuwekwa kwa ajili ya wanadamu wenyewe katika mambo yamhusuyo Mungu, ili watoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi[16]; nao wanaishi kati ya wanadamu wengine kama ndugu. Maana ndivyo alivyoishi Yesu aliye Bwana wetu na Mwana wa Mungu, mtu aliyetumwa na Baba kwa wanadamu, ambaye alikaa nasi, akataka kuwa sawa na ndugu zake katika mambo yote, isipokuwa dha-mbi[17]. Mfano wake huo walikwisha kuufuata Mitume watakatifu; na Mtakatifu Paulo, Mwalimu wa mataifa, “aliyetengwa kwa kuihubiri Injili ya Mungu” (Rum 1:1) anatangaza kwamba amekuwa hali zote kwa watu wote ili apate kuwaokoa wote[18]. Hivyo mapadre wa Agano Jipya wametengwa kwa namna fulani ndani ya Taifa la Mungu kwa ajili ya wito wao na Daraja yao; ila si kwa lengo la kufarakana [na taifa hilo] wala na mtu yeyote, bali kwa kujitoa mhanga katika kazi aliyowaitia Bwana[19]. Nao wasingeweza kuwa wahudumu wa Kristo kama wasingekuwa mashahidi na watoaji wa uzima ulio tofauti na ule wa kidunia; lakini pia wasingeweza kuwatumikia wanadamu kama wangejitenga na maisha yao na mazingira yao[20]. Kwa huduma yao wenyewe wapaswa wasiifuatishe namna ya dunia hii[21]; lakini wakati huohuo hawana budi kuishi wakijichanganya na watu kama wachungaji wema wanaojua vizuri kondoo zao, na kuwakumbuka hata wale wasio wa zizi hili, ili nao waisikie sauti ya Kristo, na wawepo kundi moja na mchungaji mmoja[22]. Kwa kuifikia shabaha hii hufaa sana zile fadhila zinazoheshimiwa katika jamii ya kibinadamu, kama vile wema wa moyo, unyofu, uthabiti wa roho na saburi, juhudi kwa ajili ya haki, ukarimu, na fadhila nyingine anazokazia mtume Paulo asemapo, “Mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo” (Flp 4:8)[23].

Sura ya Pili

HUDUMA YA MAPADRE

I - MAJUKUMU YA MAPADRE

Mapadre, wahudumu wa neno la Mungu

4. Taifa la Mungu hukusanywa asili ya yote kwa njia ya neno la Mungu aliye hai[24] ambalo watu wote wanayo haki kulitafuta midomoni mwa mapadre[25]. Maana, maadam hakuna anayeweza kuokolewa pasipo kabla kuamini[26], mapadre huwajibika kabla ya yote kuihubiri Injili ya Mungu[27] kwa watu wote kama washiriki wa Maaskofu, ili waushikilie utume wa Bwana asemapo, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (Mk 16:15)[28]; na hivyo waweze kuliweka na kulikuza taifa la Mungu. Maana kwa neno liletalo wokovu, imani inawashwa mioyoni mwa wasioamini na kulishwa mioyoni mwa waaminio; vilevile kwa imani jumuiya ya waamini inaasilika na kukua kadiri alivyoandikwa Mtume, “Imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Rum 10:17). Kwa hiyo mapadre huwiwa na watu wote, kwa maana hupaswa kuwapasha wote habari ya ukweli wa Injili[29] walio nao katika Bwana. Hivyo mapadre, wawe wanatoa mbele ya watu ushuhuda wa maisha yaliyo safi yenye kuwahimiza kumtukuza Mungu[30]; wawe wanalihubiri fumbo la Kristo kwa wasioamini kwa mahubiri ya wazi; wawe wanafundisha katekesi au wanafafanua mafundisho ya Kanisa; wawe wanajishughulisha kuchunguza matatizo ya nyakati zao katika mwanga wa Kristo: basi, katika nafasi hizo zote wajibu wao ni kufundisha siyo hekima yao wenyewe, bali neno la Mungu na kuwaalika kwa bidii watu wote katika uongofu na utakatifu[31]. Na kuhubiri kwa mapadre, ambako mara nyingi ni kugumu sana katika mazingira ya dunia ya nyakati zetu, ijapo kunataka kuleta matunda mengi zaidi akilini mwao wanaosikiliza, hakuwezi tu kueleza neno la Mungu kwa ujumla na kinadharia, bali lazima kulinganishe ukweli usiokoma wa Injili na mazingira ya maisha ya kila siku.

Kwa namna hii, huduma ya neno hutolewa kwa mitindo mbalimbali na kulingana na mahitaji tofauti ya wasikilizaji na kadiri ya karama mbalimbali za wahubiri. Kwenye nchi au mazingira visivyo vya kikristo, kwa njia ya ujumbe wa Injili wanadamu wanavutwa katika imani na katika sakramenti za wokovu [32]; na kwenye jumuiya ya wakristo wenyewe, kuhubiriwa kwa neno ni ya lazima kwa huduma ya sakramenti zenyewe, hasa kuwaelekea wale wanaoonyesha kuwa hawaelewi au hawayaamini kutosha wanayoyatenda; maana hizo sakramenti ni sakramenti za imani inayozaliwa na kulishwa kwa neno [33]. Jambo hili hufaa hasa kwa Liturujia ya Neno katika adhimisho la Misa, ambapo unaundwa umoja usiogawanyika kati ya tangazo la kifo na ufufuko wa Bwana, jibu la watu wanaosikiliza na sadaka yenyewe ambayo kwayo Kristo amelithibitisha Agano Jipya katika damu yake; na waamini wanajiunga na sadaka hii kwa matoleo yao na kwa kuipokea sakramenti [34].

Mapadre, wahudumu wa sakramenti na wa Ekaristi

5. Mungu, ambaye peke yake ndiye Mtakatifu na mwenye kutakatifuza, alitaka kujitwalia wanadamu wawe washiriki na wasaidizi wake, ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza. Ndiyo maana mapadre huwekwa wakfu na Mungu, kwa njia ya Askofu, hivi kwamba washirikishwe kwa namna ya pekee ukuhani wa Kristo, na katika maadhimisho matakatifu watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu katika liturujia, kwa njia ya Roho wake[35]. Maana wao kwa njia ya ubatizo huwaingiza wanadamu katika taifa la Mungu; kwa njia ya sakramenti ya kitubio huwapatanisha wakosefu na Mungu na Kanisa; kwa mafuta ya wagonjwa huwatuliza wago-njwa; na hasa kwa adhimisho la Misa hutolea, kwa namna ya sakramenti, dhabihu ya Kristo. Lakini wanapotoa sakramenti zote, mapadre – kama alivyokwisha kushuhudia Mt. Ignasi shahidi wakati wa Kanisa la mwanzo[36] – wameunganika kihierarkia na Askofu kwa namna mbalimbali; na hivyo wanamwakilisha katika kila kusanyiko (congregationibus) la waamini[37].

Sakramenti zote, kama vile huduma zote za kikanisa na matendo ya kitume, zimeunganika kiundani na Ekaristi takatifu na huelekea kwayo[38]. Maana ndani ya Ekaristi takatifu yamo manufaa yote ya kiroho ya Kanisa[39], yaani Kristo mwenyewe, aliye Pasaka yetu na mkate ulio hai; naye, kwa njia ya Mwili wake (carnem suam) uhuishwao na Roho Mtakatifu na yenye kuhuisha, anawapa uzima wanadamu ambao kwa njia hii wanaalikwa na kuhimizwa kujitoa wenyewe pamoja naye, na kutoa pia matatizo yao, na viumbe vyote. Kwa sababu hii Ekaristi hujiweka kama chemchemi na kilele cha uinjilishaji wote, hivi kwamba wakatekumeni wanaingizwa polepole katika kushiriki Ekaristi, na waamini waliokwisha tiwa muhuri wa ubatizo takatifu na wa kipaimara wanaingizwa kikamilifu katika Mwili wa Kristo (Corpori Christi) kwa njia ya Ekaristi.

Hivyo kusanyiko la kiekaristi (Eucharistica Synaxis) ni kiini cha jumuiya ya waamini inayoongozwa na padre. Kwa hiyo mapadre wanawafundisha waamini kutoa dhabihu ya kimungu kwa Mungu Baba katika sadaka ya Misa, na kuunganisha na dhabihu hiyo toleo la maisha yao. Aidha, katika roho ya Kristo Mchungaji, mapadre wanawafunza pia kuweka dhambi zao kwa moyo wa toba chini ya mamlaka ya Kanisa katika sakramenti ya kitubio, kusudi wapate kumwongokea Bwana kila siku zaidi na zaidi, wakikumbuka maneno yake, “Tubuni, kwa maana Ufalme wa mbinguni umekaribia” (Mt 4:17). Tena, wanawafundisha waamini kuyashiriki maadhimisho ya kiliturujia na kuchota ndani yake roho ya sala iliyo nyofu; wanawahimiza wawe na roho ya sala inayozidi kuwa kamili kwa maisha yao yote, kulingana na neema na mahitaji ya kila mtu; wanawaonya wote wazitimize wajibu zitokanazo na hali yao, na kuwavuta walio wakamilifu zaidi wayashike mashauri ya kiinjili kwa namna inayofaa zaidi kwa kila mmoja. Hivyo, wanawafunza waamini ili wapate kumwimbia Bwana mioyoni mwao kwa zaburi na tenzi za rohoni, na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo[40].

Masifu na shukrani ambazo waamini wanamtolea Mungu katika adhimisho la Ekaristi, mapadre wanaziendeleza katika masaa mengine ya siku kwa njia ya Sala ya Vipindi, ambayo kwayo humwomba Mungu kwa jina la Kanisa na kwa ajili ya watu wote waliokabidhiwa kwao, na kwa ulimwengu mzima pia.

Nyumba ya sala ni mahali inapoadhimishwa na kutunzwa Ekaristi; tena ni mahali ambapo waamini hukusanyika; ambapo uwepo wa Mwana wa Mungu aliye Mkombozi wetu na aliyejitoa katika altare ya sadaka huheshimiwa uwe tegemeo na faraja ya waamini. Ndiyo maana nyumba hii haina budi kuwa safi na yenye kufaa kwa sala na ibada takatifu[41]. Ndani yake wachungaji na waamini hualikwa kukiitikia kwa moyo wa shukrani kipaji chake Yule anayemimina daima maisha ya kimungu katika viungo vya mwili wake kwa njia ya ubinadamu wake[42]. Mapadre wajishughulishe kustawisha ipasavyo ujuzi na sanaa za kiliturujia, ili, kwa njia ya huduma yao ya kiliturujia, jumuiya za kikristo zilizokabidhiwa kwao zitoe sifa izidiyo kuwa kamilifu kwa Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.

Mapadre, walezi wa Taifa la Mungu

6. Mapadre wanaendeleza kazi ya Kristo Kiongozi na Mchungaji (Capitis et Pastoris) kwa kiasi cha mamlaka kinachowapasa na kwa jina la Askofu. Hivyo wanaikusanya Familia ya Mungu kama jumuiya inayohuishwa katika umoja na wanaiongoza kwenda kwa Baba kwa njia ya Kristo katika Roho Mtakatifu[43]. Kwa ajili ya huduma hii, kama vile kwa majukumu mengine ya mapadre, inatolewa mamlaka ya kiroho ijaliwayo kwa lengo la kujenga[44]. Lakini katika kulijenga Kanisa, mapadre hupaswa kuwa na tabia ya ukarimu wa pekee kwa watu wote, wakiiga mfano wa Bwana. Nao hawana budi kutenda kwa mujibu wa matakwa ya mafundisho na maisha ya kikristo, wala siyo kwa kuwapendeza watu[45]; tena wawafunze na pia kuwaonya kama wana wapenzi[46], kadiri ya maneno ya Mtume asemaye, “Lihubiri neno wakati ukufaao na wakati usiokufaa; karipia, kemea na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho” (2Tim 4:2)[47].

Kwa sababu hiyo ni wajibu wa mapadre, walio walezi katika imani, kujishughulisha wao wenyewe au wakiwatumia wengine ili kusudi kila mwamini aongozwe katika Roho Mtakatifu kuendeleza wito wake maalum kwa mujibu wa Injili, kutekeleza mapendo yaliyo manyofu na yenye kutenda na kutumia ule uhuru ambao kwa huo Kristo alituokoa [48]. Ibada nzurinzuri na mashirika yenye kustawi, yote hayo thamani yao itakuwa ni ndogo sana ikiwa hayawalei watu waufikie ukomavu wa maisha ya kikristo [49]. Na ili kuhamasisha ukomavu huo, mapadre watamsaidia kila mtu katika kutambua madai ya matukio mbalimbali ya maisha yake – yawe makubwa ama madogo – na kuona ndani yake utashi wa Mungu. Aidha, wakristo wafundishwe kwamba wasiishi kwa ajili yao wenyewe tu, bali kadiri ya madai ya sheria mpya ya mapendo, ambayo hutaka kila mtu atumie kipimo kile cha neema alichojaliwa kwa ajili ya wenzake [50], hivi kwamba wote watimize kikristo wajibu wao katika jamii ya kibinadamu.

Lakini, ijapo mapadre wanapaswa kuwatumikia watu wote, hata hivyo wanakabidhiwa hasa walio maskini na wanyonge zaidi, ambao Bwana mwenyewe alitaka kujionyesha ameunganika nao kwa namna ya pekee[51], na ambao uinjilishaji wao umewekwa kama ishara ya kazi ya kimasiya[52]. Na vijana nao wafuatiliwe kwa bidii ya pekee, kama vile watu wa ndoa na wazazi; hutarajiwa kuwa hawa watu wanajikusanya kirafiki katika makundi, ili wapate kusaidiana wao kwa wao na kuishi kwa urahisi na ukamilifu zaidi kama wakristo katika mazingira magumu wanamoishi. Aidha, mapadre wakumbuke kuwa watawa wote – wanaume kama vile wanawake – ni sehemu yenye heshima ya pekee katika nyumba ya Bwana, na kwa sababu hiyo hustahili kushughulikiwa kwa utunzo wa pekee, ili wazidi kuendelea katika utimilifu wa kiroho kwa manufaa ya Kanisa zima. Na hatimaye mapadre wawashughulikie hasa wagonjwa na wanaokaribia kufa, wakiwatembelea na kuwafariji katika Bwana[53].

