WARAKA ENSIKLIKA
PACEM IN TERRIS
(AMANI DUNIANI)
WA BABA MTAKATIFU
YOHANE XXIII
KWA MAPATRIARKA, MAPRIMATE, MAASKOFU WAKUU,
MAASKOFU, NA WAKUU WA MAHALI WENGINE WOTE
WALIO NA AMANI NA USHIRIKA NA KITI CHA KITUME;
KWA MAKLERI NA WAAMINI WA DUNIA YOTE,
NA KWA WATU WOTE WENYE MAPENZI MEMA:
KUHUSU KUIMARISHA AMANI KATI YA WATU WOTE
KATIKA UKWELI, HAKI,
UPENDO NA UHURU [1]
UTANGULIZI
Utaratibu wa ulimwengu
1. Amani duniani, ambayo watu wa nyakati zote waliitamani kwa hamu kubwa sana, haiwezi kujengwa wala kuimarishwa isipokuwa kwa kulinda kitakatifu utaratibu uliowekwa na Mungu.
Kwa njia ya maendeleo ya sayansi mbalimbali na vumbuzi za teknolojia mpya, tumefahamu zaidi kwamba utaratibu wa ajabu unafanya kazi katika viumbe na katika nguvu za asili, na kwamba mtu ana cheo maalum, kiasi cha kuweza kutambua utaratibu huo na kutengeneza nyenzo ili kutawala nguvu hizi na kuzigeuza ziwe kwa manufaa yake.
2. Lakini kabla ya yote maendeleo ya kisayansi na uvumbuzi wa kiteknolojia vinadhihirisha ukuu usio na mipaka wa Mungu, aliyeumba mtu na ulimwengu mzima. Naam, aliumba ulimwengu kutoka katika kutokuwepo, akaujaza hekima na wema wake. Kwa hiyo, Mzaburi mtakatifu humsifu Mungu kwa maneno haya, “Wewe, Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote” (Zab 8:1); na pia, “Ee, Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia” (Zab 104:24). Tena, Mungu aliumba mtu “kwa mfano na sura yake” (taz. Mwa 1:26), akampa utashi huru, akamweka bwana wa viumbe vyote. Kwa hiyo, Mzaburi hutamka hivi, “Umemfanya mdogo punde kuliko malaika; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako; umevitia vitu vyote chini ya miguu yake” (taz. Zab 8:5-6).
Utaratibu kati ya watu
3. Migogoro kati ya mtu na mtu na kati ya mataifa inakinzana na utaratibu mzuri sana huu wa ulimwengu; inaelekea kwamba sheria inayotegemeza mahusiano kati ya watu na kati ya mataifa ni sheria ya mwenye nguvu zaidi tu.
Lakini Muumba wa ulimwengu amechapisha mtimani mwa mtu utaratibu ambao dhamiri yake inamdhihirishia, na 1kumwagiza aufuate kwa bidii kubwa: “(Watu wa mataifa) waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia” (Rum 2:15). Na kwa kweli hayo mambo yasingeweza kuwa tofauti. Maana, vitu vyote alivyovifanya Mungu vinaakisi hekima yake isiyo na mipaka; nayo hekima inaakisiwa wazi zaidi kwa viumbe vile ambavyo kiwango chake cha utimilifu ni cha juu zaidi (taz. Zab 19:8-11).
4. Lakini pana dhana isiyo sahihi ambayo mara nyingi inasababisha matata. Maana, wengi wanafikiri kwamba mahusiano ya watu na serikali zao yatawaliwe na sheria zilezile zinazotawala nguvu za ulimwengu na viumbe visivyo na akili. Lakini si hivyo; maana, sheria zinazohusu wanadamu ni za aina tofauti, na lazima tuzitafute pale ambapo Baba wa viumbe vyote aliziandika, yaani ndani ya maumbile ya wanadamu.
Maana, ni sheria hizo zinazowafundisha wazi wanadamu jinsi inavyowapasa kutengeneza mahusiano ya wao kwa wao katika jamii, na jinsi yanavyotakiwa kuwa mahusiano ya raia na maofisa ya serikali za nchi zao, na pia mahusiano kati ya serikali mbalimbali; na hatimaye jinsi kila mtu na kila jumuiya ya kitaifa vinavyohusiana na jumuiya ile ya watu wa dunia nzima ambayo manufaa ya pamoja ya watu wote yanadai kwa nguvu itimizwe.
I
UTARATIBU KATI YA WANADAMU
Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu
5. Kabla ya yote hatuna budi kuzungumza juu ya utaratibu ambao lazima uwepo kati ya wanadamu. Kama tukitaka jumuiya yoyote ya kibinadamu iwe yenye utaratibu mzuri na wa kufaa, lazima iwekwe kama msingi wake kanuni hii: kila mtu ni binadamu, yaani, nafsi iliyo na akili na utashi huru; na kila mtu ana haki na wajibu ambavyo vyote vinatokana moja kwa moja na asili yake hiyo.Kwa hiyo haki na wajibu hivyo ni vya watu wote, visivyovunjika na visivyobatilika [2].
Na kama tukifikiria hadhi ya mtu kulingana na kweli zilizofunuliwa na Mungu, hatuna budi kuitathmini hata zaidi sana, kwa maana watu walikombolewa kwa damu ya Kristo Yesu, wakafanywa wana wa Mungu na rafiki zake kwa neema itokayo juu, wakawekwa kuwa warithi wa utukufu wa milele.
Haki
Haki ya kuishi na kuwa na maisha mazuri
6. Tukiongea juu ya haki za binadamu, tutambue kwamba kila mtu ana haki ya kuishi, ya uzima wa mwili, ya kuwa na vitu vinavyohitajika ili maisha yake yawe mazuri, hasa chakula, mavazi, nyumba, mapumziko, matibabu, huduma za jamii za lazima.Kutokana na hayo, kila mtu ana haki ya kusaidiwa kijamii anapopatwa na maradhi, ulemavu, ujane, uzee, kutokuwa na kazi, na kila anapopungukiwa na mahitaji ya lazima kwa maisha bila kosa lake lolote [3].
Haki zinazohusu tunu za kimaadili na kiutamaduni
7. Zaidi ya hayo, haki ya asili hudai kila mtu aheshimiwe, astahiwe, awe na uhuru wa kuchunguza ukweli, wa kutamka na kusambaza rai zake, wa kushughulikia sanaa yoyote ile, ingawa kwa sharti ya kwamba hayo yote yasipingane na utaratibu wa kimaadili na manufaa ya wote; na hudai pia mtu ataarifiwe kwa makini juu ya matukio yahusuyo umma.
Kutokana na haki ya asili, watu wote wana haki ya kushiriki ukuaji wa ustaarabu; na kwa hiyo ni lazima kila mtu aweze kupata elimu nzuri ya msingi, na mafunzo ya ufundi na ya elimu ya juu yanayolingana na kiwango cha maendeleo ya elimu cha nchi yake.Ni lazima kila bidii na juhudi zifanywe ili kila mtu aweze kufikia viwango vya juu vya elimu, kadiri iwezekanavyo kulingana na karama zake, na kuchukua dhima na majukumu katika jamii zinazolingana na karama hizo za maumbile na ujuzi alioupata [4].
Haki ya kumwabudu Mungu kulingana na maongozi ya dhamiri nyofu
8. Kati ya haki za binadamu hatuna budi kuhesabu pia haki ya kila mtu ya kumwabudu Mungu kadiri ya kanuni nyofu ya dhamiri yake, na kuungama dini yake kibinafsi na hadharani. Maana, kama anavyofundisha wazi Laktantio, “Tumezaliwa kwa ajili ya kumpa Mungu aliyetuumba heshima inayompasa, iliyo ya haki, na kumtambua na kumfuata yeye peke yake. Nasi tumefungamana na kushikamana na Mungu kwa njia ya kifungo hicho cha utauwa, ambacho hata jina la dini yenyewe linatokana nacho” [5]. Na pia mtangulizi wetu Papa Leone XIII alitamka mambo hayohayo kwa kusema, “Uhuru huu wa kweli, naam, uhuru huu ulio wa wana wa Mungu, ambao hulinda kwa kweli hadhi ya binadamu, una nguvu kuliko kila ukatili na ujeuri; na daima Kanisa ameutamani na kuupenda sana. Ndio uhuru wa aina hii ambao Mitume waliudai sikuzote, Watetezi wa dini walitamka kwa maandishi yao, Mashahidi wengi sana waliutukuza kwa damu yao” [6].
Haki ya mtu kuchagua hali ya kuishi anayoipenda zaidi
9. Watu wana pia haki ya kuchagua hali ya kuishi wanayoipenda zaidi; kwa hiyo wana haki ya kujenga familia yao, ambamo mume na mke wana usawa wa haki na wajibu, au ya kufuata wito wa upadre au wa utawa [7].
Familia, inayojengwa juu ya msingi wa ndoa iliyofungika kwa uhuru, iliyo moja na isiyovunjika, lazima ihesabiwe kuwa chembe ya kwanza na ya asili ya jamii ya binadamu. Kwa hiyo inabidi familia izingatiwe sana kiuchumi na kijamii, na pia katika uwanja wa utamaduni na maadili, ili familia iimarishwe na kusaidiwa kutimiza jukumu lake.
Haki ya kuwatunza na kuwalea watoto kwanza kabisa ni juu ya wazazi wao [8].
Haki zinazohusu uchumi
10. Kama tukifikiria uwanja wa uchumi, ni dhahiri kwamba kadiri ya haki ya asili mtu ana haki ya kuwa na kazi, na pia ya kuweza kutumia kwa uhuru uwezo wake binafsi katika kazi [9].
Haki hizo lazima ziungane na haki ya kufanya kazi katika hali na mazingira visivyoathiri uzima wa mwili au maadili ya mtu, wala visivyodhuru mchakato wa kukua kwa vijana hadi wafikie ukomavu wa utu. Na kuhusu wanawake, lazima waweze kufanya kazi kwa namna inayopatana na haja na wajibu vinavyotokana na hali yao ya wake na mama [10].
Kutokana na hadhi yake, mtu ana pia haki ya kujishughulisha na utendaji wa uchumi kulingana na kiwango chake cha uwajibikaji [11]. Inabidi kusisitiza haki ya mfanyakazi ya kupata ujira unaolingana na vigezo vya haki, ambao kwao, kadiri iwezekanavyo kutokana na uwezo wa kifedha wa nchi, mfanyakazi pamoja na familia yake aweze kuwa na kiwango cha maisha unaopatana na hadhi ya kibinadamu. Mtangulizi wetu Pius XII alisema kuhusu hayo, “Wajibu wa mtu wa kufanya kazi, ulio wa asili, unaendana na haki, ambayo vilevile ni ya asili, ya kudai kupata mahitaji kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya familia yake kwa njia ya hiyo kazi anayofanya. Nalo ndilo kadiri ya amri kuu ya asili ya kwamba mtu ahifadhiwe” [12]. Kutokana na asili ya mtu, yeye ana haki ya kuwa na mali binafsi, ikiwa na pamoja na vyombo vya uzalishaji. Kama tulivyosema katika waraka mwingine, “(Hiyo) ni haki inayotegemeza sana hadhi ya mtu, na kusaidia sana kutenda kwa uwajibikaji katika nyanja zote, pamoja na kuchangia uthabiti na utulivu wa maisha ya kifamilia na ukuaji wa utajiri na amani katika nchi” [13].
Hatimaye, inafaa kusisitiza kwamba haki ya kumiliki mali binafsi lazima iwe na dhima ya kijamii [14].
Haki ya kukusanyika na kuunda vyama
11. Wanadamu wana tabia ya kijamii, ndiyo sababu wana haki ya kukusanyika pamoja na kuunda vyama. Wana pia haki ya kuvipa vyama hivyo mifumo inayofikiriwa kufaa zaidi kutimiza malengo yake, na ya kutenda ndani ya vyama hivyo kwa uhuru na kadiri ya uwajibikaji wao ili kuyafikia malengo hayo [15].
Kama tulivyotia mkazo katika Ensiklika yetu Mater et Magistra (Mama na Mwalimu), inafaa sana kuasisi shirika na vyama vya kiwango cha kati kwa ajili ya kutimiza malengo ambayo mtu binafsi hawezi peke yake kuyafikia. Shirika na vyama hivyo ni vyombo muhimu sana ili kulinda hadhi na uhuru wa binadamu, pamoja na kutozuia uwajibikaji wa kila mtu [16].
Haki ya kuhama na kuhamia mahali
12. Kila mtu ana haki ya kusafiri na ya kukaa mahali popote palipo ndani ya mipaka ya taifa lake. Kama pana sababu halali, inabidi mtu aruhusiwe kuhamia nchi nyingine na kukaa huko [17]. Kuwa raia wa taifa fulani, kamwe hakunyimi ukweli wa kuwa mwanafamilia wa familia ya binadamu na raia wa jamii ya kiulimwengu na wa umoja wa watu wote.
Haki zinazohusu siasa
13. Hufungamana na hadhi ya mtu pia haki ya kushika nafasi hai katika maisha ya umma na kuchangia kadiri ya uwezo wa kila mmoja kwa ajili ya kutekeleza manufaa ya watu wote. Maana, kama alivyosema mtangulizi wetu Papa Pius XII, “Binadamu, mbali na kuwa mlengwa na mhusika wa kutendewa tu katika maisha ya kijamii, kinyume chake ni mtendaji, msingi na madhumuni yake, na ndivyo lazima atambuliwe na kuheshimiwa” [18].
Ni haki ya msingi ya mtu pia ulinzi wa kisheria wa haki zake: ulinzi wenye kufaa, usio na mapendeleo, unaoongozwa na vigezo vilivyo haki kabisa.
Kwa kunukulu tena Papa Pius XII: “Kutokana na utaratibu wa kisheria, ulioagizwa na Mungu, mtu anayo haki isiyobatilika ya kuwa na usalama kisheria, na kwa hiyo kuwa na ujumla wa haki unaolindwa dhidi ya kila tendo la wengine linalojaribu kuuharibu” [19].
Wajibu
Uhusiano usiovunjika baina ya haki na wajibu wa kila mtu
14. Haki asilia tunazozizungumzia haiwezekani kuzitenganisha na zinahusisha wajibu utakaotumika pamoja na mtu huyohuyo. Haki hizo na wajibu hupata asili yao, nguvu zao na kutokuharibika kwao kutoka sheria ya maumbile (natural law), ambayo huhakikisha haki na kuamuru wajibu.
Hivyo, kwa mfano, haki ya mtu kuishi inahusisha wajibu wa kulinda maisha yake; haki ya kuwa na maisha mazuri inahusisha wajibu wa kuishi kwa kujiheshimu; haki ya kuwa huru katika kutafuta ukweli, inaendana na wajibu wa kufanya juhudi katika kutafuta kwa upana na kina huo ukweli.
Kuwiana haki na wajibu kati ya watu mbalimbali
15. Hayo yakiisha kukubalika, kinachofuata ni kwamba katika jamii ya kibinadamu haki moja ya asili ya mtu mmoja inasababisha wajibu unaoendana nayo kwa watu wengine; yaani, wajibu wa kuitambua na kuiheshimu haki hiyo. Kila haki ya msingi ya binadamu inapata nguvu zake kimaadili katika sheria ya kimaumbile inayoiweka, tena inaamuru wajibu unaoendana nayo. Hivyo, wale wanaodai haki zao, na halafu husahau au hawajali kupokea wajibu zinazotokea, ni watu wanaojenga kwa mkono mmoja na kwa mkono mwingine wanabomoa.
Katika kushirikiana
16. Kwa vile wanadamu ni viumbe jamii kwa maumbile, ni lazima waishi pamoja na kushauriana kwa kila jambo kwa pamoja. Kwamba watu lazima watambue haki zao na kutekeleza wajibu wao ndilo jambo la muhimu sana kwa jamii iliyo na sheria inayofaa. Lakini, matokeo yake ni kuwa kila mtu atachangia kwa moyo wake wote katika kuendeleza sheria kwa raia ambapo haki na wajibu ndio hutazamwa kwa ufasaha zaidi na kwa umakini zaidi.
Kwa mfano, haisaidii kitu kukubali tu kwamba mtu ana haki ya kupata mahitaji muhimu katika maisha, kama sisi nasi hatufanyi juhudi, kila mmoja kadiri ya nguvu alizo nazo, ili kila mtu awe na mahitaji ya kutosha kwa maisha yake.
Hivyo, jamii sio lazima tu iwe na sheria zinazofaa, lakini lazima pia iwape watu rasilimali za kutosha. Na hilo linadai utambuzi na utekelezaji wa haki na wajibu kwa pamoja, bali pia kuhusisha na kushirikisha watu wote katika kufanikisha miradi mbalimbali ambayo kwa ustaarabu wetu uliopo inawezekana ikasaidia zaidi kuongeza mahitaji.
Kwa moyo wa uwajibikaji
17. Utu wa mtu unahitaji kwamba katika utendaji wake aweze kufurahia na kufuata mawazo yake na uhiari wake. Hivyo, kwa kushirikiana na wenzake, kuna kila sababu ya kwa nini haki zake zitambulikane, atekeleze majukumu yake kadiri ya sheria na kuwa na ushirikiano wa kutosha na watu wengine ni kitu cha msingi sana katika maamuzi yake binafsi. Kila mtu lazima atende kadiri ya matakwa yake, kushuhudia na kujitambua kuwa ni mwenye majukumu, sio kwa kulazimishwa kutoka nje au kwa kushawishiwa kwa kupewa zawadi.
Hakuna ubinadamu katika jamii ambayo imeunganishwa pamoja kwa kulazimishwa. Maana hali hiyo, mbali na kuhamasisha, kama ilivyo ada, maendeleo na ukamilifu wa mtu, inakuwa kikwazo kwa uhuru wake.
Watu kuishi jamii katika ukweli, haki, upendo na uhuru
18. Jamii ya watu haiwezi kuhesabiwa yenye utaratibu mzuri, mafanikio na yenye kuufaa utu wa binadamu, isipokuwa imejengwa katika kweli. Mt. Paulo alionya hivi kuhusu jambo hilo: “Basi, uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake” (Efe 4:25). Na ndivyo itakavyokuwa kama kila mtu atakuwa na ujuzi wa kutambua haki zake na wajibu wake kwa wenzake. Jamii za watu, kama tuonavyo taswira yake, inahitaji kwamba watu waongozwe kwa usawa kuheshimu haki za wengine na kutekeleza wajibu wao. Pia inahitaji kwamba wazingatie ule upendo ambao utawafanya wajisikie kuwapenda wengine kama wanavyojipenda wenyewe, na kuwachochea kushiriki mema yao na wengine na kujishughulisha katika dunia ili kuwafanya watu wote wawe warithi sawa wa thamani bora za kiakili na kiroho. Wala hilo halitoshi; kwani jamii ya watu huendelezwa katika uhuru, kama vile katika kutumia namna ambayo inaendana na utu wa washirika wake, ambao wametunukiwa akili, kusudi waweze kuwajibika kwa matendo yao.
19. Na hivyo, ndugu waheshimiwa na wana wapendwa, jamii ya binadamu sharti kimsingi itambulike kuwa ni ya kiroho. Kwa njia yake na katika mwanga wa ukweli, watu hawana budi kushirikishana ujuzi wao, waweze kutekeleza haki zao na kutimiza wajibu zao, watiwe moyo kujitafutia tunu za kiroho, kwa pamoja wasaidiane kuchota furaha halisi kutoka mema ya ulimwengu. Daima wawe tayari kuwapa wengine yaliyo mazuri sana yatokanayo na urithi wa utamaduni wao. Kwa juhudi wajitahidi kupokea na kuishi mafanikio ya kiroho ya wengine. Tunu hizi hazivutii tu, bali zinatoa pia malengo na shabaha ya kila kilicho na mwelekeo wa dhana za kitamaduni, taasisi na kijamii, miundo na vyama vya kisiasa, sheria na miundo mingine ambayo kwayo jamii inaundwa kwa nje na kuendelezwa daima.
Utaratibu wa kimaadili wenye kama msingi halisi Mungu wa kweli
20. Sasa basi, utaratibu uliopo katika jamii ya watu kwa jumla si wa kiwiliwili, ila wa kimaadili. Misingi yake ni ukweli; na unatekelezwa katika haki; unahitaji kuzingatiwa na kukamilishwa na upendo; unadai utengenezwe upya daima katika jamii ambamo sifa ya ubinadamu inaongezeka zaidi na zaidi.
Lakini utaratibu wa namna hii – unaohusisha watu wote, kikamilifu na kwa ujumla, usiobadilika kamwe katika misingi yake – unapata chanzo chake katika Mungu, aliye nafsi na anayepita upeo wa binadamu. Yeye ndiye kweli ya kwanza na wema mkuu; na chanzo kikuu hicho ndicho ambacho jamii ya watu, lazima ikizingatie, ikiwa inataka kuwa hai kweli, imetengemaa, yenye usitawi na inayotambua utu wa watu [20]. Hivi ndivyo Mt. Tomaso humaanisha anaposema, “Akili za binadamu ni kiwango ambacho kinapima ubora wa mastahili ya matakwa ya wanadamu, na kwa hilo inatokana na sheria ya milele ambayo ni akili zenyewe za kimungu. ... Hivyo ni wazi kwamba ubora wa matakwa ya binadamu unategemea zaidi sana sheria ya milele kuliko akili za binadamu” [21].
Ishara za nyakati
21. Kuna vitu vitatu ambavyo vinasanifu nyakati zetu za sasa. Awali ya yote tunagundua mafanikio endelevu katika hali za kiuchumi na kijamii za wafanyakazi. Walianza kwa kudai haki zao za msingi hasa katika taratibu za kiuchumi na kijamii, kisha waliendelea na madai yao ya haki katika siasa pia. Mwishowe waligeuzia umakini wao katika kupata manufaa ya kielimu kwa jamii zao. Hivyo, leo wafanyakazi, popote ulimwenguni hupaza sauti zao na kudai wasinyanyaswe na kutendewa chini ya matakwa ya wengine, kana kwamba hawana akili wala uhuru. Bali, wao wanasisitiza wathaminiwe kama wanadamu wenye uwezo wa kushirikiana katika nyanja zote za jamii ya watu: katika duru ya kiuchumi na kijamii, katika serikali, na katika maeneo ya kiutamaduni na kielimu.
22. Pili, nafasi ambazo wanawake sasa wanazo katika maisha ya kisiasa ni dhahiri kwa watu wote. Pengine haya ni maendeleo ambayo yanatokea na kukua kwa haraka miongoni mwa mataifa ya Kikristo. Lakini pia yanaenea, ingawa kwa polepole, miongoni mwa mataifa ambayo ni warithi wa mapokeo mengine na yalijazwa na tamaduni tofauti. Wanawake wanazidi kutambua hadhi yao ya asili. Mbali na kuridhika na hali waliyo nayo, na kukubali kuhesabiwa na kutumiwa kama chombo fulani, wanadai kuhesabiwa kama binadamu, wenye haki na wajibu unaowahusu katika maisha ya nyumbani na vilevile katika maisha ya umma.
23. Mwishowe, katika nyakati hizi za sasa, tunakabiliana na jamii ambayo mfumo wake unabadilika na kukua upya siku kwa siku kwa upande wa kijamii na kisiasa pia. Kwa vile watu wote ama wameshajipatia uhuru wa kisiasa, au wako mbioni kuupata, punde si punde hakutakuwa tena na taifa litakalotawala juu ya taifa jingine, wala hakutakuwa na mtu atakayeathiriwa na nguvu za kigeni.
24. Hivyo, katika dunia nzima watu ama ni watu wa taifa huru au baada ya muda si mrefu watakuwa hivyo; wala hakuna taifa siku hizi linalokubali kutawaliwa na mamlaka ya kigeni. Kuwepo kwa muda mrefu kwa tabia ya unyonge ya matabaka fulani, sababu ya hali zao kijamii na kiuchumi, jinsia, au nafasi zao katika taifa ikilinganishwa na tabia ya kujikweza ya matabaka mengine ya wenye nacho, kwa haraka inakuwa kama kitu kilichopitwa na nyakati.
Kinyume chake, leo inaonekana kuwa limeenea sana wazo la kwamba watu wote ni sawa katika utu. Na hivyo, katika mafundisho ya maadili, walau katika kiwango cha nadharia, hakuna nafasi tena kwa kukubali ukandamizaji wa watu kutokana na rangi zao. Yote haya yana umuhimu mkubwa katika kuanzisha jamii ya watu yenye kuzitilia mkazo kanuni za msingi tulizoorodhesha hapo juu. Kwani, mtu kufahamu haki zake lazima hakutamzuia kutambua pia wajibu wake. Kuwa na haki kunahusisha wajibu wa kuzitekeleza haki hizo, kwa vile ndio muonekano wa utu wa binadamu. Na kuwa na haki vilevile kunahusisha kutambua na kuheshimu haki za watu wengine.
25. Iwapo jamii inaundwa katika misingi ya haki na wajibu, watu wanaelewa haraka thamani za kiroho na za kiakili, wala sio wagumu katika kuelewa ni nini maana ya ukweli, haki, upendo, na uhuru. Na zaidi wanakuwa na ufahamu wa kuwa wanachama wa jamii hiyo. Wala si hilo tu. Kwa misingi kama hiyo, hufanikiwa sana kuwa na ufahamu juu ya Mungu wa kweli – Mungu aliye nafsi ambaye ndiye mkuu kuliko maumbile ya binadamu. Hutambua kuwa uhusiano wao na Mungu unaunda msingi wa kweli wa maisha yao – maisha ya ndani ya kiroho, na maisha ambayo wanaishi katika jamii na wenzao.
II
MAHUSIANO BAINA YA WATU
NA MAMLAKA YA UMMA NDANI YA JAMII MBALIMBALI ZA KISIASA
Umuhimu wa kuwepo na mamlaka na asili yake ya kimungu
26. Jamii ya binadamu haiwezi kuwa na utaratibu na usitawi bila kuwapo watu wenye mamlaka halali, wanaohakikisha taasisi zinalindwa na kujitoa, kadiri inavyowezekana, kufanya kazi na kushughulikia maslahi ya watu wake wote.
Mamlaka hiyo, kama anavyofundisha Mt. Paulo, inatoka kwa Mungu: “Hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu”(Rum 13:1-6). Sehemu hii ya waraka wa Mtume inafasiriwa na Mt. Yohane Krisostomi kama ifuatavyo: “Unasemaje? Labda kila mtawala amewekwa na Mungu? Hapana, sisemi hilo: hapa haina maana ya mtawala mmoja mmoja, bali utawala wenyewe. Sasa, ukweli kwamba kuna mamlaka na kwamba awepo anayetoa amri na anayetii si suala la bahati nasibu, bali ni kutokana na hekima ya kimungu” [22]. Mungu, kwa kweli, amewaumba wanadamu wajumuikaji kwa asili; na kwa sababu hapawezi kuwa na “jamii inayojisimamia kama hakuna anayewatangulia wengine, akimwongoza kila mmoja kwa tija na kwa umoja wa nyenzo kuelekea hatma moja, unafuata ukweli kwamba katika maisha ya pamoja mamlaka inayotawala ni ya lazima; ambayo si vinginevyo na jamii, ni kwa asili, na hivi basi inatoka kwa Mungu” [23].
27. Mamlaka si nguvu isiyo na mipaka: badala yake ni uwezo wa kuamrisha kwa fikra sahihi. Matokeo yake, kwa hiyo, ni kwamba anayetoa amri anafanya hivyo akiongozwa na utaratibu wa kimaadili, ambao una msingi wake katika Mungu, ambaye ndiye chimbuko na hatma yake. Kuhusu hilo, mtangulizi wetu Pius XII ndivyo anavyoonya: “Utaratibu wenyewe usiolinganika wa viumbe na wa hatma unaoonyesha mtu kama nafsi inayojitegemea, yaani mwenye wajibu na haki zisizovunjika, mzizi na hatma ya maisha yake ya kijamii, unalikumbatia pia Dola kama jumuiya ya lazima iliyovikwa mamlaka, ambayo bila ya hayo taifa hilo halingalidumu na wala lisingaliishi. ... Na kwa sababu utaratibu ule usiolinganika, katika mwanga wa fikra sahihi, na juu ya yote mwanga wa imani ya Kikristo, hauwezi kuwa na asili nyingine ila katika Mungu aliye na nafsi, muumba wetu, hivi basi hadhi ya mamlaka ya kisiasa ni hadhi ya ushiriki wa mamlaka ya Mungu” [24].