Lakini jukumu la kuwa mchungaji haliishi tu katika kuwashughulikia waamini mmoja mmoja; bali haina budi kupanuliwa hasa katika kuunda jumuiya halisi ya kikristo. Na ili kuchochea ipasavyo roho ya kijumuiya, ni lazima hiyo roho isilenge tu katika Kanisa mahalia, lakini pia katika Kanisa lote zima. Jumuiya mahalia haiwezi kujishughulisha tu na waamini wake, bali inapaswa pia kujaa roho ya kitume ili kuwafungulia wanadamu wote njia iongozayo kwa Kristo. Lakini jumuiya imekabidhiwa kabla ya yote wakatekumeni na waamini wapya (neophytos) wanaotakiwa kulelewa hatua kwa hatua katika kujua na kuishi maisha ya kikristo.

Walakini haiwezekani kuijenga jumuiya ya kikristo kama haijaweka mzizi na bawaba yake katika maadhimisho ya Ekaristi takatifu, ambayo kutoka kwayo ni lazima yaanzishwe malezi yote yanayodhamiria kuunda roho ya kijumuiya[54]. Na kwa upande wake maadhimisho ya Ekaristi, ili yapate kuwa makamilifu na manyofu, hayana budi kuwaongoza watu kwenye matendo mbalimbali ya mapendo na ya kusaidiana, na pia kwenye utendaji wa kimisioni na kwenye mitindo mbalimbali ya ushuhuda wa kikristo.

Aidha, kwa njia ya mapendo, sala, mfano na matendo ya toba, jumuiya ya kikanisa inatenda kazi halisi ya kimama kwa minajili ya kuwafanya watu wamkaribie Kristo. Maana, kwa wale wasioamini bado, jumuiya inapata kuwa chombo kinachofaa kwa kuonyesha na kusahilisha njia iletayo kwa Kristo na Kanisa lake; na kwa wale waliokwisha amini ni kichocheo, lishe na tegemeo katika vita vya kiroho.

Lakini katika kuijenga jumuiya ya kikristo mapadre wasitumikie kamwe itikadi au kundi fulani la kibinadamu, bali, kama wajumbe wa Injili na wachungaji wa Kanisa, wajitolee kwa dhati ili kukuza kiroho Mwili wa Kristo.

II - UHUSIANO WA MAPADRE NA WENGINE

Uhusiano na Askofu

7. Mapadre wote, pamoja na Maaskofu, wanashiriki katika ukuhani uleule na ulio mmoja wa Kristo na pia huduma yake hivi kwamba umoja huo wa uwakfu na utume hudai ushirika wa kihierarkia kati ya mapadre na Daraja ya Maaskofu[55]. Pengine ushirika huu unaonyeshwa kwa namna bora katika konselebrasio ya kiliturujia, wakati mapadre wameunganika na Maaskofu na kukiri kuwa wanaadhimisha Ekaristi takatifu[56]. Hivyo, kwa ajili ya kipaji cha Roho Mtakatifu kijaliwacho kwa mapadre katika maadhimisho ya Daraja takatifu, Maaskofu hawana budi kuwaangalia mapadre kama wasaidizi na pia washauri wa lazima katika huduma na kazi ya kufundisha, kutakatifuza na kuongoza taifa la Mungu[57]. Jambo hilo limethibitishwa kwa nguvu tangu awali ya Kanisa katika hati za kiliturujia, ambapo huo-mbwa rasmi kwa Mungu ili amshushie padre mwekwa wakfu “roho ya neema na shauri, ili alisaidie na kuliongoza taifa lake kwa moyo ulio safi”[58], vilevile kama roho ya Musa huko jangwani ilivyoshamirishwa juu ya wale watu sabini wenye busara[59], ambao “kwa msaada wao Musa aliweza kuuongoza kwa urahisi umati usiohesabika wa watu”[60]. Kwa ajili ya ushirikiano huu wa pamoja katika ukuhani huohuo na huduma, Maaskofu wawaangalie mapadre kama ndugu na rafiki[61] na waujali sana, kwa kila kinachowezekana, ustawi wao kimwili na hasa kiroho. Maana Maaskofu ndio wanaobeba wa kwanza wajibu wa utakatifu wa mapadre wao[62]: hivyo wanapaswa kushughulikia kwa kila bidii mafunzo ya kudumu ya mapadre wao[63]. Wawe tayari kuwasikiliza, na zaidi wawe wao wenyewe kuwaomba watoe mawaidha yao na kuchunguza kwa pamoja masuala yahusuyo madai ya kazi ya kichungaji na manufaa ya jimbo zima. Na ili jambo hili liweze kutimizwa kiutendaji, iundwe halmashauri (senatus)[64] ya mapadre inayowakilisha makleri wote; nayo kwa mashauri yake imsaidie ifaavyo Askofu katika uongozi wa jimbo. Nalo lifanyike kwa namna inayolingana zaidi na mazingira na mahitaji ya siku za leo[65], na kadiri ya mtindo na kanuni zinazohitaji kuamuliwa.

Kwa upande wao, mapadre wazingatie utimilifu wa sakramenti ya Daraja waliojaliwa Maaskofu; kwa hiyo wayastahi ndani yao mamlaka ya Kristo aliye Mchungaji Mkuu. Na hivyo waunganike na Askofu wao kwa upendo na utii ulio mnyofu [66]. Utii huo wa mapadre uliojaa roho ya ushirikiano unaasilika katika ushirika wenyewe na huduma ya kiaskofu, ambao mapadre wanajaliwa kwa njia ya sakramenti ya Daraja na utume wa kikanisa ( missionem canonicam) [67].

Muungano huu kati ya Mapadre na Maaskofu ni wa lazima hasa siku hizi, maadam kwa sababu mbalimbali siku za leo shughuli za kitume zinapaswa kuwa za aina mbalimbali, na pia zinatakiwa kuvuka mipaka ya parokia au jimbo fulani. Hivyo hakuna padre awezaye kutekeleza kazi yake kikamilifu ijapo hufanya kazi peke yake na kwa kutengana na wenzake, tena bila kuunganisha juhudi zake na zile za mapadre wengine, chini ya mamlaka yao wanaoongoza Kanisa.

Uhusiano kati yao

8. Mapadre, waliowekwa katika Daraja ya Upadre kwa njia ya maadhimisho ya upadirisho ( ordinationem), wameunganika wote kati yao kwa udugu wa ndani utokanao na sakramenti; lakini kwa namna ya pekee wote wanaunda urika ( Presbyterium) mmoja katika jimbo wanaloitwa kulitumikia chini ya Askofu wao. Maana wajaposhika kazi mbalimbali, hata hivyo wanatekeleza huduma ileile moja ya kipadre kwa ajili ya watu. Maana mapadre wote utume wao ndio kuchangia katika kazi ileile, haidhuru wawe wanafanya kazi za parokia ama za nje ya parokia, wanajishughulisha katika utafiti uhusuo elimu ya kikristo na mafundisho, ama wanafanya kazi za mikono – na kwa njia hii wanashiriki hali ya maisha ya wafanyakazi, iwapo mtindo huu uonekane unafaa na kuidhinishwa na Askofu – au hatimaye wanatenda kazi nyingine za kitume au zinazolenga katika utume. Ni dhahiri kwamba wote hutenda kazi kwa lengo lilelile, yaani kwa kuujenga Mwili wa Kristo; nalo ladai dhima mbalimbali na matengenezo mapya, hasa nyakati zetu. Kwa hiyo ni ya lazima sana mapadre wote, wa kijimbo kama vile wa kitawa, wasaidiane wao kwa wao, hivi kwamba sikuzote wawe washiriki wa ukweli [68]. Hivyo kila padre ameunganika na wenzake kwa vifungo maalum vya mapendo ya kitume, vya huduma na udugu: na hali hii inaashiriwa kiliturujia tangu nyakati za kale katika ibada ambapo mapadre wanaoshiriki maadhimisho ya Daraja wanaalikwa kumwekea mikono mteule mpya pamoja na Askofu mweka-wakfu; vilevile inaashiriwa wakati wanapoadhimisha Ekaristi takatifu kwa pamoja na kwa moyo wa umoja. Aidha, kila padre ameunganika na mapadre wenzake kwa kifungo cha mapendo, sala, na kila namna ya ushirikiano, akionyesha kwa njia hii ule umoja ambao kwao Kristo alitaka wanafunzi wake wawe wamekamilika katika umoja, ili ulimwengu ujue ya kuwa Mwana alitumwa na Baba [69].

Kwa sababu hizi, mapadre wazee wapaswa kuwajali kweli mapadre vijana kama ndugu wakiwasaidia wanapopiga hatua zao za kwanza kazini katika shughuli na wajibu za huduma yao; na wajitahidi kuelewa mfumo wa mawazo yao ijapo inawezekana ni tofauti, na pia watazame kwa wema maazimio yao. Na mapadre vijana, kwa upande wao, waheshimu umri na mang’amuzi ya mapadre wazee, washauriane nao mintarafu mambo yahusuyo roho za watu, na wapende kufanya kazi pamoja.

Wakisukumwa na roho ya udugu, mapadre wasipuuze ukarimu[70], wafanyizie ufadhili na kushirikiana mali zao[71]; wawashughulikie kwa utunzo wa pekee wenzao walio wagonjwa, wenye huzuni, wanaolemewa na kazi nyingi mno, walio wapweke au ugenini kama vile wanaodhulumiwa[72]. Ni vema pia wapende kujumuika ili kushinda pamoja kwa furaha katika kupumzika kidogo na kustarehe, wakikumbuka maneno aliyosema Bwana kwa kuwaalika Mitume waliolemewa na uchovu mwingi, “Njoni ninyi kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo” (Mk 6:31). Aidha, inafaa mapadre waweze kusaidiana wao kwa wao kukuza maisha ya kiroho na elimu, na wapate pia kushirikiana kati yao kwa manufaa zaidi katika huduma yao na katika kuepukana na hatari za upweke. Kwa lengo hilo aina fulani ya kuishi pamoja ihimizwe, yaani mtindo mmojawapo wa jumuiya unaoweza kupata sura mbalimbali kulingana na mahitaji tofauti ya kibinafsi na kichungaji: maana wanaweza kuishi katika nyumba moja pale iwezekanapo, au kushiriki meza, au walau kukutana mara kwa mara na kila baada ya muda uliopangwa. Vilevile havina budi kutiliwa maanani na kuhimizwa kwa bidii vile vyama ambavyo, kulingana na katiba yao iliyoidhinishwa na mamlaka husika ya kikanisa, vinahamasisha utakatifu wa mapadre katika utekelezaji wa huduma yao na ambavyo kwa njia hii vinadhamiria kuutumikia urika mzima wa mapadre.

Na hatimaye, mapadre, kwa ajili ya ushirikiano uleule katika upadre, wajue kuwa wamewajibika hasa juu ya wenzao wanaohangaika katika shida; wawatolee msaada mapema na pengine wawaonye kwa upole, ikiwa inahitajika. Na wao walioanguka katika kosa fulani, wawatazame daima kwa mapendo ya kidugu na huruma, wawaombee bila kukoma na kujio-nyesha katika kila nafasi kama ndugu halisi na rafiki.

Uhusiano na walei

9. Mapadre wa Agano Jipya, kwa ajili ya sakramenti ya Daraja wana kazi bora na ya lazima ya baba na mwalimu katika taifa la Mungu na kwa mafaa ya taifa la Mungu; lakini hata hivyo ni wafuasi wa Bwana sawasawa kama vile waamini wote wengine na wanashirikishwa Ufalme wake kwa neema ya wito wa Mungu[73]. Miongoni mwao waliozaliwa upya kwa maji ya ubatizo, mapadre ni ndugu kati ya ndugu[74], kama viungo vya Mwili uleule mmoja wa Kristo, ambao ujenzi wake ni wajibu wa watu wote[75].

Kwa sababu hiyo, katika kutekeleza jukumu lao la kuiongoza jumuiya, mapadre wanapaswa kufanya kazi si kwa lengo la kufuatilia masilahi zao, bali kwa ajili ya utumishi wa Kristo tu [76]; nao waunganishe juhudi zao na zile za waamini walei, wakiufuata kati yao mfano wa Mwalimu, ambaye kati ya wanadamu “hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi” (Mt 20:28). Mapadre hawana budi kutambua na kuhamasisha heshima ya walei kwa moyo mnyofu, kama vile dhima yao maalum katika utume wa Kanisa. Aidha, mapadre wawe na heshima kuu kwa uhuru ulio wa haki unaowajuzu wote katika mji wa hapa duniani. Wawe tayari kuzisikiliza kauli za walei, wakizingatia matarajio yao kwa roho ya udugu; wanufaike mang’amuzi yao na ufundi wao katika nyanja mbali-mbali za amali ya kibinadamu, hivi kwamba wapate kutambua pamoja nao ishara za nyakati. Madhali [mapadre] wanao uwezo wa kupambanua ni roho zipi zitokazo kwa Mungu [77], wanapaswa kutambua kwa hisia za imani karama ambazo, ziwe ni ndogo ama kubwa, zinajaliwa kwa walei kwa mitindo mingi mbalimbali; mapadre wazipokee kwa furaha na kuzistawisha kwa makini. Miongoni mwa karama za Mungu zipatikanazo kwa wingi kati ya waamini, zastahili uangalifu wa pekee zile zinazowasukuma watu wengi kwa maisha ya kiroho yaliyo ya juu zaidi. Na vilevile, kwa taraja mapadre wawakabidhi walei kazi kwa huduma ya Kanisa, wakiwaachia uhuru wa kutenda na nafasi ifaayo; na zaidi wawaalike kuanzisha kazi wao wenyewe kwa namna inayofaa [78].