28. Mamlaka inayojikita kwenye vitisho tu, au kimsingi kwavyo, au katika woga wa adhabu, au katika ahadi za kuvutia za zawadi, haiwezi kuwasukuma binadamu kwa tija kufikia manufaa ya wote; na kama hata ingalitokea hivyo, hilo lisingalilingana na hadhi ya watu, yaani ya viumbe huru wenye akili. Mamlaka ni hasa nguvu ya kimaadili; ni lazima kwa hiyo kwa nafasi ya kwanza, iiguse dhamiri, yaani kwenye wajibu ambao kila mmoja anao wa kuchangia kwenye manufaa ya wote. Lakini kwa kuwa binadamu wote ni sawa kwa hadhi ya asili, hakuna anayeweza kumlazimisha mwingine toka ndani. Mungu pekee anaweza, kwa sababu yeye peke yake ndiye anayeona na kuhukumu tabia za siri katika roho ya mtu.
29. Mamlaka ya kibinadamu inaweza kumlazimisha mtu kimaadili tu kama hiyo imeungana kiundani na mamlaka ya Mungu, na ni ushiriki wa hiyo [25].
Kwa mtindo huo hata hadhi ya raia inalindwa, kwani utii wao kwa mamlaka si swala la mtu kuwa chini ya mtu mwingine, bali katika maana yake halisi ni tendo la uchaji kwa Mungu muumba na mjaliaji, ambaye ameamuru mahusiano ya maisha ya pamoja yaratibiwe na mpango uliowekwa na yeye mwenyewe; kumcha Mungu, si kujidhalilisha, bali ni kujiinua na kuwa na hadhi ya kiutawala, kwani kumtumikia Mungu ni kutawala [26].
30. Mamlaka, kama ilivyosemwa, inatakiwa na utaratibu wa kimaadili na asili yake ni Mungu mwenyewe. Kila inapotokea mamlaka kuwa na sheria au amri zinazopingana na matakwa ya Mungu, zinakuwa hazina nguvu ya kulazimisha dhamiri, kwa sababu “ni lazima kumtii Mungu kuliko wanadamu” (Mdo 5:29). Katika hali hiyo mamlaka inapoteza hadhi yake na inageuka kuwa ukandamizaji. “Sheria ya kibinadamu inakuwa sheria tu pale inapoendana na utashi sahihi na inatokana na sheria ya milele (ya Mungu). Kumbe sheria hiyo ikiwa inakinzana na utashi, inakuwa ni sheria chafu; kwa hali hiyo haiwi tena sheria na badala yake linakuwa tendo la ukatili” [27].
31. Hata hivyo ukweli kwamba mamlaka hutoka kwa Mungu haimaanishi kuwa wanadamu hawana uwezo wa kuwachagua wale ambao wataongoza dola, au kuamua ni aina gani ya serikali wanayoitaka, na kubainisha utaratibu na mipaka ya watawala wanapotekeleza mamlaka yao. Kwa hiyo fundisho la hapo juu linapatana na serikali yoyote inayofuata kweli mfumo wa kidemokrasia [28].
Utekelezaji wa manufaa ya wote: sababu ya kuwepo mamlaka za umma
32. Wanadamu wote, kama binafsi na kama vikundi vya kati, wanatakiwa kutoa michango yao maalumu katika ustawi wa wote pamoja. Na pato kuu la hili ni kuwa wanatakiwa wapatanishe maslahi yao binafsi na mahitaji ya wengine, na kutoa mali na huduma zao kama watawala watakavyoagiza; hata hivyo, haki idumishwe na watawala watende ndani ya mipaka ya uwezo wao. Yaani, wale walio na mamlaka katika nchi, na wawe na matendo yasiyo na mawaa na ambayo kimaadili ni mazuri au, walau yanalenga kwenye manufaa ya nchi.
Lakini upatikanaji wa manufaa ya wote ni sababu pekee ya kuwepo kwa utawala wa kiraia. Katika kushughulikia manufaa ya wote, kwa hiyo, watawala lazima waheshimu asili yake, na wakati huohuo waweke sawa sheria zao wanazotunga ili kufikia mahitaji ya mazingira na wakati husika [29].
Mambo ya msingi ya manufaa ya wote
33. Miongoni mwa yanayounda manufaa ya wote, ni lazima kwa hakika kuzifikiria tabia za makundi ya watu zinazowatofautisha na makundi mengine ya watu [30]. Lakini tunu na tabia hizo si kila kitu katika kutimiza manufaa ya wote. Kwa vile manufaa ya wote yanafungamana kwa undani na maumbile ya kibinadamu, hayawezi kuwepo yote kabisa endapo mwanadamu hatafikiriwa wakati wote. Kwa hiyo, umakini uwe hasa katika asili ya manufaa ya wote na kile ambacho kinaleta uwepo wake [31].
34. Kwa hiyo, lazima tuongeze pia kuwa ni katika asili ya manufaa ya wote ndipo kila raia anayo haki ya kuchangia katika jumuiya ya kisiasa, ingawa kwa namna tofauti, kulingana na majukumu yake, mastahili yake na mazingira. Kwa hiyo kila mamlaka ya umma lazima ijitahidi kukuza manufaa ya wote kwa ajili ya maslahi ya wote, pasipo kumpendelea mwananchi yeyote binafsi au kundi la wananchi. Kama Papa Leo XIII alivyosisitiza: “ Mamlaka ya umma isiwe nyenyekevu kwa faida ya mtu yeyote binafsi, au kwa watu wachache, kwa vile ilianzishwa kwa ajili ya manufaa ya wote.” [32]. Hata hivyo, uzingatiaji wa haki na usawa wakati mwingine unawadai wale walio madarakani kuwajali zaidi walio wanyonge katika jamii, kwani hawa wana hali ngumu, hasa inapofika wakati wa kulinda haki zao na kutetea maslahi yao halali [33].
35. Lakini hapo, tunapenda kuwaonya wana Wetu kuwa manufaa ya wote ni suala ambalo linagusa mahitaji ya mtu mzima, kimwili na kiroho. Kwa hiyo mamlaka za umma ni lazima zijishughulishe kukidhi mahitaji hayo kwa mtindo na kwa kiwango ambavyo vinalandana; ila kwamba lakini vikue kwa pamoja, katika kuitambua hierarkia ya tunu, ustawi katika mali na katika mahitaji ya kiroho [34].
Kanuni hizi zinapatikana kwa uwazi katika ule ukurasa wa ensiklika yetu Mater et Magistra ambapo tumesisitiza kuwa manufaa ya wote “lazima yazingatie hali zile za kijamii ambazo zinaruhusu maendeleo ya kweli ya nafsi ya mwanadamu” [35].
Lakini akiwa na mwili na roho isiyokufa, mtu hawezi katika maisha haya yenye kufa kukidhi mahitaji yake na kupata furaha kamili. Kwa hiyo, hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza manufaa ya wote zisihatarishe uzima wake wa milele, bali zimsaidie pia kuupata huo [36].
Shughuli za mamlaka za umma na haki na wajibu wa mtu
36. Kiujumla inakubalika leo kuwa manufaa ya wote yanalindwa vizuri pale haki za watu na wajibu zinapopata dhamana. Kazi kubwa ya watawala ni kuhakikisha kuwa hizi haki zinatambuliwa, kuheshimiwa, kuratibiwa, kulindwa na kukuzwa, na kila mtu anawezeshwa kutimiza wajibu wake kirahisi zaidi. Kwa kuwa “kulinda haki zisizokiukwa za mwanadamu, na kurahisisha utendaji wa wajibu zake, ni wajibu msingi wa kila kiongozi wa umma.” [37].
Kwa hiyo, serikali yoyote ambayo imekataa kuzitambua haki za binadamu au imezikiuka, haiwezi tu kushindwa kutimiza wajibu wake, bali maagizo yake yatakosa kabisa nguvu ya kisheria [38].
Mfumo mwanana na wenye tija wa kulinda haki na wajibu wa binadamu
37. Kwa hiyo shughuli ya msingi ya mamlaka za umma ni kuweka nidhamu na kutengeneza mahusiano kati ya binadamu kiasi kwamba haki za kundi moja haziwezi kuwa kikwazo kwa wengine au tishio kwa hao wengine kuzitumia haki zao; na mamlaka hizo ziwasindikize watu kutekeleza wajibu zao; na tena ni wajibu wao kulinda kwa tija au kurudisha utekelezaji wa haki hizo [39].
Wajibu wa kuhamasisha haki za binadamu
38. Kwa kuongeza, wakuu wa dola lazima watoe mchango chanya katika kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mtu kulinda haki zake na kutimiza wajibu wake, na aweze kufanya hivyo kwa urahisi. Kama kuna kitu tumejifunza katika shule ya mang’amuzi, kwa hakika ni hiki: katika dunia ya sasa hasa, siasa, uchumi na utamaduni wa upendeleo kati ya wananchi unazidi kuenea zaidi na zaidi hasa pale viongozi wa umma wanaposhindwa kuchukua hatua madhubuti katika maeneo haya. Na pato lake ni kuwa haki za binadamu na wajibu hukosa ufanisi.
39. Uongozi wa umma kwa hiyo lazima ulipatie uangalifu na umakini suala la maendeleo ya kijamii na kiuchumi, na la maendeleo ya huduma muhimu kulingana na ongezeko la mfumo wa uzalishaji. Huduma hizo ni pamoja na utengenezaji wa barabara, usafirishaji, mawasiliano, maji safi ya kunywa, nyumba, huduma za afya, mazingira mazuri ya kurahisisha shughuli za kidini, na vifaa vya maburudisho. Na ni lazima wahakikishe kuwa wanaweka mifumo yenye uhakika ili kwamba kunapokuwa na matukio mabaya au matukio yanayodai uwajibikaji mkubwa zaidi wa familia, kila mtu asikose mahitaji muhimu kwa kuishi maisha ya hadhi. Serikali inatakiwa pia isionyeshe nguvu na ufanisi mchache katika kutoa nafasi za ajira nzuri, zilizopangwa kulingana na uwezo wa wafanyakazi. Ni lazima ihakikishe kuwa wafanyakazi walipwa mshahara wa haki na unaojitosheleza, na waruhusiwe kuwa na hali fulani ya uwajibikaji katika masuala ya viwanda wanamofanyia kazi. Lazima ifanikishe uundwaji wa vikundi vya kati, kusudi maisha ya kijamii ya watu yawe bora zaidi na kidogo yasiwabane. Mwisho, ni lazima ihakikishe kuwa kila mmoja anazo dhana na nafasi ya kushiriki kadiri iwezekanavyo katika faida za kitamaduni.
Mlingano kati ya aina mbili za utendaji wa mamlaka za umma
40. Manufaa ya wote yanahitaji mamlaka za umma, kuhusiana na haki za binadamu, zifanye mambo mawili: kwanza ni kuunda na kulinda, na pili kuhamasisha. Katika suala hili lakini ni lazima kuwe na umakini mkubwa ili matendo hayo mawili yaratibiwe kwa hekima. Ni lazima kuzuia kwamba isitokee kuwa zinapolindwa haki za baadhi ya watu au vikundi fulani vya kijamii, zinatengenezwa nafasi za upendeleo; pia ni lazima kuzuia ili isitokee kwamba katika kuhamasisha haki za binadamu zinavunjwa haki nyingine za binadamu huyo huyo. “Ni lazima daima ithibitishwe kanuni kwamba uwepo wa serikali katika uchumi usipunguze juhudi binafsi za wananchi, bali kuwahakikishia uwanja mpana zaidi, katika kuweka ulinzi kwa wote na kwa kila mwananchi” [40].
Na hivi hata mamlaka za umma ni lazima ziwe na mwelekeo huo katika kutekeleza shughuli zao mbalimbali zinazolenga kukuza utekelezaji wa haki za binadamu na kupunguza makali ya utekelezaji wa wajibu kwa wote katika maisha ya kijamii.
Muundo na utendaji wa mamlaka za umma
41. Haiwezekani kusema mara moja na kwa milele, ni upi muundo bora zaidi ambao mamlaka za umma inabidi zifuate, na pia mtindo sahihi zaidi wa kuzingatia katika kutekeleza majukumu yake maalum, yaani jukumu la kutunga sheria, la kiutawala na la kimahakama.
Ni wazi kwamba muundo na utendaji wa mamlaka za umma haviwezi kukosa kufungamana na hali za kihistoria za jumuiya za kisiasa: hali zinazobadilika kadiri ya eneo na muda. Lakini tunafikiri kwamba muundo na mipango ya kisheria na kisiasa ya jumuiya ni lazima itoe majibu kwa mahitaji ya watu kwa kuzingatia mgawanyo wa mamlaka unaolandana na majukumu matatu ya mamlaka ya umma. Katika uongozi umahiri na utendaji wa mamlaka za umma vinatafsiriwa kisheria; na uhusiano kati ya raia na watumishi unaratibiwa pia kisheria. Hali hii inawawekea mazingira mazuri raia katika kuziishi haki zao na kutimiza wajibu zao.
42. Lakini, ili muundo huo wa kisheria na kisiasa wa jamii uliogusiwa hapo juu uwe na faida kwa watu ni lazima mamlaka za umma ziwe makini katika kutatua matatizo ya watu katika mazingira yale zinamofanya kazi; na ni lazima kila mmoja atekeleze wajibu zake bila uzembe. Hii inamaanisha kuwa mamlaka inayohusika na utungaji wa sheria inafuata kimaadili mwongozo wa katiba na inatafsiri vilivyo mahitaji ya manufaa ya wote katika mabadiliko yasiyokoma. Pia kwamba mamlaka ya utendaji inazitumia sheria kwa busara ikizitambua kiundani katika uchambuzi yakinifu wa kila jambo halisi; na kwamba mamlaka ya kimahakama inasimamia haki bila upendeleo, bila kuuvutikia upande fulani wenye ushawishi mkubwa zaidi. Na inamaanisha kuwa kila raia na mawakala, katika kutekeleza wajibu zao wanapewa ulinzi wa kisheria wenye tija katika mahusiano yaliyopo kati yao na kati ya raia na watumishi [41].
Mpango wa kisheria na dhamiri ya kimaadili
43. Hakuna shaka kwamba mfumo wa kisheria wa Dola unaoendana na kanuni za kimaadili na haki, na unaowiana na kiwango cha makuzi ya jumuiya ya kisiasa ya nchi ile, umejenga misingi kwa ajili ya utekelezaji wa manufaa ya wote.
Lakini maisha ya kijamii katika nyakati zetu hizi yanatofautiana, yana matata na ni ya kimwendo kasi, kiasi kwamba hata taratibu za kisheria, hata kama zimetungwa kwa umahiri mkubwa na kwa kutazama mbali, bado hazikidhi mahitaji.
Zaidi ya hayo mahusiano kati ya raia, kati ya raia na mawakala kwa upande mmoja na mamlaka za umma kwa upande mwingine, na vivyo hivyo kati ya mamlaka za umma zenyewe ndani ya Taifa lilelile, mara nyingi huonekana kuwa tata hivi kiasi cha kutoeleweka kama yataweza kweli kuratibiwa na mifumo ya sheria iliyo imara. Hivi watu wenye mamlaka ili wakati huohuo wawe watii kwa mifumo ya kisheria iliyopo, wakizingatia vitu mbalimbali vilivyomo na mielekeo yake, wakiwa tayari kuziona hali mbalimbali zitokanazo na maisha ya kijamii; pia wakilinganisha mfumo wa kisheria na maendeleo ya kimazingira na kutatua kwa mtindo ulio bora zaidi matatizo mapya, ni lazima wawe na fikra zilizo sahihi juu ya asili na upana wa wajibu wao; na ni lazima wawe watu watulivu na wenye maadili, wenye kutazama mbali, ili waweze kutafsiri kwa haraka na bila kuyumba mambo katika uhalisia wake, na wawe na utashi thabiti ili waweze kutenda kwa haraka na kwa tija [42].
Ushiriki wa raia katika maisha ya kijamii
44. Ni hitaji la hadhi ya ubinadamu wao kwamba washiriki katika maisha ya kijamii, hata kama ushiriki wao unategemea sana kiwango cha makuzi kilichofikiwa na jumuiya ya kisiasa ambayo wao ni sehemu yake.
Kupitia ushiriki katika maisha ya kijamii watu wanafunguliwa milango zaidi kuelekea kwenye manufaa makubwa zaidi. Na kutokana na hali ilivyo siku hizi, wale wanaosimamia jamii, kwa vile huweza kukutana na kujadiliana mara kwa mara na raia wao, wanapata nafasi ya kufahamu kwa undani zaidi ni nini kilicho muhimu kwa ajili ya manufaa ya wote; na katika mfumo kama huo unaoruhusu, baada ya kipindi maalum, kuwepo na mabadilishano ya watu katika nyadhifa za kiuongozi, mamlaka ya maofisa hao, mbali na kudhoofika na kuzeeka, inapata nguvu mpya kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii ya binadamu [43].
Ishara za nyakati
45. Katika mfumo wa kisheria wa jumuiya ya kisiasa katika nyakati hizi za kisasa, kuna kwanza kabisa tamko la haki za msingi za binadamu: tamko ambalo si mara chache, linaingizwa kwenye katiba za nchi au linakuwa ni sehemu ya katiba yenyewe.
Halafu, kuna mwelekeo wa kuweka kisheria, kwa kutunga waraka unaoitwa katiba ya nchi, njia ambazo kwazo mamlaka zinaundwa; na pia mahusiano yao, maeneo ya wajibu wao, mitindo na njia zinazopasika kufuatwa katika utendaji wao.
Yanawekwa kwa hiyo kisheria mahusiano kati ya raia na mamlaka za umma kwa mtindo wa haki na wajibu. Na inawekwa wazi kuwa wajibu wa kwanza wa mamlaka za umma ni kutambua, kuheshimu, kuunda kwa utulivu, kulinda na kuhamasisha haki na wajibu wa raia.
Ni kweli kwamba halikubaliki wazo lolote lenye kufanya matakwa ya mtu mmoja au kikundi yawe ndio msingi na chanzo pekee cha haki na wajibu za raia na yenye kuunganisha katiba za kisiasa na mamlaka za kiserikali [44].
46. Lakini mielekeo ambayo imegusiwa bila shaka ni ishara kwamba binadamu, katika zama za sasa, wamekuwa na utambuzi zaidi wa hadhi yao: utambuzi ambao, maadamu unawasukuma kushiriki maisha ya jumuiya, unadai pia kwamba haki za mtu – haki zisizonyang’anyika na zisizovunjika – zithibitishwe katika sheria zinazotungwa. Na unadai pia kwamba mamlaka za umma zitengenezwe kwa kufuata taratibu zilizowekwa na katiba, na watekeleze wajibu zao ndani ya mfumo wa kisheria.
III
MAHUSIANO BAINA YA JUMUIYA ZA KISIASA
Hizo nazo zina haki na wajibu
47. Sisi pia tunasisitiza lile lililofundishwa kwa namna ya kudumu na wale waliotutangulia: jumuiya za kisiasa baina yao zina haki na wajibu; hivyo hata mawasiliano kati yao yazingatie ukweli, haki, mshikamano hai na uhuru. Sheria ya maadili inayosimamia mahusiano kati ya watu binafsi inasimamia pia mahusiano kati ya jumuiya za kisiasa.
Jambo hilo si gumu kulielewa tukijua kwamba wawakilishi wa jumuiya za kisiasa, wanapotenda kwa niaba na kwa manufaa ya jumuiya zao, hawawezi kuisahau heshima yao; hivyo hawawezi kuivunja kanuni ya maumbile yao, ambayo ni sheria ya kimaadili.
Ingekuwa ajabu sana hata kufikiri tu kwamba mtu anapowekwa kuitawala mali ya wote hulazimishwa kuukana utu wote; wakati walichaguliwa kwa kazi hiyo yenye heshima kubwa kwa sababu walionekana washiriki wenye utajiri zaidi wa sifa za kibinadamu na kati ya watu bora katika jamii.
Zaidi ya hayo, mamlaka ni sharti la utaratibu wa kimaadili katika jamii ya watu; hivyo mamlaka haiwezi kuupinga utaratibu huo. Ikiwa inatokea hivyo, basi mamlaka inapoteza msingi wa kuwepo kwake. Kwa sababu hiyo Bwana alionya: “Basi, enyi wafalme, sikilizeni; enyi waamuzi wa miisho ya dunia jifunzeni; sikieni ninyi mtawalao watu wengi, na kujisifia umati wa mataifa. Kwa maana mlipewa falme zenu na Bwana, na milki zenu za Aliye juu, ambaye atazichunguza kazi zenu, na kuyahojihoji mashauri yenu” (Hek 6:1b-3).
48. Mwishowe inafaa kukumbuka kwamba hata katika kuratibisha mawasiliano kati ya jumuiya za kisiasa, mamlaka itumike kwa kulenga manufaa ya wote, ambayo ndiyo sababu ya kuwepo mamlaka hiyo. Lakini jambo la msingi kwa manufaa ya wote ni kuutambua na kuuheshimu utaratibu wa kimaadili. “Utaratibu kati ya jumuiya za kisiasa lazima uinuliwe juu ya mwamba usiovunjika na usiobadilika wa kanuni ya kimaadili, jinsi ilivyoonyeshwa na Muumba kwa njia ya utaratibu wa asili na uliochongwa mioyoni mwa watu kwa namna isiyofutika. ... Kama taa ing’aayo, kwa miali ya kanuni zake, lazima uongoze utendaji wa watu na wa mataifa, ambao wanapaswa kuifuata miongozo ya kufaa na yenye manufaa, la sivyo wataipoteza kama katika tufani kazi zote na ari zote walizotumia kwa kuujenga utaratibu mpya” [45].
Katika ukweli
49. Kanuni wa kwanza ni kwamba mahusiano kati ya jumuiya za kisiasa lazima yaratibiwe katika ukweli. Ukweli huo kabla ya yote unadai kwamba katika uhusiano huo kila aina ya ubaguzi uondolewe; na hivyo itambuliwe kanuni msingi ya kwamba jumuiya zote za kisiasa ni sawa kutokana na heshima ya asili. Kwa sababu hiyo kila jumuiya ya kisiasa ina haki ya kuwepo, ya kuwa na maendeleo, ya kuwa na vyombo vinavyofaa ili maendeleo yapatikane, na kuwa mdau wa kwanza katika utekelezaji huo; pia ina haki ya kufikiriwa vizuri na kuheshimiwa ipasavyo.
Kati ya watu mara nyingi kuna tofauti, ambazo zinaweza kuwa kubwa pia, tofauti katika ujuzi, katika fadhila, katika uwezo wa kubuni, katika umilikaji wa mali. Lakini jambo hilo kamwe haliwezi kuhalalisha madai ya ukuu juu ya watu wengine; bali linakuwa sababu kwa kila mmoja na kwa wote kuwajibika zaidi katika kusaidiana kwa lengo la kuinuliana.
Kwa namna hiyo mataifa yanaweza kutofautiana katika maendeleo ya kisayansi na utamaduni au maendeleo ya kiuchumi; lakini hali hiyo kamwe haiwezi kuhalalisha madai ya wengine kuwa juu ya wengine kwa unyanyasaji; bali inaweza kuwa sababu ya kuwa na ari zaidi katika kuleta maendeleo ya wote.
50. Kiasilia hakuna mtu aliye juu ya mtu mwingine; bali watu wote kwa asili wana heshima sawa. Kutokana na hilo, kati ya jumuiya za kisiasa hakuna jumuiya iliyo kiasilia juu ya jumuiya nyingine au jumuiya iliyo chini ya jumuiya nyingine: jumuiya zote kwa asili zina heshima sawa, kwa sababu zimejengwa kama mwili ambao viungo vyake ni watu wenyewe. Basi, tusisahau kwamba mataifa ya watu yana sababu za kuguswa sana katika masuala yanayohusu heshima yao, nalo kwa haki.
Ukweli unadai kwamba katika matukio mbalimbali yanayowezeshwa na maendeleo ya vyombo –shughuli ambazo zinawezesha kufahamiana kati ya watu wenye tamaduni tofauti – watu waongozwe na uchambuzi mtulivu. Hatuwezi kukataa kuwa halali tabia ya mataifa ya kupendelea kuonyesha yaliyo mazuri katika maisha yao. Bali lazima kukataa kata mifumo ya kuhabarisha ambayo, kwa kuficha ukweli, inawadhalilisha taifa moja au lingine kwa kuharibu bila haki heshima yao [46].
Kuzingatia haki
51. Mahusiano kati ya jumuiya za kisiasa lazima yaratibishwe kwa kuzingatia haki: nalo, maana yake ni kwamba, zaidi ya kutambua haki za kila mmoja, lazima wajibu zitekelezwe.
Jumuiya za kisiasa zina haki za kuwepo, za kuwa na maendeleo, za kuwa na vyombo vinavyowawezesha kupata hayo maendeleo: na haki ya kuwa wadau wa kwanza katika kuleta hayo maendeleo; jumuiya hizo zina haki pia ya kuheshimiwa ipasavyo: hivyo basi jumuiya hizo za kisiasa zinapaswa pia kuziheshimu kila aina ya haki zilizotajwa hapo juu; na kuyaacha matendo yanayovunja haki hizo. Kama vile inavyokuwa mtu binafsi anapohusiana na mtu mwingine, mmoja hawezi kufaidi kwa kumletea hasara mwingine, vivyo hivyo zinapohusiana jumuiya za kisiasa, jumuiya moja haiwezi kujiendeleza kwa kuzibana na kuzinyanyasa zingine. Hapa inafaa kukumbuka ilivyoandikwa na Mtakatifu Augustino: “Tukiondoa haki, falme za dunia zinakuwa nini kama si majambazi wakubwa?” [47].
Ni kweli, hata kati ya jumuiya za kisiasa inaweza kuibua, na kweli inaibua, misuguano yenye ushindani, lakini migongano lazima itatuliwe na mifarakano ipatiwe ufumbuzi si kwa kutumia nguvu, kwa utapeli au udanganyifu, bali, kama inavyofaa kwa wanadamu, kwa maelewano, kwa kuzingatia uchambuzi tulivu wa mambo na mwafaka wenye haki.
Namna ya kuwatendea makundi madogo
52. Na mintarafu jambo hilo, ni muhimu kuzingatia ule mkondo wa kihistoria (ambao kuanzia karne ya 19 ulienea duniani mwote na kuongeza nguvu hadi leo), ambao kwao watu wa taifa moja waling’ang’ania kujipatia haki ya kuungana kuwa nchi huru yenye serikali yake. Lakini, kutokana na sababu mbalimbali, mara nyingine haiwezekani kulinganisha mipaka ya kijiografia na mipaka ya kikabila: kutokana na hilo yanaibua suala la makundi madogo na matatizo makubwa yanayoendana nayo.
Lazima kusema wazi kabisa kwamba tendo ambalo linalenga kuwanyanyasa na kuwamaliza watu wa makundi hayo madogo ni kosa kubwa la uvunjifu wa haki; na ni kubwa zaidi ikiwa ni tendo linalolenga kuyafuta kabisa makundi hayo.
Kumbe, ni tendo la kuzingatia haki wenye mamlaka watoe mchango wao wenye kusaidia maendeleo ya kibinadamu ya makundi hayo madogo, kwa mikakati inayofaa kwa kuendeleza lugha yao, utamaduni wao, mila na desturi zao, raslimali na miradi yao ya kiuchumi [48].
53. Hapa lakini lazima tuweke wazi kwamba watu wa makundi madogo, kutokana na kupambana na hali waliyo nayo au kutokana na historia yao, wanaweza kushawishika, na si mara chache, kuweka mkazo sana katika mila zao mpaka kuzipa umuhimu kuliko tunu za kibinadamu; kana kwamba utu ungepimwa kwa vigezo vya utaifa. Lakini ingekuwa wazo la busara zaidi kwa watu hao kutambua pia mema yanayotokana na hali yao maalum. Wangetakiwa kugundua kwamba kuhusiana siku kwa siku na watu wenye utamaduni tofauti na wa kwao kunaweza kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya ubunifu na tunu zao wenyewe. Na polepole waweza kupokea katika maumbile yao tunu zile zilizo sifa bainifu za mataifa mengine. Lakini, hayo yote yataweza kutokea tu kama makundi haya ya wachache wataingia katika namna fulani ya muungano na watu ambao wanaishi kati yao, na kujifunza kushiriki katika desturi zao na njia yao ya kuishi. Wala hayataweza kutekelezwa ikiwa watapanda mbegu za fitina, zenye kuzaa tu mavuno ya madhara makubwa, yanayofifisha maendeleo ya mataifa.