Na hatimaye, mapadre wamewekwa kati ya walei ili kuwaongoza wote katika umoja wa mapendo, “kwa pendo la udugu wakipendana wao kwa wao; kwa heshima wakiwatanguliza wenzao” (Rum 12:10). Hivyo ni juu yao kupatanisha fikira mbalimbali hivi kwamba katika jumuiya ya waamini asiwepo anayejisikia kama mgeni. Nao ni watetezi wa mafaa ya kijumuiya wanayoyalinda katika jina la Askofu, na wakati huohuo ni watangazaji kabambe wa ukweli, wakiwaepusha waamini wasichukuliwe huko na huku na kila upepo wa elimu[79]. Hasa wawashughulikie wale walioacha kushiriki katika sakramenti au pengine waliokata tamaa hata katika imani; kama wachungaji wema wasiache kuwatafuta.

Wakiyazingatia maagizo mintarafu ekumeni[80], wasiwasahau ndugu ambao hawajaonja ushirika kamili na sisi katika Kanisa.

Na hatimaye wawatazame kama watu waliokabidhiwa kwao wale wote wasiomjua Kristo Mkombozi wao.

Kwa upande wao, walei waitambue deni waliyo nayo kwa mapadre na watende nao kwa mapenzi ya mtoto kwa wazazi, maana ndio wachungaji na baba zao. Aidha, wakishiriki mishughuliko yao, wajitahidi iwezekanavyo kuwasaidia mapadre wao kwa sala na amali, hivi kwamba wapate kuyashinda kwa urahisi zaidi matatizo yawezayo kujitokeza na kuzitimiza kwa manufaa zaidi wajibu zao[81].

III - KUWATAWANYA MAPADRE NA WITO WA KIPADRE

Juhudi kwa Kanisa zima

10. Kipaji cha kiroho walichopewa mapadre katika maadhimisho ya Daraja hakiwaandai kwa utume mfinyu uliofungwa katika mipaka myembamba, bali huwaandaa kwa utume wa wokovu ulio mpana sana na wa kiulimwengu “hata kuufikia mwisho kabisa wa dunia” (Mdo 1:8). Maana kila huduma ya kipadre hushiriki katika upana uleule wa kiulimwengu wa utume ambao Kristo aliwakabidhi Mitume. Ukuhani wa Kristo wanaoshirikishwa kweli mapadre, hauna budi kuwaelekea mataifa yote na nyakati zote, wala hauwezi katu kufungwa ndani ya mipaka yoyote ya ukoo, taifa na umri, kama ilivyoashiriwa kwa namna ya kifumbo katika mfano wa Melkisedeki[82]. Hivyo mapadre wakumbuke kuwa wanapaswa kuyashughulikia makanisa yote. Na mapadre wa yale majimbo yenye wingi zaidi wa wito wajionyeshe kuwa wapo tayari kutekeleza kwa hiari huduma yao katika nchi au misioni au kazi zile zinazohangaikia uhaba wa mapadre; ila kwanza wakubaliwe ama waalikwe na Askofu wao.

Aidha, kanuni za kuingizwa au kuachishwa katika jimbo ( incardinatione et excardinatione) lazima zitengenezwe upya hivi kwamba mapokeo hayo ya kale yasifutwe, lakini yalinganishwe zaidi na mahitaji ya kichungaji ya siku za leo. Na pale panapohitajika kwa sababu za kitume, urahisishwe mtawanyiko ufaao wa mapadre na pia utekelezaji wa shughuli maalumu za kichungaji kwa ajili ya makundi ya kijamii mbalimbali katika sehemu ama nchi kadhaa ama pengine duniani kote. Kwa lengo hili itafaa kuunda seminari za kimataifa, majimbo maalum au prelatura binafsi na taasisi nyingine ya namna hii ambapo wataweza kuandikishwa au kuingizwa mapadre kwa manufaa ya Kanisa zima, kadiri ya kanuni zitakazowekwa kwa kila moja ya taasisi hizo na kwa kuziheshimu daima haki za Maaskofu wa mahali.

Lakini kwa vyovyote, kadiri iwezekanavyo, mapadre wasitumwe mmoja mmoja kwenye nchi mpya, hasa wakati hawajajua vizuri bado lugha na desturi zake: ni vema zaidi waende wawili au watatu pamoja kama wanafunzi wa Bwana[83] ili waweze kusaidiana wao kwa wao. Inafaa pia kushughulikia kwa uangalifu maisha yao ya kiroho na afya yao ya mwili na akili; aidha, kadiri iwezekanavyo, ni vema mahali na mazingira ya kazi yaandaliwe kwa ajili yao kwa kulingana na hali ya kila mmoja wao. Wakati huohuo hufaa sana wale wanaoelekea kwenda nchi nyingine wajitahidi kuijua lugha inayoongelewa huko, na pia tabia mahsusi ya kisaikolojia na kijamii ya taifa lile ambalo wao wanatamani kulitumikia kwa unyenyekevu. Hivyo watafungamana nalo kikamilifu zaidi na kufuata mfano wa Mtume Paulo aliyeweza kusema juu yake mwenyewe, “Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi...” (1Kor 9:19-20).

Juhudi kwa kustawisha miito

11. Kristo, aliye Mchungaji na Mwangalizi wa roho zetu[84], aliweka Kanisa lake hivi kwamba lile taifa aliloliteua na kulinunua kwa damu yake mwenyewe[85] liwe daima na mapadre wake, wala wakristo wasiwe kamwe kama kondoo wasio na mchungaji[86]. Wakiyajua mapenzi hayo ya Kristo, Mitume, kwa onyo la Roho Mtakatifu, waliona kuwa ni wajibu wao kuwachagua wahudumu “watakaofaa kuwafundisha na wengine” (2Tim 2:2). Nayo ndiyo dhima iliyo sehemu ya utume wa kipadre wenyewe, na ambayo kwa njia yake padre hushiriki bidii za Kanisa zima ili katika taifa la Mungu hapa duniani wasikosekane kamwe watendakazi. Lakini maadamu “kuna maslahi shirika kati ya rubani na abiria wa meli”[87], basi taifa lote la Mungu lazima lifundishwe kuwa ni wajibu wake kutoa mchango wake kwa njia mbalimbali – kwa sala isiyokoma na kwa njia nyinginezo ziwezekanazo[88] – ili Kanisa liwe daima na wale mapadre linaowahitaji kwa kutimiza utume wake wa kimungu. Hivyo, awali ya yote, mapadre wajishughulishe sana kuwaelewesha waamini ubora na ulazima wa upadre kwa njia ya huduma ya neno na ushuhuda wao wa maisha yanayoionyesha wazi roho ya utumishi na furaha halisi ya kipasaka. Nao, pasipo kujali kazi wala matatizo, wawasaidie wale ambao, kwa kipimo chenye busara, wanawaona kuwa wanafaa kwa huduma iliyo bora namna hii, wawe ni vijana ama watu wazima; ili wapate fursa ya kujiandaa ifaavyo na hatimaye kuitwa na Maaskofu; lakini yote yatendeke daima katika heshima ya uhuru wao wa nje na wa ndani. Kwa lengo hilo hufaa mno uongozi wa kiroho wenye uangalifu na busara. Aidha, kuhusu wazazi, walimu, na wale wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine katika kuwalea watoto na vijana, hawa wote wapaswa kuwafunza watoto na vijana hivi kwamba wapate kuijua juhudi ya Bwana kwa ajili ya kondoo zake na kuyazingatia mahitaji ya Kanisa; na hivyo wajiweke tayari kuuitikia wito wa Bwana kwa moyo mkuu, wakimjibu pamoja na nabii, “Mimi hapa, nitume mimi” (Isa 6:8). Lakini sauti hii ya Bwana inayoita isingojewe kama kitu kitakachofikia kwa namna ya ajabu masikioni pa yule atakayekuwa padre. Bali ni sauti inayodai kutambuliwa na kuchambuliwa kwa njia ya zile ishara anazotumia Bwana kila siku ili kuwaelewesha wakristo wenye busara mapenzi yake; na mapadre wanahusika kuchunguza kwa uangalifu ishara hizo[89].

Tena mapadre wanakabidhiwa kwa mkazo vile vyama vinavyohusu miito (Opera vocationum), viwe vya kijimbo ama vya kitaifa[90]. Katika mahubiri, katekesi, na magazeti lazima yaelezwe kwa upana mahitaji ya Kanisa mahalia na ya Kanisa lote zima, na inapasa kudhihirisha wazi kabisa maana na umuhimu wa huduma ya kipadre. Ionyeshwe kuwa huduma hii huchukua wajibu mzito, lakini wakati huohuo pia huleta furaha isiyosemeka; na hasa ionyeshwe kwamba, kwa njia ya huduma hii, kama wanavyofundisha Mababa wa Kanisa, yawezekana kumtolea Kristo ushuhuda ulio bora[91].

Sura ya Tatu

MAISHA YA MAPADRE

I - WITO WA MAPADRE KUWA WAKAMILIFU

Wajibu wa kutafuta ukamilifu

12. Kwa njia ya sakramenti ya Daraja takatifu Mapadre wanafananishwa na Kristo Kuhani, kama wahudumu wa Kichwa chao, kwa madhumuni ya kukuza na kujenga Mwili wake wote ulio Kanisa, kama washiriki wa Daraja ya Maaskofu. Tangu kuwekwa wakfu katika ubatizo, wao, vilevile kama waamini wote, walipokea ishara na kipaji cha wito, na neema ambayo ni kubwa sana kiasi kwamba hata katika hali ya udhaifu wa kibinadamu[92], wana uwezo na wana wajibu wa kutafuta ukamilifu kadiri ya usemi wa Bwana, “Basi, ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu” (Mt 5:48). Lakini mapadre hasa inawapasa kuuelekea ukamilifu huo, kwa sababu wao waliopokea kwa mara nyingine uwakfu kwa Mungu kwa njia ya ordinasio (in Ordinis receptione), wanateuliwa katika hali ya kuwa vyombo vilivyo hai vya Kristo aliye Kuhani wa milele, ili waendeleze katika mfululizo wa nyakati kazi yake ya ajabu, ambaye alirudisha [katika hali iliyo bora] ubinadamu wote kwa uwezo wa juu[93]. Na kwa vile kila padre, kwa namna yake pekee, anatenda katika jina na nafsi ya Kristo mwenyewe, hujaliwa pia neema ya pekee inayomwezesha, wakati anapowatumikia watu waliokabidhiwa kwake na pia taifa zima la Mungu, aweze kukaribia zaidi ukamilifu wa yule ambaye yeye padre anamwakilisha, na udhaifu wa kibinadamu wa mwili wake unaponywa na utakatifu wa Yule ambaye kwa ajili yetu alifanywa Kuhani mkuu “mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji” (Ebr 7:26).

Kristo, ambaye Baba alimtakatifuza na kumweka wakfu, kwa kumtuma ulimwenguni[94], “alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema” (Tit 2:14), na hivyo, kwa njia ya mateso aliingia katika utukufu wake[95]; hali kadhalika mapadre, waliowekwa wakfu kwa mpako wa Roho Mtakatifu na kutumwa na Kristo wanahinisha ndani yao wenyewe matendo ya mwili na wanajitolea kwa dhati katika utumishi wa watu, na kwa namna hii wanaweza kuendelea katika [njia ya] utakatifu waliojaliwa katika Kristo, hata kuwa mtu mkamilifu[96].

Kwa njia hiyo, wakitimiza huduma ya Roho na ya haki[97], wanaimarishwa katika maisha ya kiroho, ikiwa, lakini, watakuwa watiifu kwa mafundisho ya Roho wa Kristo anayewapa uhai na kuwaongoza. Kwa sababu, ni kwa njia ya matendo matakatifu wanayotimiza kila siku, kama vile kwa njia ya huduma yao nzima, wanayotimiza kwa kushirikiana na Askofu na wao kwa wao, kwamba wanapata mwelekeo bora kwa ajili ya ukamilifu wa maisha [yao]. Lakini, ni utakatifu wenyewe wa mapadre, kwa upande wake, unaosaidia kwa vikubwa kutimiliza kwa mafanikio huduma yao. Kwa sababu, kama ni kweli kwamba neema ya Mungu ina uwezo wa kutimiza kazi ya wokovu hata kwa njia ya wahudumu wasiostahili, hata hivyo Mungu kwa kawaida anapenda kudhihirisha [matendo] makuu yake kwa kutumia wale ambao, wakijifanya watiifu mbele ya misukumo na uongozi wa Roho Mtakatifu, wanaweza kusema pamoja na Mtume, kutokana na umoja wa ndani walio nao na Kristo na utakatifu wa maisha: “Ni hai, wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu” (Gal 2:20).

Kwa sababu hiyo Mtaguso Mkuu huu, kwa madhumuni ya kufikia malengo yake ya kichungaji ya upyaisho wa ndani wa Kanisa, ya uenezaji wa Injili duniani pote na ya dialogia na ulimwengu wa leo, unawasihi kwa moyo mapadre wote wazitumie nyenzo zenye kufanikisha ambazo Kanisa linaweka mikononi mwao[98], kusudi waelekee zaidi na zaidi kwenye utakatifu unaowawezesha kuwa vyombo vya kufaa siku kwa siku zaidi kwa utumishi wa taifa zima la Mungu.

Utekelezaji wa majukumu matatu ya kipadre unadai na kusababisha utakatifu

13. Mapadre watafikia utakatifu kwa njia iliyo yao pekee ikiwa watatekeleza katika Roho wa Kristo majukumu yao kwa bidii ya dhati na bila kuchoka.