Mshikamano wenye utendaji
54. Mahusiano baina ya jumuiya za kisiasa lazima yazingatiwe ukweli na haki. Lakini mahusiano hayo yanahitaji kuchangamshwa pia na mshikamano wenye utendaji kupitia namna mbalimbali ya ushirikiano zinazowezekana na zenye matunda mazuri kwa wakati wetu: ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kiafya, na wa burudani na michezo. Kuhusu suala hilo lazima kuzingatia daima kwamba sababu ya kuwa na mamlaka katika jamii si kwa kuwafunga na kuwabana watu ndani ya jumuiya zao za kisiasa; bali ni kwa kuwezesha manufaa ya wote katika jumuiya hizo za kisiasa; lakini manufaa ya wote lazima ieleweke na iendelezwe kama sehemu ya manufaa ya familia nzima ya binadamu.
Hilo linamaanisha kwamba licha ya kila jumuiya ya kisiasa kufuatilia faida yake bila kupeana hasara, lazima ziungane nguvu zao ili kufikia malengo ambayo yasingepatikana bila hilo: lakini katika nafasi kama hiyo lazima kuwa waangalifu sana ili kilicho faida kwa kundi moja kisiwe hasara kwa wengine, bali wao pia waweze kufaidi kwa namna fulani.
Manufaa ya wote katika ngazi ya dunia inadai kwamba jumuiya za kisiasa zisaidie mawasiliano, katika kila sekta, baina ya wananchi na baina ya taasisi za kati.
55. Duniani kuna idadi kubwa ya makabila yenye tofauti kubwa au ndogo kati yao. Lakini kilicho cha pekee cha kabila moja hakipaswi kugeuzwa kama gereza ambapo watu wanazuiliwa kuwasiliana na watu wa makabila mengine. Jambo hilo lingegongana sana na wakati wetu ambapo umbali kati ya mataifa ni kama umefutwa. Hatuwezi kusahau kwamba ingawa upekee wa makabila unawezesha kutofautisha kabila moja na lingine, makabila yote yanashirikiana mambo ya msingi yaliyo sawa, na kwa maumbile yao yanalenga kukutana katika mambo ya kiroho. Zaidi wanaendelea kuzipokea tunu za kiroho, zaidi wanapata fursa ya kukamilika bila mipaka. Kwa hiyo lazima wapewe haki na wajibu wa kuishi kwa kufungamana baina yao.
Ulinganifu kati ya watu, ardhi na mtaji
56. Inafahamika kwamba duniani kuna nchi yenye maeneo makubwa yanayoweza kulimwa lakini wana watu wachache; katika nchi nyingine hakuna uwiano kati ya utajiri wa raslimali asilia na mtaji uliopo. Hali hiyo pia inadai kwamba mataifa yajenge mahusiano ya kusaidiana, kwa kurahisisha baina yao mzunguko ya mitaji, mali na watu [49].
Hapa inafaa kusema kwamba, kila inapowezekana, inaonekana kwamba ni lazima mtaji utafute nguvukazi na wala si kinyume chake.
Kwa namna hiyo watu wengi wanaweza kupata fursa halisi ya kuboresha maisha yao bila kulazimishwa kuhama kwao kwa kwenda sehemu nyingine; na jambo kama hilo haliwezi kutokea bila kuleta huzuni kubwa, na bila kuwa na vipindi vigumu mpaka watu watulie maishani mwao na katika jamii.
Shida ya wakimbizi wa kisiasa
57. Bwana ametuwashia moyoni mwetu hisia ya kuwa baba mwenye upendo wa wanadamu wote, hivyo twasikia uchungu sana tunapofikiria jambo la wakimbizi wa kisiasa. Jambo ambalo limekuwa kubwa sana na linaloficha daima mateso mengi na makali.
Kwa bahati mbaya jambo hilo linaashiria kwamba kuna tawala za kisiasa ambazo hazihakikishi kila mtu apewe uhuru wa kutosha, uhuru unaomwezesha mtu aishi kwa kuheshimu utu, bali katika tawala hizo unajadiliwa au hata unapingwa uhalali wa uhuru wa namna hiyo. Jambo hilo, bila shaka, linaonyesha kupinduliwa kwa mfumo wa utaratibu wa kuishi pamoja, kwa sababu mamlaka katika jamii imewekwa ili kuendeleza manufaa ya wote, na msingi wa hilo ni kuutambua uhuru wa mtu na kuulinda.
Si jambo la ziada kukumbuka kwamba wakimbizi wa kisiasa ni watu; na hivyo wanastahili kupewa haki zote zinazomhusu mtu. Haki hizo hazifutwi wanaponyimwa uraia katika jumuiya za kisiasa wanapotoka.
Kati ya haki za binadamu ipo ile ya kujiunga na jumuiya ya kisiasa ambapo mtu anaamini kwamba ataweza kuishi vizuri yeye na familia yake kwa siku za mbele. Kutokana na hilo, jumuiya hiyo – ndani ya mipaka ya manufaa ya wote kwa maana sahihi – inawajibika kukubali kuingia kwa watu hawa na vilevile kusaidia ili watu hawa wapya wafungamane na jamii mzima.
58. Tunafurahi kupata fursa ya kutoa pongezi ya dhati kwa mipango yote yaliyoibuliwa na kuendelezwa kutokana na mshikamano wa kibinadamu na upendo wa kikristo kwa lengo la kupunguza ukali wa mateso yanayotokana na mtu kuhama na kwenda kujiunga na jamii nyingine.
Na tupate pia nafasi ya kuwatangazia watu waadilifu, ili wawe na shukrani, zile shughuli nyingi na za namna mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi maalum za kimataifa katika uwanja huo nyeti.
Kukomeshwa kwa ulimbikizaji wa silaha
59. Kwa upande mwingine, tumehuzunishwa sana kuona jinsi zilivyokuwa zikilimbikizwa silaha, ambazo mpaka sasa zinaendelea kutengenezwa, katika nchi zilizoendelea zaidi kiuchumi. Sera hii inadai mchango wa sehemu kubwa ya raslimali za kiakili na kifedha, na matokeo yake ni kwamba watu wa mataifa hayo yenyewe wanalemewa na mzigo mzito, wakati nchi nyingine zinakosa misaada wanayohitaji ili kuendelea kiuchumi na kijamii.
Katika mazingira ya leo – wengi husema – amani haiwezi kupatikana isipokuwa kwa misingi ya uwiano ulio sawa wa akiba za silaha, na dhana hiyo inakuwa sababu ya kujilundikia silaha. Kwa hiyo, ikiwa nchi moja inaongeza nguvu zake za kijeshi, hutokea kwamba nchi nyinginezo mara moja hufanya juhudi ya kuongeza vilevile silaha zao. Na kama nchi moja ina silaha za nyuklia, nchi nyingine zinaona kuwa ni halali na wajibu kujilimbikizia pia wao silaha za aina hiyo, zenye nguvu sawasawa za kuangamiza.
60. Kutokana na hayo, watu huishi sikuzote katika mafadhaiko na hofu ya kwamba dhoruba isiyoepukika ingeweza kulipuka wakati wowote kwa nguvu za kutisha. Nao wana sababu ya kuhofia hivyo, kwa sababu hakika silaha hizo zipo. Na ijapo ni vigumu kuamini kwamba yupo anayejichukulia madaraka na wajibu wa kuanzisha mauaji na maharibifu ambayo vita ingeleta, hali kadhalika haiwezekani kukataa kwamba mlipuko wa vita ungeweza kusababishwa na tukio la bahati au lisilotabiriwa.
Zaidi ya hayo, ingawa nguvu za ajabu za silaha za kisasa zinaweza kuwa kama kizuizi, kuna sababu ya kuhofia kwamba hata majaribu tu ya silaha za nyuklia huweza, yakiendelea kufanywa, kuleta hatari kubwa kwa maisha ya viumbe duniani.
Kwa hiyo, hisia za haki, busara na heshima kwa utu wa binadamu zinadai kwa msisitizo kukomeshwa kwa ulimbikizaji wa silaha; pia kwamba akiba za silaha zilizolundikwa katika nchi mbalimbali zipunguzwe zote popote na kwa wakati mmoja katika kila nchi husika; kwamba silaha za nyuklia zipigwe marufuku. Hatimaye, zifanyike jitihada za kufikia maafikiano ya kupunguza silaha, pamoja na mfumo wa udhibiti wenye ufanisi. “Lazima kuzuia kwa nguvu zote – alionya mtangulizi wetu Papa Pius XII – kwamba janga la vita vya dunia pamoja na maangamizo yake ya kiuchumi na kijamii, na laana zake na upotovu wa maadili, umeze tena kwa mara ya tatu familia za wanadamu wote” [50].
61. Lakini, kila mtu lazima azingatie kwamba haiwezekani mchakato wa kusitisha ulimbikizaji wa silaha, yaani kupunguza silaha na – jambo ambalo ni muhimu zaidi – kuziondoa kabisa, ni jambo lisilowezekana, isipokuwa unafanyika kwa utimilifu, yaani, kama hata roho zisipoathirika. Yaani, ni lazima kila mtu atoe mchango wake katika juhudi ya kufuta hofu na matarajio mapotovu ya vita katika roho za watu. Nalo linadai kwamba kanuni za msingi ambazo wakati wa sasa zinategemeza amani katika ulimwengu wa leo zibadilishwe na kanuni nyingine kabisa, ya kwamba amani ya kweli na ya kudumu baina ya mataifa inategemea tu kuheshimiana na kuaminiana, wala si usawa wa nguvu za silaha. Sisi tunaamini kwamba lengo hili linaweza kufikiwa, kwa sababu hilo ni jambo ambalo si tu linashauriwa na akili nyofu, lakini pia ni la kutamanika na la kufaa kuliko mema yote.
62. Nalo ni lengo ambalo, kwanza kabisa, linadaiwa na akili. Ni wazi, au walau ingetakiwa kuwa wazi kwa wote, kwamba mahusiano baina ya mataifa, sawasawa kama ilivyo baina ya watu binafsi, hayana budi kuratibiwa siyo kwa nguvu za silaha, bali kwa kuendana na kanuni za akili na busara: yaani, kanuni za ukweli, haki na mshikamano hai wenye utendaji.
Halafu, ni lengo ambalo Sisi tunaamini linatamaniwa kwa dhati. Maana, ni nani asiyetamani kwa moyo wote kuepukana na tishio la vita, na kuona amani inalindwa na kuimarishwa zaidi na zaidi siku kwa siku?
Hatimaye, hilo ni lengo linalosababisha mema mengi, kwani kutoka amani wote wanapata faida: watu binafsi, familia, mataifa, na familia nzima ya binadamu. Onyo la Mtangulizi wetu Papa Pius XII bado linalia vikali masikioni mwetu: “Katika amani, hakuna kinachopotea; ila vyote huweza kupotea kwa vita” [51].
63. Kwa hiyo, Sisi kama wakili wa Yesu Kristo hapa duniani – Yeye aliye Mwokozi wa ulimwengu na Mtendaji wa amani – na kama mfasiri wa tamaa za ndani kabisa za familia nzima ya binadamu, kwa kufuata upendo wetu wa kibaba kwa watu wote, tunaona kuwa ni wajibu wetu kuomba na kusihi kila mtu, hususan viongozi wa Mataifa, wasinyime juhudi na bidii katika kuhakikisha kwamba mahusiano baina ya watu yanafuata mkondo ulio kadiri ya akili na heshima ya kiutu.
Katika maamuzi ya pamoja, wao walio na hekima na madaraka zaidi, wazingatie kwa makini suala la kuyafikia maafikiano ya haki na kiutu kuhusu mahusiano baina ya Mataifa duniani kote. Na matengenezo ya mahusiano hayo hayana budi kuwa na misingi ya kuaminiana, ya ukweli katika majadiliano, na ya nia ya kutekeleza kiaminifu masharti yaliyokubaliwa. Na suala hili lazima lichunguzwe katika vipengele vyake vyote, kusudi kionekane wazi ni kipi ambacho, kutokana na hicho, huwezekana kujiwekea mikataba iliyo kweli ya kirafiki, ya kudumu na yenye manufaa katika matokeo yake.
Kwa upande wetu, Sisi tutaendelea kusali na kumwomba Mungu bila kukoma, ili aweze kuzibariki kazi hizo kwa msaada wake, na kuzifanya ziweze kuleta matunda mema.
Katika uhuru
64. Aidha, mahusiano baina ya Mataifa lazima yaratibiwe kadiri ya kanuni ya uhuru. Na maana yake ni kwamba hakuna nchi yenye haki ya kuchukua hatua yoyote ambayo italeta ukandamizaji usio wa haki juu ya nchi nyingine, au iliyo kujiingiza bila sababu katika shughuli zake. Kinyume chake, nchi zote zinatakiwa kufanya bidii ili kukuza katika nchi nyinginezo utambuzi wa wajibu wao, roho ya ujasiriamali, na azimio la kufanya juhudi katika kujishughulisha kwa ajili ya maendeleo yake katika kila fani.
Ukuaji wa nchi zinazoendelea kiuchumi
65. Watu wote wameunganika katika asili moja na jamii moja, katika Ukombozi wa Kikristo, na katika hatma yao kwa Mungu. Nao huitwa wote kuunda familia moja ya Kikristo. Kwa sababu hiyo, katika Ensiklika yetu Mater et Magistra, Sisi tulitoa wito kwa nchi zilizo tajiri zaidi kusaidia kwa kila namna Mataifa yale ambao bado wako katika mchakato ya kujipatia maendeleo ya kiuchumi [52].
Na sasa twaweza kuhakikisha kwa furaha kwamba wito wetu ulipokelewa kwa moyo na kwa upana, na tunatumaini kwamba katika miaka ijayo utapokelewa hata kwa upana zaidi, na hivyo kuwezesha nchi zilizo maskini zaidi kupata upesi kiwango cha maendeleo ya kiuchumi kitakachowawezesha raia wake kuishi maisha yanayolingana na hadhi yao ya binadamu.
66. Si bure kurudia tena na tena kwamba mikakati ya ushirikiano ili kusaidia nchi hizo inatakiwa itekelezwe kwa kuheshimu na kuhakikisha uhuru wao. Zenyewe hazina budi kuwa, na kujitambua kuwa, wawajibikaji na watendaji wa kwanza katika kutekeleza mikakati ya maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii; kwamba zenyewe zinatakiwa pia kubeba mzigo ulio mkubwa wa mikakati hiyo.
Kuhusu jambo hilo, Mtangulizi wetu Papa Pius XII aliwahi kufundisha kwa busara kuwa: “Utaratibu mpya ulioundwa juu ya kanuni za kimaadili, ni kinga bora dhidi ya ukiukwaji wa uhuru, umoja na usalama wa nchi nyingine, bila kujali ukubwa wa eneo lao au uwezo wao wa kujilinda. Ingawa haikosi kwamba Mataifa makubwa, kutokana na uwezo wao mkubwa na mali nyingi yalizo nazo, yatadai kuweka yenyewe sheria na miongozo kwa ajili ya kuratibisha mahusiano na Mataifa madogo, hata hivyo Mataifa madogo haya hayawezi kunyimwa haki yao – katika muktadha wa manufaa ya wote – ya kuwa na uhuru wao wa kisiasa, na uwezo wa kutoegamia upande wowote katika migogoro baina ya Mataifa. Taifa lolote haliwezi kunyimwa haki hiyo, ambayo iliwekwa na kudaiwa na sheria ya maumbile, vilevile na sheria za kimataifa. Hayo Mataifa madogo yanayo pia haki ya kulinda maendeleo yao ya kiuchumi. Kwa namna hiyo tu, yaani kwa kuhakikishiwa kiutendaji matumizi ya haki hizo, Mataifa madogo yataweza kuhamasisha kwa mafanikio manufaa ya watu wote, hali kadhalika usitawi wa watu wake, kimwili, kitamaduni na kiroho" [53]. Kwa hiyo, Mataifa yaliyo tajiri, katika kutoa misaada ya aina mbalimbali kwa Mataifa maskini, lazima yaziheshimu tunu, desturi na taasisi zenye maadili za nchi. Ni lazima pia yaondokane na kila sera yenye lengo la kuyatawala Mataifa mengine. Ikiwa hayo yatatekelezwa, basi “mchango mkubwa utakuwa umeshatolewa kwa ajili ya kuunda jumuiya ya dunia nzima, ambamo kila nchi pekee, kwa kutambua haki na wajibu wake, huweza kutenda katika kiwango cha usawa na nyingine kwa ajili ya kutekeleza manufaa ya wote" [54].
Ishara za nyakati
67. Nyakati hizi zetu, watu huzidi kuwa na hakika kwamba migogoro inayoweza kuzuka baina ya Mataifa haina budi kusuluhishwa kwa njia ya majadiliano na makubaliano, wala si kwa kutumia silaha.
Twatambua kwamba imani hiyo hutokana hasa na hofu kuhusu nguvu haribifu za silaha za kisasa; tena hukuzwa na tishio la maangamizi na maharibifu makubwa, pamoja na huzuni nyingi kwa familia nzima ya wanadamu, ambazo huweza kuletwa na matumizi ya silaha hizo. Kwa sababu hiyo, katika nyakati hizi zetu za sasa, zinazojisifia kwa uvumbuzi wa nguvu ya kiatomiki, ni kichaa na jambo lisilo la maana kabisa kudhani kuwa vita ni njia inayofaa ya kurudisha haki zilizovunjwa.
Hata hivyo, mara nyingi twaona kwa huzuni kwamba kati ya Mataifa hutawala hofu kama sheria iliyo kuu, nayo inasababisha yatumie gharama kubwa ajabu kwa kujipatia silaha. Nayo yanafanya hivyo, husema – wala hatuna sababu ya kutoyaamini – , si kwa lengo la kushambulia, lakini kwa kuyazuia mataifa mengine yasithubutu kushambulia.
Kuna kila sababu ya kuwa na matumaini kwamba, kwa kukutana pamoja na kuwa na majadiliano, watu wataweza hatimaye kuyatambua vizuri zaidi yale yanayowaunganisha, ambayo hutokana na maumbile ya asili waliyo nayo wote. Pia kwamba watatambua kuwa moja ya mahitaji muhimu sana ya maumbile yao ya asili ni hili kwamba kinachotakiwa kutawala kati yao na wale wenye uhusiano nao si woga bali ni upendo. Na ni sifa bainifu ya upendo kuwavuta watu washirikiane pamoja kwa namna mbalimbali, katika umoja wa mioyo na ya malengo; nao ni umoja wenye kuleta mema mengi.
IV
MAHUSIANO YA WATU
NA YA JUMUIYA ZA KISIASA
NA JUMUIYA YA DUNIA NZIMA
Kutegemeana kwa jumuiya za kisiasa
68. Maendeleo ya hivi karibuni katika sayansi na teknolojia yaliathiri kwa kina desturi za watu. Maendeleo hayo yaliwahimiza watu, popote duniani walipo, kukuza ushirikiano na mshikamano kati yao. Maana siku hizi imeongezeka sana usambazaji wa bidhaa, wa fikara na ujuzi, pia uwezo wa watu wa kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Jambo hilo limesababisha ongezeko la ajabu la mahusiano kati ya watu binafsi, kati ya familia mbalimbali na asasi za kati za nchi mbalimbali, na baina ya serikali za hizo nchi. Kuna pia ongezeko la kasi la hali ya kutegemeana kiuchumi kati ya nchi mbalimbali. Kila uchumi wa nchi moja huzidi kutegemeana na ule wa nchi nyinginezo, na hivyo unakuwepo kama uchumi mmoja tu wa dunia nzima unaotokana na uunganishaji wa uchumi wa kila taifa kwa wakati mmoja huuhuu. Hatimaye, kwa kila nchi, maendeleo ya kijamii, utaratibu, usalama na amani, yote hayo yamefungamana na maendeleo ya kijamii, utaratibu, usalama na amani ya nchi nyingine zote.
Kutokana na hayo, ni wazi kwamba hakuna nchi yenye kuweza kufanikisha maslahi yake mbali na nchi nyingine, wala, katika hali hiyo, kuweza kujiendeleza kama inavyotakiwa. Kwani usitawi na maendeleo ya kila nchi, kwa upande mmoja, ni matokeo, na, kwa upande mwingine, ni sababu ya usitawi na maendeleo ya nchi nyingine zote.
Makasoro katika utaratibu wa mamlaka ya umma katika kufuatilia manufaa ya wote
69. Umoja wa familia ya binadamu utakuwepo muda wote kwa sababu jamii yake ni wanadamu ambao wote kwa asili wana hadhi iliyo sawa. Kwa sababu hiyo, kutakuwa daima na madhumuni ya lazima – yanayotokana na asili ya binadamu – ya kukuza manufaa ya wote pamoja yaani manufaa yaliyo kwa maslahi ya familia nzima ya binadamu.
Zamani, watawala na serikali za nchi hutazamiwa kukidhi manufaa ya wote kwa njia za kawaida za kidiplomasia, au kwa mikutano na majadiliano ya wenye mamlaka ya juu, au kwa kufanya mikataba na maafikiano; yaani, kwa kutumia njia na mbinu zilizokuwa zikipendekezwa kadiri ya sheria za kimaumbile, au na sheria za nchi au za kimataifa.
70. Lakini, katika siku hizi zetu mahusiano baina ya Mataifa mbalimbali yamepatiwa mabadiliko makubwa. Kwa upande mmoja, mada ya manufaa ya wote huibua masuala nyeti, mazito na magumu – hasa kuhusu kulinda amani na usalama duniani pote. Kwa upande mwingine, viongozi wa serikali za nchi moja moja, wakiwa katika hadhi ya kisheria iliyo sawa kati yao, ingawa wanazidi kufanya mikutano na kujitahidi kubuni mbinu za kisheria zenye kufaa, wanashindwa kulifikia lengo hilo. Wala si kwamba wanakosa mapenzi mema na juhudi, bali kwamba mamlaka waliyo nayo hailingani na mahitaji ya dunia ya leo.
Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba mfumo na muundo wa maisha ya kisiasa katika ulimwengu wa leo, na ushawishi wa mamlaka ya umma katika nchi zote za dunia, hauwiani na jukumu la kustawisha manufaa ya wote katika mataifa yote.
Uhusiano baina ya mada za kihistoria za manufaa ya wote na mfumo wa mamlaka za umma
71. Sasa, tukizingatia kwa makini maana ya ndani ya manufaa ya wote, kwa upande mmoja, na asili na dhima ya mamlaka ya umma, kwa upande mwingine, hatuna budi kuona kwamba kuna muungano wa lazima kati yake. Kwa hiyo, utaratibu wa kimaadili kama vile unavyodai kuwepo mamlaka ya umma kama chombo cha kusitawisha manufaa ya wote, hali kadhalika unadai kwamba mamlaka hiyo iwe na uwezo wa kulifikia lengo lake hilo. Kutokana na hayo, taasisi za kiraia ambazo zimekabidhiwa mamlaka hiyo, na kuitumia ili kutekeleza malengo yake, zinaundwa na kutenda kwa namna inayofaa: yaani, ziwe na muundo unaosaidia kwa ufanisi kutimiliza manufaa ya wote kwa njia na mbinu ambazo zinaendana na mageuzi ya hali halisi ya siku hizi.
Leo, manufaa ya wote pamoja yanaleta masuala ambayo yanahusu dunia nzima; masuala ambayo, kwa hali hiyo, hayawezi kutatuliwa isipokuwa na mamlaka ya umma yenye nguvu, muundo na miundombinu iliyoenea sawasawa na masuala yenyewe, na iliyo na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi katika dunia nzima. Kutokana na hayo, ni utaratibu wenyewe wa kimaadili ambao unadai isimikwe mamlaka maalum ya umma yenye muundo wa jumla wa namna hiyo.
Mamlaka za umma zilizosimikwa kwa makubaliano ya pamoja, wala si kwa mabavu
72. Lakini, mamlaka hiyo ya jumla yenye madaraka katika eneo la dunia nzima na vyombo vya kufaa ili kuyafikia manufaa ya wote pamoja lazima isimikwe kwa idhini ya nchi zote, wala si kwa mabavu. Kwani mamlaka ya namna hiyo, inayotakiwa kutimiza jukumu lake kwa mafanikio, lazima ikubali kutenda kwa usawa kwa wote, na kwa uwajibikaji kwa kuzingatia daima manufaa ya watu wote pamoja, kwa kuachana na mapendeleo kwa upande wowote. Maana, ikiwa mamlaka ya dunia ingalisimikwa na mataifa yenye nguvu kwa kutumia mabavu, ingesababisha hofu na mashaka kuwa itatumiwa ili kuhifadhi maslahi ya wachache, au kuunga mkono taifa moja pekee; na hivyo athari na ufanisi vya utendaji wake vingepunguzwa.
Kwani, hata kama unaweza ukawepo utofauti mkubwa baina ya mataifa kwa habari ya maendeleo ya kiuchumi na nguvu za kijeshi, kila taifa linatambua kuwa ni suala muhimu na nyeti usawa wake na mataifa mengine kwa upande wa hadhi yake ya kisheria na ubora wa mwenendo wake wa maisha. Kwa sababu hiyo, mataifa yanayo haki ya kutokubali kuamuriwa na mamlaka iliyosimikwa kwa mabavu, iliyowekwa bila mchango wao, au wasioidhinishwa na maafikiano ya hiari yao.
Manufaa ya watu wote na haki za binadamu
73. Kama vile manufaa ya wote katika taifa moja moja yasivyoweza kuamuliwa isipokuwa kwa kuzingatia utu wa binadamu, hali kadhalika kwa manufaa ya wote ya mataifa yote pamoja. Kwa hiyo, mamlaka ya umma ya jumuiya ya dunia nzima pia haina budi kuazimia kuwa na lengo kuu hili: kutambua, kuheshimu, kulinda na kusitawisha haki za binadamu. Na hilo laweza kutekelezwa ama kwa utendaji wake wa moja kwa moja, ikitakiwa, au kwa kuasisi duniani kote mazingira na vyombo viwezavyo kuwasaidia viongozi wa serikali za kila taifa kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao maalumu.
Kanuni ya auni
74. Kama vile, katika kila nchi mahusiano baina ya mamlaka ya serikali na watu binafsi, familia na taasisi za kati yanaongozwa na kanuni ya auni, hali kadhalika ni vema kwamba kanuni hiyo iratibishe pia mahusiano baina mamlaka ya dunia nzima na mamlaka ya serikali ya kila taifa. Jukumu maalum ya mamlaka hiyo ya dunia nzima lazima liwe lile la kutathmini na kusuluhisha masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni yanayoathiri manufaa ya watu wote pamoja. Nayo ni masuala ambayo, kwa jinsi ulivyo uzito, uenezi na haraka yake, ni magumu mno kwa serikali ya taifa moja moja kuweza kuyatatua kwa mafanikio likitenda kazi peke yake.
Lakini, bila shaka si juu ya mamlaka ya dunia nzima kulazimisha utendaji wa serikali ya taifa moja, wala kujichukulia dhima yoyote ya madaraka yake. Kinyume chake, lengo lake kuu ni kujitahidi kuandaa duniani mazingira ambamo mamlaka ya kiserikali ya kila nchi, raia wake na makundi ya kati, huweza kutekeleza kazi zao, kutimiza wajibu wao, na kudai haki zao kwa usalama ulio mkubwa zaidi [55].
Ishara za nyakati
75. Kama wote wanavyojua, tarehe 26 Juni, mwaka 1945 liliundwa Shirikisho la Umoja wa Mataifa – linalojulikana kwa kifupi kama UNO; ambalo chini ya mwavuli wake yaliongezeka baadaye Mashirika madogo mengine, ambayo wanachama wake huteuliwa na mamlaka ya serikali ya Mataifa mbalimbali. Kwa Mashirika hayo hukabidhiwa majukumu muhimu sana, ya kutimizwa katika kila nchi, kwenye nyanja za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu na kiafya. Shirikisho la Umoja wa Mataifa lengo lake mahsusi ni kudumisha na kuimarisha amani baina ya mataifa, pia kuhamasisha na kusaidia mahusiano ya kirafiki baina yake, yenye misingi katika kanuni za usawa, kuheshimiana, ushirikiano mpana katika kila fani ya utendaji wa kibinadamu.