Kwa kuwa wahudumu wa Neno la Mungu, wao husoma na kusikiliza kila siku Neno hilihili ambalo watakiwa walifundishe kwa wengine; na kama wanajitahidi pia katika kulishika ndani yao wenyewe, basi hapo wanakuwa wanafunzi wa Bwana wanaokamilika siku kwa siku, kadiri ya maneno ya Mtume Paulo kwa Timotheo: “Uyatafakari hayo, ukae katika hayo, ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.” (1Tim 4:15-16). Kwa sababu, kwa kufikiri jinsi watakavyoweza kuwapa pia wengine kwa njia iliyo bora yale ambayo wametafakari[99], wataonja moyoni utamu wa “utajiri wake Kristo usiopimika” (Efe 3:8) na Hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi[100]. Bila kusahau kwamba mwenye kufungua mioyo ni Bwana[101], na kwamba uwezo hautokani na wao, bali na uweza wa Mungu[102], katika tendo lenyewe la kuhubiri Neno, watajiunga moyoni na Kristo Mwalimu na watakuwa wanaongozwa na Roho wake. Hivyo, kwa kuungana na Kristo, hushirikiana katika mapendo ya Mungu, ambaye fumbo lake, lililositirika tangu zamani zote[103], limefunuliwa katika Kristo.

Katika jukumu la kuwa wahudumu wa matakatifu, na hasa katika sadaka ya Misa, mapadre watenda kwa namna ya pekee katika jina na nafsi ya Kristo, ambaye alijitoa sadaka kwa ajili ya kuwatakatifuza wanadamu. Ndiyo sababu mapadre wanaalikwa kuiga kile wanachokifanya, kwa maana kwamba wakiadhimisha fumbo la kifo cha Bwana, wanatakiwa kufanya jitihada kujihinisha katika miili yao kwa habari ya fasiki na tamaa[104]. Katika fumbo la sadaka ya Ekaristi ambamo mapadre wanatekeleza wadhifa wao mkuu, tendo la ukombozi wetu hutimizwa pasipo katizo[105]. Kwa sababu hiyo adhimisho la kila siku [la Misa] linahimizwa sana, kwa vile ni daima tendo la Kristo na la Kanisa lake, hata kama hakuna uwezekano waamini kuhudhuria[106]. Hivyo mapadre, kwa kujiunga na tendo la Kristo Kuhani, wanajitolea kila siku kikamilifu kwa Mungu; na kwa kujilisha mwili wa Kristo wanashiriki moyoni mapendo ya Yule anayejitoa kama chakula kwa waamini. Hali kadhalika, wanapotoa Sakramenti wanajiunga na nia na mapendo ya Kristo; nalo wanalitekeleza kwa namna iliyo kuu katika Sakramenti ya Upatanisho, wakiwa wako tayari kwa moyo daima kuitoa wakati wowote wanapoombwa na waamini kwa sababu halali. Katika kusali ofisyo ya kimungu (Officio Divino) wao wanalipatia Kanisa sauti, ambalo ladumu katika kusali kwa niaba ya wanadamu wote pamoja na Kristo ambaye “yu hai sikuzote ili atuombee” (Ebr 7:25).

Kwa kulisimamia na kulichunga taifa la Mungu, mapadre wanahimizwa na mapendo ya Mchungaji Mwema watoe maisha yao kwa ajili ya kundi lao[107], wakiwa tayari pia kutoa maisha yao, wakifuata mfano wa mapadre ambao, pia nyakati zetu, hawakurudi nyuma walipokabiliana na kifo; na kwa vile nao ni walezi katika imani, kwa kuwa pia hao “wana ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Kristo” (Ebr 10:19) wanamkaribia Mungu “wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani” (Ebr 10:22); wanadumu katika tumaini imara mbele ya waamini wao[108], ili wapate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizohizo wanazofarijiwa wenyewe na Mungu[109]. Kama wasimamizi wa jumuiya wanafuatilia uasketi (ascesim) ulio halisi wa wachungaji wa roho, kwa kujinyima faida zao na kutazamia siyo yanayowafaa wao wenyewe, bali yale yaliyo manufaa kwa wengi, wapate kuokolewa[110]. Tena, kwa maendeleo yasiyokoma katika ukamilifu wa utekelezaji wa kazi za kitume na, ikitakiwa, wakiwa tayari pia kutumia mbinu mpya ya kichungaji, chini ya uongozi wa Roho wa upendo uvumaye atakako[111].

Umoja na mpangilio wa maisha ya mapadre

14. Katika ulimwengu wa leo, kwa vile wajibu ambazo wanadamu lazima wazishike ni nyingi, na matatizo ya aina mbalimbali yanayowahangaisha ni makubwa sana, na mara nyingi lazima wafanye bidii kuyatatua haraka, mara nyingi watu wanajikuta katika hali ambazo ni rahisi kujitapanya katika mambo mengi mbalimbali. Pia mapadre, hali wamezama na kusambaratika katika shughuli nyingi mbalimbali zinazotokana na utume wao, wanayo haki kujiuliza kwa fadhaa nyingi kama watamudu kweli kuoanisha mtima wa maisha ya ndani na harakati za nje. Na kwa kweli, ili kupata huo umoja wa maisha haitoshi tu kuweka utaratibu wa nje wa kazi za kitume, wala kuwa na utekelezaji tupu wa mazoezi ya ibada yangawa ni ya manufaa sana katika kuusitawisha. Lakini mapadre wanaweza kuufikia umoja wa maisha wakifuata, katika utekelezaji wa huduma yao, mfano wa Kristo Bwana ambaye chakula chake kilikuwa ni kuyafanya mapenzi ya Yule aliyemtuma kutimiliza kazi yake [112].

Kusema kweli, Kristo, ili kuendelea kufanya daima mapenzi hayohayo ya Baba hapa ulimwenguni kwa njia ya Kanisa, anatenda kazi kwa njia ya wahudumu wake, na hivyo hubaki daima asili na chemchemi ya umoja wa maisha ya mapadre. Kwa hiyo, ili kuufikia, wanatakiwa kujiunga na Kristo katika kutambua mapenzi ya Baba na katika kujitolea kwa ajili ya kundi walilokabidhiwa[113]. Hivyo wakimwakilisha Mchungaji Mwema, katika utekelezaji wenyewe wa uchungaji wa mapendo watakikuta kifungo cha ukamilifu wa upadre kitakachotimiza umoja katika maisha yao na katika utendaji wao; kwa upande mwingine, mapendo hayo ya kichungaji[114] yatokana hasa na sadaka ya Ekaristi, ambayo inaonekana kwa hiyo kuwa kweli mtima na mzizi wa maisha yote ya mapadre, kiasi kwamba roho ya kipadre inafanya bidii kuakisi katika nafsi yake yale yanayotimizwa altareni. Lakini hilo haliwezekani, isipokuwa mapadre wenyewe wakipenyeza zaidi na zaidi katika fumbo la Kristo kwa njia ya sala.

Na kusudi kuweza kuhakikisha katika utendaji umoja wa maisha, wazingatie kila wanachoanzisha ili kuona ni nini mapenzi ya Mungu juu yake[115], yaani waangalie kama lile wanaloanzisha lakubaliana na miongozo ya utume wa kiinjili ya Kanisa, kwa sababu uaminifu kwa Kristo hauwezi kutenganika na uaminifu kwa Kanisa lake. Kwa sababu hiyo, mapendo ya kichungaji yanadai kwamba mapadre, wasipotaka kupiga mbio bure[116], daima watende kazi katika kifungo cha ushirika na Maaskofu na ndugu wengine katika upadre. Wakienenda kwa kufuata kanuni hii, mapadre wataona umoja wa maisha yao katika umoja wenyewe wa utume wa Kanisa, na hivyo watakuwa wameunganika na Bwana wao, na kwa njia yake na Baba katika Roho Mtakatifu, ili kupata kujazwa faraja na furaha[117].

II - MASHARTI YA PEKEE YA KIROHO 

KATIKA MAISHA YA MAPADRE

Unyenyekevu na utii

15. Kati ya fadhila zinazohitajika zaidi kwa huduma ya mapadre, inabidi ukumbukwe ule moyo ambao unawafanya wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya Yule aliyewatuma[118]. Kazi ya kimungu ambayo walichukuliwa na Roho Mtakatifu kwayo[119] inapita nguvu na uwezo pia hekima ya wanadamu; kwa sababu: “Mungu alivichagua vitu vidhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu” (1Kor 1:27). Kwa hiyo, mhudumu wa Kristo anatambua udhaifu wake na kufanya kazi kwa unyenyekevu, akihakiki ni nini impendezayo Bwana[120] na, hali amefungwa na Roho[121], anaongozwa katika yote na mapenzi yake Yule anayetaka watu wote waokolewe; nayo mapenzi ataweza kuyagundua na kuyafuata katika mambo ya kila siku, akiwatumikia kwa unyenyekevu wote waliokabidhiwa kwake na Mungu kutokana na dhima anayotakiwa kutekeleza, na matukio mbalimbali ya maisha yake.

Lakini huduma ya kipadre, kwa vile ni huduma ya Kanisa lenyewe, haiwezi kutekelezwa isipokuwa katika ushirika wa kikanisa ( communione hierarchica) wa mwili mzima. Kwa hiyo, mapendo ya kichungaji yanadai kwamba mapadre, wakitenda kazi katika ushirika huo, kwa utii watolee matashi yao katika utumishi wa Mungu na wa ndugu, huku wakipokea na kutimiza kwa moyo mwaminifu maagizo au mapendekezo ya Baba Mtakatifu, ya Askofu wao na ya wakubwa wengine; wakijitapanya kwa furaha [122] katika wajibu wowote watakaokabidhiwa, hata kama ni wa chini au mdogo tu. Kwa kufanya hivyo wanalinda na kuimarisha hali ya umoja wenye maana na ndugu katika huduma, hasa na wale ambao Bwana amewaweka kama wasimamizi wenye kuonekana wa Kanisa lake; tena wanafanya kazi kwa ajili ya ujenzi wa Mwili wa Kristo, ambao hukua “kwa msaada wa kila kiungo” [123]. Utii huo, unaoelekeza kwenye uhuru uliokomaa wa wana wa Mungu, unadai kwa tabia yake kwamba mapadre, katika utekelezaji wa utume wao, waongozwe na mapendo katika kutafuta kwa busara njia mpya zenye kuleta manufaa zaidi kwa Kanisa. Na wakati huohuo wapendekeze kwa imani na kueleza wazi mahitaji ya kundi walilokabidhiwa, wakiwa tayari daima kujiweka chini ya uamuzi wa wale wenye wadhifa wa juu katika uongozi wa Kanisa la Mungu.

Kwa unyenyekevu huo na utii wenye uwajibikaji, mapadre wajifananisha na Kristo, na wanafikia hatua ya kuwa na nia ileile ya Kristo Yesu “ambaye alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa... akawa mtii mpaka mauti” (Flp 2:7-8) na kwa utii huu ameshinda kule kutotii kwa Adamu na kukukomboa, kama anavyosema Mtume: “Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja, watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki” (Rum 5:19).

Kupokea kwa moyo useja na kuutazama kama ni neema

16. Kujikatalia tamaa kikamilifu na kwa daima kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni, kadiri ya shauri la Kristo Bwana [124] ambako kwa karne na hata nyakati zetu kunachaguliwa kwa uradhi na kunafuatwa na waamini wengi kwa namna inayosifika, daima imetazamwa na Kanisa kama hali yenye kufaa sana kwa maisha ya kipadre. Ni kwa wakati mmoja ishara na kichocheo cha mapendo ya kichungaji, na chimbuko mahsusi la uzaaji wa kiroho katika ulimwengu [125]. Ni kweli kwamba [useja, kwa msingi,] hautakiwi na maumbile yenyewe ya ukuhani, kama ilivyo wazi katika utaratibu wa Kanisa la awali [126] na katika mapokeo ya Makanisa ya Mashariki, ambapo zaidi ya wale ambao, pamoja na Maaskofu wote, wanachagua kwa msaada wa neema kutunza useja, wapo pia mapadre bora waliooa. Lakini Mtaguso huu, ukishauri useja wa kikanisa, hauna kwa njia yoyote lengo la kubadilisha nidhamu iliyo tofauti inayodumu kwa uhalali katika Makanisa ya Mashariki, ila unawahimiza kwa upendo wale wote ambao walipewa Daraja ya upadre wakiwa katika hali ya ndoa wadumu katika wito mtakatifu, wakiendelea kutolea kwa upana na ukarimu maisha yao kwa ajili ya kundi walilokabidhiwa [127].

Useja lakini una mahusiano ya namna nyingi yenye manufaa na upadre kwa sababu utume wa kipadre, lengo lake ni utumishi wa utu mpya ambao Kristo, aliye mshindi wa mauti, humfufua ulimwenguni kwa njia ya Roho wake, nao asili yake “si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu” (Yn 1:13). Kwa kutunza ubikira, au useja, kwa ufalme wa mbinguni[128] mapadre wanajiweka wakfu kwa Kristo kwa njia mpya na kuu, na wanaambatana naye bila kusita na kwa moyo usiogawanyika[129] na wanajitoa kwa furaha katika Yeye na kwa ajili yake kwa utumishi wa Mungu na wa wanadamu. Tena wanatumikia kwa utayari Ufalme wake na kazi yake ya kuzaa upya kwa mbinguni, na kwa hali hiyo wako tayari kupokea ubaba ulio mpana zaidi katika Kristo. Na kwa njia hii wanatangaza mbele ya watu kwamba lengo lao ni kujitolea tu kwa ajili ya wajibu wa kuwaongoza waamini kwenye arusi na mume mmoja, na kuwaleta kwa Kristo kama bikira safi[130], wakikumbusha kwa njia hiyo ile ndoa ya kifumbo aliyoweka Mungu na itakayodhihirishwa wazi katika ulimwengu ujao ambapo Kanisa lina Kristo kama mume wake pekee[131]. Wao tena wanakuwa ishara iliyo hai ya ulimwengu ule ujao, uliopo tangu sasa kwa njia ya imani na ya mapendo, ambapo wana wa ufufuo wala hawaoi wala hawaolewi[132].

Kwa sababu hizi zenye misingi katika fumbo la Kristo na la utume wake, useja ambao kwanza ulikuwa unashauriwa kwa mapadre, baadaye umekuwa sharti kwa sheria katika Kanisa la kiroma kwa wote wenye kuelekea kupokea Daraja takatifu. Mtaguso Mkuu huu kwa mara nyingine unakubali na kuidhinisha sheria hizo kwa ajili ya wale wanaoelekea upadre; kwa imani katika Roho kwamba kipaji cha useja, kinacholingana sana na ukuhani wa Agano Jipya, kinajaliwa kwa hisani na Mungu Baba, ikiwa wote wanaoshiriki ukuhani wa Kristo kwa njia ya Sakramenti ya Upadre, naam, na pia Kanisa zima, wanakiomba kwa unyenyekevu na bidii. Aidha, Mtaguso Mkuu unawahimiza mapadre, ambao kwa kutegemea neema ya Mungu wanakubali kwa hiari yao useja mtakatifu kulingana na mfano wa Kristo, ili waushike kwa ushujaa na kwa moyo wote na kudumu kwa uaminifu katika hali hiyo, wakiwa wanathamini sana kipaji cha ajabu ambacho Mungu Baba aliwajalia na Bwana alikisifia kwa wazi [133], na kwa kuzingatia pia mafumbo makubwa ambayo ndani yake yanamaanishwa na kutimizwa. Na katika ulimwengu wa leo, kama kujikatalia tamaa kikamilifu kunatazamwa na watu wengi kama fumbo lisilowezekana, basi mapadre wanatakiwa kuomba kwa unyenyekevu mkuu na udumifu, pamoja na Kanisa zima, ili kupewa neema ya uaminifu ambao haukataliwi kamwe kwa wale wanaoomba, pamoja na kutumia misaada ya kimungu na ya kawaida ambayo wote waweza kuipokea. Hasa wasipuuzie zile kanuni za uwalii ( normas asceticas) zilizodhaminiwa na mang’amuzi ya Kanisa, ambazo siku hizi zinadumu kuwa na manufaa. Mtaguso Mkuu huu unawasihi mapadre – na sio hao tu, bali pia waamini wote – kutunza kipaji hiki cha thamani kilicho useja wa kipadre, na kumwomba Mungu, wote, ili alijalie Kanisa lake [kipaji hicho] daima na kwa utele.

Umaskini wa hiari na mtazamo kwa malimwengu

17. Mapadre, kwa ajili ya mahusiano ya urafiki na ya udugu kati yao na kwa watu wengine, watajifunza kuheshimu tunu za kiutu na kuvithamini vitu vilivyoumbwa kama ni vipaji vya Mungu. Lakini, kwa kuishi ulimwenguni lazima wazingatie pia kwamba, kadiri alivyosema Bwana na Mwalimu wetu, wenyewe sio wa ulimwengu[134]. Kwa hiyo, huku wakitumia ulimwengu huu, kama hawautumii sana[135], waweza kuufikia ule uhuru ambao, wakiondolewa na kila wasiwasi usio wa mpango, wanakuwa watiifu kwa kusikia sauti ya Mungu katika maisha ya kila siku. Kutokana na uhuru na utiifu huo kitamea kile kiasi cha rohoni kinachowezesha kujihusianisha kwa uadilifu na ulimwengu na malimwengu pia. Uhusiano huo ni muhimu kwa mapadre, kwa vile utume wa Kanisa hutekelezwa kati ya ulimwengu, na mali za dunia ni za kufaa kwa ukomavu wa mtu binafsi. Kwa hiyo wawe na moyo wa shukrani kwa ajili ya vitu vyote ambavyo Mungu Baba amewajalia ili waweze kuendesha maisha yenye utaratibu. Lakini ni lazima waweze kutambua katika mwanga wa imani yale yote yanayowapata, kusudi wajisikie kama wanasukumwa kutumia kwa adili mali kulingana na mapenzi ya Mungu, wakikataa kuzipokea zile zenye kudhuru utume wao.

Mapadre, kwa vile Bwana ni “fungu lao na urithi wao” (Hes 18:20), watakiwa kutumia malimwengu kwa ajili tu ya malengo yale ambayo mafundisho ya Kristo Bwana na sheria za Kanisa vinasema zinaweza kutumiwa.

Kuhusu mali za Kanisa – zinavyoitwa hasa – mapadre watakiwa kuzisimamia kama inavyotakiwa na hali yenyewe ya mali hizo, kulingana na sheria za Kanisa, na kwa kusaidiwa, kadiri inavyowezekana, na wataalamu walei. Wanatakiwa kuzitumia kila mara mali hizo kwa malengo yale ambayo Kanisa linaweza kumiliki mali ili kuyafanikisha, yaani: kuratibisha ibada za Mungu; utoaji wa riziki za heshima kwa makleri; mategemezo ya matendo ya kichungaji na ya huruma, hasa kwa ajili ya maskini[136]. Zaidi ya hayo, kwa habari za mali wanazojipatia wanapotekeleza ofisio yoyote ya kikanisa (ecclesiastici officii), Mapadre na vilevile Maaskofu – ijapo zinadumu haki maalum zikiwepo[137] – wanatakiwa kuzitumia kwanza kwa ajili ya maponeo (sustentationem) yao ya haki na kwa utimilizaji wa wajibu wa dhima yao; kitakachobaki wapende kutoa kwa mema ya Kanisa na kwa matendo ya huruma. Wasitumie wadhifa wa kikanisa kama njia ya kujipatia faida, wala wasitumie mapato yanayotokana nao kwa kusudi la kuongeza mali za familia au za ukoo wao[138]. Ndiyo sababu mapadre, bila kuangalia sana moyoni mali[139] wanatakiwa kuepukana daima na kila uchu wa mali na kutojiingiza katika aina yoyote ile ya biashara.

Kwa kweli hao wanaalikwa kuambatana na umaskini wa hiari, ambao wakiushika wanaweza kufanana na Kristo kwa namna inayoonekana wazi zaidi na kumudu kutekeleza kwa utayari wote huduma takatifu. Kwa sababu Kristo akawa maskini kwa ajili yetu, yeye aliyekuwa tajiri, ili umaskini wake ukawe kwetu utajiri[140]. Mitume, kwa upande wao walitoa ushuhuda kwa mifano ya nafsi zao kwamba kipaji cha Mungu, kilicho cha bure, kinatakiwa kutolewa bure[141], wakiwa wamejua kuwa na vingi na kupungukiwa[142]. Lakini pia matumizi ya pamoja ya vitu, kwa kiasi fulani, kulingana na mfano wa hali ile ya kuwa na mali zote shirika, inayosifiwa katika historia ya Kanisa la awali[143], inasaidia kwa kiwango kikubwa kuandaa njia kwa ajili ya mapendo ya kichungaji. Aidha, kwa hali ya maisha ya namna hiyo mapadre wanaweza kutekeleza vema kimatendo roho ya umaskini kadiri Kristo alivyoshauri.

Kwa hiyo Mapadre, kama vile na Maaskofu pia, hali wamesukumwa na Roho wa Bwana aliyempaka mafuta Mwokozi na kumtuma kuwatangazia maskini habari njema[144], wajitahidi kuepukana na yale yawezayo kuwafanya maskini wajitenge na kuondoka, na hata zaidi kuliko wanafunzi wengine wa Bwana waondoe nyumbani mwao kila aina ya majivuno. Waandae nyumba zao kwa namna ambayo yeyote asiweze kuzifikiri kuwa hazifikiki, wala asiogope kuzikaribia hata kama ni mtu wa hali nyonge sana.

III - MISAADA KWA MAISHA YA MAPADRE

Misaada ya kukuza maisha ya kiroho

18. Mapadre, ili kuweza kukuza muungano na Kristo katika hali zozote za maisha yao, pamoja na kutekeleza kwa uwajibikaji huduma yao, wamepewa nyenzo ambazo ni za wote, na nyinginezo maalum, za kawaida au nyingine mpya, ambazo Roho Mtakatifu hajakoma kuibusha kati ya watu wa Mungu, na ambazo Kanisa linazipendekeza – au mara nyingine hata linaziamuru[145] – kwa ajili ya kutakatifuza wanakanisa. Kati ya misaada yote ya kiroho yana nafasi ya pekee yale matendo ambayo waamini, kwa njia yake wanajilisha Neno wa Mungu katika namna mbili, ya Maandiko Matakatifu na ya Ekaristi[146]. Ni dhahiri kwa wote umuhimu wa kuitumia hiyo [misaada] kwa lengo la kila padre la kujikuzia utakatifu.

Mapadre, kwa kuwa ni wahudumu wa neema ya sakramenti, wanajiunga kwa ndani na Kristo Mwokozi na Mchungaji kwa kupokea kwa manufaa sakramenti, hasa kwa njia ya sakramenti ya Kitubio ya mara kwa mara, kwa vile hicho, kinachotakiwa kuandaliwa kwa kuhoji dhamiri kila siku, kinachochea kwa vikubwa toba ya moyoni iliyo ya lazima mbele ya Baba wa huruma. Katika mwanga wa imani, inayolishwa na somo la kimungu (lectione divina), wenyewe waweza kutafuta kwa makini kusudi wapate kuvumbua katika matukio mbalimbali ya maisha ishara za mapenzi ya Mungu na misukumo ya neema yake, ili kuwa watiifu zaidi na zaidi katika kukabili kila hitaji la utume waliopenda kuupokea katika Roho Mtakatifu. Mfano mzuri sana wa utiifu huo wanaweza kuuona daima katika Bikira Maria mtakatifu, ambaye chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu alijitolea kwa moyo wote kwa ajili ya fumbo la Ukombozi wa wanadamu[147]. Yeye ndiye Mama wa Kuhani mkuu na wa milele, Malkia wa Mitume, na mlinzi wa huduma yao. Hivyo mapadre wamheshimu na kumpenda kwa upendo na ibada za kimwana.

Aidha mapadre, kwa ajili ya kutekeleza huduma yao kiaminifu, wawe na moyo wa kupenda kuongea kila siku na Kristo Bwana kwa kwenda kumtembelea katika tabernakulo na kutimiza ibada ya binafsi mbele ya Ekaristi Takatifu. Wakubali kwa furaha kutumia muda fulani kwa ajili ya ritriti ya kiroho, na wastahi sana uongozi wa roho (directionem spiritualem). Kwa njia mbalimbali – hasa kwa sala ya kutafakari, iliyozoeleka kuwa ya manufaa, na kwa njia mbalimbali za sala, kadiri ya mapendeleo ya kila mmoja – mapadre wanaweza kutafuta na kuomba kwa ari kwa Mungu ili roho halisi ya kuabudu ambayo itawafanya, wao pamoja na watu waliokabidhiwa, wajiunge kwa moyo na Kristo, aliye mshenga wa Agano Jipya, na hivyo kuweza kulia, kama waliofanywa wana: “Aba, yaani, Baba!” (Rum 8:15).

Taaluma na maarifa ya kichungaji

19. Katika madhehebu takatifu ya ordinasio Askofu huwakumbushia mapadre kwamba wanatakiwa kuwa “wamekomaa katika maarifa”, pia kwamba mafundisho yao yawe “dawa ya rohoni kwa taifa la Mungu” [148]. Hivyo basi, inabidi kwamba elimu ya mhudumu mtakatifu iwe takatifu nayo, kwa vile inatoka katika chemchemi iliyo takatifu na inaelekeza kwenye kikomo kilicho kitakatifu vilevile. [Hivyo, elimu] inatakiwa itokane kwanza kabisa na kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu [149]; lakini pia inalishwa kwa manufaa na kusoma maandishi ya Mababa watakatifu na Walimu [wa Kanisa] na maandishi mengineyo ya Mapokeo. Pamoja na hayo, inafaa mapadre wafahamu vizuri hati za Majisterio, hasa zile za Mitaguso mikuu na ya Mapapa, ili waweze kutoa majibu yanayofaa kwa hoja zinazojadiliwa na watu wa nyakati zetu. Pia inafaa watafute maoni ya wanateolojia mabingwa wenye mafundisho yaliyo sahihi.

Lakini ni kweli kwamba katika nyakati zetu elimu ya kidunia na pia taaluma takatifu zinaendelea kwa mwendo wa kasi kuliko nyakati zilizopita; kwa hiyo inafaa mapadre wazingatie suala la kujiendeleza daima katika taaluma yao ya teolojia na katika elimu yao kwa jumla, kusudi kuwa na hali inayofaa ili kuweza kujadiliana na watu wa nyakati zao hizi.

Lakini, ili kurahisisha wajibu wa mapadre wa kujiendeleza kielimu na kujifunza mitindo ya uinjilishaji na ya utume iliyo bora zaidi, iandaliwe kwa ajili yao kwa makini misaada yenye kufaa, kwa kuilinganisha kwa busara na mazingira ya mahali. Misaada hiyo itakuwa kama kozi au makongamano; uanzishaji wa vituo kwa ajili ya masomo ya kichungaji; ufunguzi wa maktaba na uratibishaji wa kufaa wa masomo unaofanywa kwa njia ya wataalamu. Maaskofu wanatakiwa kuzingatia jinsi gani wataweza, kila mmoja peke yake au kimajimbo, kupata mfumo bora wa kuwawezesha mapadre wao wote – hasa miaka michache baada ya ordinasio[150] – wahudhurie kwa vipindi mbalimbali, kozi za kujiendeleza katika taaluma za teolojia na mitindo ya kichungaji. Kozi hizi, lengo lake ni kuwasaidia pia kuimarisha maisha yao ya kiroho na kuwawezesha kubadilishana mang’amuzi ya kitume na mapadre wenzao[151]. Kwa njia ya misaada yote hiyo na mingine kama hiyo, kuwepo na uangalizi wa pekee kwa maparoko walioteuliwa karibuni na kwa wale waanzao uchungaji mpya au wanaohamishwa katika jimbo au nchi nyingine.