Thibitisho lililo muhimu kwa namna ya pekee la mtazamo wa mbali wa Shirikisho hilo ni Taarifa ya Ulimwengu juu ya Haki za Binadamu iliyopitishwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba, mwaka 1948. Utangulizi wa Taarifa hiyo unatamka kwamba utambuzi halisi na heshima kamili kwa haki zote, na uhuru unaoendana nazo, kama zinavyoelezwa katika Taarifa hii ni lengo linalotakiwa kutafutwa na kila watu na kila taifa.
Tunaelewa kwamba juu ya vipengele fulani vya Taarifa kulikuwa na upinzani wa hapa na pale; na bila shaka kulikuwa na sababu yake. Hata hivyo, lakini, tunafikiri kwamba hati hiyo lazima itambulike kama hatua muhimu katika njia inayoelekea kuunda utaratibu wa kisheria na kisiasa ya jumuiya ya nchi zote zilizomo duniani. Taarifa hii ni thibitisho kuu la hadhi ya kibinadamu kwa watu wote; na utetezi wa haki ya kila mmoja kuwa huru katika kuutafuta ukweli, kufuatilia kanuni za maadili, kushika majukumu ya haki, na kuishi maisha ya kiutu kwelikweli. Pia inatamka uhalali wa haki nyingine zilizounganika na hizo.
Kwa hiyo, tunatazamia sana kwamba Shirikisho la Umoja wa Mataifa liweze kulinganisha zaidi na zaidi muundo wake na mbinu zake za kiutendaji na upana na fahari ya majukumu yake. Na isiwe mbali mno ile siku, ambapo kila mtu anaweza kukuta katika Shirikisho hilo ulinzi bora wa haki zake binafsi; yaani, haki zile ambazo zatokana moja kwa moja na hadhi yake kama binadamu, na ambazo, kwa sababu hiyo, ni za wote, hazinyang’anyiki wala hazivunjiki.Hayo yote yanatamanika sana, kwa vile wakati wa sasa watu wanashiriki zaidi katika maisha ya umma ya nchi yao, na – kwa kufanya hivyo – waonyesha kukua kwa utayari wa kuwajibika katika shughuli za watu wote. Watu wanatambua zaidi na zaidi kwamba ni viungo hai vya familia ya wanadamu wote duniani.
V
MAUSIA YA KIUCHUNGAJI
Wajibu wa kushiriki katika maisha ya umma
76. Hapa kwa mara nyingine tena tunawahimiza wana wetu wawe washiriki hai katika maisha ya umma, na kufanya kazi kwa pamoja kwa faida ya jumuiya nzima ya binadamu, hali kadhalika kwa jumuiya zao za kisiasa. Ni muhimu zaidi wao wajitahidi katika mwanga wa imani ya kikristo, na upendo ukiwa kama kiongozi wao, kuhakikisha kuwa kila taasisi, iwe ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, au ya kisiasa, isije ikawa kikwazo, bali isaidie kurahisisha hali bora ya mtu, yote ya kimwili na kiroho.
Umahiri wa kisayansi, uwezo wa kiteknolojia, mazoea ya kiufundi
77. Na bado, kama wanataka kuujaza utamaduni kwa mawazo yaliyo bora na kanuni za kikristo, haitoshi kwa wana wetu kuangazwa na mwanga wa imani wa kimbingu na kuwaka hamasa kwa muda, ni lazima wajihusishe wenyewe katika kazi za taasisi hizi, na kujitahidi kuzishawishi kwa ufanisi toka ndani.
Lakini katika utamaduni na ustaarabu kama wetu, ambao unafahamika zaidi kwa elimu yake ya kisayansi na vumbuzi zake za kitaalamu, ni hakika kuwa hakuna mtu anayeweza kujiingiza katika maisha ya umma, endapo hana uwezo wa kisayansi, uwezo wa kitaaluma, na amebobea katika fani yake aifanyayo.
Umahiri wa kisayansi, kiteknolojia na kiufundi unachangia pamoja na tunu za kimaadili kwa utendaji bora
78. Hata hayo, lakini, lazima ieleweke kuwa, ingawa ni muhimu, hayatoshi katika kufanya mahusiano ya maisha ya kila siku yalingane na kiwango cha kweli cha utaratibu wa kiutu, kinachojikita kama inavyotakiwa katika ukweli, na ambao kipimo na shabaha ni haki, nguvu yake tendaji ni upendo na mbinu ya utekelezaji ni uhuru.
Ili sera hizi ziweze kufanya kweli kazi, watu kwanza kabisa wanatakiwa kuziendesha shughuli zao za kawaida kulingana na sheria ambazo zinaongoza kila moja ya hizo shughuli, kwa kuchunguza kanuni ambazo zinalingana na asili yake. Pili, matendo ya watu lazima yaendane na sheria za mfumo wa kimaadili. Hii maana yake kuwa tabia zao lazima ziakisi ufahamu wao wa kutenda haki binafsi na kutimiza wajibu binafsi. Akili inao wajibu mwingine wa kufanya. Katika utii kwa mpango wa Mungu na amri za Mungu kwa kuheshimu ukombozi wetu na kukataa maongozi ya dhamiri, watu lazima wafanye shughuli zao za kawaida kwa namna ile inayoweza kuzihusianisha tunu kuu za kikristo na zile za kisayansi, kiteknolojia na kitaaluma.
Waamini wang’amua umoja wa imani ya kidini na utendaji katika dunia
79. Katika nchi zenye asili ya kikristo, kwa sasa, taasisi za umma zinaonyesha maendeleo makubwa ya kisayansi, na maendeleo ya kiufundi na zinamiliki vitendea kazi vya kutosha katika kufikia malengo ya kila aina. Hata hivyo ieleweke kuwa taasisi hizi mara kwa mara, lakini kwa umbali, zinaathiriwa na malengo na roho ya kikristo.
Mmoja anaweza kuuliza sababu ya hili, kwani watu ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia – na wanaendelea bado kuchangia – uanzishwaji wa taasisi hizi ni watu ambao ni wakristo kweli, na ambao wanaishi maisha yao walau kwa sehemu fulani, kadiri ya mashauri ya Injili. Kwa maoni yetu ufafanuzi upo katika mpasuko fulani kati ya imani na matendo. Umoja wao wa ndani na wa kiroho lazima urejeshwe, ili imani iwe mwanga na upendo uwe motisha ya shughuli zao zote.
Maendeleo ya jumla ya wanadamu walio kwenye malezi
80. Tunazingatia pia kuwa sababu nyingine ya mfarakano huo wa mara kwa mara kati ya imani na matendo kwa wakristo ni ukosefu wa elimu ya mafundisho ya kikristo na maadili ya kikristo. Katika mahali pengi nguvu zinazowekwa kwa ajili ya masomo ya kidunia mara nyingi hazilingani na zinazowekwa katika masomo ya dini. Mafunzo ya kisayansi yanafikia upeo wa juu, wakati mafunzo ya kidini hayaendelei zaidi ya ile hatua ya msingi. Ni muhimu kwa hiyo, mafundisho yanayotolewa kwa vijana yawe kamili na endelevu, na yatolewe kwa namna ambayo maadili mema na ukuzaji wa tunu za kidini viendane na elimu ya kisayansi na maendeleo endelevu ya kiufundi. Vijana lazima pia wafundishwe namna ya kuyatimiza majukumu yao kwa namna ile inayofaa kweli [56].
Bidii ya kudumu
81. Tunadhani kuwa inafaa kuonyesha jinsi ilivyo vigumu kuelewa, kwa usahihi wa kutosha, uhusiano uliopo kati ya madai halisi ya haki na mazingira ya maisha ya wanadamu; yaani kutambua viwango na namna ambavyo kwa hivyo, kanuni na maagizo ya kimafundisho inabidi yatumike katika hali halisia ya jamii ya binadamu.
Na kutambua viwango vile na namna zile ni vigumu zaidi katika nyakati kama za kwetu, ambazo ni za mishughuliko mingi mno. Hata hivyo, hizi ni nyakati ambapo kila mmoja anapaswa kutoa mchango wake kwa ajili ya manufaa ya wote. Kila siku ni mbele yetu hitaji la kulinganisha vizuri zaidi uhalisia wa maisha ya kijamii na madai ya haki. Kwa sababu hiyo, watoto wetu wana kila sababu ya kutokufikiri kwamba wanaweza kuacha bidii zao na kuridhika na malengo yale ambayo yamekwisha patikana.
Bali wanadamu wote wanatakiwa kuyahesabia kama kitu ambacho bado ni kidogo yale yaliyotendwa katika kusawazisha hali halisi ya viwanda, ya umoja wa wafanyakazi, ya vyama vya mafundi, ya bima, ya taasisi za kiutamaduni, ya sheria, ya siasa; hali halisi ya taasisi zilengazo utamaduni, afya, burudani, spoti; kusawazisha hali halisi ya nyanja hizo na viwango halisi vinavyodaiwa na nyakati kama hizi za kiatomiki na za ugunduzi wa angani: nyakati ambazo familia ya binadamu imeshaingia ndani yake na imeshaanza mwendo wake mpya ikiwa na mitazamo yenye upana usio na mipaka. Wanadamu wayaone hayo kama kitu kilicho kidogo hasa wakiyalinganisha na yale ambayo bado hayajatendeka.
Mahusiano kati ya Wakatoliki na Wasio Wakatoliki katika nyanja za uchumi, jamii na siasa
82. Kanuni za kimafundisho zilizowekwa bayana katika hati hii zinatoka au zinadokezwa na madai yaliyomo moja kwa moja katika maumbile yenyewe ya binadamu, na chanzo chake kipo, hasa, kwenye haki asilia. Kwa hiyo zinatoa nafasi kubwa kwa Wakatoliki ya kukutana na kuelewana na Wakristo wasio na umoja kamili na hiki Kiti cha Kitume na pia na watu ambao hawajaangazwa na imani katika Yesu Kristo. Watu ambao, lakini, ndani yao mna mwanga wa akili na ndani yao uadilifu wa asili pia unapatikana na kutenda kazi. “Katika mahusiano hayo wana wetu wawe macho ili msimamo wao uwe daima thabiti wasije wakatia katika hali ya wasiwasi mafundisho ya dini na maadili. Lakini wakati huohuo waonekane kwamba wanasukumwa na moyo wa kuelewana, hawatafuti faida yao na wana mwelekeo wa kutenda kwa uaminifu katika kutekeleza mambo yaliyo mema yenyewe au yana uhusiano wowote na wema halisi” [57].
83. Lakini isitokee kamwe kwamba kosa na mkosefu vinalinganishwa, hata kama ni suala la kosa linalotendeka kwenye uwanja wa maadili au wa dini (au kama ni ujuzi mdogo usiotosheleza katika nyanja hizo). Mkosefu daima – na kwanza kabisa – ni binadamu, na katika nafasi zote anabaki na hadhi yake ya kibinadamu; na anatakiwa ahesabiwe na kutendewa daima kadiri ya hadhi kubwa namna hii. Aidha, katika kila mwanadamu hitaji la kuvunja mipaka ya ukosefu ili kutafuta njia ya ukweli (hitaji linalodaiwa na asili yake) halizimiki kamwe. Na kazi ya Mungu ndani yake haikomi. Kwa sababu hii, yule ambaye katika nafasi fulani ya maisha yake hana imani sahihi, au anayakubali mawazo ya kimakosa, anaweza kuangazwa na ukweli kesho na kuuamini. Mikutano na maafikiano, katika vitengo mbalimbali vya malimwengu, kati ya Wakatoliki na Wasio na Imani au Wenye Imani isiyo sahihi kwa sababu ya kushika mafundisho fulani mapotovu, yanaweza kuwa fursa kwa kuvumbua ukweli na kuuheshimu.
84. Aidha, inabidi ieleweke kuwa haiwezekani mafundisho ya kifalsafa yasiyo kweli juu ya asili, mwanzo na mwisho wa ulimwengu yafananishwe na mavuguvugu ya kihistoria yenye malengo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa, hata kama mavuguvugu haya yalianzishwa na mafundisho hayo na yanasukumwa nayo hadi sasa. Kweli mafundisho, baada ya kuendelezwa na kuwekewa mipaka, yanabaki na kudumu daima kama yalivyo; wakati mavuguvugu yaliyotajwa, kwa vile yanafanya kazi katika mazingira ya kihistoria, lazima yaathiriwe na mazingira hayo na lazima yabadilike hata kwa kiwango kikubwa. Aidha, nani anaweza kukana kwamba katika mavuguvugu yale, kwa kadiri yanavyolingana na kanuni za akili adilifu na yanapokea nia safi za binadamu, yanapatikana mambo chanya na yanayostahili kukubaliwa?
85. Kwa hiyo, inaweza ikatokea kwamba urafiki fulani au mahusiano ya kiutendaji ambayo hadi jana yalikuwa yakidhaniwa kwamba hayafai au hayana faida, leo yanaweza kuwa nayo, au pengine kesho. Kuamua kama wakati umewadia, pamoja na kupanga taratibu na viwango vya mshikamano huo katika kufanikisha malengo ya kiuchumi, ya kijamii, ya kiutamaduni, ya kisiasa, maadilifu na yanayoufaa wema halisi wa jumuiya, hayo ni shida ambazo zinaweza kutatuliwa kwa fadhila ya busara tu. Fadhila ambayo ni kiongozi katika fadhila zote zinazoratibu maisha ya kimaadili, ya kila mmoja binafsi na ya jamii nzima. Kwa sababu hiyo, kwa upande wa Wakatoliki uamuzi huo kwanza kabisa ni juu ya wale wanaoishi na kufanya kazi katika vitengo maalum vya umma, ambapo huwa matatizo hayo yanakuwepo. Nao watakiwa kuamua daima kwa kufuata kanuni za haki asilia, mafundisho ya kijamii ya Kanisa na maagizo ya viongozi wa Kanisa. Maana, haifai kabisa kusahau kwamba Kanisa lina haki na wajibu si tu ya kulinda kanuni za mfumo wa kimaadili na wa kidini, bali pia ya kuwapa watoto wake maagizo kwa kutumia mamlaka yake katika nafasi ya malimwengu, inapotakiwa kuhukumu juu ya matumizi ya kanuni hizo katika mazingira halisi [58].