Hatimaye, Maaskofu waangalie sana ili mapadre anuwai wajibidishe katika masomo ya ndani ya elimu ya kimungu kusudi wasikosekane kamwe maprofesa wamilisi kwa ajili ya shule za kikanisa, na wataalamu wawezao kuwaelekeza pia mapadre wengine na waamini kwa mafundisho yaliyo ya lazima kwa wote. Aidha, kwa hayo yote yanahimizwa maendeleo katika taaluma takatifu, yaliyo muhimu kwelikweli kwa Kanisa.

Kuwapatia mapadre tunzo za halali

20. Mapadre wanajishughulisha muda wote kwa utumishi wa Mungu katika kutekeleza wajibu walizokabidhiwa. Kwa hiyo wastahili kupewa ujira ulio wa haki, kwa vile “mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake” (Lk 10:7)[152], na kwamba “Bwana ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili” (1Kor 9:14). Kwa misingi hii, kama hakuna njia nyingine ya kuwapa mapadre posho ya haki, basi ni juu ya waamini wenyewe kushughulikia hilo, kwa sababu mapadre wanafanya kazi kwa manufaa yao. Yaani, waamini wana faradhi ya kufanyiza mapadre wasikose vifaa vya kuishi maisha manyofu na yenye heshima. Ni wajibu wa Maaskofu kuwakumbushia waamini faradhi hiyo na kushughulika, kila mmoja katika jimbo lake au, na ingekuwa afadhali, kwa kuungana katika kundi lenye maslahi katika ukanda uleule, ili zitungwe sheria zenye kuhakikisha kuwa tunzo lenye heshima linatolewa kwa wale wanaoshika au walioshika wadhifa kwa utumishi wa taifa la Mungu. Kuhusu aina ya ujira wa kumpa kila mhudumu, inabidi kuzingatia wadhifa wenyewe ulivyo, na pia mazingira mbalimbali ya nyakati na mahali. Ujira huo kwa vyovyote utakuwa uleule kwa wote waliopo katika hali ileile, na uwe wa kutosha kwa mahitaji yao. Maana yake uwawezeshe mapadre kutoa mishahara ya haki kwa wafanyakazi katika nyumba zao, pia kuweza wenyewe kuwasaidia, kwa namna fulani, wanaohitaji msaada, kwa sababu huduma hiyo kwa ajili ya maskini ilikuwa inasifiwa sana katika Kanisa tangu awali. Katika kupanga kiwango cha ujira wa mapadre hakuna budi kuzingatia pia kwamba huohuo utawasaidia pia kulipia muda wa kutosha wa likizo kila mwaka. Pia ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kama Mapadre wanafaulu kupata likizo hiyo.

Kwa vyovyote, lililo la maana ni kutazama wadhifa wanaotekeleza wahudumu watakatifu. Kwa hiyo, mfumo wote unaojulikana kama mfumo wa kibenefizio (systema beneficiale) lazima ufutwe au walau utengenezwe upya kutoka kwa msingi, ili kusudi sehemu inayohusu benefizio yenyewe – yaani, haki ya kupewa maslahi kutokana na ofisio ile ya kikanisa – ikawe bila maana, na itangulizwe kwa umuhimu ofisio ya kikanisa yenyewe. Aidha, tangu sasa, kwa jina la ofisio ya kikanisa inamaanishwa wadhifa wowote unaotolewa kwa namna ya kudumu kwa lengo la kiroho.

Fungu la pamoja na pensheni

21. Lazima kuzingatia daima mfano wa waamini katika Kanisa la awali la Yerusalemu, ambapo “walikuwa na vitu vyote shirika” (Mdo 4:32) na “kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji” (Mdo 4:35). Kwa hiyo, ni ya manufaa makubwa sana kwamba, angalau katika nchi ambayo riziki za makleri (cleri sustentatio) zinatokana kwa sehemu zilizo kubwa na matoleo ya waamini, riziki zinazopatikana kwa njia hiyo zikusanywe na taasisi maalum ya kijimbo. Askofu atasimamia taasisi hiyo, kwa kusaidiwa na mapadre walioteuliwa kwa shughuli hizo, pia wa walei wataalamu katika mambo ya fedha, pale ambapo panaonekana inafaa. Inapendekezwa pia kwamba, kadiri iwezekanavyo, iundwe katika kila jimbo au katika kila nchi fungubia (massa bonorum communis) ambamo Maaskofu wanaweza kuchota ili kukidhi masharti mbele ya watu wanaofanya kazi kwa ajili ya Kanisa na kwa kukabili mahitaji mbalimbali ya jimbo. Aidha, kwa njia ya fungukikoa hiyo majimbo yenye uwezo zaidi kifedha wataweza kuyasaidia yale yasiyo na fedha nyingi, ili wingi wao uwafae upungufu wao[153]. Pia fungukikoa hiyo inafaa iundwe hasa kutokana na matoleo ya waamini; lakini zinaweza kuingia pia mali zenye asili nyinginezo za kuukiliwa kisheria (iure determinandis).

Zaidi ya hayo, katika nchi zile ambapo pensheni kwa ajili ya makleri haijapangwa vema, Mabaraza ya Maaskofu yaishughulikie kwa kuafikiana na sheria za kikanisa na za kiserikali ili kuanzisha, kwa mfano, taasisi za msaada za kijimbo zinazojitegemea au zinazoshirikishana; au kwa taasisi zenye kuhudumia eneo kubwa, kwa mfano wa majimbo anuwai; kisha kwa taasisi zenye kutoa huduma katika nchi nzima. Kwa aina yoyote ile, taasisi hizo zatakiwa kushughulika, chini ya uangalizi wa kihierarkia, huduma ya afya na ya kijamii, pia tunzo la heshima kwa mapadre walio wagonjwa au wasiojiweza au ni wazee. Mapadre kwa upande wao, wasaidie taasisi hizo zinazoundwa, wakisukumwa na moyo wa mshikamano kwa ajili ya mapadre wenzao, unaowafanya washiriki matatizo yao [154]. Tena, wazingatie pia kwamba kwa kufanya hivyo, wataepukana na mafadhaiko kwa ajili ya siku za mbeleni, na hivyo wataweza kwa roho iliyokomaa kutekeleza umaskini wa kiinjili na kujitolea kikamilifu kwa wokovu wa nafsi. Hatimaye, wale wenye wajibu wafanye bidii kusudi taasisi za misaada za nchi mbalimbali zenye kushughulikia sekta ileile zipate kushirikiana, kwa sababu kwa kufanya hivyo zitapata kuimarika na kuenea.

HITIMISHO NA HIMIZO

22. Mtaguso Mkuu huu pamoja na kukumbuka furaha za maisha ya kipadre, hauwezi kuyasahau vilevile na magumu ambayo mapadre hawana budi kuyakabili katika mazingira ya maisha ya leo. Tena, unakumbuka namna hali za uchumi na za kijamii, na hata maadili ya binadamu, zinavyokuwa na mageuzi; pia jinsi ngazi ya tunu zinazothaminiwa na watu inavyobadilika. Kwa sababu hiyo, wahudumu wa Kanisa, na mara nyingine pia waamini wenyewe, wanaweza pengine kujisikia wageni kabisa katika ulimwengu huu, wakajiuliza kwa wasiwasi kwa njia gani na kwa maneno ya aina gani wataweza kuwasiliana nao. Vizuio vipya kwa imani, utovu wa mafanikio – inavyoonekana – katika jitihada zinazofanywa, upweke mgumu wanamoishi, vinaweza kuwa hatari kubwa ya kukatisha tamaa.

Lakini ulimwengu huu, ambao leo unakabidhiwa kwa upendo na kwa huduma ya wachungaji wa Kanisa, [huu] Mungu aliupenda, mpaka akamtoa Mwanae pekee kwa ajili yake[155]. Ukweli ni kwamba ulimwengu huu, uliofungwa katika dhambi nyingi, lakini uliotajirishwa na mema mengi pia, unalipatia Kanisa mawe yaliyo hai[156] ambayo kwa pamoja yanasaidia kujenga maskani ya Mungu katika Roho[157]. Naye Roho Mtakatifu mwenyewe, kama kwa upande mmoja analisukuma Kanisa kufungua njia mpya za kuufikia ulimwengu wa leo, kwa upande mwingine anashauri na kuhimiza mabadiliko yenye kufaa katika huduma ya kipadre.

Mapadre wakumbuke kwamba katika kutekeleza kazi yao hawapo upweke kamwe, kwa sababu uweza wa Mungu unawasimamia. Wawe na imani katika Kristo aliyewaita kushiriki ukuhani wake; na kwa imani hiyo wajishughulishe katika huduma yao kwa matumaini makubwa, wakijua kwamba Mungu ana uwezo wa kuwaongezea mapendo[158]. Pia wakumbuke kwamba karibu nao wapo ndugu wenzao katika upadre, na hasa waamini wa ulimwengu mzima. Na kweli kuna ushirikiano wa mapadre wote katika kutekeleza azimio la Wokovu la Mungu, ambalo ni fumbo la Kristo, yaani sakramenti (au fumbo) iliyositirika katika Mungu tangu zamani zote[159]. Azimio hilo halitimiliki isipokuwa polepole, kwa njia ya mshikamano wa huduma mbalimbali zinazotimizwa kwa ajili ya kujenga Mwili wa Kristo hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wake. Kwa vile hayo yote yamefichwa pamoja na Kristo katika Mungu[160], kwa njia ya imani hasa inawezekana kuyafahamu. Kwa sababu viongozi wa taifa la Mungu wanatakiwa kuenenda katika imani wakifuata mfano wa Ibrahimu mwamini, ambaye kwa imani “alipoitwa aliitikia, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi: akatoka asijue aendako” (Ebr 11:8). Maana mgawaji wa mafumbo ya Mungu anaweza kufananishwa na yule mtu anayepanda mbegu shambani, ambaye Bwana anasema juu yake: “akiwa akilala na kuondoka, usiku na mchana, mbegu inamea na kukua, asivyojua yeye” (Mk 4:27).

Bwana Yesu aliyesema, “Jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33), kwa maneno hayo hakuliahidia Kanisa lake ushindi kamili katika dunia hii. Mtaguso Mkuu unafurahi kuona kwamba dunia iliyomwagiwa mbegu ya Injili, inatoa matunda mahali mahali, chini ya uongozi wa Roho wa Bwana ambaye amejaza ulimwengu na amemimina katika mioyo mingi ya mapadre na ya waamini roho ya kimisionari kwelikweli. Kwa ajili ya hayo yote Mtaguso Mkuu unawashukuru kwa upendo mkubwa mapadre wote wa dunia nzima: “Basi, atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Yesu Kristo” (Efe 3:20-21).

 

Mambo yote yaliyoamuliwa katika dikrii hii, na kila moja kati yao, yamewapendeza Mababa wa Mtaguso Mkuu. Nasi, kadiri ya mamlaka ya kitume tuliyopewa na Kristo, na pamoja na Mababa waheshimiwa, katika Roho Mtakatifu, tunayakubali, tunayaidhinisha na tunayathibitisha. Na yale yote yaliyoamuriwa kwa pamoja katika Sinodi hii, tunaamuru yawekwe kwa ajili ya utukufu wa Mungu.

 

Roma, katika Kanisa la Mt. Petro, 7 Desemba 1965

 

Mimi mwenyewe, Paulo, Askofu wa Kanisa Katoliki

(zinafuata sahihi za Mababa)

 

  



[1] Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, 4 desemba 1963: AAS 56 (1964), uk. 97ss.; Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, 21 novemba 1964: AAS 57 (1965), uk. 5ss.; Decr. De pastorali Episcoporum munere in Ecclesia, Christus domino, 28 oktoba 1965: AAS 58 (1966), uk. 673 ss.; Decr. De institutione sacerdotali, Optatam totius, 28 oktoba 1965: AAS 58 (1966), uk. 713 ss.
[2] Taz. Mt 3:16; Lk 4:18; Mdo 4:27; 10:38.
[3] Taz. 1Pet 2:5 na 9.
[4] Taz. 1Pet 3:15.
[5] Taz. Ufu 19:10. – Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 35: AAS 57 (1965), uk. 40-41.
[6] Taz. Conc. Trid., sess. XXIII, cap. 1 na can. 1: Denz. 957 na 961 (1764 na 1771).
[7] Taz. Yn 20:21. – Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 18: AAS 57 (1965), uk. 21-22.
[8] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 33-36.
[9] Taz. ibid.
[10] Taz. Pontificale romanum, De Ordinatione presbiterorum, Utangulizi. Maneno hayo yanapatikana tayari katika Sacramentarium veronensis: ed. L. C. Moehlberg, Roma, 1956, uk. 122; vilevile katika Missale Francorum: ed. L. C. Moehlberg, Roma, 1957, uk. 9; na pia katika Liber Sacramentorum Romanae Ecclesiae: ed. L. C. Moehlberg, Roma, 1960 uk. 25; na pia katika Pontificale romano-germanicum: ed. Vogel-Elze, Città del Vaticano, 1963, vol. I, uk. 34.
[11] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 10: AAS 57 (1965), uk. 14-15.
[12] Taz. Rum 15:16.
[13] Taz. 1Kor 11:26.
[14] Mt. Augustinus, De Civitate Dei, 10, 6: PL 41, 284.
[15] Taz. 1Kor 15:24.
[16] Taz. Ebr 5:1.
[17] Taz. Ebr 2:17; 4:15.
[18] Taz. 1Kor 9:19-23 Vulg.
[19] Taz. Mdo 13:2.
[20] “Juhudi ile ya ukamilifu wa kiroho na kimaadili yachochewa hata kwa nje na hali linamoishi Kanisa. Nalo Kanisa haliwezi kusimama tisti lenye kutojali mabadiliko ya mambo ya kibinadamu yalizungukayo, wenye kuliathiri na kuweka mipaka juu ya mwenendo wake, kwa njia nyingi. Kama kila mmoja ajuavyo, Kanisa halijitengi na jamii ya wanadamu, bali laishi ndani yake. Kwa hiyo wanakanisa huvutwa, na kujifunza utamaduni wao, hupokea sheria na kuzikubali desturi. Mahusiano hayo ya Kanisa na jamii ya wanadamu yasababisha sikuzote hali yenye shida, itaabishayo sana, hasa leo... Hivyo Mtume Paulo mwenyewe alivyowafundisha wakristo wa kizazi cha kwanza, “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati na haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?... Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?” (2Kor 6:14-15). Walezi na walimu wafanyao kazi katika Kanisa wapaswa kuwakumbusha vijana wakatoliki hali yao hii ya pekee na wajibu wao utokanao nayo wa kuishi katika ulimwengu, wala si kuwa wa ulimwengu, kadiri ya sala ya Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake: “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu” (Yn 17:15-16). Na Kanisa lashika sala hii kama ni ya kwake mwenyewe.

Lakini utofauti huu ni sio utengano, wala si ubaridi, wala woga, wala dharau. Kanisa linapojitofautisha na jamii ya wanadamu, halipingani nayo, bali laungana nayo”. (Paulus VI, Litt. Encic. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964), uk. 627 na 638).

[21] Taz. Rum 12:2.
[22] Taz. Yn 10:14-16.
[23] Taz. Mt. Polycarpus, Epis. ad Philippenses, VI, 1: “Mapadre wawe wepesi wa rehema na huruma kwa ajili ya watu wote, wawarudishe wapoteao, na kuwatembelea wagonjwa wote, bila kusahau mjane, yatima na maskini, bali kuwa daima tayari kutenda mema mbele ya Mungu na watu. Waepukane na hasira, upendeleo na hukumu isiyo ya haki, wakiepa kila choyo, na kutokuwa na haraka ya kuamini mambo juu ya mtu fulani, wala kuwa wakali katika hukumu, wakijua kwamba sisi sote tu wadeni wa dhambi”: (ed. F. X. Funk, Patre Apostolici, I, uk. 273).
[24] Taz. 1Pet 1:23; Mdo 6:7; 12:24. “[Mitume] walihubiri neno la kweli na wakazaa Makanisa”: Mt. Augustinus, Enarr. in Ps., 44, 23: PL 36, 508.
[25] Taz. Mal 2:7; 1Tim 4:11-13; 2Tim 4:5; Tit 1:9.
[26] Taz. Mk 16:16.
[27] Taz. 2Kor 11:7. Juu ya Mapadre, kama washiriki wa Maaskofu, huwezekana kusema yaleyale yanayosemwa juu ya Maaskofu. Taz. Statuta Ecclesiae Antiqua, c. 3 (ed. Ch. Munier, Paris, 1960, uk. 79); Decretum Gratiani, C. 6, D. 88 (ed. Friedberg, I, 307); Conc. Trid., sess. V, Decr. 2: juu ya kusoma na kuhubiri Maandiko Matakatifu, n. 9 ( Conc. Oec. Decreta, ed. Herder, Roma, 1962, uk. 645); ibid., sess. XXIV , Decr. De reform., can. 4 ( COD, uk. 739). Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 25: AAS 57 (1965), uk. 29-31.
[28] Taz. Constitutiones Apostolorum, II, 26, 7: “Mapadre wawe walimu wa maarifa ya kimungu, kwa kuwa Bwana mwenyewe alitutuma akisema, ‘Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi...’”: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones Apostolorum, I, Paderborn, 1905, uk. 105. – Sacramentarium Leonianum, na Sacramentaria nyingine hadi Pontificale Romano, Utangulizi katika Madhehebu ya Upadirisho: “Kwa majaliwa haya, Ee Bwana, uliwaunganisha na Mitume wa Mwanao walimu wengine wa imani, ambao kwa njia yao waliujaza ulimwengu wahubiri (au “mahubiri”) wenye kufuata ( secundis)”. – Liber Ordinum Liturgiae Mozarabicae, Utangulizi katika Madhehebu ya Upadirisho: “Kama mwalimu wa watu na kiongozi wa walio chini yake, aitunze imani katoliki kwa utaratibu, na kuwatangazia wote wokovu wa kweli”: ed. M. Férotin, Le Liber Ordinum en usage dans l’église Wisigothique et Mozarabe d’Espagne: Monumenta Ecclesiae Liturgica, vol. V, Paris, 1904, col. 55, lin. 4-6.
[29] Taz. Gal 2:5.
[30] Taz. 1Pet 2:12.
[31] Taz. madhehebu ya Upadirisho katika Kanisa la Iskanderia (Misri) la Wajakobiti: “...Wakusanye watu wako kwa neno la mafundisho, kama vile mama mlishi anavyowalisha watoto wake”: H. Denzinger,  Ritus Orientaliu, Tom. II, Würzburg, 1863, uk. 14.
[32] Taz. Mt 28:19; Mk 16:16. – Tertullianus, De baptismo, 14, 2: Corpus Christianorum, Series latina, I, uk. 289, 11-13. – Mt. Athanasius, Adv. Arianos, 2, 42: PG 26, 237AB. – Mt. Hieronymus, In Matth., 28, 19: PL 26, 226D: “Kwanza wanayafundisha mataifa yote, pili wanawatia maji wale waliofundishwa. Kwa maana haiwezekani mwili hupate sakramenti ya ubatizo kabla roho haijapokea ukweli wa imani”. – Mt. Thomas, Expositio primae Decretalis, § 1: “Mwokozi wetu alipowatuma wanafunzi wake kuhubiri, aliwausia matatu: la kwanza, kufundisha imani, la pili, kuwalisha waamini kwa sakramenti...”: ed. Marietti, Opuscula Theologica, Torino-Roma, 1954, 1138.
[33] Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, n. 35, 2: AAS 56 (1964), uk. 109.
[34] Taz. ibid., nn. 33, 35, 48, 52, uk. 108-109, 113, 114.
[35] Taz. ibid., n. 7, uk. 100-101. – Pius XII, Litt. Encicl. Mystici Corporis, 29 juni 1943: AAS 35 (1943), uk. 230.
[36] Mt. Ignatius M., Smirn., 8, 1-2: ed. F. X. Funk, uk. 240. – Constitutiones Apostolorum, VIII, 12, 3: ed. F. X. Funk, uk. 496. – Id ., VIII, 29, 2: ibid., uk. 532.
[37] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 33-36.
[38] “Ekaristi ndiyo kama ukamilisho wa maisha ya kiroho, na utimilizo wa sakramenti zote”: Mt. Thomas, Summa Theol. III, q. 73, a. 3 c. – Taz. pia Summa Theol. III, q. 65, a. 3.
[39] Taz. Mt. Thomas, Summa Theol. III, q. 65, a. 3 ad 1; q. 79, a. 1 c, na ad 1.
[40] Taz. Efe 5:19-20.
[41] Taz. Mt. Hieronymus, Epist., 114, 2: “...vikombe vitakatifu, vitambaa vitakatifu na vyombo vyote vingine vihusuvyo ibada ya Mateso ya Bwana... kwa sababu ya ushirikiano na Mwili na Damu vya Bwana, vistahiwe kwa heshima ileile ya Mwili na Damu yake”: PL 22, 934. – Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 122-127: AAS 56 (1964), uk. 130-132.
[42] “Wasiache kuitembelea kila siku Sakramenti Takatifu, itakiwayo kutunzwa mahali pa heshima kubwa, kwa utukufu mkuu katika makanisa, kadiri ya sheria za kiliturujia. Kwa kuwa kuitembelea ndiko onyesho la shukrani, amana ya upendo, na deni ya maabudu yapasayo kwa ajili ya Kristo Bwana aliyemo humo”: Paulus VI, Litt. Encicl. Mysterium Fidei, 3 septemba 1965: AAS 57 (1965), uk. 771.
[43] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 33-36.
[44] Taz. 2Kor 10:8; 13:10.
[45] Taz. Gal 1:10.
[46] Taz. 1Kor 4:14.
[47] Taz. Didascalia, II, 34, 3; II, 46, 6; II, 47, 1; Constitutiones Apostolorum, II, 47,1: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, I, uk. 116, 142 na 143.
[48] Taz. Gal 4:3; 5:1 na 13.
[49] Taz. Mt. Hieronymus, Epist., 58, 7: “Zinafaa nini kuta zing’aazo kwa vito, ikiwa Kristo hufa kwa njaa katika nafsi ya mtu maskini?”: PL 22, 584.
[50] Taz. 1Pet 4:10nk.
[51] Taz. Mt 25:34-45.
[52] Taz. Lk 4:18.
[53] Yawezekana kutaja pia tabaka nyingine za watu, k. v. wahamiaji, na wasio na makao, n.k. Habari zao zapatikana katika Conc. Vat. II, Decr. De pastorali Episcoporum munere in Ecclesia Christus Dominus, n. 18: AAS 58 (1966), uk. 682.
[54] Taz. Didascalia, II, 59, 1-3: “Katika mafundisho yako agiza na kuwaonya watu waende kanisani, wasikose kabisa, wakusanyike daima, wasilipunguze Kanisa kwa kuondoka na hivyo kuuondolea Mwili wa Kristo kiungo kimoja. Kwa kuwa ninyi ni viungo vya Kristo msijitenge na Kanisa kwa kutokusanyika; kwa kuwa, kadiri ya ahadi yake, Kristo, aliye kichwa chenu, yupo na kushirikiana nanyi, msiwe wenye kutojali nafsi zenu, wala kumtenganisha Mwokozi na viungo vyake, wala kufarakisha ama kutawanya Mwili wake”: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, I, uk. 170. – Paulus VI, Hotuba kwa wakleri wa Italia waliohudhuria warsha ya 13 ya “Wiki ya upyaisho wa kichungaji” ya Orvieto , 6 septemba 1963: AAS 55 (1963), uk. 750 ss.
[55] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk.35.
[56] Taz. Constitutionem Ecclesiasticam Apostolorum (inavyotajwa), XVIII: Mapadre ni sÚmmustai (wahudumu washiriki) na sunep…macoi (wapiganaji washiriki) wa Maaskofu: ed. Th. Schermann, Die allgemaine Kirchenordnung, I, Paderborn, 1914, uk. 26; A. Harnack, Die Quellen der Sog. Apostolischen Kirchenordnung, T. u. U., II, 5, uk. 13, 18 na 19. – Pseudo-Hieronymus, De Septem Ordinibus Ecclesiae: “...katika baraka washirikiana na Maaskofu katika mafumbo”: ed. A. W. Kalff, Wurburg, 1937, uk. 45. – Mt. Isidorus Hispalensis, De Ecclesiasticis Officiis, II, c. 7: “Waongoza Kanisa la Kristo na kushirikiana na Maaskofu katika kuadhimisha Ekaristi, hali kadhalika katika mafundisho ya watu na wajibu wa kuhubiri”: PL 83, 787.
[57] Taz. Didascalia, II, 28, 4: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, I, uk. 108. – Constitutiones Apostolorum, II, 28, 4; II, 34, 3: ibid., 109 na 117.
[58] Ibid., VIII, 16, 4: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, I, uk. 523. – Taz. Epitome Constitutiones Apostolorum, VI: ibid., II, uk. 80, 3-4. – Testamentum Domini: “...umjalie Roho ya neema, shauri na ukarimu, roho ya upadre... awasaidie na kuwaongoza watu wako kwa matendo, kwa uchaji na kwa moyo mweupe”: trad. I. E. Rahmani, Manz, 1899, uk. 69. Vilevile katika Trad. Apost.: ed. B. Botte, La Tradition Apostolique de Saint Hippolyte, Münster i.W., 1963, uk. 20.
[59] Taz. Hes 11:16-25.
[60] Taz. Pontificale romanum, Madhehebu ya Upadirisho, Utangulizi; maneno yayo hayo yapo pia katika Sacramentario leoniano, Sacramentario gelasiano na Sacramentario gregoriano. Kama hayo yapatikana pia katika Liturujia za Mashariki: taz. Trad. Apost.: “...umwangalie mtumishi wako huyu, ukamjalie roho ya neema na ya shauri ya mapadre, ili awasidie na kuwaongoza watu wako kwa moyo mweupe kama ulivyoangalia Taifa lako teule na kumwamuru Musa awachague wazee uliowajaza roho ile uliyomjalia mtumishi wako”: kutoka tafsiri ya zamani ya kilatini cha Verona, ed. B. Botte, La Tradition Apostolique de Saint Hippolyte, Essai de reconstruction, Münster i.W., 1963, uk. 20. – Constitutiones Apostolorum, VIII, 16, 4: ed. F. X. Funk, I, uk. 522, 16-17. – Id ., VIII, 29, 2: ibid., uk. 532. – Epitome Constitutiones Apostolorum, VI: ibid., II, uk. 20, 5-7. – Testamentum Domini: trad. I. E. Rahmani, Manz, 1899, uk. 69. – Euchologium Serapionis, XXVII, ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, II, uk. 190, lin. 1-7. – Ritus Ordinationis in Ritu Maronitarum: trad. H. Denzinger, Ritus Orientalium, II, Würzburg, 1863, uk. 161. – Miongoni mwa Mababa huweza kurejewa: Theodorus Mopsuestenus, In 1Tim 3,8: ed. Swete, II, uk. 119-121. – Theodoretus, Quaestiones in Numeros, XVIII: PG 80, 369C-372B.
[61] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 28: AAS 57 (1965), uk. 35.
[62] Taz. Ioannes XXIII, Litt. Encic. Sacerdotii Nostri primordia, 1 agosti 1959: AAS 51 (1959), uk. 576. – Mt. Pius X, Exhortatio ad clerum, Haerent animo, 4 agosti 1908: S. P. X Acta, vol. IV (1908), uk. 237 ss.
[63] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De pastorali Episcoporum munere in Ecclesia Christus Dominus, nn. 15 na 16: AAS 58 (1966), uk. 679-681.
[64] Mt. Ignatius M., Magn., 6, 1: “Ndiyo maana nawasihi, mjibidishe kuyatenda yote katika uelewano wa kimungu. Maana Askofu huongoza kwa niaba yake Mungu, na mapadre kwa niaba ya baraza la Mitume; aidha mashemasi, ninaowapenda sana, nao wamekabidhiwa utumishi wa Yesu Kristo ambaye hapo awali, kabla ya karne, alikuwa kwa Baba, na hatimaye akadhihirika”: ed. F. X. Funk, uk. 195. – Id., Trall., 3, 1: “Kadhalika na wote wawaheshimu mashemasi kama Yesu Kristo, na pia Askofu aliye kielelezo cha Mungu Baba. Tena wote wawastahi mapadre kama baraza la Mitume, kwa kuwa pasipo hao hata Kanisa halipo”: ibid., uk. 204. – Mt. Hieronymus, In Isaiam, II, 3: PL 24, 61D: “Hata sisi tunayo katika Kanisa Senato yetu, yaani Halmashauri ya mapadre”.
[65] Katika Sheria ya Kanisa kuna habari ya Kapitulo ya Kathedrali, kama “Senato na Halmashauri” ya Askofu ( CIC, can. 391), au, pale isipokuwepo, jopo la washauri wa Jimbo (taz. CIC, cann. 423-428). Hutamanika taasisi hizo zitengenezwe upya ili ziyafalie zaidi mazingira na mahitaji ya siku hizi. Kama inavyoonekana wazi halmashauri hii ni tofauti na Halmashauri ya kichungaji iliyoongelewa katika Mtaguso Mkuu, Dikrii ya utume wa kichungaji wa Maaskofu katika Kanisa Christus Dominus, 28 oktoba 1965, n. 27, na ambamo wajumbe ni pia walei na ambayo inashughulikia tu masuala yanayohusu kazi ya kichungaji. Kuhusu Mapadre kama washauri wa Maaskofu, tazama: Didascalia, II, 28, 4: ed. F. X. Funk, Didascalia et Constitutiones, I, uk. 108. – Constitutiones Apostolorum, II, 82, 4: ibid., I, uk. 109. – Mt. Ignatius M., Magn., 6, 1: ed. F. X. Funk, uk. 194. – Id., Trall., 3, 1: ibid., uk. 204. – Origenes, Contra Celsum, III, 30: Mapadre ni washauri, yaani boÚleutai: PG 11, 957D-960A.
[66] Taz. Paulus VI, Hotuba kwa Maparoko na wahubiri wa kipindi cha Kwaresima wa mji wa Roma iliyotolewa katika Cappella Sistina, tarehe 1 machi 1965: AAS 57 (1965), uk. 326.
[67] Taz. Constitutiones Apostolorum, VIII, 46, 39: “Mapadre... wasifanye lolote bila maamuzi ya Maaskofu, kwa maana yeye ndiye aliyekabidhiwa watu wa Mungu, na kwake zitatakwa roho zao”: ed. F. X. Funk, uk. 577.
[68] Taz. 3Yoh 8.
[69] Taz. Yn 17:23.
[70] Taz. Ebr 13:1-2.
[71] Taz. Ebr 13:16.
[72] Taz. Mt. 5:10.
[73] Taz. 1The 2:12; Kol 1:13.
[74] Taz. Mt 23:8. – “Inatupasa kujifanya kuwa ndugu wa watu hapo tunapotaka kuwa wachungaji wao na baba zao na walimu wao”: Paulus VI, Litt. Encycl. Ecclesiam suam, 6 agosti 1964: AAS 56 (1964) uk. 647.
[75] Taz. Efe 4:7 na 16. – Constitutiones Apostolorum, VIII, 1, 20: “Askofu asijione kuwa bora kuliko mashemasi au mapadre, wala mapadre kuliko walei, kwa kuwa muundo wa jumuiya hutegemea hawa na hawa”: ed. F. X. Funk, I, uk. 467.
[76] Taz. Flp 2:21.
[77] Taz. 1Yoh 4:1.
[78] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 37: AAS 57 (1965), uk. 42-43.
[79] Taz. Efe 4:14.
[80] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De Oecumenismo Unitatis redintegratio: AAS 57 (1965), uk. 90 ss.
[81] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 37: AAS 57 (1965), uk. 42-43.
[82] Taz. Ebr 7:3.
[83] Taz. Lk 10:1.
[84] Taz. 1Pet 2:25.
[85] Taz. Mdo 20:28.
[86] Taz. Mt 9:36.
[87] Pontificale romanum, Madhehebu ya Upadirisho.
[88] Taz. Decr. De institutione sacerdotali, Optatam totius, n. 2: AAS 58 (1966), uk. 714-715.
[89] “Sauti ya Mungu inayoita inatokea kwa njia mbili, ambazo ni nzuri sana na zinaelekezana: moja ni njia ya ndani, ile ya neema, ile ya Roho Mtakatifu, ule mvuto wa ndani usiosemeka, ambao ‘sauti ya ukimya’ na ya uweza wa Bwana inasema mtimani mwa nafsi ya mtu; ile nyingine ni ya nje, ya kibinadamu, inasikika, ina maana kijamii, kisheria na ‘inagusika’, ni ile ya wahudumu wenye sifa wa Neno la Mungu, ile ya Mitume, ile ya hierarkia, ambayo ni chombo cha lazima kilichoanzishwa na matashi ya Kristo kiwe chombo kinachoweza kutafsiri katika lugha ya mang’amuzi ujumbe wa Neno na wa amri ya Mungu. Hayo ndiyo mafundisho ya kikatoliki kwa kufuata Mtakatifu Paulo: Wamwaminije yeye wasiyemsikia... Imani, chanzo chake ni kusikia (Rum 10:14 na 17)”: Paulus VI, Allocutio habita die 5 machi 1965: L’Osservatore Romano, 6 mei 1965, uk. 1.
[90] Taz. Decr. De institutione sacerdotali, Optatam totius, n. 2: AAS 58 (1966), uk. 714-715
[91] Hivyo wafundishavyo Mababa wa Kanisa wakifafanua neno ya Kristo kwa Petro, “Wanipenda?... Lisha kondoo zangu” (Yn 21:17): hivyo Mt. Ioannes Chrysostomus, De sacerdotio, II, 2: PG 48, 633. – Mt. Gregorius Magnus, Reg. Past. Liber, p. I, c. 5: PL 77, 19A.
[92] Taz. 2Kor 12:9.
[93] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Ad catholici sacerdotii, 20 des. 1935: AAS 28 (1936), uk. 10.
[94] Taz. Yn 10:36.
[95] Taz. Lk 24:26.
[96] Taz. Efe 4:13.
[97] Taz. 2Kor 3:8-9.
[98] Taz. kati ya mengine:

Mt. Pius X, Himizo kwa makleri Haerent animo, 4 ago 1908: Mt. Pius X Acta, vol. IV (1908), uk. 237nk.

Pius XI, Litt. Encycl. Ad catholici sacerdotii, 20 des. 1935: AAS 28 (1936), uk. 5nk.

Pius XII, Adhort. Ap. Menti nostrae, 23 sep. 1950: AAS 42 (1950), uk 657nk.

Ioannes XXIII, Litt. Encycl. Sacerdotii nostri primordia, 1 ago 1959: AAS 51 (1939), uk 545nk.

[99] Taz. Mt. Tomaso, Summa Theol., II-II, q.188, a.7.
[100] Taz. Efe 3:9-10.
[101] Taz. Mdo 16:14.
[102] Taz. 2Kor 4:7.
[103] Taz. Efe 3:9.
[104] Taz. Pontificale romanum, Madhehebu ya Upadirisho.
[105] Taz. Missale romanum, Oratio super oblata dominicae IX post Pentecostem.
[106] “Misa, hata kama inaadhimishwa na padre peke yake, wala hivyo si ya kibinafsi, bali ni tendo la Kristo na la Kanisa, katika sadaka litoleayo, lajifunza kujitoa lenyewe kama sadaka ya kiulimwengu na inaweka uwezo ule wa kuokoa, ulio wa pekee sana wala hauna mipaka, unaotokana na msalaba, kwa ajili ya ulimwengu mzima na wokovu wake. Kwa sababu kila Misa inayoadhimishwa inatolewa sio tu kwa wokovu wa nafsi kadha wa kadha, bali kwa wokovu wa ulimwengu mzima (...). Kwa hiyo tunaagiza kwa himizo la kibaba kwamba mapadre, ambao ni furaha yetu ya pekee na taji yetu katika Bwana, waadhimishe Misa kwa namna inayostahili na kwa uchaji kila siku”: Paulus VI, Litt. Encycl. Mysterium Fidei, 3 sept. 1965: AAS 57 (1965) uk. 761-762. Taz. Conc. Vat. II, Const. De Sacra Liturgia, Sacrosanctum Concilium, nn. 26 na 27: AAS 56 (1964) uk. 107.
[107] Taz. Yn 10:11.
[108] Taz. 2Kor 1:7.
[109] Taz. 2Kor 1:4.
[110] Taz. 1Kor 10:33.
[111] Taz. Yn 3:8.
[112] Taz. Yn 4:34.
[113] Taz. 1Yoh 3:16.
[114] “Uwe wajibu wa mapendo kuwachunga kundi la Bwana”: Mt. Augustinus, Tract. in Io., 123, 5: PL 35, 1967.
[115] Taz. Rum 12:2.
[116] Taz. Gal 2:2.
[117] Taz. 2Kor 7:4.
[118] Taz. Yn 4:34; 5:30; 6:38.
[119] Taz. Mdo 13:2.
[120] Taz. Efe 5:10.
[121] Taz. Mdo 20:22.
[122] Taz. 2Kor 12:15.
[123] Taz. Efe 4:11-16.
[124] Taz. Mt 19:12.
[125] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 42: AAS 57 (1965), uk. 47-49.
[126] Taz. 1Tim 3:2-5; Tit 1:6.
[127] Taz. Pius XI, Litt. Encycl. Ad catholici sacerdotii, 20 des. 1935: AAS 28 (1936), uk. 28.
[128] Taz. Mt 19:12.
[129] Taz. 1Kor 7:32-34.
[130] Taz. 2Kor 11:2.
[131] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 42 na 44: AAS 57 (1965), uk. 47-49 na 50-51; Decr. De accomodata renovatione vitae religiosae, Perfectae Caritatis, n. 12: AAS 58 (1966), uk. 707.
[132] Taz. Lk 20:35-36; Pius XI, Litt. Encycl. Ad catholici sacerdotii, 20 des. 1935: AAS 28 (1936), uk. 24-28; Pius XII, Litt. Encycl. Sacra Virginitas, 25 machi 1954: AAS 46 (1954), uk. 169-172.
[133] Taz. Mt 19:11.
[134] Taz. Yn 17:14-16.
[135] Taz. 1Kor 7:31.
[136] Conc. Antioch., can. 25: Mansi 2, 1327-1328; Decretum Gratiani, c. 23, S. 12, q. 1: ed. Friedberg, I, uk. 684-685.
[137] Ieleweke zinaongelewa hapa hasa haki na kawaida zilizopo katika Makanisa ya Mashariki.
[138] Conc. Paris., a. 829, cap. 15: MGH, Legum sectio III, Concilia, t. 2, pars 6, 622; Conc. Trid., Sess. XXV, Decr. de reform., cap. 1: Conc. Oec. Decreta, ed. Herder, Romae 1962, uk. 760-761.
[139] Taz. Zab 62(61):11.
[140] Taz. 2Kor 8:9.
[141] Taz. Mdo 8:18-25.
[142] Taz. Flp 4:12.
[143] Taz. Mdo 2:42-47.
[144] Taz. Lk 4:18.
[145] Taz. CIC, can. 125 nk.
[146] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De accomodata renovatione vitae religiosae, Perfectae Caritatis, n. 6: AAS 58 (1966), uk. 705; Const.dogm. De Divina Revelatione, Dei verbum, n. 21: AAS 58 (1966), uk. 827.
[147] Taz. Conc. Vat. II, Const. dogm. De Ecclesia, Lumen Gentium, n. 65: AAS 57 (1965), uk. 64-65.
[148] Pontificale romanum, Madhehebu ya Upadirisho.
[149] Taz. Conc. Vat. II, Const.dogm. De Divina Revelatione, Dei verbum, n. 25: AAS 58 (1966), uk. 829.
[150] Kozi hii siyo ileile kozi ya kichungaji ya kuihitimu mara tu baada ya ordinasio, na inayoongelea katika dikrii Optatam totius, juu ya malezi ya waseminari, 28 oktoba 1965, n. 22.
[151] Taz. Conc. Vat. II, Decr. De pastorali Episcoporum munere in Ecclesia Christus Dominus, n. 16: AAS 58 (1966), uk. 681.
[152] Taz. Mt 10:10; 1Kor 9:7; 1Tim 5:18.
[153] Taz. 2Kor 8:14.
[154] Taz. Flp 4:14.
[155] Taz. Yn 3:16.
[156] Taz. 1Pet 2:5.
[157] Taz. Efe 2:22.
[158] Taz. Pontificale romanum, Madhehebu ya Upadirisho.
[159] Taz. Efe 3:9.
[160] Taz. Kol 3:3.