Hatua kwa hatua
86. Hawakosekani watu wenye ukarimu wa pekee ambao, wakikabiliana na mazingira ambapo madai ya haki hayatekelezwi au yanatekelezwa kwa kiwango kisicho cha kutosha, wanajisikia kuwaka tamaa ya kurekebisha, wakivuka awamu zote kwa hatua moja tu; kana kwamba wangetaka kutumia kitu kinachoweza kufanana na mapinduzi.
Isisahaulike kuwa kufanya mambo hatua kwa hatua ni sheria ya maisha katika sehemu zake zote; kwa sababu hiyo hata katika taasisi za kibinadamu haiwezekani kuboresha mambo ila kwa kufanya kazi ndani yake hatua kwa hatua.
“Wokovu na haki vinapatikana si katika mapinduzi – alitangaza Pius XII – bali katika mabadiliko ya polepole yanayopangwa kwa pamoja. Mabavu, kazi yake daima ni kubomoa si kujenga; kuwasha tamaa, si kuzituliza; kulimbikiza chuki na uharibifu, si kuwafanya maadui kuwa ndugu; na yaliwapeleka watu na vyama vya kisiasa katika hitaji zito la kujenga tena polepole, baada ya majaribu makali, juu ya magofu ya ugomvi” [59].
Kazi kubwa sana
87. Kuna kazi kubwa sana juu ya watu wote wenye mapenzi mema: kazi ya kurudisha mahusiano ya maisha ya kawaida ya wanadamu katika ukweli, katika haki, katika upendo, katika uhuru: mahusiano ya maisha ya kawaida ya wanadamu kati ya watu binafsi; kati ya raia na jumuiya zao za kisiasa; kati ya jumuiya zenyewe za kisiasa kati yao; kati ya watu binafsi, familia, taasisi za kati na jumuiya za kisiasa, kwa upande mmoja, na jumuiya ya dunia nzima, kwa upande mwingine. Hii ni kazi nzuri sana, sawa na ile ya kutekeleza amani ya kweli katika utaratibu uliowekwa na Mungu.
88. Bila shaka, kulingana na ukubwa wa hitaji, wanaofanya hiyo kazi ya kutengeneza upya mahusiano ya maisha ya kijamii kadiri ya vigezo vilivyodokezwa hapo juu si wengi; iwaendee pongezi yetu ya kibaba, na uwaendee mwaliko wetu wenye nguvu wa kukazana katika kazi yao kwa ari mpya daima. Na linatufariji tumaini kwamba idadi yao itaongezeka, hasa kati ya waamini. Ni amri katika kuwajibika; ni dai katika upendo. Kila mwamini, katika dunia yetu hii, anatakiwa kuwa cheche ya nuru, mahali pa upendo, chachu inayoleta uhai katika umati wa watu: na atakuwa hivyo kweli, akizidi, rohoni mwake, kuishi katika ushirika na Mungu.
Maana, hakuna amani kati ya wanadamu kama amani haimo ndani ya kila mmoja wao, yaani kama kila mmoja hazitii ndani yake taratibu zinazotakwa na Mungu. “Nafsi yako – anajiuliza Mt. Augustino – inataka kushinda tamaa zako mbaya? Imtii yule aliye juu na itakishinda kilicho chini. Na ndani yako mtakuwa na amani: ya kweli, ya uhakika, iliyoratibika vizuri sana. Ni upi utaratibu wa amani hiyo? Mungu huiamuru nafsi, nafsi huuamuru mwili; hakuna kitu kilichoratibika vizuri zaidi” [60].
Mfalme wa amani
89. Maneno yetu haya, ambayo tulitaka kuyaelekeza kwenye matatizo yanayoisumbua zaidi familia ya wanadamu, katika wakati wa sasa, na ambayo – katika utatuzi wake – yanategemea maendeleo sahihi ya jamii, ni maneno ambayo yanatoka katika tamaa ya moyoni ya watu wote wenye mapenzi mema: yaani, uimarishaji wa amani duniani.
Kama wakili wa yule ambaye habari ya kinabii inamwita Mfalme wa amani (taz. Isa 9:6) – hata kama tunajisikia mdogo mno na kwamba hatustahili – Sisi tuna wajibu wa kutumia nguvu zetu zote kwa kuimarisha amani hiyo. Lakini amani inabaki tu sauti ya maneno, kama haikai juu ya utaratibu ule ambao Ensiklika hii imeeleza kwa tumaini lenye imani: utaratibu wenye msingi katika haki, upatao uhai kutoka kwa upendo na utekelezwao katika uhuru.
90. Hii ni kazi ambayo ni nzuri na kubwa kiasi kwamba nguvu za kibinadamu haziwezi peke yake kufanikisha, hata kama zinasukumwa na mapenzi mema ya kusifiwa. Ili jamii ya wanadamu iwe kioo safi inayoakisi vizuri Ufalme wa Mungu, msaada kutoka juu unahitajika. Kwa sababu hiyo, dua zetu, siku hizi takatifu, zinapanda kwa ari zaidi kwa yule aliyeshinda dhambi katika mateso na kifo chake – dhambi ambayo inasambaratisha watu na kuleta misiba, fitina na utosawa – kwake Yeye ambaye amewapatanisha wanadamu na Baba wa mbinguni katika damu yake: “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja… Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu” (Efe 2:14.17).
Na kwenye Liturujia ya siku hizi inaimbwa habari: “Bwana wetu Yesu Kristo baada ya kufufuka akakaa katikati ya wanafunzi wake na kusema: Amani iwe kwenu. Na wanafunzi walifurahi walipomwona Bwana” [61]. Yeye anatupa amani, yeye analeta amani: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” (Yn 14:27). Hii ndiyo amani tunayoiomba kwake kwa maombi yetu yenye uchaji.
91. Aweke mbali na moyo wa watu yale yanayoihatarisha; na awageuze watu, wawe mashahidi wa ukweli, haki, na upendo wa kindugu. Awaangaze viongozi wa mataifa, ili pamoja na kujali ustawi wa raia wao walinde na kutetea tunu kubwa ya amani; auchochee utashi wa wote ili kuvuka mipaka inayotenganisha, ili kukuza vifungo vya upendano, ili kuwaelewa wengine, ili kuwasamehe wale waliotenda maovu; kwa sababu ya nguvu ya amani mataifa yote ya dunia yawe kama ndugu na ndani yao ikue na itawale daima amani inayotamaniwa sana.
Ndugu (Maaskofu) Waheshimiwa, nina furaha ya kuwapa ninyi na Mapadre wa Majimbo na wa Mashirika na Waamini wa Majimbo yenu, hasa wale watakaofanya bidii zote ili kutekeleza mafundisho yetu, baraka ya kitume, inayoleta neema za mbinguni, kama dhamana ya amani hii na kwa nia ya kwamba itang’aa katika jumuiya za kikristo mlizokabidhiwa, hasa kwa faida ya walio wanyonge zaidi na wenye kuhitaji zaidi msaada na ulinzi. Hatimaye, kwa watu wote wenye mapenzi mema, ambao wao nao ni walengwa wa Ensiklika yetu hii, tunaomba sana kutoka kwa Mungu aliye juu afya na usitawi wa maisha.
Imetolewa huku Roma, kwenye Kanisa la Mt. Petro, katika Karamu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tarehe 11 Aprili 1963, mwaka wa tano wa Upapa wetu.
YOHANE XXIII
Tanbihi
[1] LATIN TEXT: Acta Apostolicae Sedis, 55 (1963), 257-304.
ENGLISH TRANSLATION: The Pope Speaks, 9 (1963), 13-48.
ITALIAN TRANSLATION: L’Osservatore romano, 11 aprile 1963; La Civiltà cattolica, 114(1963), II, 105ss.
[2] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24; and John XXIII's sermon, Jan. 4, 1963, AAS 55 (1963) 89-91.
[3] Cf. Pius XI's encyclical letter Divini Redemptoris, AAS 29 (1931) 78; and Pius XII's broadcast message, Pentecost, June 1, 1941, AAS 33 (1941) 195-205.
[4] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24.
[5] Divinae Institutiones, lib. IV, c.28.2; PL 6.535.
[6] Encyclical letter "Libertas praestantissimum," Acta Leonis XIII, VIII, 1888, pp. 237-238.
[7] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24.
[8] Cf. Pius XI's encyclical letter Casti connubii, AAS 22 (1930) 539-592, and Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24.
[9] Cf. Pius XII's broadcast message, Pentecost, June 1 ,1941, AAS 33 (1941) 201.
[10] Cf. Leo XIII's encyclical letter Rerum novarum, Acta Leonis XIII, XI, 1891, pp. 128-129.
[11] Cf John XXIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 422.
[12] Cf. Pius XII's broadcast message, Pentecost, June 1, 1941, AAS 33 (1941) 201.
[13] John XXIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 428.
[14] Cf. ibid., p. 430; TPS v. 7, no. 4, p. 318.
[15] Cf. Leo XIII's encyclical letter Rerum novarum, Acta Leonis XIII, XI, 1891, pp. 134-142; Pius XI's encyclical letter Quadragesimo anno, AAS 23 (1931) 199-200; and Pius XII's encyclical letter Sertum laetitiae, AAS 31 (1939) 635-644.
[16] Cf. AAS 53 (1961) 430.
[17] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1952, AAS 45 (1953) 36-46.
[18] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1944, AAS 37 (1945) 12.
[19] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 21.
[20] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 14.
[21] Summa Theol. Ia-IIae, q. 19, a.4; cf. a.9.
[22] In Epist. ad Rom. c. 13, vv. 1-2, homil. XXIII; PG 60. 615.
[23] Leo XIII's encyclical epistle Immortale Dei, Acta Leonis XIII, V, 1885, p. 120.
[24] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1944, AAS 37 (1945) 15.
[25] Cf. Leo XIII's encyclical epistle Diutumum illud, Acta Leonis XIII, 11, 1881, p. 274.
[26] Cf. ibid., p. 278; also Leo XIII's encyclical epistle Immortale Dei, Acta Leonis XIII, V, 1885, p. 130.
[27] Summa Theol. Ia-IIae, q. 93., a.3 ad 2um; cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1945, AAS 37 (1945) 5-23.
[28] Cf. Leo XIII's encyclical epistle Diuturnum illud, Acta Leonis XIII, II, 1881, pp. 271-273; and Pius XII's broadcast message, Christmas 1944, AAS 37 (1945) 5-23.
[29] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 13, and Leo XIII's encyclical epistle Immortale Dei, Acta Leonis XIII, V, 1885, p. 120.
[30] Cf. Pius XII's encyclical letter Summi Pontificatus, AAS 31 (1939) 412-453.
[31] Cf. Pius XI's encyclical Mit brennender Sorge, AAS 29 (1937) 159, and his encyclical letter Divini Redemptoris, AAS 29 (1937) 65-106.
[32] Leo XIII's encyclical letter Immortale Dei." Acta Leonis XIII, V, 1885, p. 121.
[33] Cf. Leo XIII's encyclical letter Rerum novarum, Acta Leonis XIII, XI, 1891, pp. 133-134.
[34] Cf. Pius XII's encyclical letter Summi Pontificatus, AAS 31 (1939) 433.
[35] AAS 53 (1961) 417.
[36] Cf. Pius XI's encyclical letter Quadragesimo anno, AAS 23 (1931) 215.
[37] Cf. Pius XII's broadcast message, Pentecost, June 1, 1941, AAS 33 (1941) 200.
[38] Cf. Pius XI's encyclical letter Mit brennender Sorge, AAS 29 (1937) 159, and his encyclical Divini Redemptoris, AAS 29 (1937) 79; and Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24.
[39] Cf. Pius XI's encyclical letter Divini Redemptoris, AAS 29 (1937) 81, and Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 9-24.
[40] John XXIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 415.
[41] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 21.
[42] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1944, AAS 37 (1945) 15-16.
[43] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1942, AAS 35 (1943) 12.
[44] Cf. Leo XIII's apostolic letter Annum ingressi, Acta Leonis XIII, XXII, 1902-1903, pp. 52-80.
[45] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1941, AAS 34 (1942) 16.
[46] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1940, AAS 33 (1941) 5-14.
[47] De civitate Dei, lib. IV, c. 4; PL 41. 115; cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1939, AAS 32 (1940) 5-13.
[48] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1941, AAS 34 (1942) 10-21.
[49] Cf. John XIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 439.
[50] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1941, AAS 34 (1942) 17, and Benedict XV's exhortation to the rulers of the belligerent powers, August 1, 1917, AAS 9 (1917) 418.
[51] Cf. Pius XII's broadcast message, August 24, 1939, AAS 31 (1939) 334.
[52] AAS 53 (1961) 440-441.
[53] Cf. Pius XII's broadcast message, Christmas 1941, AAS 34 (1942) 16-17.
[54] John XXIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 443.
[55] Cf. Pius XII's address to Young Members of Italian Catholic Action, Rome, Sept. 12, 1948, AAS 40 (1948) 412.
[56] Cf. John XXIII's encyclical letter Mater et Magistra, AAS 53 (1961) 454.
[57] Ibid., p. 456.
[58] Ibid., p. 456; cf. Leo XIII's encyclical epistle Immortale Dei, Acta Leonis XIII, V, 1885, p. 128; Pius XI's encyclical letter Ubi arcano, AAS 14 (1922) 698; and Pius XII's address to the Union of International Sodalities of Catholic Women, Rome, Sept. 11, 1947, AAS 39 (1947) 486. AAS 39 (1947) 486.
[59] Cf. Pius XII's address to Italian workers, Rome, Pentecost, June 13, 1943, AAS 35 (1943) 175.
[60] Miscellanea Augustiniana . . . St. Augustine, Sermones post Maurinos reperti, Rome, 1930, p. 633.
[61] Responsory at Matins, Feria VI Within the Octave of Easter.
© Copyright 1963 - Libreria Editrice Vaticana
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana