UFASIRI WA BIBLIA Ufasiri wa matini za Biblia unaendelea kuwa jambo linalovutia sana hadi siku za leo, ukisababisha majadiliano ya motomoto ambayo katika miaka hii ya mwisho yamechukua pia sura mpya. Kwa sababu ya umuhimu wa kimsingi wa Biblia kwa ajili ya imani ya kikristo, kwa maisha ya Kanisa na kwa mahusiano baina ya wakristo na waamini wa dini nyingine, basi Tume ya Kipapa ya Biblia imehimizwa kutoa maoni yake mintarafu mada hiyo.
Suala la ufasiri wa Biblia si uvumbuzi wa nyakati zetu, kama pengine inavyodaiwa. Biblia yenyewe yathibitisha kuwa ufasiri wake unaleta magumu mbalimbali. Maana, pamoja na sehemu zake zinazoeleweka kwa dhahiri zimo nyingine zisizoeleweka vizuri. Mathalani, Danieli anaposoma sehemu kadhaa za kitabu cha Yeremia alikuwa akijihoji kwa kirefu kuhusu maana yake (Dan 9:2). Tena, kadiri ya Matendo ya Mitume, mtu wa Kushi wa karne ya kwanza alikuwa katika hali ileile mintarafu sehemu fulani ya kitabu cha Isaya (Isa 53:7-8), akitambua kwamba anahitaji msaada wa mwenye kumfasiria (Mdo 8:30-35). Na hatimaye Waraka wa pili wa Petro unashuhudia kwamba “hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu” (2Pet 1:20); na tena, kwa upande mwingine, unasisitiza kuwa katika nyaraka za Mtume Paulo “yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe” (2Pet 3:16). Hivyo, suala hilo ni la zamani, lakini katika mfululizo wa nyakati suala hilo limekithiri: maana, karne ishirini ama thelathini zamtenganisha tayari msomaji na matukio na misemo vinavyosimuliwa katika Biblia; na hilo halina budi kuleta magumu mbalimbali. Kwa upande mwingine, kwa sababu ya maendeleo ya sayansi za kibinadamu, masuala yahusuyo ufasiri yamekuwa tata zaidi katika nyakati za leo. Mbinu kadhaa za kisayansi zimekamilishwa kwa ajili ya utafiti juu ya matini za kale. Sasa je, kwa kiasi gani mbinu hizo zaweza kutazamwa kuwa zinaufaa ufasiri wa Maandiko Matakatifu? Kwa muda mrefu busara ya kichungaji ya Kanisa imelijibu swali hilo kwa utaratibu sana, kwa sababu mara nyingi mbinu hizo (ingawa zina mazuri yanayokubaliwa ndani yake) zilikuwa zinafungamana na rai zilizo kinyume cha imani ya kikristo. Ila maendeleo mazuri yamefanyika, yenye hatua maalum katika mfululizo wa hati za Mababa Watakatifu, kuanzia na ensiklika Providentissimus Deus ya Leo XIII (18 Novemba 1893) hadi ensiklika Divino afflante Spiritu ya Pius XII (30 Septemba 1943). Tena maendeleo hayo yamethibitishwa na tamko Sancta Mater Ecclesia (21 Aprili 1964) la Tume ya Kipapa ya Biblia, na hususan na hati ya kidogma Dei Verbum ya Mtaguso Mkuu wa Vatikano II (18 Novemba 1965). Hivyo, mwelekeo huo wenye kujenga unaleta na kuonyesha wazi matunda yake. Mitaala ya kibiblia imehimizwa sana katika Kanisa Katoliki na thamani yake ya kisayansi imegunduliwa zaidi na zaidi kati ya wasomi na waamini. Dialogia ya kiekumeni imerahisishwa sana. Biblia imezidi kuathiri theolojia, na kutoa mchango wake kwa upyaisho wa theolojia. Shauku ya Biblia imeongezeka kati ya wakatoliki, ikiyasaidia maendeleo ya maisha ya kikristo. Nao wote waliopata mafunzo madhubuti katika uwanja huo hudhani kuwa sasa haiwezekani kuirudia tena awamu ya ufasiri wa maandishi iliyotangulia ile ya kiuhakiki. Maana hao hutazama awamu iliyotangulia kama isiyotosheleza tena. Lakini, pindi mbinu ya kisayansi iliyosambaa zaidi – yaani mbinu ya “kihistoria-kiuhakiki” – inapotumika kwa kawaida katika ufafanuzi, hata ule wa kikatoliki, papo hapo mbinu hii inajadiliwa tena, na kutiliwa mashaka: kwa upande mmoja katika mazingira ya kisayansi, kwani mbinu na njia nyingine zimejitokeza; kwa upande mwingine, kwa sababu ya malalamiko ya wakristo wengi wanaodhani kuwa mbinu hii haitoshelezi kwa upande wa imani. Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, linavyoeleza jina lake lenyewe, inazingatia hasa mabadiliko ya kihistoria ya matini mbalimbali au ya mapokeo yake katika mfululizo wa nyakati – utaratibu huu huitwa “diakronia”. Lakini katika mahali na mazingira fulani mbinu hii inashindana siku hizi na mbinu nyingine zinazosisitiza umuhimu wa kuzielewa matini mbalimbali kwa kuzitazama kwa jumla katika fani yake – utaratibu huu huitwa “sinkronia”, uwe kuhusu lugha yake, ama utungaji, ama muundo wa masimulizi, ama, tena, juhudi yake ya kushawishi. Na tena, mbinu za kidiakronia hujishughulisha kuielewa historia ya utungaji wa matini katika nyakati zilizopita. Lakini badala yake siku hizi walio wengi wanapendelea kuzihoji matini zenyewe wakiziweka katika mtazamo wa nyakati za sasa: yaani mtazamo wa kifalsafa, kiudodosinafsi, kisosholojia, kisiasa, n.k. Wingi huo wa mbinu na njia huthaminiwa na wengine kama dalili ya utajiri, Lakini wengine bado wanauelewa kama sababu ya fujo kubwa. Nayo fujo – iwe ya kweli au ya kusingizia – inawaletea hoja mpya wapinzani wa ufafanuzi wa kisayansi. Kwao, mgongano huo wa fasiri mbalimbali huonyesha kwamba hakuna faida yoyote itokanayo katika kuzipitisha matini za Biblia chini ya madai ya mbinu za kisayansi, kinyume chake kuna hasara kubwa. Tena hawa husisitiza kuwa ufafanuzi wa kisayansi matokeo yake ni kuzusha mashaka na wasiwasi kuhusu vipengele vingi ambavyo kwanza vilikuwa vimekubalika kwa amani. Na wakati huohuo wafafanuzi wengi hushawishiwa kuyakubali maoni yanayopingana na imani ya Kanisa mintarafu masuala makuu sana, kama vile kuchukuliwa mimba kwa Yesu na Mama Bikira, miujiza yake Yesu na pia ufufuko wake na umungu wake. Na ufafanuzi wa kisayansi, hata pale ambapo hauleti mashaka haya, kwa vyovyote, kadiri ya wengine, ni mtindo usiozaa chochote kuhusu mafanikio ya maisha ya kikristo. Badala ya kufungua mlango wa kuingia kwa urahisi na uhakika zaidi katika chemchemi zilizo hai za Neno la Mungu, unaifanya Biblia kuwa kitabu kilichofungwa, ambacho ufasiri wake daima ni mgumu na wenye kudai utaalamu wa hali ya juu. Hivyo ufasiri wa Biblia unakuwa mada kwa ajili ya wataalamu wachache waliobobea. Wengine wanawabandikia hao msemo ule wa Injili, “Mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia” (Lk 11:52; taz. Mt 23:13). Kutokana na hayo, yadhaniwa kuwa ni lazima nafasi ya ufafanuzi wa kisayansi – ulio kazi nzito na ya saburi – ichukuliwe na mbinu nyingine zilizo sahili zaidi, kama vile mojawapo ya mbinu za kisinkronia zinazotazamwa kuwa zatosha. Au pengine yashauriwa kuwa bora ule ufasiri wa Biblia uitwao “wa kiroho”, yaani usomaji unaoongozwa tu na kariha (inspiration) ya kila mmoja binafsi na wenye lengo la kuilisha kariha hiyo tu. Wengine wanatafuta katika Biblia hasa picha fulani ya Kristo kadiri ya maoni yao binafsi, na kuridhisha kwa hisia zao binafsi za kidini. Na wengine tena wanadai kuyapata moja kwa moja katika Biblia majawabu kwa kila swali la kibinafsi ama la kijumuiya. Aidha ni vingi vidhehebu vinavyodai kuwa ni wa kweli ufasiri wa aina moja tu, nao ndio unaopatikana kwa njia ya ufunuo wao binafsi.
Kwa sababu hizo, yafaa kuvichunguza kwa makini vipengele mbalimbali vya ufasiri wa kibiblia vilivyopo hadi leo; tena kuzingatia upinzani, malalamiko na matarajio yanayotolewa kuhusu suala hilo; kutathmini fursa zinazofunguliwa na mbinu na njia mpya; na hatimaye kujaribu kuueleza wazi uelekeo unaowiana zaidi na utume wa ufafanuzi katika Kanisa Katoliki. Hayo ndiyo madhumuni ya hati hii. Tume ya Kipapa ya Biblia inataka kuzionyesha njia za kupitia ili kuufikia ufasiri wa Biblia ulio aminifu zaidi kwa maumbile yake ya kibinadamu na ya kimungu kwa pamoja. Hati hii haijidai kuamua mintarafu masuala yote yahusuyo Biblia, kama vile, k.m., theolojia ya uvuvio. Bali Tume hiyo inadhamiria kueleza zile mbinu zinazoweza kusaidia kwa manufaa ili kuuthamini utajiri wote uliopo katika matini za Biblia, kusudi Neno la Mungu lipate kuwa zaidi na zaidi chakula cha kiroho kwa wanashirika wa taifa lake; tena liwe kwao chemchemi ya maisha ya imani, tumaini na upendo, na hivyo kuwa pia nuru kwa wanadamu wote (Taz. Dei Verbum,21). Ili kuifikia shabaha hiyo, hati hii: 1. itaeleza kwa kifupi mbinu na njia[1] mbalimbali zinazotumika, pamoja na kuonyesha msaada zinaotoa na mipaka yake; 2. itachunguza masuala kadhaa ya hemenetiki; 3. itatafakari juu ya vipengele vilivyo maalum vya ufasiri wa kikatoliki wa Biblia na uhusiano wake na fani nyingine za kitheolojia; 4. hatimaye itazingatia nafasi ambayo ufasiri wa Biblia unashika katika maisha ya Kanisa. I. A. Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ni mbinu ya lazima kwa ajili ya uchambuzi wa kisayansi wa maana ya matini za kale. Maadam Maandiko Matakatifu – yaliyo “Neno la Mungu katika lugha ya kibinadamu” – yametungwa na watunzi wa kibinadamu katika sehemu zake zote na machimbuko yake yote, ufahamu wake sahihi unakubali utumiaji wa mbinu hii kama halali, unauhitaji, na tena zaidi, unaudai. Ili kuitathmini sawasawa mbinu hii katika hali yake ya sasa, yafaa kutupa jicho katika historia yake. Baadhi ya vipengele vya mbinu hii ya kiufasiri ni vya kale sana. Tangu zamani vilitumika na wafafanuzi wa kigiriki kwa kufasiri maandishi ya fasihi bora ya Kigiriki na Kilatini (classical literature); na baadaye, wakati wa Mababa wa Kanisa, vikatumika na waandishi kama Orijene, Yeronimo na Augustino. Lakini wakati huo mbinu yenyewe ilikuwa haijakamilishwa. Miundo yake ya siku za leo ni matokeo ya ukamilishaji uliofanyika hasa kuanzia zama za wahumanisti wa “Mwamsho wa elimu mpya” (Renaissance humanists) kwa njia ya utaratibu walioanzisha wa kuyarudia machimbuko ya maandishi asilia (recursus ad fontes). Hivyo, ingawa uhakiki wa matini za Agano Jipya ulijiendeleza kama fani ya kisayansi kuanzia tu karne ya 19, yaani wakati ulipojitenga na textus receptus (yaani, matini zilizokubalika kimapokeo), kumbe uhakiki wa kifasihi(au wa maandishi) chanzo chake kinapatikana kuanzia karne ya 17, kwa uvumbuzi wa Richard Simon. Msomi huyo alionyesha kwamba katika vitabu vya Pentateuko kuna masimulizi yanayorudiwa mara mbili, tena kuna hitalafu katika maudhui yake, pamoja na tofauti za mtindo wa ufasaha. Basi hayo yote yalionekana kuwa hayapatani kirahisi na wazo la kuwa mtunzi wa vitabu hivyo ni mtu mmoja tu, yaani Musa. Katika karne ya 18 Jean Astruc alijaribu kutoa sababu kwamba Musa alitumia machimbuko mengi (hasa mawili muhimu zaidi) ili kutunga kitabu cha Mwanzo; lakini baadaye uhakiki ukapinga zaidi na zaidi wazo la kuwa Musa mwenyewe ndiye mtunzi wa Pentateuko. Nao uhakiki wa kifasihi kwa muda mrefu ukafanya bidii kwa lengo la kupambanua machimbuko mbalimbali ya matini. Hivyo, katika karne 19 ikakamilishwa nadharia iliyoitwa “ya kihati” (documentary hypothesis) kwa minajili ya kueleza uhariri wa Pentateuko. Kadiri ya nadharia hiyo, ndani ya Pentateuko zimechangamana hati nne, ambazo kwa sehemu zinafanana; nazo zaitwa ile ya kiYahvisti (J); ile ya kiElohisti (E), ile ya kiDeuteronomisti (D), na ile ya kikuhani (P: kutoka Kijerumani “Priester”). Mintarafu hati hii ya kikuhani huenda aliitumia mhariri wa mwisho ili kuzifunganisha hati zote kwa pamoja. Kwa njia inayofanana, ulielezwa pia utungaji wa Injili ndugu tatu (Sinoptiki), ambazo ndani yake zina mambo mengine yanayolingana, na mengine yanayohitilafiana. Hivyo imebuniwa nadharia iitwayo ya “machimbuko asilia mawili” (“two source” hypothesis), ambayo kadiri yake Injili za Mathayo na Luka huenda zilitungwa kutokana na machimbuko mawili ya msingi: yaani, kwa upande mmoja, Injili ya Marko, na, kwa upande mwingine, mkusanyo fulani wa maneno ya Yesu (uitwao Q, kutoka katika Kijerumani Quelle, m.y. “chimbuko”). Katika kiini chake, nadharia hizi mbili zinatumika bado hadi leo katika ufafanuzi wa kisayansi, ijapokuwa zinaleta ubishi. Kwa kutarajia kuweka sawa mfuatano wa matini za Biblia kadiri ya wakati wa utungaji wake, uhakiki wa kifasihi ulifanya kazi tu ya kuzitenga sehemu mbalimbali za matini na kuzichambua, ili kupambanua machimbuko yake. Katika harakati hiyo uhakiki ulikuwa hauzingatii kwa kutosha muundo wa mwisho wa matini yenyewe ya Biblia, na pia ujumbe inaoueleza katika hali yake ya mwisho (yaani kazi ya wahariri ilithaminiwa kidogo tu). Kwa sababu hiyo ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki uliweza kuonekana kama mbinu yenye kupindua na kudhuru matini, hasa kwa sababu baadhi ya wafafanuzi wa wakati huo walikuwa wanatoa maoni yenye kukanusha Biblia. Maana waliathiriwa na mbinu za historia linganishi ya dini mbalimbali – kama zilivyotekelezwa wakati huo – na pia na dhana za kifalsafa. Hermann Gunkel aliondoa mbinu hii katika mipaka finyu ya uhakiki wa kifasihi wenye mtazamo wa namna hii. Naye, ijapo aliendelea kuvitazama vitabu vya Pentateuko kama mikusanyo ya hati, alifanya utafiti kuhusu mfumo wa pekee wa vifungu vyake mbalimbali akijaribu kuainisha utanzu wa kila kimoja (k.m. “hadithi” au “utenzi”), pia mazingira asilia au Sitz im Leben (k.m. mazingira ya kisheria, ya kiliturujia, n.k.). Na utafiti huo kuhusu tanzu za fasihi ukaunganika na “uchambuzi wa kiuhakiki wa fani” (Formgeschichte) uliozinduliwa na Martin Dibelius na Rudolf Bultmann katika ufafanuzi wa Injili ndugu (Sinoptiki). Naye Bultmann alichanganya mitaala hiyo ya “Formgeschichte” na hemenetiki ya Biblia iliyoathiriwa na falsafa ya “ki-eksistensialisti” ya Martin Heidegger. Matokeo yake yakawa kwamba mbinu ya Formgeschichte ikazusha mara nyingi mashaka mazito. Lakini mbinu hiyo, kwa yenyewe, ilileta matokeo ya kuonyesha kinaganaga zaidi kwamba mapokeo yaliyorekodiwa katika Agano Jipya yamepata asili yake na muundo wake wa msingi katika jumuiya ya kikristo, yaani Kanisa la mwanzoni; na hapo ndipo mahubiri ya Yesu mwenyewe yalipoingia katika mahubiri (ya mitume) yanayotangaza kuwa Yesu ndiye Kristo. Aidha, baada ya Formgeschichte ilijitokeza mbinu ya Redaktionsgeschichte, yaani “uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri”. Hiyo mbinu inajaribu kuuvumbua mchango wa binafsi ulioletwa na kila mwinjili, na mawaidha ya kitheolojia yaliyoongoza kazi yake ya uhariri. Hivyo, kwa kutumia mbinu hii ya mwisho, mfululizo wa hatua mbalimbali za mbinu ya kihistoria-kiuhakiki umekamilika zaidi: toka uhakiki wa matini tunaingia uhakiki wa kifasihi unaoyagawa maandishi yenyewe ili kutafuta machimbuko yake; kishapo tunaingia uchambuzi wa kiuhakiki wa tanzu, na hatimaye uchanganuzi wa uhariri ambao unaizingatia matini katika utungaji wake. Hivyo basi, imewezekana kuelewa wazi zaidi azma ya watunzi na wahariri wa Biblia, kama vile ujumbe wao kwa walengwa wa kwanza. Ndiyo sababu mbinu ya kihistoria-kiuhakiki imejipatia nafasi muhimu sana hadi leo. Kanuni za msingi za mbinu ya kihistoria-kiuhakiki katika muundo wake halisi ndizo zifuatazo: Ni mbinu ya kihistoria, si tu kwa sababu inaelekea matini za kale – na hapa inazungumziwa Biblia – na kutafiti maana yake ya kihistoria; bali hasa kwa sababu inajaribu kugundua kwa dhahiri michakato ya kihistoria ya utungaji wa matini za Biblia; nayo ni michakato ya kidiakronia ambayo pengine imetatizwa kwa sababu ya kuchukua muda mrefu. Na matini hizo za Biblia, katika hatua mbalimbali za utungaji wake, ziliwaelekea wasikilizaji au wasomaji wa jamii mbalimbali, walioishi katika mazingira tofauti ya mahali na nyakati. Ni mbinu ya kiuhakiki, kwa maana katika kila hatua yake inatenda kazi kwa msaada wa vigezo vya kisayansi vilivyo halisi iwezekanavyo (kuanzia hatua ya uhakiki wa matini hadi uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri); nayo mbinu inadhamiria kumwezesha msomaji wa nyakati zetu kuelewa maana ya matini za Biblia, ambayo mara nyingi ni vigumu kuipata. Maadamu ni mbinu ya uchanganuzi wa kisayansi, inachunguza matini ya Biblia kama ifanyavyo kwa matini nyingine zozote za kale na kuieleza kama ufasaha wa kibinadamu. Lakini, hata hivyo inamsaidia mfafanuzi kuelewa vizuri zaidi maudhui ya ufunuo wa kimungu, hususan kwa njia ya uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri wa matini. Katika awamu ya sasa ya maendeleo yake, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki inapitia hatua hizo zifuatazo: Uhakiki wa matini – unavyofanyika tangu muda mrefu zaidi – unafungua mfululizo wa kazi za kisayansi. Unazingatia ushuhuda wa miswada (manuscripts) iliyo ya kale zaidi na bora zaidi, na pia wa papiri, pia wa tafsiri za kale na wa Mababa wa Kanisa. Tena, ikifuata kanuni maalum, inafanya bidii kutambua matini ya Biblia inayokaribia zaidi ile ya asili. Aidha matini inafanyika utafiti kiisimu (wa kimofolojia na wa kisintaksi) na kisemantiki, unaotumia maarifa yatokanayo na mitaala ya filolojia ya kihistoria. Ndipo uhakiki wa maandishi unapojibidisha kugundua katika matini mwanzo na \mwisho wa kila sehemu yenye umoja ndani yake, iwe ndefu ama fupi; tena unanuia kuhakikisha mshikamano (internal coherence) uliomo ndani ya matini. Na pengine kuna masimulizi yanayorudia mara mbili, ama tofauti zisizopatana kati yake, na dalili nyingine za namna hii; hayo yote huonyesha kuwa baadhi ya matini zimechanganya pamoja hati mbalimbali. Hivyo hizo matini zinagawanywa katika sehemu ndogo zenye umoja kati yake, na hizo sehemu zinapelelezwa mintarafu machimbuko yanayoweza kuwa asili yake. Halafu juhudi za uhakiki wa tanzu zinaelekea kutambua tanzu za fasihi na mazingira zilimochipuka, tena tabia maalum ya kila utanzu, na historia ya mabadiliko yake. Kisha, uhakiki wa mapokeo inazitia matini katika mikondo ya mapokeo ambayo inachunguzwa nao ili maendeleo yake katika mtiririko wa historia yaeleweke. Na hatimaye uhakiki wa uhariri unatafiti mabadiliko yaliyoletwa kabla ya hizo matini kupata sura yake ya mwisho, na kisha unachambua sura hiyo ya mwisho ukijitahidi kupambanua maelekeo yake maalum. Kwa hiyo, kati ya hatua hizo zote, zile za kwanza zinafanya bidii ili kuifafanua matini pamoja na asili yake, kwa mtazamo wa kidiakronia; lakini hatua hiyo ya mwisho inamalizia kwa uchunguzi wa kisinkronia: yaani inafafanua matini kwa yenyewe, kwa kuzingatia mahusiano yaliyopo kati ya sehemu zake mbalimbali; na mwishowe huizingatia kama ujumbe kwa watu wa nyakati zake. Na hapo ndipo yaweza kuchunguzwa dhima ya matini ya kuathiri kiutendaji (function pragmatique). Ikiwa matini zinazochambuliwa zinaingia katika utanzu wa kifasihi ulio wa kihistoria, ama zinahusiana na matukio ya historia, uhakiki wa kihistoria yatimiliza kazi ya uhakiki wa kifasihi kwa kueleza vizuri uzito wake wa kihistoria, kadiri ya maana ya kisasa ya usemi huo. Basi, kwa njia hii zaangazwa hatua mbalimbali za maendeleo halisi ya ufunuo wa kibiblia. Je, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ina thamani ipi, hasa katika awamu ya sasa ya maendeleo yake? Ni mbinu ambayo, ikitumika kwa namna iliyo nyofu, haina kisamkasa (a priori) kwa yenyewe. Ila kama matumizi yake yanaandamana na kisamkasa, hilo basi halitokani na mbinu yenyewe, bali na maamuzi na kihemenetiki yanayouongoza ufasiri, nayo yaweza kuwa ya mapendeleo. Katika asili yake mbinu hii ilielekezwa kwenye uhakiki wa machimbuko na kwenye historia ya dini mbalimbali; hivyo ikaleta matokeo ya kuufungua mlango mpya wa kuiendea Biblia, ikionyesha kuwa Biblia ni mkusanyo wa maandishi ambayo, ilivyo mara nyingi, hasa katika Agano la Kale, si kazi ya mwandishi mmoja; na pengine miswada yake ilipitia historia ndefu kabla haijafikia kuchukua sura yake ya mwisho. Na historia hiyo hufungamana kabisa na historia ya taifa la Israeli au ya Kanisa la mwanzoni. Kabla ya mbinu hii kutokea, ufasiri wa Biblia wa kiyahudi au wa kikristo ulikuwa haukuelewa kwa dhahiri mazingira halisi mbalimbali ya kihistoria ambamo Neno la Mungu lilitia mizizi yake. Ulikuwa ukiyaelewa kwa ujumla na kwa mbali. Na mapambano yakatokea baina ya ufafanuzi wa kimapokeo na mbinu ya kisayansi, nayo yakaleta maumivu; maana mwanzoni hiyo mbinu ya kisayansi ilikuwa imeachana kwa makusudi na mtazamo wa imani na pengine iliipinga imani. Lakini baadaye mbinu hiyo ikajionyesha kuwa ya kufaa: yaani ilipojiokoa na athari hizo za nje (external prejudices) ikaleta ufahamu sahihi zaidi wa ukweli wa Maandiko Matakatifu (taz. Dei Verbum, 12). Kadiri ya Divino afflante Spiritu, utafiti wa maana sisisi ya Maandiko ndio wajibu mahsusi wa ufafanuzi; lakini ili kuutekeleza huo wajibu inahitajika kuzipambanua tanzu za kifasihi za matini (Taz. Enchiridion Biblicum [=EB], 560); nalo, basi, lafanyika kwa njia ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki. Bila shaka, matumizi halisi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki huonyesha mipaka yake, maana hubana utafiti wa maana ya matini ya Biblia ndani ya mazingira ya kihistoria kwa wakati ilipotungwa, wala haijali uwezekano wa maana nyingine zilizojidhihirisha katika mihula iliyofuata ya ufunuo wa kibiblia na ya historia ya Kanisa. Japo hivyo, mbinu hii imechangia katika utungaji wa vitabu vya thamani kubwa vya ufafanuzi na vya theolojia ya kibiblia. Tangu muda mrefu limeachwa wazo la kufungamanisha mbinu hiyo na mfumo wa kifalsafa. Na hivi karibuni mwelekeo wa kiufafanuzi umejitokeza wenye kuielekeza mbinu hii ili izingatie hasa fani (form) ya matini kuliko maudhui (content) yake; lakini mwelekeo huo ulisahihishwa kwa msaada wa semantiki ya ngazi mbalimbali (semantiki ya maneno, ya sentensi na ya matini) na pia wa uchunguzi wa jinsi matini zinavyoathiri kiutendaji (aspect pragmatique). Aidha, mintarafu matumizi ya uchanganuzi wa kisinkronia wa matini ndani ya utaratibu wa mbinu hii, yatupasa tukubali kuwa ni kazi halali kwani kinachozingatiwa hapo ni matini katika hali yake ya mwisho, ambayo ndiyo yenye Neno la Mungu, wala si uhariri wa katikati. Lakini inabaki kuwa chunguzi za kidiakronia ni za lazima ili kufahamisha mkikimkiki wa kihistoria uliomo ndani ya Maandiko Matakatifu na kudhihirisha utajiri wa mchangamano wake: kwa mfano, kanuni ya Agano (Kut 21-23) huonyesha mazingira ya kisiasa, kijamii na kidini ya jamii ya kiisraeli yaliyo tofauti na yale yanayoonyeshwa na kanuni za sheria nyinginezo zihifadhiwazo katika Kumbukumbu la Torati (Kum 12-26) na katika Mambo ya Walawi (sheria za utakatifu, Law 17-26). Kumbe miaka ya nyuma mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ilikemewa kwa maana ilizingatia mno mandhari ya kihistoria katika ufafanuzi; lakini sasa yabidi kukwepa isiingie katika tabia iliyo kinyume ya kuusahau umuhimu wa historia na kuuzingatia ufafanuzi wa kisinkronia tu. Basi, kwa ujumla madhumuni ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ni kuipambanua maana iliyonuiwa na waandishi na wahariri hasa kwa utaratibu wa kidiakronia. Kwa msaada wa mbinu na njia nyinginezo, mbinu hiyo humfungulia msomaji wa nyakati zetu mlango wa kupata maana ya matini ya Biblia, tulivyoipokea sisi.
B. Mbinu mpya za uchanganuzi wa kifasihi Hakuna mbinu yoyote ya kisayansi kwa mtaala wa Biblia iwezayo kuudhihirisha utajiri wote wa matini za Biblia. Yoyote ile iwe thamani yake, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki haiwezi kudai kuyatosheleza masuala yote. Nayo kwa vyovyote huacha gizani masuala mengi yahusuyo maandishi yanayofanyiwa utafiti. Hivyo hatutashangaa tukiona kuwa siku hizi mbinu na njia nyinginezo hutolewa ili kuchimba zaidi masuala fulani fulani yastahiliyo kuchunguzwa kwa makini. Katika ibara hii B tutaeleza baadhi ya mbinu za uchanganuzi wa kifasihi zilizojitokeza hivi karibuni. Halafu katika ibara zifuatazo (C, D, E) tutazichunguza kwa kifupi njia mbalimbali, ambazo baadhi yake zahusiana na mtaala wa mapokeo, nyingine na “sayansi za kibinadamu”, na nyingine tena na mazingira maalumu ya kisasa. Na hatimaye (F) tutauzingatia usomaji wa kifundamentalisti wa Biblia unaokataa kila jitihada ya kimpangilio ya ufasiri. Hivi basi, ufafanuzi wa Biblia ukifaidi maendeleo ya mitaala ya kiisimu na kifasihi andishi ya nyakati zetu, hutumia zaidi na zaidi mbinu mpya za uchanganuzi wa kifasihi, na hasa uchanganuzi wa kibalagha, uchanganuzi wa kisimulizi, na uchanganuzi wa kisemiotiki. Kwa kusema ukweli, uchanganuzi wa kibalagha kwa wenyewe si mbinu mpya. Ila kilicho kipya ni, kwa upande mmoja, matumizi yake yenye utaratibu kwa ajili ya kuifasiri Biblia, na, kwa upande mwingine, kuchanua na kusitawi kwa “balagha mpya”. Balagha ni sanaa ya kutunga hotuba zenye kushawishi. Na kwa sababu maandishi yote ya Biblia ni kwa namna fulani matini zenye kushawishi, ujuzi fulani wa balagha ni sehemu mojawapo ya elimu ya kawaida ya wafafanuzi. Uchanganuzi wa kibalagha lazima uendeshwe kwa utaratibu wa kiuhakiki, kwa maana ufafanuzi wa kisayansi ni kazi ambayo haina budi kuyatii madai ya roho ya kiuhakiki. Chunguzi nyingi za siku za karibuni zimezingatia kwa makini kuwepo kwa balagha katika Maandiko. Inawezekana kuainisha njia tatu tofauti. Ya kwanza ina msingi katika balagha bora (classical rethoric) ya Kigiriki na ya Kilatini; ya pili hutazama taratibu za utungaji za kisemiti; na ya tatu hufuatilia tafiti za kisasa ziitwazo “balagha mpya”. Mazingira yoyote yale ya hotuba huleta kuwepo kwa mambo matatu: msemaji (au mwandishi), hotuba (au matini) na wasikilizaji (au walengwa). Hivyo yatokana kwamba balagha bora hutofautisha mambo matatu yenye kuchangia katika ufasaha wa hotuba: mamlaka ya mlumbaji, hoja zinazotolewa katika hotuba kwa kushawishi, na hisia zinazoamshwa katika wasikilizaji na hotuba yenyewe. Tofauti za mazingira na za walengwa huathiri sana mtindo wa kuongea. Kuanzia Aristotle, balagha bora yaainisha tanzu tatu za ufasaha: utanzu wa kihukumu (mbele ya mahakama), utanzu wa kimajadiliano (katika mikutano ya kisiasa), na utanzu wa kidhihirisho (katika ibada). Madhali balagha iliathiri sana utamaduni wa kiyunani, idadi inayozidi kuongezeka ya wafafanuzi hutumia vitabu vya balagha bora ili kuchambua vizuri zaidi mandhari kadhaa za maandishi ya kibiblia, hasa yale ya Agano Jipya. Aidha, wafafanuzi wengine huvitazama kwa makini vipengele mahsusi vya mapokeo ya kifasihi ya kibiblia. Nayo yakiwa yameasisiwa katika utamaduni wa kisemiti, huonyesha kupendelea sana mitungo ya kiurari, ambayo huweka mahusiano maalum kati ya sehemu mbalimbali za matini. Utafiti wa mitindo ya aina nyingi ya usambamba na wa taratibu nyingine za utungaji za kisemiti wawezesha kupambanua kinaganaga zaidi muundo wa kifasihi wa matini na hivyo kuufikia ufahamu mzuri zaidi wa ujumbe wake. Ikichukua mtazamo mpana zaidi, “balagha mpya” haitaki kuwa tu orodha ya tamathali za lugha, ya maarifa ya walumbaji, au ya mitindo ya hotuba. Mbinu hiyo inatafiti ni kwa sababu gani matumizi fulani ya lugha yalifikia lengo lililokusudiwa na kufaulu kusadikisha dhana fulani; tena inajaribu kuyaeleza mambo yalivyo, ikikataa kujifungia ndani ya mipaka ya uchanganuzi wa mitindo ya ufasaha tu; huyatilia maanani ipasavyo mazingira ya majadiliano; na hatimaye inachambua mitindo na tungo kama vyombo vya kuchochea utendaji kwa wasikilizaji. Kwa lengo hilo yanufaika na kutumia michango ya hivi karibuni ya fani mbalimbali kama vile isimu, semiotiki, anthropolojia na sosholojia. Kuhusu Biblia, “balagha mpya” yajaribu kupenya katika mtima wa lugha ya ufunuo ikitazamwa kabisa kama lugha ya kidini yenye kushawishi, pia yajaribu kutathmini jinsi inavyoathiri mazingira ya kijamii ya mawasiliano. Hivyo, uchanganuzi wa kibalagha huutajirisha mtaala wa uhakiki wa matini, na kwa sababu hiyo unastahili heshima kubwa, hususan katika machakura yake ya hivi karibuni. Nao unauponya uzembe ulioendelea kwa kitambo kirefu na kuvumbua ama kuiangaza zaidi mitazamo mipya. “Balagha mpya” ina haki kuutilia mkazo uwezo wa lugha wa kuathiri na kushawishi. Maana Biblia si tangazo tu la kweli mbalimbali, lakini ni pia ujumbe wenye dhima ya mawasiliano katika mazingira fulani; tena ni ujumbe wenye nguvu ya kupeleka hoja zake na wenye mkakati wa kibalagha. Lakini hata hivyo uchanganuzi wa kibalagha, wa kila aina, una mipaka yake. Mathalani unapoeleza tu mitindo ya ufasaha, mara nyingi matokeo yake yanahusu mitindo tu. Nao uchanganuzi huo ni hasa wa kisinkronia; hivyo hauwezi kudai kuwa mbinu yenye kujitegemea na kujitosheleza. Tena unapoelekezwa kwa matini za kibiblia maswali mengi yanazuka: Je, watunzi wa hizo matini walikuwa washiriki wa matabaka yenye elimu ya juu? Je, kwa kiasi gani hawa walishikilia sheria za balagha ili kuyatunga maandishi yao? Je, ni balagha ipi inayofaa zaidi kusudi kulichambua andiko fulani: ile ya kigiriki-kilatini au ile ya kisemiti? Je, hatuingizwi katika hatari ya kuzihusisha baadhi ya matini za Biblia na miundo ya kibalagha yenye hali ya juu mno? Lakini, maswali haya – na mengine tena – yasije yakatukatisha tamaa tusitumie aina hiyo ya uchanganuzi; ila tu yatuhimiza tuitumie kwa upambanuzi mnyofu. Ufafanuzi wa kisimulizi unatoa mbinu ya kufahamu na kuwasilisha ujumbe wa Biblia ambayo inahusiana na mtindo wa usimulizi na wa ushuhuda. Na mtindo huo ni namna ya msingi ya mawasiliano kati ya watu, hata katika Maandiko Matakatifu. Maana Agano la Kale lazieleza habari za historia ya wokovu ambayo masimulizi yake yenye nguvu yanakuwa kiini cha ungamo la imani, cha liturujia na cha katekesi (taz. Zab 78:3-4; Kut 12:24-27; Kum 6:20-25; 26:5-10). Kwa upande wake, tangazo la kerigma ya kikristo lina ndani yake masimulizi ya mfululizo ya maisha, ya kifo na ya ufufuko wa Yesu Kristo; ndiyo matukio ambayo Injili hutusimulia kinaganaga. Katekesi nayo yaelezwa kwa mtindo wa masimulizi (taz. 1Kor 11:23-25). Mintarafu njia ya kisimulizi inafaa kutofautisha kati ya mbinu za uchanganuzi na tafakuri ya kitheolojia. Siku hizi zinatolewa mbinu nyingi za uchanganuzi. Baadhi yake huanzia toka utafiti wa mitindo ya masimulizi ya kale. Nyingine zaasisika katika aina hii au ile ya “naratolojia” (elimu simulizi) ya nyakati zetu, ambayo yaweza kuhusiana kwa namna fulani na semiotiki. Uchanganuzi wa kisimulizi huyazingatia kwa makini katika matini mambo yahusuyo msuko wa historia, watendaji na mtazamo wa msimulizi. Aidha huichunguza namna historia inavyosimuliwa ili kumnasa msomaji akaingie katika “ulimwengu wa masimulizi” na katika mfumo wake wa tunu. Mbinu nyingi zinatofautisha baina ya “mwandishi halisi” na “mwandishi mdokezwa”, “msomaji halisi” na “msomaji mdokezwa”. “Mwandishi halisi” ndiye mtu aliyeyatunga masimulizi. Na kwa jina “mwandishi mdokezwa” inamaanishwa taswira ya mwandishi ambayo inadokezwa hatua kwa hatua wakati wa kusoma (yaani, mwenye utamaduni wake, hulka yake, maelekeo yake, imani yake, n.k.). Tena huitwa “msomaji halisi” kila mtu aikaribiaye matini, kuanzia walengwa wa asili walioisoma au kuisikia, hadi wasomaji au wasikilizaji wa siku za leo. Na kwa jina “msomaji mdokezwa” humaanishwa yule anayekusudiwa na matini yenyewe au ambaye anaathiriwa nayo; yaani yule mwenye uwezo wa kutumia akili na hisia zake ili kuingia katika ulimwengu wa masimulizi, na hapo kuitikia kwa ile namna iliyonuiwa na mwandishi halisi kwa njia ya mwandishi mdokezwa. Hivyo basi, matini fulani inaendelea kuwaathiri wasomaji kwa kiasi wasomaji halisi (k.m. sisi wenyewe tuishio mwishoni mwa karne ya ishirini) wanachoweza kujifananisha na msomaji mdokezwa. Wajibu mojawapo wa msingi wa ufafanuzi ni kuirahisisha kazi hiyo ya kujifananisha. Uchanganuzi wa kisimulizi unaandamana na namna mpya ya kuutathmini uzito wa matini. Yaani, wakati mbinu ya kihistoria-kiuhakiki inazingatia matini kama “dirisha” liwezeshalo kutazama na kuhoji kuhusu muhula fulani (si tu mintarafu matukio yanayosimuliwa, bali pia kuhusu hali ya jumuiya ambayo kwayo yenyewe yalisimuliwa); kumbe, kwa njia ya uchanganuzi wa kisimulizi husisitizwa kuwa matini ni pia kama “kioo”, yaani inaonyesha picha fulani ya ulimwengu – “ulimwengu wa masimulizi” – yenye kuiathiri mitazamo ya msomaji na kumfanya azishike tunu kadhaa kuliko nyingine. Na tafakuri ya kitheolojia imejiambatanisha na aina hiyo ya mtaala, iliyo ya kifasihi tu, kwa sababu imezingatiwa kuwa Maandiko Matakatifu yana maumbile ya masimulizi, na hivyo ya ushuhuda pia; na jambo hilo lina uzito wake kwa ajili ya kuishikilia imani. Tena, toka mbinu hii imechimbuka hemenetiki inayolenga katika utendaji na uchungaji. Na hiyo ni njia mojawapo iliyoshikwa ili kuzuia matini iliyovuviwa (ya Biblia) isishushwe katika hali ya kutazamwa tu kama mkusanyo wa hoja za kitheolojia zinazoelezwa mara nyingi kadiri ya mitindo na lugha isivyotokana na Maandiko. Hivyo, ufafanuzi wa kisimulizi unapewa wajibu – katika mazingira mapya ya kihistoria – wa kuzirudishia heshima yake namna za mawasiliano na uashiriaji zilizo mahsusi za masimulizi ya kibiblia. Nalo kwa lengo la kuifungulia mlango mpana zaidi nguvu ya Biblia kwa ajili ya wokovu. Unasisitizwa pia ulazima wa “kuusimulia wokovu” (mandhari ya “kitaarifa” ya simulizi) na tena wa “kusimulia kwa minajili ya wokovu” (mandhari ya “kiutendaji”). Maana simulizi la kibiblia lina ndani yake – ama kwa wazi ama sivyo, kadiri ya nafasi mbalimbali – mwito kwa msomaji uhusuo maisha yake yote. Kwa ajili ya ufafanuzi wa Biblia, uchanganuzi wa kisimulizi ni msaada wazi, kwa sababu unawiana na maumbile ya kisimulizi ya sehemu nyingi za matini ya Biblia. Hivyo, uchanganuzi huo unaweza kuchangia kuwezesha kupita toka maana ya matini ndani ya mazingira yake ya kihistoria – inavyopatikana kadiri ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki – hadi kufikia maana iliyo nayo kwa msomaji wa siku za leo; kazi ambayo mara nyingi ni ngumu. Lakini, kwa upande mwingine, kutofautisha kati ya “mwandishi halisi” na “mwandishi mdokezwa” kunaongeza ugumu wa masuala ya ufasiri. Aidha, uchanganuzi wa kisimulizi hauwezi tu kutumia taratibu zile zilizokwisha kupangwa ili kuzifasiri matini za Biblia; bali unapaswa kufanya bidii kusudi ujilinganishe na upekee wa kila matini. Mkabala (approach) wake wa kisinkronia unadai kukamilishwa na mitaala ya kidiakronia. Lakini, kwa upande mwingine, uchanganuzi huo unapaswa kujitahadhari na mwelekeo wowote ule ukanyao kila tengenezo la kimafundisho la yale yaliyomo katika masimulizi ya Biblia. Ungefanya hivyo ungepingana na mapokeo ya kibiblia yenyewe ambayo yanalitenda tengenezo la namna hii; tena ungepingana na mapokeo ya kikanisa yaliyoendelea kuitumia njia hii. Na hatimaye inafaa kusisitiza kuwa haiwezekani kuitazama ile nguvu ambayo Neno la Mungu – katika umbo lake la kisimulizi – linayo juu ya maisha ya watu kama kigezo kitoshacho cha kwamba limefahamika barabara. Kati ya mbinu ziitwazo za kisinkronia, yaani zilizomakinika juu ya utafiti wa matini ya Biblia kama ilivyo katika hatua yake ya mwisho, upo pia uchanganuzi wa kisemiotiki; nao tangu miaka ishirini iliyopita umejiendeleza sana katika mazingira fulani ya kitaaluma. Mwanzoni mbinu hii iliitwa kwa neno la jumla “Umuundo” (Structuralism), na inaweza kujisifia kumhesabu kama mwasisi wake mwanaisimu mswisi Ferdinand de Saussure. Huyo, mwanzoni mwa karne hii alitengeneza nadharia ambayo kwayo kila lugha ni mfumo wa mahusiano yanayofuata kanuni maalumu. Wanaisimu wengi na wasomi wa fani za kifasihi walichangia sana kwa maendeleo ya mbinu hii. Walio wengi zaidi wa wasomi wa Biblia wanaoitumia semiotiki kwa mtaala wa Biblia hurejea kwa Algirdas J. Greimas na kwa Shule ya Paris aliyoiasisi mwenyewe. Njia au mbinu nyinginezo za kufanana na hiyo ya kisemiotiki, ambazo zimeasisika katika isimu ya kisasa, zinajiendeleza mahali pengine. Hapo tutaeleza na kuichambua kifupi mbinu ya Greimas. Semiotiki ina misingi yake juu ya kanuni au dhanio hizi tatu zilizo kuu: Kanuni ya kujitimiliza (immanence): kila matini inaunda umoja wa uashiriaji; na uchanganuzi huzingatia matini yote, lakini matini hiyo tu; wala hauzitafuti data nyingine nje yake, kama vile mwandishi, walengwa, matukio yasimuliwayo, na historia ya uhariri. Kanuni ya muundo wa maana: hakuna maana nyingine ya matini isipokuwa kwa njia ya mahusiano na katika mahusiano, na hasa uhusiano wa utofauti; hivyo uchanganuzi wa matini ni juhudi ya kuugundua mfumo wa mahusiano yaliyopo katika matini (k.m. uhusiano wa upinzani, wa uthibitisho, n.k.). Na kutokana na mfumo huo maana ya matini inajengwa. Kanuni ya sarufi ya matini: kila matini yafuata sarufi maalum, yaani utaratibu fulani wa kanuni na miundo; na katika ujumla wa sentensi tunaouita usemi (discourse) kuna viwango mbalimbali, kila kimoja kikiwa na sarufi yake. Maudhui ya jumla ya matini huweza kuchanganuliwa katika viwango vitatu tofauti: Kiwango cha kisimulizi. Katika masimulizi yanachunguzwa mabadiliko yanayopeleka tokea hali ya mwanzo hadi ya mwisho. Na ndani ya mwendo huo wa kisimulizi, uchanganuzi unajaribu kuzigundua awamu mbalimbali zinazofuatana kimantiki kati yake na ambazo zinapigisha hatua za mabadiliko toka hali moja hadi nyingine. Aidha, katika kila awamu yanaelezwa mahusiano kati ya “dhima” zilizo nazo baadhi ya “atanti” (au “wahusika”) ambazo zasababisha hali mbalimbali na mabadiliko yake. Kiwango cha kiusemi. Uchanganuzi huo una vitendo vitatu: (a) kugundua na kuziainisha tamathali, yaani elementi za uashiriaji wa matini (yaani watendaji, nyakati, na mahali); (b) kuueleza mwendo inaoufuata kila tamathali katika matini, ili kuelewa namna matini inavyoitumia; (c) kuzitafiti thamani za kidhamira za tamathali. Na kitendo hicho cha mwisho kinalenga katika kutambua ni “kwa ajili ya nini” (=thamani) tamathali hizo zinafuata mwendo fulani katika matini. Kiwango cha kimantiki-kisemantiki: Ni kiwango kiitwacho cha kina; tena ni cha kidhahania zaidi. Nacho hutokana na dhana ya kwamba nyuma ya miundo ya kisimulizi na kiusemi ya kila usemi hufichama fani za kimantiki na viashiria. Katika kiwango hicho uchanganuzi unashughulikia kuieleza mantiki inayoratibisha miundo ya msingi ya miendo ya kisimulizi na kitamathali ya matini. Kwa kuitekeleza kazi hiyo yanatumika maarifa yaitwayo “mraba wa kisemiotiki”, yaani tamathali inayotumia mahusiano baina ya misamiati miwili iliyo “kinyume” kati yake na misamiati miwili “inayopingana” (k.m. nyeupe na nyeusi; nyeupe na si nyeupe; nyeusi na si nyeusi). Wanadharia wa mbinu ya kisemiotiki hawamalizi kuleta maendeleo katika mbinu hii. Na tafiti za kisasa zinahusu hasa utamkaji (enunciation) na mwingiliano matini (intertextuality). Mwanzoni mbinu hii ilitumika kwa matini za kisimulizi za Maandiko – na hapo ni rahisi zaidi; lakini siku hizi inazidi kutumika pia kwa aina nyingine za semi za kibiblia. Maelezo ya hapo juu mintarafu semiotiki, na hasa kuhusu dhanio zake, yanahisisha michango na pia mipaka ya mbinu hii. Maana, yenyewe inakazia kwamba kila matini ya Biblia ina mshikamano ndani yake ambao unafuata taratibu maalum za kiisimu; hivyo semiotiki inachangia katika ufahamu wetu wa Biblia, iliyo neno la Mungu lielezwalo kwa lugha ya kibinadamu. Semiotiki yaweza kutumika kwa mtaala wa kibiblia, ila kwa sharti ya kwamba mbinu hii itenganishwe na dhanio zilizoendelezwa katika falsafa ya Umuundo, yaani ukanushaji wa wahusika na wa elementi mbalimbali zipatikanazo nje ya matini. Biblia ni Neno juu ya uhalisi, ambalo Mungu amelitamka katika historia, na ambalo anatuelekezea leo kwa njia ya waandishi wa kibinadamu. Njia ya kisemiotiki haina budi kuwa wazi mbele ya historia: kwanza historia ya watendaji katika matini, na baadaye historia ya waandishi wake na wasomaji wake. Hivyo kwa wale wanaoutumia uchanganuzi wa kisemiotiki hatari ni kubwa ya kukwama katika utafiti wa nje wa maudhui, lakini pasipo kuukamata ujumbe wa matini. Uchanganuzi wa kisemiotiki unaweza kuiamsha katika wakristo hamu ya kuzichunguza matini za Biblia na kuvumbua baadhi ya maana zake bila ya kuwa na maarifa yote ya kihistoria yanayohusu utungaji wa matini na mazingira yake ya kijamii-kiutamaduni. Ila uchanganuzi huo usipotee katika vificho vya lugha yenye utata; na tena ufundishwe kwa namna iliyo rahisi katika vipengele vyake vya msingi. Kwa jinsi hiyo unaweza kufaa katika kazi yenyewe ya kichungaji, ili pia watu wasio na utaalamu wa pekee wapate kwa namna fulani kujitwalia Maandiko Matakatifu katika maisha yao. C. Njia zenye msingi katika Mapokeo Mbinu za kifasihi tulizozieleza huhitilafiana na mbinu ya kihistoria-kiuhakiki kwa sababu humakinika zaidi katika umoja uliomo ndani ya matini zinazochunguzwa; lakini hata hivyo hazitoshelezi kwa ajili ya ufasiri wa Biblia, kwa maana hulizingatia kila andiko kwa lenyewe. Sasa, Biblia haijidhihirishi kama mkusanyo wa matini zisizo na uhusiano wowote kati yake, bali kama jumla ya shuhuda za Mapokeo makuu yaleyale. Ili kuiridhisha kwa ukamilifu mada ya mtaala wake, ufafanuzi wa kibiblia hauna budi ulitilie maanani jambo hilo. Nao ndio mtazamo uliotumika na njia mbalimbali zilizojitokeza hivi karibuni. Njia ya “kikanoni” ilizaliwa mnamo miaka ishirini iliyopita huko Marekani; asili yake ilikuwa pale ilipogunduliwa kwamba mbinu ya kihistoria-kiuhakiki mara nyingine inashindwa kukifikia kiwango cha kitheolojia katika hatima zake. Hivyo, njia hii inanuia kuufikisha ufasiri kwenye hatua ya kushikilia wajibu wake wa kitheolojia, kuanzia na fremu wazi la imani, yaani, Biblia katika umoja wake. Ili kutekeleza wajibu huo inafasiri kila matini ya Biblia katika mwanga wa kanoni ya Maandiko, yaani wa Biblia ipokelewayo na jumuiya ya waamini kama kanuni ya imani. Inajaribu kuingiza kila matini ndani ya mpango ule mmoja wa Mungu, kwa minajili ya kuufikia uhusisho (actualization) wa Maandiko Matakatifu katika nyakati zetu. Ila njia hii haijidai kuchukua nafasi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, bali inatarajia kuikamilisha. Mitazamo miwili tofauti imetolewa: Brevard S. Childs anazingatia hasa matini katika sura yake ya kikanoni ya mwisho (kitabu au mkusanyo), iliyokubalika na jumuiya kama mamlaka ili kueleza imani ya jumuiya yenyewe na kuyaelekeza maisha yake. Kumbe, James A. Sanders, kuliko kuzingatia sura hiyo ya mwisho ya matini iliyokubalika, anatilia maanani hasa “mchakato wa kikanoni” wa Maandiko, au kukua kwake hatua kwa hatua, ambayo jumuiya ya waamini imeyakubali kuwa na mamlaka ya kikanuni. Uchambuzi wa kiuhakiki wa mchakato huo unachunguza jinsi mapokeo ya kale yalivyotumika upya katika mazingira mapya, kabla hayajaunda umoja wa kudumu, lakini unaoweza kukamilishwa tena, wenye mshikamano, na unaopatanisha yale yasiyoafikiana. Na kutoka kwake jumuiya ya waamini huchota kitambulisho chake. Wakati wa mchakato huo, yalitumika maarifa ya kihemenetiki ambayo bado yanatumika, hata baada ya kuweka kanoni rasmi; mara nyingi maarifa hayo yanaingia katika utanzu wa “kimidrashi”; nayo yanalenga katika kuzilinganisha na wakati huu matini za Biblia na kuusaidia mwingiliano wa kudumu baina ya jumuiya na Maandiko yake, yakitafiti ufasiri unaokusudia kuyafanya mapokeo yawiane na wakati huo. Njia ya kikanoni kwa haki inapinga uthamini wa kupita kiasi wa kile kinachodhaniwa kuwa cha asili na cha kale kana kwamba chenyewe tu ni halisi. Kumbe Maandiko yaliyovuviwa ndiyo yale ambayo Kanisa limeyakubali kama kanuni ya imani yake. Na kuhusu hilo, huwezekana kuitilia mkazo hali ya mwisho ambayo kila kitabu kinayo siku hizi, na pia umoja ambao vitabu vinauunda kwa pamoja kama kanoni. Kila kitabu kinakuwa cha Biblia katika mwanga tu wa kanoni nzima. Jumuiya ya waamini ndiyo mazingira yanayofaa kwa ufasiri wa matini za kikanoni. Imani na Roho Mtakatifu hutajirisha ufafanuzi ndani ya jumuiya yenyewe; na hatimaye mamlaka ya Kanisa, yafanyayo kazi kwa huduma ya jumuiya, lazima yahakikishe kuwa ufasiri ni mwaminifu kwa mapokeo makuu yaliyotunga matini (taz. Dei Verbum, 10). Njia ya kikanoni inapambana na matatizo mengi, hasa inapojaribu kueleza “mchakato wa kikanoni”. Je, kutokana na nini yawezekana kusema kuwa matini fulani ni ya kikanoni? Inaonekana kwamba yawezekana mara tu jumuiya inapoipa mamlaka ya kikanuni, hata kabla matini yenyewe haijafikia hali yake ya mwisho. Hivyo, hemenetiki ya “kikanoni” inaweza kuzungumziwa tangu pale ambapo marudio ya mapokeo, yanayofanyika kwa kuzingatia mandhari mpya za mazingira (ya kidini, kiutamaduni, kitheolojia), yanatunza umoja wa ujumbe. Lakini hapo swali linazuka: Je, mchakato wa ufasiri ulioleta kwenye uundaji wa kanoni unapaswa kukubalika kama kanuni ya ufasiri wa Maandiko hadi siku za leo? Kwa upande mwingine, mahusiano changamano baina ya kanoni ya kiyahudi ya Maandiko na kanoni ya kikristo yanazusha masuala mengi mintarafu ufasiri. Kanisa la kikristo limepokea kama “Agano la Kale” maandishi yaliyokuwa na mamlaka katika jumuiya ya kiyahudi-kiyunani, lakini baadhi yake hayapo katika Biblia ya kiyahudi, au yapo lakini kwa tungo tofauti. Kwa hiyo kongoo (corpus) ni tofauti. Ndiyo maana ufasiri wa kikanoni hauwezi kuwa sawa kwa vile kila matini lazima isomwe kwa kuhusiana na mshikamano wa kongoo nzima. Lakini, zaidi ya hayo, Kanisa lasoma Agano la Kale katika mwanga wa tukio la kipasaka – yaani kifo na ufufuko wa Yesu Kristo –, ambayo linaleta kitu kilicho kipya kabisa na kinachotimiliza na kuikamilisha maana ya Maandiko kwa mamlaka yake yenye enzi (taz. Dei Verbum, 4). Na upambanuzi huo mpya wa maana ya maandiko ni sehemu halisi ya imani ya kikristo. Lakini hauwezi kubatilisha ufasiri wa kikanoni ulioitangulia Pasaka ya kikristo, kwa sababu ni lazima kuiheshimu kila hatua ya historia ya wokovu. Kwani kubatilisha uzito wa maana ya Agano la Kale kungekuwa kung’oa mizizi ya Agano Jipya kutoka katika historia. 2. Njia itumiayo mapokeo ya kifasiri ya kiyahudi Agano la Kale lilichukua sura yake ya mwisho katika mazingira ya Uyahudi (Judaism) wa karne nne ama tano kabla ya nyakati za kikristo. Nayo yalikuwa pia mazingira ya asili ya Agano Jipya na ya Kanisa changa. Wingi wa uchunguzi kuhusu historia ya kale ya Uyahudi – na hasa tafiti zilizochochewa na uvumbuzi wa Kumrani – umeonyesha mchangamano wa ulimwengu wa kiyahudi, katika nchi ya Israeli na katika Mtawanyiko (diaspora), katika kipindi hicho. Ufasiri wa Biblia umeasilika katika mazingira haya. Ushuhuda mmojawapo wa kale zaidi wa ufasiri wa kiyahudi wa Biblia ni tafsiri yake ya Kigiriki iitwayo ya Septuajinta. Kadhalika targumim za Kiaramu ndio ushuhuda mwingine wa jitihada ileile iliyoendelezwa hadi siku za leo, kwa kulimbikiza mkusanyo wa ajabu wa mbinu za kitaaluma kwa ajili ya uhifadhi wa matini ya Agano la Kale na ufafanuzi wa maana ya matini za Biblia. Tangu mwanzo wafafanuzi wa kikristo walio bora, kuanzia na Orijene na Mt. Yeronimo, walijitahidi kupata faida kutokana na elimu ya kibiblia ya kiyahudi kwa minajili ya ufahamu ulio mzuri zaidi wa Maandiko. Na wafafanuzi wengi wa nyakati zetu wanafuata mfano wao. Mapokeo ya kale ya kiyahudi yanatusaidia hasa kuijua Septuajinta, iliyo Biblia ya kiyahudi, na ambayo imekuwa baadaye sehemu ya mwanzo ya Biblia ya kikristo, walau katika karne nne za kwanza za Kanisa, na huko Mashariki hadi siku za leo. Aidha, maandishi ya kiyahudi yaliyo nje ya kanoni na yaitwayo “apokrifa” au “ya kati ya maagano”, yametufikia kwa wingi na ya aina aina; hata hayo ni chemchemi muhimu kwa ufasiri wa Agano Jipya. Mbinu za kifafanuzi zilizotumika na Uyahudi wa mielekeo mbalimbali, zinapatikana katika Agano la Kale lenyewe, kwa mfano katika vitabu vya Mambo ya Nyakati kwa kuhusiana na vitabu vya Wafalme; pia katika Agano Jipya, mathalani katika baadhi ya hoja za Mt. Paulo kuhusu Maandiko. Utofauti wa tanzu (mifano, istiari, diwani na koja, kusoma upya (relectures), mbinu za “pesher”, namna ya kuunganisha matini ambazo vinginevyo zingekuwa za aina mbalimbali, zaburi na tenzi, maono, funuo na ndoto, maandishi ya kihekima) umo katika Agano la Kale, na Agano Jipya pia, kama vile katika fasihi ya mazingira yoyote ya kiyahudi kabla na baada ya wakati wa Yesu. Targumim na Midrashim ni namna ya kuhutubia na kufasiri Biblia katika sekta nyingi za Uyahudi wa karne za mwanzoni. Wafafanuzi walio wengi wa Agano la Kale wanatafuta msaada kwa wafasiri, wanasarufi na wanamsamiati wa kiyahudi wa Enzi ya Kati (mediaeval) na wa baadaye ili kuzielewa sehemu za kizakiza ama maneno yanayotumika kwa nadra au mara moja tu. Na siku hizi katika majadiliano ya kifafanuzi marejeo kwa maandishi hayo ya kiyahudi yanaonekana kuwa mengi zaidi kuliko hapo nyuma. Utajiri wa elimu ya kiyahudi uliowekwa kuitumikia Biblia, tangu asili yake wakati wa kale hadi siku za leo, ni msaada kati ya ile yenye kipaumbele kwa ajili ya ufafanuzi wa Maagano yote mawili, ila kwa sharti ya kuutumia kwa upambanuzi mzuri. Uyahudi wa kale ulikuwa na mitindo mbalimbali. Mtindo wa kifarisayo, ambao baadaye ulishinda kati ya marabi, haukuwa mtindo pekee. Matini za kale za kiyahudi zilienea katika muda wa karne kadhaa; hivyo, ni muhimu kuzipanga kadiri ya nyakati zake kabla ya kuanza kuzilinganisha. Lakini hasa mazingira ya jumla ya jumuiya hizi mbili, yaani ya kiyahudi na ya kikristo, ni tofauti kabisa: kwa namna nyingi mbalimbali dini ya kiyahudi inaainisha taifa fulani na pia utendaji wa kimaadili kutokana na andiko lililofunuliwa na Mungu na kutokana na mapokeo simulizi; kumbe, kinachokusanya jumuiya ya kikristo ni imani katika Bwana Yesu aliyekufa na kufufuka, na ambaye sasa yu hai, ndiye Masiya na Mwana wa Mungu. Basi, kuhusu ufasiri wa Maandiko vyanzo hivi viwili tofauti vinaleta mazingira mawili ambayo ni tofauti kabisa, ijapo vipengele vinavyoelekeana na kufanana ni vingi. 3. Njia ichunguzayo historia ya athari ziletwazo na matini Njia hii ina misingi yake juu ya kanuni mbili: a) matini inapata kuwa kazi ya kifasihi pindi tu inapokutana na wasomaji ambao wanaihuisha kwa kuitwaa; b) kuitwaa huko kwa matini kunaweza kuwa tendo la mtu binafsi au la kijumuiya; tena ni tendo linaloweza kutekelezwa katika nyanja mbalimbali (wa kifasihi, kisanaa, kitheolojia, kiroho, kitawa); na hatimaye kunachangia katika kufanya matini yenyewe ieleweke vizuri zaidi. Ijapokuwa njia hii ilikuwa inafahamika kwa kiasi fulani tangu nyakati za kale, siku hizi imejiendeleza zaidi kati ya miaka 1960 na 1970 katika mitaala ya kifasihi, wakati uhakiki ulipojihusisha kuchunguza mahusiano kati ya matini na wasomaji wake. Ufafanuzi wa kibiblia ulikuwa hauna budi kufaidika kutokana na utafiti huo, na zaidi kufuatana na kwamba hemenetiki ya kifalsafa kwa upande wake ilikuwa ikisisitiza ya kuwa ni lazima umbali fulani uwepo baina ya maandishi na mwandishi wake, kama vile kati ya maandishi na wasomaji wake. Kadiri ya mtazamo huo, ilianza kuingizwa katika kazi ya ufasiri historia ya athari zilizoletwa na kitabu au sehemu fulani ya Maandiko (“Wirkungsgeschichte”). Na bidii inafanyika i1i kupima maendeleo ya ufasiri katika mtiririko wa nyakati kuhusiana na kero za wasomaji, pia ili kutathmini umuhimu wa dhima ya mapokeo katika kuiweka wazi maana ya matini za Biblia. Kuhojiana kati ya matini na wasomaji wake kunaleta mkikimkiki fulani, kwa sababu matini inawaathiri wasomaji na kuwazushia hisia kadhaa; tena inasikiza mwaliko wake unaoitikiwa nao kibinafsi au kijumuiya. Naye msomaji kwa vyovyote si mtu aishiye peke yake, bali daima hushiriki mazingira fulani ya kijamii, naye yumo ndani ya mapokeo fulani. Hivyo, huikaribia matini kwa maswali yake, tena hufanya uchambuzi na kupendekeza ufasiri wake, na hatimaye huweza kutunga maandishi mengine ama kujishughulisha na mambo mengine yatokanayo moja kwa moja na anavyosoma yeye Maandiko. Mifano ya namna hii imeshakuwa mingi. Historia ya usomaji wa Wimbo ulio Bora inatupatia ushuhuda bora; nao huonyesha jinsi kitabu hiki kilivyopokelewa siku za Mababa wa Kanisa, au kwenye mazingira ya kimonaki ya kilatini katika Enzi za Kati (mediaeval); au tena kwa mtu mshiriki Mungu (mystical writer) kama Mt. Yohane wa Msalaba. Hivyo, njia hii inatuwezesha kuvumbua kiundani zaidi vipengele vyote vya maana za andiko hilo. Kadhalika, mintarafu Agano Jipya yawezekana na yafaa kuiangaza maana ya kifungu fulani (kwa mfano, cha kijana tajiri wa Mt 19:16-26) kwa kuonyesha wingi wa matunda kilichouleta katika mtiririko wa historia ya Kanisa. Lakini, historia huthibitisha pia kuwepo kwa mitindo ya ufasiri yenye kupotosha na ya uongo, iletayo matokeo mabaya na ambayo ilisababisha, kwa mfano, madhulumu ya Wayahudi, au ubaguzi wa kikabila, au mauzauza za kimilenia. Hivyo basi, huonekana kwamba njia hii haiwezi kuwa fani inayojitegemea, bali ambayo hudai upambanuzi. Ni lazima kujitahadhari na tabia ya kuibagua awamu moja au nyingine ya historia ya athari ya matini fulani na kuiweka kama kanuni pekee ya ufasiri wake. D. Njia zitumiazo sayansi za kibinadamu Ili kujishirikisha, Neno la Mungu limetia mizizi yake ndani ya maisha ya jumuiya za kibinadamu (taz. YbS 24:12) na kujipasulia njia katika mielekeo ya kisaikolojia ya watu mbalimbali waliotunga maandishi ya Biblia. Katika hilo yatokana kwamba sayansi za kibinadamu – hasa sosholojia, anthropolojia na saikolojia – zaweza kuchangia kwa ajili ya ufahamu bora zaidi wa mandhari kadhaa za matini. Walakini yafaa kukumbuka kwamba ziko shule mbalimbali, zenye kuhitilafiana kwa vikubwa kuhusu maumbile yenyewe ya sayansi hizo. Ikiisha semwa hivyo, basi wafafanuzi sio wachache wamenufaika hivi karibuni kutokana na aina hiyo ya utafiti. Matini za kidini zinafungamana na jamii zile zilipoasilika. Ni wazi kwamba kauli hiyo yazihusu pia matini za Biblia. Hivyo, uchambuzi wa kiuhakiki wa Biblia hudai ujuzi ulio kamili zaidi, iwezekanavyo, wa desturi za kijamii zilizokuwa kawaida ya mazingira ambamo mapokeo ya kibiblia yalitengenezwa. Na aina hiyo ya taarifa za kijamii-kihistoria haina budi kukamilishwa kwa maelezo sahihi ya kisosholojia ambayo, kwa vyovyote, yatapaswa kufasiri kisayansi uzito wa mazingira ya kijamii ya maisha. Katika historia ya ufafanuzi, tangu muda mrefu mtazamo wa kisosholojia umepata nafasi yake; na ushuhuda wa nafasi hiyo ndio mkazo ambao uchambuzi wa kiuhakiki wa fani (“Formgeschichte”) umeyatilia mazingira ya asili ya matini (“Sitz im Leben”): inakubalika kuwa mapokeo ya kibiblia yanabeba athari ya mazingira ya kijamii-kiutamaduni yaliyoyafikisha kwetu. Katika miaka thelathini ya kwanza ya karne ya ishirini, Shule ya Chicago ilichunguza hali ya kisosholojia-kihistoria ya Ukristo wa mwanzoni; na hivyo iliutilia uhakiki wa kihistoria hamasa maridhawa katika mwelekeo huo. Na hatimaye katika miaka hiyo ishirini ya mwisho (1970-1990) njia ya kisosholojia imekuwa sehemu husika ya ufafanuzi wa matini za Biblia. Mengi ndiyo maswali yanayozuka katika uwanja huo kwa ufafanuzi wa Agano la Kale. Mathalani, ni lazima kujiuliza ni ipi mitindo mbalimbali ya mifumo ya kijamii na kidini iliyofahamika na Israeli katika mwenendo wa historia yake. Ukizingatiwa muhula uliotangulia uundaji wa dola kamili, je yawezekana kuwa mtindo wa kiethnolojia wa jamii iliyogawanyika kikabila na isiyo na uongozi kamili uwe msingi maridhawa kwa kujenga chochote? Je, imekuwaje kuwa shirikisho la makabila mbalimbali yasiyo na mshikamano imara lipate kuwa dola yenye mfumo wa kiufalme, na tokea hapo tena lipate kuufikia uundaji wa jumuiya inayoasilika tu katika vifungo vya kidini na kinasaba? Je, ni mageuzi yapi ya kiuchumi, kijeshi au ya namna nyingine yoyote ile yaliyoletwa katika muundo wa jamii, kutokana na kuyaunganisha makabila yote chini ya mamlaka moja ya kisiasa na kidini, hadi kuufikia mfumo wa kiufalme? Je, uchunguzi wa kanuni za kimwenendo zilizokuwepo katika Mashariki ya kale na katika Israeli hausaidii kuzielewa Amri Kumi (za Mungu) kwa manufaa zaidi kuliko majaribio ya uchanganuzi wa kifasihi pekee yanayotaka kuithibitisha matini ya asili? Kuhusu ufafanuzi wa Agano Jipya ni wazi kwamba maswali ni tofauti. Tunayataja baadhi yake: ili kueleza mtindo wa maisha ya Yesu na wanafunzi wake kabla ya Pasaka, je, yaweza kupewa uzito gani nadharia ya “uamsho wa kikarama” (charismatic movement) wa watu wenye kutembeatembea, wasio na makao kamili, wala familia, wala mali? Tena kutokana na wito wa Yesu wa kuzifuata nyayo zake, je, kulikuwa na uwiano halisi baina ya tabia ya Yesu ya kuacha kabisa yote na tabia ya washiriki wa uamsho wa kikristo baada ya Pasaka, katika mazingira mbalimbali ya Ukristo wa mwanzoni? Na hatimaye, je, tuna habari gani kuhusu muundo wa kijamii wa jumuiya zilizoanzishwa na Mt. Paulo, kwa kuuzingatia kwa kila moja utamaduni ulioenea katika miji zilimoishi? Kwa ujumla, njia ya kisosholojia inailetea kazi ya ufafanuzi mtazamo ulio mpana zaidi na kutoa michango mingi mizuri. Ujuzi wa data za kisosholojia, zinazosaidia kuelewesha mwendo wa kiuchumi, kiutamaduni na kidini wa mazingira ya Biblia, ni wa lazima katika fani ya uhakiki wa kihistoria. Wajibu unaoukabili ufafanuzi, wa kuzingatia kwa makini ushuhuda wa imani ya Kanisa la kitume, hauwezi kutekelezwa hadi mwisho na kwa utaratibu sahihi pasipo utafiti wa kisayansi kufanyika, ambao uchunguze mahusiano ya ndani kati ya matini za Agano Jipya na maisha ya kijamii ya Kanisa la mwanzoni. Matumizi ya mitindo inayotolewa na sayansi ya kisosholojia yanawapatia wasomi wa historia wanaozichunguza nyakati za Biblia uwezo mkubwa wa kutengeneza upya mbinu zao; ila mitindo itumiwayo haina budi kulinganishwa na masuala yanayopelelezwa. Na hapo yafaa kusisitiza pia hatari zilizopo katika njia ya kisosholojia pindi inapotumika katika ufafanuzi. Kwa kuwa kazi ya sosholojia ni kuchunguza jamii zilizo hai, basi shida lazima itokee pale mbinu zake zinapodaiwa kutumika kwa kuchunguza mazingira ya kihistoria yahusuyo nyakati za kale. Maana matini za Biblia na za nje ya Biblia hazitupatii habari na hati za kutosha ili kutoa picha ya jumla ya jamii za nyakati hizo. Aidha, mbinu ya kisosholojia inatilia maanani zaidi vipengele vihusuvyo uchumi na taasisi za maisha ya kibinadamu, kuliko masuala yanayoelekea maisha ya kibinafsi na ya kidini. 2. Njia itumiayo anthropolojia ya kiutamaduni Njia ichunguzayo matini za Biblia kwa kutumia tafiti za anthropolojia ya kiutamaduni inahusiana kiundani na njia ya kisosholojia. Upambanuzi baina ya njia hizo mbili waweza kufanyika yakizingatiwa kwa wakati mmoja masuala mbalimbali, kama vile uelekeo wa njia hizo, mbinu zake na vipengele vya maisha vinavyovuta zaidi kila moja ya njia hizo. Maana, kwa upande mmoja, njia ya kisosholojia – tulivyosema hapo juu – inachunguza hususan vipengele vihusuvyo uchumi na taasisi; kwa upande mwingine, njia ya kianthropolojia inajishughulisha na jumla ya vipengele vingine vingi vinavyoakisiwa katika lugha, sanaa na dini; lakini pia katika mavazi, mapambo, sherehe, dua, visasili na hadithi za kale, ngano na kila chote kihusucho ethnografia. Aghalabu, anthropolojia ya kiutamaduni inajaribu kuzieleza sifa bainifu za watu wa aina mbalimbali katika mazingira yao ya kijamii – kama vile, k.m., “mtu wa kimediterania” –; na kazi hiyo inadai utafiti mintarafu mazingira ya shambani au mjini, na pia kuzingatia tunu zinazokubalika na jamii yenyewe (heshima na aibu, siri, uaminifu, mapokeo, mtindo wa malezi na wa elimu); tena inadai utafiti kuhusu namna udhibiti wa kijamii unavyotekelezwa, na hata kuzingatia mawazo yaliyoenea mintarafu familia, nyumba, ukoo, hali ya mwanamke; na hatimaye kuzichunguza zile dhima za kijamii zenye kupambana baina yake (bwana / mtumishi; mmilikaji / mpangaji; mfadhili / mfadhiliwa; mwungwana / mtumwa); nayo yote bila kusahau dhana za utakatifu na unajisi, miiko, ibada za kutoka katika hali moja hadi kuingia nyingine, uchawi, asili ya mali, ya madaraka, ya taarifa, n.k. Katika msingi wa masuala hayo mbalimbali “ainisho” (typologies) na “mitindo” (models) kadhaa vinaweza kutengenezwa, vyenye kuzihusu tamaduni nyingi. Aina hiyo ya uchunguzi yaweza kuwa na manufaa kwa ufasiri wa matini za Biblia, na kweli inatumika kwa kuchunguza dhana kama ukoo na nasaba katika Agano la Kale, au ya hali ya mwanamke katika jamii ya kiyahudi, ya athari ya ibada zihusuzo kilimo, n.k. Katika matini zinazosimulia mafundisho ya Yesu – mathalan mifano – hata vipengere vidogo vidogo vinaweza kuangazwa kwa msaada wa njia hiyo. Ndivyo itokeavyo pia kwa dhana kadhaa za msingi, kama ile ya Ufalme wa Mungu, au kwa jinsi ya kujali wakati katika historia ya wokovu, au tena kwa hatua zilizofanya Wakristo wa mwanzoni waunganike pamoja katika jumuiya. Njia hii inawezesha kutofautisha vizuri zaidi katika ujumbe wa kibiblia mambo yale yadumuyo, ambayo yana msingi wake katika maumbile ya binadamu, na yale yalinganayo zaidi na masuala ya muda ya tamaduni fulani. Hata hivyo, pia njia hii, sawa na nyingine zenye mtazamo ya pekee, haiwezi kwa yenyewe kueleza michango maalum ya Ufunuo. Yafaa kulishika jambo hilo pindi matokeo ya kazi yake yatathminiwapo. 3. Njia za kisaikolojia na kiudodosinafsi Saikolojia na theolojia hazikuacha kamwe kuzungumzana. Katika nyakati zetu, tafiti za kisaikolojia zimepanua na kuelekezwa kwenye uchunguzi wa miundo ya kimkikimkiki ya ung’amuzi fiche (subconscious); nazo zimeleta majaribio mapya ya ufasiri wa matini za kale, na hivyo pia za Biblia. Vitabu vizima vimeandikwa kuhusu ufasiri wa kiudodosinafsi wa matini za Biblia. Na majadiliano ya motomoto yamefuata: je, kwa kipimo gani na kwa masharti yapi tafiti za kisaikolojia na kiudodosinafsi zaweza kuchangia katika kuelewa kwa undani zaidi Maandiko Matakatifu? Chunguzi za kisaikolojia na kiudodosinafsi zinaleta utajiri fulani kwa ufafanuzi wa Biblia, kwa sababu kwa njia yake matini za Biblia zaweza kueleweka vizuri zaidi kama mang’amuzi ya maisha na kanuni za mwenendo. Inavyoeleweka wazi, dini ipo daima katika hali ya majadiliano na ung’amuzi fiche. Tena, inashiriki kwa vikubwa katika kuzielekeza vema ari za kibinadamu. Hatua ambazo uhakiki wa kihistoria unazipita kadiri ya mbinu yake zinahitaji kukamilishwa kwa uchunguzi wa viwango mbalimbali vya hali halisi iliyoelezwa katika matini. Saikolojia na udodosinafsi hujibidisha kusonga mbele katika utafiti wa namna hiyo. Zenyewe zinafungua njia kwa ufahamu wa Maandiko katika viwango vyake vingi, na zinasaidia kufumbua lugha ya kibinadamu ya Ufunuo. Saikolojia na, kwa namna nyingine, udodosinafsi zimeleta hasa ufahamu mpya wa ishara (symbol). Lugha ya kiishara inawezesha kueleza sehemu za mang’amuzi ya kidini ambazo hazifikiki kwa mantiki ya kidhana tu, lakini ambazo, hata hivyo, zina thamani kuhusu suala la ukweli. Kwa hiyo, upelelezi unaoshirikisha mbinu mbalimbali, unaoongozwa na wafafanuzi pamoja na wanasai-kolojia au na wanaudodosinafsi, hakika unaleta manufaa yenye misingi ya uhalisia na yanayothibitishwa katika uchungaji. Mifano mingi ingeweza kutolewa inayoonyesha ulazima wa juhudi ya pamoja ya wafafanuzi na wanasaikolojia: nalo kwa minajili ya kuelewa vizuri zaidi maana ya kanuni za ibada, ya sadaka na ya miiko; tena kwa kuieleza lugha ya kitaswira ya Biblia, maana ya kiistiari ya masimulizi ya miujiza, na nguvu ya kidrama ya maono au ya maneno ya kiapokaliptiki. Siyo tu suala la kulifasiri lugha ya kiishara ya Biblia, bali pia la kuielewa dhima yake katika kulifunua fumbo na kuzusha hoja: ndipo uhalisi wenye kutisha (“numinous”) wa Mungu unapokutana na binadamu. Ni wazi kwamba mazungumzano kati ya ufafanuzi na saikolojia ama udodosinafsi kwa lengo la kuifahamu vizuri zaidi Biblia lazima yaongozwe kwa vigezo vya kiuhakiki na kuijali mipaka ya kila fani. Kwa vyovyote, saikolojia au udodosinafsi zenye tabia ya kukana Mungu (atheistic) zisingeweza kufasiri mambo ya imani. Saikolojia na udodosinafsi zinafaa kwa kusisitiza upana wa uwajibikaji wa binadamu, lakini haziwezi kufuta ukweli wa dhambi na wa wokovu. Kwa upande mwingine, inabidi kujitahadhari ili hisia binafsi za kidini (spontaneous religiosity) zisichanganywe na ufunuo wa kibiblia; tena ili isisahauliwe tabia ya kihistoria ya ujumbe wa Biblia ambayo inauhakikishia ujumbe wenyewe thamani ya tukio pekee. Aidha, tunasisitiza kwamba haiwezekani kuuzungumzia “ufafanuzi wa kiudodosinafsi” kana kwamba ungekuwepo wa mtindo mmoja tu. Kwa kweli, kutokana na nyanja mbalimbali za saikolojia, na kufuatana na shule tofauti, kuna wingi wa maarifa unaoweza kuleta mwanga wa kufaa kwa ufasiri wa kibinadamu na wa kitheolojia wa Biblia. Kuyapendelea maoni ya shule moja tu kama yangekuwa ukweli pekee hakuyasaidii mafanikio ya juhudi inayofanyika kwa pamoja, bali zaidi huyadhuru. Sayansi za kibinadamu haziwezi kufungwa katika mipaka tu ya sosholojia, anthropolojia ya kiutamaduni na saikolojia. Fani nyingine za sayansi nazo zinaweza kufaa kwa ufasiri wa Biblia. Na katika nyanja hizo zote ni lazima kuuheshimu utaalamu wa kila fani na pia kutambua kwamba si rahisi mtu mmoja awe ni stadi katika ufafanuzi na wakati huohuo pia katika sayansi hii au hiyo ya kibinadamu. Ufasiri wa matini fulani daima hutegemea msimamo wa mawazo wa wasomaji wake na kero zao. Hao wanazingatia hasa baadhi ya mandhari na, hata pasipo kujitambua, wanaziacha nyingine. Kwa hiyo, hapana budi baadhi ya wafafanuzi katika kazi yao watumie mitazamo mipya inayolingana na mikondo ya mawazo ya kisasa na ambayo hadi leo haijapewa nafasi ya kutosha. Inafaa wafanye hivyo kwa upambanuzi wa kiuhakiki. Siku hizi makini inavutwa hasa na vuguvugu za ukombozi na ufeministi (utetezi wa usawa wa wanawake) Theolojia ya ukombozi ni suala changamano ambalo haliwezi kuchukuliwa vyepesi. Kama harakati ya kitheolojia, iliimarika mnamo mwanzoni mwa miaka ya sabini. Asili yake, pamoja na mazingira ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya nchi za Amerika ya Kusini, inapatikana katika matukio makuu mawili ya kikanisa: mosi, Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ambao ulitamka wazi azimio lake la “aggiornamento” (= kujiweka kisasa) na la kuzielekeza kazi za kiuchungaji za Kanisa kwenye mahitaji ya ulimwengu wa leo; pili, Mkutano Mkuu wa II wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini uliofanyika Medellin mwaka 1968, ambao ulilinganisha mafundisho ya Mtaguso na mahitaji ya Amerika ya Kusini. Halafu harakati hii imesambaa hata katika nchi nyingine za dunia (Afrika, Asia, na watu weusi wa Marekani). Ni vigumu kupambanua kama ipo theolojia “moja” ya ukombozi na kuainisha mbinu yake. Kadhalika, ni vigumu kueleza ipasavyo namna yake ya kusoma Biblia, na baadaye kuonyesha michango inayotoa na mipaka yake pia. Yawezekana kusema kwamba theolojia hiyo haitumii mbinu maalum, bali, kutokana na mitazamo yake maalum ya kijamii-kiutamaduni na ya kisiasa, inasoma Biblia kwa kuyalenga mahitaji ya watu, ambao wanatafuta ndani ya Biblia chakula cha kulisha imani yao na maisha yao. Badala ya kujifungia ndani ya ufasiri unaoitazama matini ilivyo, na kuyazingatia yale matini ambayo inayasema kulingana na mazingira ilipoasiliwa, basi inatafuta ufasiri unaozaliwa kutokana na hali halisi ya maisha ya watu. Ikiwa hao wanaishi katika hali ya kugandamizwa, Biblia inakimbiliwa ili kutafuta ndani yake chakula kiwezacho kuwategemeza watu katika mapambano yao na matarajio yao. Maana hali iliyopo haipaswi kusahauliwa, bali, kinyume chake, kuzingatiwa ili iangazwe kwa mwanga wa Neno la Mungu. Hivyo, kutokana na mapambano hayo, utendaji halisi wa kikristo utajitokeza, nao utaelekea kuibadili jamii kwa njia ya haki na upendo. Katika imani, Maandiko yanageuka kuwa mkikimkiki wa ukombozi wa binadamu katika hali yake yote. Kanuni zake ndizo zifuatazo: Mungu yupo katika historia ya watu wake ili kuwakomboa. Naye ndiye Mungu wa walio maskini, ambaye hawezi kuvumilia ugandamizaji wala udhalimu. Ndiyo sababu ufafanuzi hawezi kutojihusisha, bali, kwa kumfuata Mungu, ni lazima ujipange upande wa maskini na kujibidiisha katika mapambano kwa ajili ya ukombozi wa wanaogandamizwa. Kushirikiana katika mapambano hayo kunawezesha maana mpya za matini za Biblia zidhihirike, ambazo zinavumbuliwa tu pindi matini zenyewe zinaposomwa katika mazingira ya mshikamano wa kweli na wanaogandamizwa. Maadamu ukombozi wa wanaogandamizwa ni mchakato wa pamoja, jumuiya ya maskini ndiyo mahali bora pa kuipokea Biblia kama neno la ukombozi. Aidha, madhali matini za Biblia ziliandikwa kwa ajili ya jumuiya, usomaji wa Biblia unakabidhiwa kwanza kwa jumuiya zenyewe. Neno la Mungu linahusiana kabisa na zama za leo, kwa sababu hasa ya uwezo wa “matukio kadhaa yenye kuweka msingi” (kutoka katika Misri, mateso na ufufuko wa Yesu) ya kusababisha matekelezo mapya katika mtiririko wa historia. Theolojia ya ukombozi ina mambo ndani yake ambayo thamani yake haiwezi kukanwa: utambuzi wenye kina wa kuwepo kwa Mungu mwenye kuokoa; msisitizo juu ya hali ya kijumuiya ya imani; hima ya utendaji uletao ukombozi wenye mizizi yake katika haki na upendo; usomaji upya wa Biblia unaojaribu kulifanya Neno la Mungu liwe mwanga na chakula cha watu wa Mungu katika mapambano yao na matarajio yao. Ndiyo inavyosisitizwa nguvu kamili iliyo nayo kwa siku za leo matini iliyovuviwa. Lakini usomaji wa Biblia wenye juhudi za namna hii unaleta hatari kadhaa ndani yake. Maadamu unahusiana na harakati inayoendelea bado, misisitizo inayofuata haina budi kuwa ya kitambo tu. Aina hii ya usomaji unamakinika hasa juu ya matini za kisimulizi na za kinabii (za Biblia) ambazo zinaangaza hali ya ugandamizaji na zinauchochea utendaji unaotaka kuleta mageuzi ya kijamii; hivyo yawezekana kuwa njia hii pengine inatazama sehemu tu ya ukweli, pasipo kuzingatia kwa mkazo ulio sawa matini nyingine za Biblia. Ni sahihi kusema kwamba ufafanuzi hauwezi kutojihusisha, lakini pia lazima ujitahadhari usifungamane na upande mmoja tu. Kwa upande mwingine, kushiriki katika harakati za kijamii na kisiasa si jukumu la moja kwa moja la mfafanuzi. Tena, baadhi ya wanatheolojia na wafafanuzi, kwa kutaka kupenyeza ujumbe wa kibiblia katika mazingira ya kijamii-kisiasa, walipaswa kutumia zana mbalimbali za uchanganuzi wa hali ya kijamii. Katika mtazamo huo, shule nyingine za theolojia ya ukombozi zilifanya uchanganuzi uliovuviwa na nadharia za kiyakinifu, na kuisoma Biblia ndani pia ya muundo huo; nalo halikukosa kuleta matatizo, hususan mintarafu kanuni ya kimaksi ya mapambano ya kitabaka. Kwa msukumo wa shida kubwa za kijamii, mkazo ulitiliwa zaidi juu ya eskatolojia ya kidunia, na pengine ukalidhuru suala la eskatolojia ya mbinguni ya Maandiko. Mageuzo ya kijamii na ya kisiasa yanafanya njia hiyo ijihoji upya na kutafuta maelekeo mapya. Kwa maendeleo yake ya baadaye na kwa manufaa yake katika Kanisa, suala kuu litakuwa kuainisha dhanio zake za kihemenetiki, kama vile mbinu zake na mshikamano wake na imani na Mapokeo ya Kanisa zima. Hemenetiki ya kifeministi (au ya mtazamokike) ya Biblia ilianzishwa mnamo mwishoni mwa karne XIX huko Marekani, katika mazingira ya kijamii-kiutamaduni ya mapambano kwa ajili ya haki za wanawake; ndipo kamati ya matengenezo ya Biblia ilipotoa “The Woman’s Bible” (“Biblia ya mwanamke”) katika vitabu viwili (New York 1885, 1898). Vuguvugu hiyo ilijidhihirisha kwa nguvu mpya na kuonyesha maendeleo makubwa kuanzia miaka ya sabini, ikifungamana na harakati ya ukombozi wa wanawake, hasa katika Amerika ya Kaskazini. Kwa kueleza kwa usahihi, inabidi kutofautisha aina mbalimbali za hemenetiki ya kifeministi ya Biblia, maana mbinu zinazotumika zahitilafiana sana. Umoja wake unatokana na dhamira hiyo moja, yaani wanawake, na pia na lengo linalokusudiwa: ukombozi wa wanawake na upatikanaji wa haki zilizo sawa na zile za wanaume. Inafaa kuzitaja hapa aina tatu za msingi za hemenetiki ya kifeministi ya Biblia: mtindo mkali, mtindo halisi-mamboleo, na mtindo wa kiuhakiki. Mtindo mkali unakataa kabisa mamlaka ya Biblia, na kushikilia nadharia ya kuwa Biblia ilitungwa na wanaume kwa madhumuni ya kuhakikisha utawala wa mwanaume juu ya mwanamke (androsentrismi). Mtindo halisi-mamboleo unaikubali Biblia kama neno la kinabii; nayo Biblia inasemwa kuwa inafaa kwa kadiri inavyoegemea upande wa wadhaifu na kwa hiyo pia upande wa wanawake; mtazamo huo unachukulika kama “kanoni ndani ya kanoni”, ili kudhihirisha wazi yale yote yanayosaidia ukombozi wa wanawake na haki zao. Mtindo wa kiuhakiki unatumia mbinu nyerevu ili kujaribu kuvumbua tena wadhifa na jukumu la wanawake wa kikristo katika kundi la wafuasi wa Yesu na katika Makanisa ya Mt. Paulo. Wakati huo – inavyodaiwa – kulikuwepo hali ya usawa; lakini hali hiyo ilisitiriwa katika maandishi ya Agano Jipya, kwa kiasi kikubwa, na hata zaidi baadaye, wakati ubabedume na androsentrismi vilipozidi kushinda. Hemenetiki ya kifeministi haikutengeneza mbinu mpya. Inatumia mbinu za kawaida za ufafanuzi, hasa ile ya kihistoria-kiuhakiki. Ila inaongeza vigezo viwili vya utafiti. Kigezo cha kwanza ndicho cha kifeministi, kinachofuata harakati ya ukombozi wa wanawake, katika mkondo mpana zaidi wa harakati ya theolojia ya ukombozi. Nacho kinatumia hemenetiki ya tuhuma: maadamu kwa kawaida historia imeandikwa na washindi, ili kufukua ukweli inafaa kutotegemea matini zenyewe, bali kutafuta ndani yake vidokezo vinavyoweza kuonyesha hali iliyo tofauti. Kigezo cha pili ni cha kisosholojia; hicho kina misingi yake katika utafiti wa jamii za nyakati za Biblia, wa tabaka zake za kijamii na wa nafasi ya wanawake ndani yake. Mintarafu maandishi ya Agano Jipya, mada ya uchunguzi si zaidi dhana ya mwanamke inavyoelezeka katika Agano Jipya, bali ni kuelewa kihistoria hali mbili tofauti za wanawake katika karne ya kwanza: yaani, kwa upande mmoja, hali yake ya kawaida katika jamii ya kiyahudi na ya kigiriki-kirumi; na kwa upande mwingine, hali iletayo mambo mapya iliyoanzishwa katika vuguvugu ya Yesu na katika Makanisa ya Mt. Paulo, ambapo iliundwa – inavyosemwa – “jumuiya ya wafuasi wa Yesu, wote wenye hali moja”. Matini mojawapo inayodaiwa kuwa msingi wa mtazamo huo ni Gal 3:28. Na lengo ni kuivumbua upya, kwa ajili ya nyakati zetu, historia iliyosahauliwa ya wadhifa wa wanawake katika Kanisa la mwanzoni. Michango mingi mizuri imeletwa kutokana na ufafanuzi wa kifeministi. Kwa njia hii wanawake wameshiriki kama watendaji hai katika utafiti wa kifafanuzi; nao wamefaulu kuvihisi – mara nyingi vizuri zaidi kuliko wanaume – uwepo, maana, na dhima vya mwanamke katika Biblia, katika historia ya asili za kikristo na katika Kanisa. Upeo wa utamaduni wa kisasa unazingatia kwa makini zaidi heshima ya mwanamke na dhima yake katika jamii na katika Kanisa; hivyo unafanya yaulizwe maswali mapya kwa matini ya Biblia, na kwa njia hii unaleta chanzo cha uvumbuzi mpya. Aidha, hisia za kike zinasaidia kufichua na kusahihisha baadhi ya fasiri zilizokuwa zinakubalika, zenye ubaguzi ndani yake na zilizolenga kuthibitisha kuwa ni halali utawala wa mwanamume juu ya mwanamke. Mintarafu Agano la Kale, chunguzi nyingi zimejibidisha kuufikia ufahamu mzuri zaidi wa sura ya Mungu. Mungu wa Biblia si matokeo ya muundo wa mawazo wa kiubabedume. Yeye ndiye Baba, lakini pia ni Mungu mwenye huruma na upendo wa kimama. Ila, ufafanuzi wa kifeministi, kwa kadiri unavyotokana na msimamo wa kiubaguzi, unaingia hatari ya kufasiri matini za Biblia kwa namna isiyo halisi, tena inayoweza kupingwa. Ili kuthibitisha msimamo wake mara nyingi ufafanuzi huo hauna njia nyingine isipokuwa kuzikimbilia hoja “ex silentio” (= zilizo kimya). Nazo, inavyoeleweka, haziaminiki sana, wala haziwezi kamwe kutosha ili kulifikia hitimisho lililo imara. Kwa upande mwingine, ufafanuzi huo umefanya jitihada ili kuielewa hali fulani ya kihistoria kwa kuvizingatia vidokezo vyepesi vinavyopatikana katika matini; tena unadhani kuwa matini hizo zinataka kuificha hali hiyo ya kihistoria. Kumbe hii si tena kazi ya ufafanuzi timamu, kwa maana inafikia hatua ya kukataa maudhui ya matini zilizovuviwa ili kupendekeza badala yake mtungo mpya tofauti na wa kinadharia tete tu. Mara nyingi ufafanuzi wa kifeministi unazusha pia suala la utawala katika Kanisa; suala ambalo, inavyojulikana, ni mada ya majadiliano na pia ya migongano. Katika uwanja huo, ufafanuzi wa kifeministi utaweza kuleta manufaa kwa Kanisa kwa kadiri tu utakavyoepukana na mitego ileile inayoilaumu, na pia utakavyozingatia mafundisho ya kiinjili kuhusu utawala kama utumishi, mafundisho yaliyoelekezwa na Yesu kwa wanafunzi wote, wanaume kwa wanawake[2]. F. Ufasiri wa kifundamentalisti Usomaji wa kifundamentalisti una asili yake katika kanuni ya kwamba Biblia, maadamu ni Neno la Mungu lenye kuvuviwa na lisilopatwa na kosa, haina budi kusomwa na kufasiriwa kisisisi katika vipengere vyake vyote. Ila usomaji huo unafasili “ufasiri sisisi” (literal interpretation) ukimaanisha ufasiri “wa kiherufi” (naively literalist), ambao unajikita katika usisisi na kukataa kila jitihada ya kuielewa Biblia kwa kuzingatia ukuzi wake katika mfululizo wa historia na maendeleo yake. Hivyo, unapinga matumizi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki kwa ufasiri wa Maandiko Matakatifu, kama vile ya mbinu yoyote nyingine ya kisayansi. Usomaji wa kifundamentalisti ulianzishwa, nyakati za Matengenezo (Reformation), kutokana na kero ya kuwa waaminifu kwa maana sisisi ya Maandiko. Baada ya karne ya Mwangazo (Enlightenment), ulijifahamisha katika Uprotestanti kama kinga dhidi ya ufafanuzi huria (liberal exegesis). Jina “Ufundamentalisti” lilitumika kwa mara ya kwanza katika Warsha ya Kibiblia ya Kimarekani iliyofanyika huko Niagara, jimbo la New York, mwaka 1895. Katika nafasi hiyo wafafanuzi waprotestanti wahifadhina (conservative) waliweka “pointi tano za ufundamentalisti”: kutokukosa kwa kila neno la Maandiko (verbal inerrancy), umungu wa Kristo, kuzaliwa kwake kutoka kwa bikira, mafundisho ya fidia kaimu (vicarious expiation), na ufufuko wa miili wakati wa ujio wa pili wa Kristo. Pindi usomaji wa kifundamentalisti ulipotapakaa katika sehemu nyingine za ulimwengu ulizalisha namna nyingine za kusoma Biblia, nazo zenye tabia ya “usisisi wa kiherufi” (literalist), katika Ulaya, Asia, Afrika na Amerika ya Kusini. Mtindo huo wa usomaji unazidi kupata washiriki wengi, katika miaka ya mwisho ya karne ya ishirini, miongoni mwa vikundi vya kidini na madhehebu, na pia kati ya Wakatoliki. Ufundamentalisti unaweza kuwa na haki kukazia uvuvio wa kimungu wa Biblia, kutokukosa kwa Neno la Mungu na kweli nyingine za kibiblia zilizomo katika pointi zile tano za msingi; lakini namna yake ya kueleza kweli hizo ina mizizi yake katika itikadi isiyo ya kibiblia, yawayo yote wayaseme wawakilishi wake. Maana, itikadi hiyo inadai kuambatana imara na kwa hakika na mazoea makali ya kimafundisho, pia inauweka kama sharti, kama chemchemi pekee ya ufundishaji kuhusu maisha ya kikristo na ya wokovu, usomaji wa Biblia unaokataa kila tabia au utafiti vya kiuhakiki. Shida ya msingi ya usomaji huo wa kifundamentalisti ni kwamba unakataa kujali tabia ya kihistoria ya ufunuo wa Biblia, na hivyo unajifanya hauwezi kuupokea kikamilifu ukweli wa Umwilisho wenyewe. Ufundamentalisti unakwepa uhusiano wa kiundani uliopo kati ya kilicho cha kimungu na kilicho cha kibinadamu katika kuhusiana na Mungu. Tena unakataa kukubali kwamba Neno la Mungu lililovuviwa lilielezwa kwa lugha ya kibinadamu na kuhaririwa, chini ya uvuvio wa kimungu, na waandishi wa kibinadamu ambao uweza na maarifa vyao vilikuwa na mipaka. Ndiyo sababu mwelekeo wake ni kujali matini ya Biblia kana kwamba imeandikwa mfano wa imla, neno kwa neno, kwa kazi ya Roho Mtakatifu; wala haufikii kutambua kuwa Neno la Mungu lilitungwa kwa lugha na semi zilizoathiriwa na mazingira ya nyakati fulani. Na kadiri yake hakuna uzingativu wowote kwa fani za kifasihi na kwa miundo ya kibinadamu ya mawazo iliyopo katika matini za Biblia, ambazo nyingi zake ndizo tunda la mchakato ulioendelea kwa muda mrefu na kubeba athari za hali mbalimbali za kihistoria. Aidha, ufundamentalisti hukazia kwa namna isivyofaa kutokukosa hata kwa vipengele vidogo vidogo (details) vya matini za Biblia, hasa kuhusu matukio ya kihistoria au mintarafu kweli zinazodaiwa kuwa na uzito wa kisayansi. Mara nyingi hukitilia maana ya kihistoria kile kisichokuwa na dai hilo, kwa sababu huyahesabu kama matukio ya kihistoria yale yote yaelezwayo au kusimuliwa kwa vitenzi vinavyotumika katika wakati uliopita; wala hauzingatii kama ipasavyo uwezekano wa kuwepo maana ya kiishara au ya kitamathali. Mara nyingi ufundamentalisti una tabia ya kutojali au kukanusha matata yaliyopo katika matini ya Biblia katika utungo wake wa Kiebrania, Kiaramu au Kigiriki. Mara nyingi hufungamana na tafsiri fulani maalum (ya Biblia), ya zamani au ya kisasa. Na vilevile huacha kuzingatia “kusoma upya” (relectures) kwa sehemu kadhaa za Biblia kunakofanyika katika Biblia yenyewe. Kuhusu Injili, ufundamentalisti haujali ukuzi wa mapokeo ya kiinjili, bali unachanganya moja kwa moja hatua ya mwisho ya mapokeo hayo (yaani waliyoyaandika wainjili) na hatua yake ya kwanza (yaani matendo na maneno ya Yesu wa kihistoria). Na wakati huohuo lapuuzwa suala lililo muhimu: yaani namna jumuiya zenyewe za kwanza za kikristo zilivyoelewa athari iliyoletwa na Yesu wa Nazareti na ujumbe wake. Kumbe, papo hapo tunao ushuhuda wa asili ya kitume ya imani ya kikristo, na pia ujumbe wake wazi. Kwa njia hii, ufundamentalisti unaumbua hulka ya wito unaotolewa na Injili yenyewe. Aidha, ufundamentalisti unaleta mitazamo finyu sana: maana unaamini kuwa kosmolojia ile ya kale, iliyokwisha futwa, bado inalingana na ukweli; na sababu yake ni kwamba inaelezwa hivyo katika Biblia. Hali hii inazuia isifanyike dialogia na upeo mpana zaidi wa mahusiano yaliyopo baina ya utamaduni na imani. Tena hutegemea usomaji usio wa kiuhakiki wa matini kadhaa za Biblia ili kuthibitisha maoni ya kisiasa na mitazamo ya kijamii vinavyoathiriwa na ubaguzi, kwa mfano ubaguzi wa kikabila, ambao haulingani katu na Injili ya Kristo. Na hatimaye, katika kushikamana kwake na kanuni ya “Maandiko tu” ufundamentalisti hutenganisha ufasiri wa Biblia na Mapokeo yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, na ambayo hujiendeleza kwa namna iliyo halisi kwa kuungana na Maandiko ndani kabisa ya jumuiya ya imani. Ufundamentalisti hauna utambuzi wa kwamba Agano Jipya limeumbika (took form) ndani ya Kanisa la kikristo na kwamba ndilo Maandiko Matakatifu ya Kanisa hili, ambalo kuwepo kwake kuliutangulia utungaji wa matini zake. Ndiyo maana, mara nyingi ufundamentalisti unapinga Kanisa, kwa kupuuza kanuni za imani, dogma na ibada za kiliturujia ambazo zimekuwa sehemu muhimu za mapokeo ya kikanisa; hali kadhalika, kwa kupuuza jukumu la kufundisha la Kanisa lenyewe. Hivyo unajionyesha kama namna ya ufasiri wa kibinafsi, ambao hautambui kuwa Kanisa limejengwa juu ya Biblia na kuchota uzima wake na msukumo wake katika Maandiko. Njia ya kifundamentalisti ni ya hatari, kwa sababu huwavuta watu wanaotafuta majibu katika Biblia kwa matatizo ya maisha yao. Na njia hiyo huweza kuwatia mauzauza kwa kutoa fasiri zenye hali ya utakatifu lakini yanayodanganya, badala ya kuwaambia wao kwamba Biblia si lazima iwe na jibu la mara moja kwa kila moja ya matatizo hayo. Bila ya kutamka, ufundamentalisti huwaalika watu katika aina fulani ya kujiua kwa mawazo. Tena unatia maishani uhakika wa uongo, kwa maana huichanganya pasipo kutambua mipaka ya kibinadamu ya ujumbe wa Biblia na udhati wa kimungu wa ujumbe huo. Mwendo wa ufafanuzi unaitwa kufikiriwa tena kwa kuzingatia hemenetiki ya kifalsafa ya siku hizi, ambayo imesisitiza dhima ya hisia-mtu (subjectivity) katika mchakato wa ujuzi, na hasa katika ujuzi wa kihistoria. Tafakuri ya kihemenetiki imepata mwamko mpya kwa uchapishaji wa kazi za Friedrich Schleiermacher, Wilhelm Dilthey, na hasa vya Martin Heidegger. Katika mkondo wa wanafalsafa hao – lakini pia kwa kutofautiana nao – wasomi kadhaa wamechimba kiundani zaidi nadharia ya hemenetiki ya siku za leo, na matumizi yake kwenye Maandiko Matakatifu. Miongoni mwao tutawataja hasa Rudolf Bultmann, Hans Georg Gadamer na Paul Ricoeur. Haiwezekani hapa kueleza kwa muhtasari wa kuridhisha fikra zao. Itoshe tu kusisitiza baadhi ya mawazo ya msingi ya falsafa yao ambayo huathiri ufasiri wa matini za Biblia [3]. Akitambua umbali wa kiutamaduni uliopo baina ya ulimwengu wa karne ya kwanza na ule wa karne ya ishirini, Bultmann amejibidisha ili uhalisi unaoongelewa na Maandiko Matakatifu uongee pia na binadamu wa nyakati zetu. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa ufahamu tangulizi unaohitajika kwa kila ufahamu, na ametengeneza nadharia ya ufasiri wa kiudhanaishi (existential) wa maandishi ya Agano Jipya. Kwa kutegemea fikra za Heidegger, Bultmann asema kwamba ufafanuzi wa matini fulani ya Biblia hauwezekani pasipo dhanio tangulizi (presuppositions) kadhaa zenye kuuongoza ufahamu wake. Na ufahamu tangulizi (“Vorverständnis”) una msingi wake katika uhusiano wa kimaisha (“Lebenverhältnis”) baina ya mfasiri na lile jambo linaloongelewa na matini. Ili kukwepa ufasiri unaotawaliwa na uhisiamtu, ufahamu tangulizi ni lazima ukubali kuongezewa kina na kutajirishwa na kile kinachoongelewa na matini, na hata kurekebishwa na kusahihishwa nacho. Tena, Bultmann anajihoji ni muundo upi wa fikra ulio sahihi kwa minajili ya kutunga maswali ambayo kuanzia nayo matini za Maandiko zitaeleweka kwa watu wa nyakati zetu. Naye anadai kuwa jawabu hupatikana katika uchanganuzi wa kiudhanaishi wa Heidegger. Kadiri yake kanuni za kiudhanaishi za ki-Heidegger zaweza kutumika katika nyanja zote, nazo zinaweka miundo na dhana zenye kufaa zaidi kwa ufahamu wa maisha ya kibinadamu yanavyofunuliwa katika ujumbe wa Agano Jipya. Gadamer vilevile akaza umbali wa kihistoria uliopo baina ya matini na mfasiri wake. Naye anafuata na kuendeleza nadharia ya “duara ya kihemenetiki” (hermeneutical circle). Vitarajio (anticipations) na dhana tangulizi (preconceptions) vinavyoathiri ufahamu wetu hutokana na mapokeo yanayotutegemeza. Nao ni jumla ya data za kihistoria na kiutamaduni zilizo mazingira yetu ya kimaisha na upeo wetu wa ufahamu. Basi, mfasiri anawajibika kuingia katika mjadala na uhalisi unaozungumziwa katika matini. Na ufahamu hupatikana katika muungano wa peo mbili tofauti, yaani upeo wa matini na ule wa msomaji wake (“Horizontverschmelzung”); nao ufahamu huwezekana ikiwa tu kuna mwingiliano (belonging, “Zugehörigkeit”), yaani uwiano wa kimsingi kati ya mfasiri na matini anayozingatia. Hemenetiki ni mchakato wa kimjadala (dialectical process): maana ufahamu wa matini fulani u daima pia ufahamu mpana zaidi apatao mfasiri juu yake mwenyewe. Mintarafu fikra za kihemenetiki za Ricoeur, awali ya yote yabidi kusisitiza umuhimu wa “dhima ya kujiweka mbali”; nayo ni utangulizi wa lazima wa kujitwalia matini kisahihi. Maana, kwanza upo umbali baina ya matini na mwandishi wake, kwa sababu matini ikiisha tungwa, kwa kiasi fulani inaanza kujitegemea yenyewe mbali na mtungaji wake; nayo inaanza safari ya ile iliyo maana yake. Pili, upo umbali baina ya matini na wasomaji wake wa baadaye; hawa hawana budi kuyaheshimu mazingira ya matini katika hali yake ya utofauti. Hivyo, mbinu za uchanganuzi wa kifasihi na wa kihistoria ni za lazima kwa ufasiri. Walakini maana ya matini fulani yaweza kupatikana kikamilifu ikiwa tu yenyewe inahusishwa (is actualized) katika maisha ya wasomaji wanaojitwalia. Nao, kutokana na hali yao, watakiwa kuzidokeza maana mpya zinazoendana na ile ya msingi inayoonyeshwa na matini. Ujuzi wa kibiblia hauwezi kujikita katika lugha tu, bali unajibidisha kuufikia uhalisi unaoongelewa na matini. Lugha ya kidini ya Biblia ni lugha ya kiishara “inayofikirisha” (“gives rise to thought”), tena ni lugha ambayo binadamu hakomi kuuvumbua utajiri mwingi wa maana yake; na hatimaye ni lugha inayolenga katika kikomo kinachopita ufahamu, na wakati huohuo inayomfanya binadamu afahamu ukweli wenye kina wa maisha yake (personal existence). Je, tuseme nini juu ya nadharia hizo za nyakati zetu zihusuzo ufasiri wa matini? Biblia ndilo Neno la Mungu kwa nyakati zote zifuatanazo katika historia. Na kutokana na hilo haiwezekani kutojali nadharia ya kihemenetiki inayowezesha kuingiza mbinu za uhakiki wa kifasihi na wa kihistoria katika mtindo wa ufasiri ulio mpana zaidi. Ni suala la kuuvuka umbali uliopo baina ya wakati wa waandishi na walengwa wa kwanza wa hizo matini za Biblia na ule wa kwetu, hivi kwamba iwezekane kuuhusisha (actualization) kwa usahihi ujumbe wa matini ili kulisha maisha ya imani ya wakristo. Kila ufafanuzi wa matini unaitwa kukamilishwa kwa njia ya “hemenetiki”, kadiri ya maana hilo neno liliyopewa siku za karibuni. Ulazima wa hemenetiki, yaani wa ufasiri wa matini katika mazingira ya siku za leo ya ulimwengu wetu, una msingi wake katika Biblia yenyewe na katika historia ya ufasiri wake. Jumla ya maandishi ya Agano la Kale na Agano Jipya hujionyesha kama tunda la mchakato wa muda mrefu wa kufasiri upya matukio ya kuweka misingi, kwa kuyahusianisha kiundani na maisha ya jumuiya za waamini. Katika mapokeo ya Kanisa wafasiri wa kwanza wa Maandiko Matakatifu, ndio Mababa wa Kanisa, walidhani kwamba ufafanuzi wao umekamilika ukiwa tu walifaulu kuitokeza maana ya matini kwa ajili ya wakristo wa nyakati zao na katika mazingira yao. Ufafanuzi ni mwaminifu kwa nia ya matini za Biblia kwa kadiri ile tu ambayo unajitahidi kupata – katika mtima wa mitungo ya matini yenyewe – uhalisi wa imani ambayo matini zinaonyesha; tena ikiwa unaunganisha uhalisi huo na mang’amuzi ya kiimani ya ulimwengu wetu. Hemenetiki ya siku za leo ni jibu lifaalo kwa falsafa umbile ya kihistoria na kwa kishawishi cha kuvitumia katika mtaala wa Biblia vile vigezo visivyoathiriwa na hisia za kibinafsi (objective), ambavyo hutumika katika sayansi asilia (natural science). Kwa upande mmoja, matukio yasimuliwayo katika Biblia ni matukio yaliyofasiriwa; kwa upande mwingine, kila ufafanuzi wa masimulizi ya matukio hayo hauna budi kuhusisha athari ya hisia (subjectivity) za mfafanuzi mwenyewe. Ufahamu sahihi wa matini ya Biblia unapatikana tu kwake yeye aliye na uhusiano wa kimaisha na kile kinachoongelewa na matini. Suala linalomkabili kila mfasiri ndilo hili lifuatalo: je, ni nadharia ipi ya kihemenetiki inayowezesha ufahamu sahihi wa uhalisi kiundani unaoongelewa na Maandiko Matakatifu; na ni nadharia ipi inayowezesha kuelezea uhalisi huo kwa namna iliyo na maana kwa binadamu wa siku za leo? Kwa kweli, inabidi kutambua kwamba baadhi ya nadharia ya kihemenetiki hazitoshi ili kuyafasiri Maandiko Matakatifu. K.m. ufasiri wa kiudhanaishi wa Bultmann unaelekeza kufunga ujumbe wa kikristo katika mipaka ya falsafa moja ya pekee. Aidha, kwa ajili ya dhanio tangulizi (presuppositions) zilizo misingi ya hemenetiki hiyo, ujumbe wa kidini wa Biblia unanyimwa sehemu kubwa ya uhalisia (objective reality) wake (kwa sababu ya kupunguza mno utakatifu wake – démytholygization); hivyo unawekwa chini ya utawala wa ujumbe wa kianthropolojia. Falsafa inakuwa kanuni ya ufasiri badala ya kuwa chombo cha ufahamu wa kile kilicho kiini kabisa cha kila ufasiri: yaani nafsi ya Yesu Kristo na matukio ya wokovu yaliyotimizwa katika historia yetu. Hivyo, ufasiri wa Maandiko, awali ya yote ni kuipokea maana iliyopo katika matukio kadhaa na, kwa namna iliyo bora zaidi, katika nafsi ya Yesu Kristo. Hii ndiyo maana ielezwayo katika matini. Na ili kuepukana na namna za usomaji zinazotegemea hisia za kibinafsi tu (purely subjective readings), ni lazima ufasiri ufaao kwa wakati huu (actualization) uwe na msingi katika uchunguzi wa matini, na dhanio tangulizi za ufasiri huo hazina budi kuhakikishwa tena na tena katika matini yenyewe. Hemenetiki ya kibiblia, ijapo ni sehemu ya hemenetiki ya jumla ya kila matini ya kifasihi na kihistoria, wakati huohuo ni kipengere pekee cha hemenetiki hiyo. Na upekee wake hutokana na kile kinachochunguzwa nayo. Kwani matukio ya wokovu na utimilifu wake katika nafsi ya Yesu Kristo vinaipa historia yote ya kibinadamu maana yake halisi. Fasiri mpya za kihistoria zitaweza tu kuwa ufunuo au uonyesho wa utajiri huo wa maana. Simulizi la kibiblia la matukio hayo haliwezi kueleweka kikamilifu na akili peke yake. Ufasiri wake hauna budi kuongozwa na matukio tangulizi (presuppositons) kadhaa, yaani, k.m. kuishi imani katika jumuiya ya kikanisa, na kuwa na mwanga wa Roho Mtakatifu. Jinsi yanavyokua maisha katika Roho, ndivyo ukuavyo pia ufahamu wa msomaji kuhusu yale yote yanayoongelewa na matini ya Biblia. B. Maana (au fahiwa) za Maandiko yaliyovuviwa Mchango wa siku za leo wa hemenetiki za kifalsafa na maendeleo ya hivi karibuni ya mtaala wa kisayansi wa fasihi mbalimbali vinauwezesha ufafanuzi wa kibiblia kuchimba ndani ya ufahamu wa wajibu wake, ambao uchangamano (complexity) wake umekuwa dhahiri zaidi. Ufafanuzi wa kale, ambao yakini haukuweza kuzingatia madai ya kisayansi ya nyakati zetu, uliihesabia kila matini ya Maandiko viwango mbalimbali vya maana. Upambanuzi uliotangaa zaidi ulikuwa kati ya maana sisisi (literal sense) na maana ya kiroho (spiritual sense). Ufafanuzi wa Enzi ya Kati (Medieval exegesis) ulipambanua katika maana ya kiroho mandhari tatu tofauti: mandhari ya kwanza inahusiana na ukweli uliofunuliwa; ya pili, inahusiana na mwenendo unaotakiwa kufuatwa; na ya tatu, na utimilifu wa nyakati za mwisho. Tokea hayo ilitungwa beti maarufu, inayojulikana kuwa ya Augustino wa Denmark (karne ya 13): “Littera gesta docet, quid credas allegoria, moralis quid agas, quid speres anagogia” (= “Maana sisisi hufunza matukio; maana ya mifano, nini usadiki; maana ya maadili, ufanye nini; maana za umilele, wapi unakoelekea”). Dhidi ya uwingi huo wa maana, ufafanuzi ya kihistoria-kiuhakiki umeshikilia – kwa wazi ama sivyo – nadharia ya umoja wa maana, ambayo kadiri yake matini haiwezi kuwa na maana mbalimbali kwa wakati mmoja. Bidii zote za ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki zinalenga kufasili ile maana halisi ya matini fulani ya Biblia kadiri ya mazingira ambamo imetungwa. Lakini nadharia hiyo hugongana sasa na fikra za sayansi za lugha na za hemenetiki za kifalsafa, zisemazo kwamba maandishi huleta maana nyingi (plurality of meanings). Suala hili si sahili, wala haliwezi kukabiliwa kwa mtazamo uleule mmoja katika tanzu zote za matini: k.m., masimulizi ya kihistoria, mifano, maaguzi, sheria, mithali, sala, tenzi, n.k. Hata hivyo, yawezekana kueleza kanuni kadhaa, tukizingatia daima tofauti ya rai mbalimbali. Si halali tu, bali ni ya lazima kujaribu kuifasili maana kamili ya matini kadiri zilivyotungwa na waandishi wake; na hiyo maana huitwa “sisisi”. Mt. Thomaso wa Akwino alikuwa amekwisha kusisitiza umuhimu wake wa msingi (S. Th., I, q. 1, a. 10, ad 1). Maana sisisi haipaswi kuchanganywa na maana ya “kiherufi” ambayo wafundamentalisti hushikamana nayo. Haitoshi kuitafsiri matini neno kwa neno ili kupata maana yake sisisi. Kwani ni lazima kuielewa matini kwa mujibu wa kaida za kifasihi za wakati wake. Ikiwa ni matini ya kiistiara, maana yake sisisi si ile itokanayo moja kwa moja na maneno yenyewe, (kwa mfano; “Viuno vyenu na viwe vimefungwa”, Lk 12:35), bali ile inayolingana na matumizi ya kiistiara ya maneno yale (“Mwe tayari kila wakati”). Tena ikiwa ni masimulizi, maana sisisi si lazima idai kuwa matukio yaliyosimuliwa hakika yamejiri; maana masimulizi hayo hayaingii moja kwa moja utanzu wa kihistoria, bali yaweza kuwa yamebuniwa tu. Maana sisisi ya Maandiko Matakatifu ndiyo ile iliyowekwa moja kwa moja na wanadamu walioyatunga kwa uvuvio wa kimungu. Nayo maana, maadamu ni tunda la uvuvio huo, ilikusudiwa na Mungu pia, aliye mtunzi mkuu. Tena inagunduliwa kwa njia ya uchanganuzi maalumu wa matini, baada ya kuiweka katika mazingira yake ya kifasihi na ya kihistoria. Jukumu la kwanza la ufafanuzi ndilo la kuongoza katika uchanganuzi huo, kwa kuzitumia fursa zote zinazowezekana za tafiti za kifasihi na za kihistoria, kwa madhumuni ya kuifasili maana sisisi ya matini za Biblia kwa usahihi kamili iwezekanavyo (Divino afflante Spiritu, EB 550). Kwa lengo hilo, mtaala wa tanzu za fasihi andishi za zamani hasa hudaiwa (ibid. 560). Je, na maana sisisi ya matini fulani ni moja tu? Kwa kawaida, ndiyo. Lakini si lazima iwe hivyo kila mara; na sababu zake ni hizo mbili zifuatazo. Kwa upande mmoja, mwandishi mtu anaweza kudhamiria maana mbili tofauti kwa wakati mmoja; nalo ni la kawaida katika ushairi. Uvuvio wa Biblia haudharau mtazamo huo wa kisaikolojia na wa lugha ya kibinadamu; na Injili ya nne huleta mifano mingi ya jambo hilo. Kwa upande mwingine, hata pale usemi wa kibinadamu unapoonekana kuleta maana moja tu, ndipo uvuvio wa kimungu huweza kuongoza huo usemi na hivi kusababisha kuwepo zaidi ya maana moja (ambivalence). Ndivyo inavyotokea katika usemi wa Kayafa katika Injili ya Yohane 11:50, ambao kwa wakati mmoja humaanisha hila potofu ya kisiasa na pia ufunuo wa kimungu. Mandhari hizo mbili zinaingia zote katika maana sisisi, kwani zote zinaeleweka kufuatana na muktadha. Na ijapo huo ni mfano wa pekee, hata hivyo ni wa maana sana; tena, lazima ututahadharishe dhidi ya dhana iliyo finyu mno ya maana sisisi ya matini zilizovuviwa. Kwa namna ya pekee, yafaa kuzingatia hali ya kimkikimkiki (dynamic aspect) ya matini zilizo nyingi. Kwa mfano, maana ya zaburi za kifalme lazima isifungwe tu ndani ya mazingira ya kihistoria ambamo zilitungwa. Akimzungumzia mfalme, mtunga zaburi alikuwa anadokeza kwa wakati mmoja mtindo wa asasi ya ufalme uliokuwepo, na mwingine unaotarajiwa na unaolingana na mpango wa Mungu; hivyo matini ya huyo mtunzi ilikuwa ikitazama mbele zaidi kuliko ile asasi ya ufalme uliojidhihirisha katika historia. Mara nyingi mno ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki umeelekea katika kupunguza maana ya matini kwa kuifungamanisha tu na mazingira maalumu ya kihistoria. Badala yake, ingebidi huo ufafanuzi ujitahidi kubainisha mwelekeo wa fikra zinazoelezwa katika matini; nao mwelekeo, mbali na kumsukuma mfafanuzi kuiwekea mipaka maana ya matini, kinyume chake umsaidie kuhisi miendelezo yake inayotabirika wazi ama sivyo. Mkondo mmojawapo wa hemenetiki ya kisasa umesisitiza tofauti ya hadhi ambayo neno la binadamu linafaidi pale linapoandikwa. Matini iliyoandikwa inaweza kutiwa katika mazingira mapya yanayoiangaza kwa namna tofauti, na yenye kuziongeza maana (meanings) mpya kwa maana, au fahiwa, (sense) yake asilia. Uwezo huo wa matini iliyoandikwa unadhihirika hasa katika matini za Biblia, zinazokubaliwa kuwa neno la Mungu. Na kweli, kitu kilichofanya jumuiya ya waamini izihifadhi hizo matini kilikuwa kusadiki kwamba zitaendelea kuleta mwanga na uzima kwa vizazi vijavyo. Hivyo, tangu awali maana sisisi ina muundo wa kuyapokea maendelezo mapya, kwa njia ya “kuzisoma upya” (relectures) matini ndani ya mazingira mapya. Ila kinachotokana na hayo si kwamba huwezekana kuipa matini ya Biblia maana yoyote ile, kwa kuifasiri kila mtu anavyopenda. Kinyume chake, ni lazima kukataa kama ufafanuzi usio wa kweli kila ufasiri ulio “mgeni” (alien) kulingana na maana iliyokusudiwa na wanadamu walioandika matini yao. Kuzikubali maana zilizo ngeni (Kifr. hétérogènes) ingekuwa sawa na kung’oa ujumbe wa Biblia katika mizizi yake, yaani neno la Mungu lililowasilishwa katika historia; na vilevile ni kuyafungulia mlango maoni ya kibinafsi yasiyoweza kudhibitiwa. Hata hivyo; haifai kulichukua neno “ugeni” (hétérogènes) katika maana iliyo finyu, yaani yenye kupinga kila uwezekano wa utimilifu ulio bora zaidi. Tukio la Pasaka, la kifo na ufufuko wa Yesu, limeyaweka mazingira ya kihistoria yaliyo mapya kabisa, ambamo huangaza upya matini za kale na kusababisha mabadiliko katika maana yake ya kwanza. Kwa namna ya pekee, matini kadhaa ambazo, katika mazingira ya kale, zilitazamwa kuwa kama chuku (hyperbole) (k.m. uaguzi ambao kwao Mungu, akiongelea mwana wa Daudi, aliahidi kwamba atauweka imara ufalme wake hata milele: 2Sam 7:12-13; 1Nya 17:11-14), matini hizo hazina budi kuchukuliwa sasa katika maana yake sisisi, kwa kuwa “Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena” (Rum 6:9). Na hapo, wale wafafanuzi walio na dhana finyu, ya “kihistoria”, ya maana sisisi, inayokubali tu ile maana itokanayo na mazingira ya kihistoria ambamo matini zilitungwa, hao watafikiri kwamba pana “ugeni” kati ya ufafanuzi huo na matini asilia. Bali wale wanaoikubali “hali ya kimkikimkiki” ya matini watatambua kuwepo mwendelezo mkubwa, na wakati huohuo kuwepo pia njia ya kuingia katika kiwango kilicho tofauti: Kristo hutawala hata milele, lakini si kwa kukikalia kiti cha kidunia cha mfalme Daudi (taz. pia Zab 2:7-8; 110:1-4). Katika nafasi kama hizo linatumika neno “maana ya kiroho”. Kwa ujumla, kadiri ya imani ya kikristo, twaweza kufasili “maana ya kiroho” kuwa ile maana inayoonyeshwa na matini za Biblia zinaposomwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu na ndani ya mazingira ya fumbo la kipasaka la Kristo na ya maisha mapya yanayotokana nalo. Nayo mazingira ni ya kweli kabisa. Agano Jipya hutambua ndani yake utimilifu wa Maandiko Matakatifu. Hivyo ni kawaida kuyasoma upya Maandiko katika mwanga wa mazingira haya mapya, ndiyo yale ya maisha katika Roho. Kutokana na fasili hiyo, mengi yaweza kusisitizwa mintarafu uhusiano baina ya maana ya kiroho na maana sisisi. Kinyume cha kauli ya kawaida, si lazima kuwepo tofauti kati ya maana hizo mbili. Kwani, pale matini ya Biblia ilizungumziapo moja kwa moja fumbo la kipasaka la Kristo ama maisha mapya yatokanayo nalo, ndipo maana yake sisisi ni tayari maana mojawapo ya kiroho. Ndicho kitokeacho kama kawaida yake katika Agano Jipya. Hivyo hutokana kwamba ufafanuzi wa kikristo mara nyingi zaidi huongelea maana ya kiroho ukilielekea Agano la Kale. Lakini hata kuanzia katika Agano la Kale pana sehemu nyingi ambapo matini zina maana ya kidini na ya kiroho kama maana yake sisisi. Na katika sehemu hizi imani ya kikristo inatambua dalili za kwanza za uhusiano wake na maisha mapya yaletwayo na Kristo. Iwapo kuna tofauti, maana ya kiroho haiwezi kamwe kunyimwa uhusiano wake na maana sisisi ambayo inaendelea kuwa msingi wake wa lazima; kama sivyo, isingewezekana kuuzungumzia “utimilifu” (fulfilment) wa Maandiko. Na kwa kweli, ili tuweze kuuzungumzia utimilifu, ni sharti uwepo uhusiano wa mfulizo na uwiano maridhawa baina ya maana hizo mbili. Lakini pia ni lazima iwepo njia ya kuingia katika kiwango kilicho bora zaidi cha uhalisi. Maana ya kiroho isichanganywe na fasiri zinazojengwa juu ya hisia za watu binafsi na zitokanazo na ubunifu wao au na utafiti wa kiakili (intellectual speculation). Maana hiyo ya kiroho inazaliwa na uhusiano wa matini na matukio ya kweli yasiyo mageni kwake, yaani tukio la kipasaka na neema zake zisizokoma; nayo ndiyo kilele cha kazi za Mungu katika historia ya Israeli, kwa manufaa ya wanadamu wote. Usomaji wa kiroho, uwe umefanyika kijumuiya ama kibinafsi, unatambua maana ya kiroho ikiwa tu utajitunza ndani ya mitazamo hiyo. Ndipo vinaweza kuhusianishwa viwango vitatu hivyo vya uhalisi: matini ya Biblia, fumbo la kipasaka, na hali halisi ya maisha katika Roho. Ufafanuzi wa kale ulikuwa na hakika kuwa fumbo la Kristo ni ufunguo wa kuyafasiria Maandiko yote; hivyo ulijibidisha kuipata maana ya kiroho katika mambo madogo madogo ya matini za Biblia – kwa mfano, katika hila agizo la sheria za kiibada – ukitumia mbinu za kirabi au ukiathiriwa na mbinu za kiistiari za kigiriki (Hellenistic allegorical method). Ufafanuzi wa siku hizi hauwezi kuzitazama mbinu za namna hii kama mtindo halisi wa ufasiri, yoyote yale yaliyokuwa manufaa yake ya kichungaji katika nyakati zilizopita (taz. Divino afflante Spiritu, EB 553). Mandhari mojawapo inayokubalika ya maana ya kiroho ni maana ya kifananisho (typological); nayo kawaida inasemwa kuwa haiyahusu Maandiko yenyewe, bali yale mambo yanayoelezwa na Maandiko: Adamu ni mfano wa Kristo (taz. Rum 5:14), gharika ni mfano wa ubatizo (1Pet 3:20-21), n.k. Ni kweli kwamba uhusiano huo, wa kitu kimoja kuwa mfano wa kingine, kwa kawaida una msingi wake katika jinsi Maandiko yanavyoeleza kile kitu cha kwanza (taz. sauti ya Abeli: Mwa 4:10; Ebr 11:4; 12:24), wala si katika kitu kile cha kwanza chenyewe. Kwa hiyo, hapo tunaweza kusema kwamba hiyo maana imo kweli katika Maandiko yenyewe. Jina hili, “maana timilifu” (sensus plenior), ni msamiati usio wa muda mrefu, nalo linazusha mijadala. Kwa jina “maana timilifu” inaelezwa maana ya kina zaidi katika matini, maana iliyotakiwa na Mungu, lakini bila kudhihirishwa wazi na mwandishi mtu. Inawezekana kuigundua katika matini fulani ya Biblia ikichunguzwa katika mwanga wa sehemu nyingine za Biblia zinazoitumia, au katika uhusiano wake na maendeleo ya ndani ya ufunuo. Hapo [maana timilifu] ni maana ile ambayo mwandishi mtakatifu anaiona katika matini iliyotangulia kuandikwa kabla yake, pale anapoinukulu katika muktadha unaoipa maana sisisi mpya; au ni maana ile ambayo mapokeo ya kimafundisho yaliyo halisi, au tamko la Mtaguso, huitia kwenye matini fulani ya Biblia. Kwa mfano, muktadha wa Mt 1:23 unaleta maana timilifu kwa maneno ya unabii ya Isa 7:14 kuhusu almah atakayechukua mimba, kwa kutumia tafsiri ya Septuajinta parthenos: “Bikira atachukua mimba”. Mafundisho ya Mababa wa Kanisa na ya Mitaguso kuhusu Utatu Mtakatifu yaleta maana timilifu ya mafundisho ya Agano Jipya kuhusu Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tamko la ufasiri juu ya dhambi ya asili lililotolewa na Mtaguso wa Trento laleta maana timilifu ya mafundisho ya Paulo katika Rum 5:12-21 kuhusu mapokeo ya kosa la Adamu kwa ajili ya wanadamu wote. Lakini, endapo udhibiti wa aina hii haupo – ama kutokana na matini ya Biblia iliyo dhahiri ama na mapokeo ya kimafundisho halisi – kudai kuikimbilia maana timilifu kungeweza kupeleka kwenye fasiri za kibinafsi zisizo na uzito wowote. Kwa kifupi, ingewezekana kuitambua maana timilifu kama njia nyingine ya kuitaja maana ya kiroho ya matini fulani ya Biblia, pale ambapo maana ya kiroho inatofautiana na maana sisisi. Msingi wake ni kwamba Roho Mtakatifu, aliye mtunzi mkuu wa Biblia, aweza kuongoza mwandishi mtu katika kuchagua maneno na sentensi kwa namna ya kwamba zenyewe zaelezea kweli ambayo yeye haitambui katika kina chake chote. Kweli hiyo yafunuliwa kwa upana zaidi baada ya muda, kwa njia ya matendo mengine ya Mungu yanayodhihirisha wazi zaidi maana ya matini, na pia – kwa upande mwingine – kwa njia ya kuingizwa matini hizo katika orodha rasmi (= “kanoni”) ya Maandiko Matakatifu. Kwa namna hiyo unaundwa muktadha mpya, unaoonyesha uwezekano wa maana nyingine tena, ambazo muktadha wa asili ulikuwa ukiziacha kivulini. III. SIFA ZA UFASIRI WA KIKATOLIKI Ufasiri wa kikatoliki hautafuti kutambulikana kwa kutumia mbinu ya kisayansi iliyo yake peke yake. Hukubali kwamba moja ya tabia za matini za Biblia ni kwamba ni kazi ya waandishi watu, waliotumia nyenzo zao na vyombo ambavyo nyakati zao na mazingira yao viliwapatia. Kwa hiyo, ufasiri wa kikatoliki unatumia kwa uhuru mbinu na njia za kisayansi zinazowezesha kuelewa vizuri zaidi maana ya matini, katika muktadha wake wa lugha, wa kifasihi, kijamii-utamaduni, kidini na kihistoria, kwa kuiangaza pia kwa uchunguzi wa machimbuko yake na kwa kujali tabia ya kila mwandishi (taz. Divino afflante Spiritu, EB 557). Kwa maana hiyo, hutoa mchango kiutendaji kwa kukuza mbinu na kwa maendeleo ya utafiti. Sifa yake inayoubainisha ni kwamba unajitia kwa dhati katika mkondo wa mapokeo hai ya Kanisa, ambayo juhudi yake ya kwanza ni uaminifu kwa ufunuo ulioshuhudiwa na Biblia. Hemenetiki za siku hizi zimedhihirisha, kama tulivyokumbusha, kwamba haiwezekani kufasiri matini bila kuanzia toka kwa “ufahamu tangulizi” wa namna moja au nyingine. Ufafanuzi wa kikatoliki hukaribia maandiko ya Biblia kwa ufahamu tangulizi unaounganisha kwa ndani utamaduni wa kisayansi wa leo na mapokeo ya kidini yanayotokea kwa Israeli na kwa jumuiya ya Wakristo wa mwanzoni. Hivyo, ufasiri wake unaendeleza mkikimkiki wa kihemenetiki unaojionyesha ndani ya Biblia yenyewe, na unaoendelea halafu katika maisha ya Kanisa. Unalingana na dai la kuwepo mvuto hai kati ya mfasiri na kitu chake, mvuto ulio moja la masharti yanayowezesha kazi yake ya ufafanuzi. Lakini kila ufahamu tangulizi una hatari zake. Kwa upande wa ufafanuzi wa kikatoliki kuna hatari ya kuzipa matini kadhaa za Biblia maana zisiyo nayo, bali ambayo ni tunda la ukuaji wa baadaye ya mapokeo. Mfafanuzi ajitahadhari na hatari hiyo. A. Ufasiri katika mapokeo ya kibiblia Matini za Biblia ni matokeo ya mapokeo ya kidini yaliyokuwapo kabla yake. Jinsi zinavyounganika na mapokeo hayo ni tofauti kila mara, kwa sababu ubunifu wa waandishi huonyesha ngazi mbalimbali. Mwaka nenda mwaka rudi, mapokeo kadhaa yameingiliana kuunda mapokeo makuu ya pamoja. Biblia ni onyesho bora la mchakato huo, ambao yenyewe ilichangia kuutekeleza na inaendelea kuuratibu. “Ufasiri katika mapokeo ya kibiblia” huweza kutazamwa kwa namna nyingi mbalimbali. Kwa usemi huo inawezekana kumaanisha jinsi Biblia inavyofasiri mang’amuzi ya msingi ya kibinadamu, au matukio ya pekee ya historia ya Israeli, au tena jinsi matini za Biblia zinavyotumia, kwa kuyafasiri, machimbuko mbalimbali, andishi au simulizi, ambayo baadhi yao huweza kutoka katika utamaduni au dini nyinginezo. Lakini, kwa sababu mada yetu ni ufasiri wa Biblia, hatutaki kujadili hapa masuala makuu hayo, bali kutoa mawazo kadhaa kuhusu ufasiri wa matini za Biblia ndani ya Biblia yenyewe. Kinachosaidia kuipa Biblia umoja wake kiundani, wa pekee katika aina yake, ni kwamba maandiko ya kibiblia ya baadaye mara nyingi hutegemea maandiko yaliyotangulia. Yanayadokeza, au yanaleta “kusoma upya” kunakoendeleza mambo mapya katika maana yake, mara nyingine tofauti sana na maana ya asili, au tena yanayarejea kwa wazi kabisa, ama kwa ajili ya kwenda kina katika maana yake, au kwa kudhihirisha utimilifu wake. Hivyo urithi wa nchi, iliyoahidiwa na Mungu kwa Ibrahimu kwa ajili ya uzao wake (Mwa 15:7.18), hugeuka kuwa kuingia katika patakatifu pa Mungu (Kut 15:17), ushirikiano wa raha ya Mungu (Zab 132:7-8) iliyowekwa kwa waamini wa kweli (Zab 95:8-11; Ebr 3:7-4:11) na, mwishowe, kuingia katika patakatifu pa mbinguni (Ebr 6:12.18-20), ulipo “urithi wa milele” (Ebr 9:15). Uaguzi wa nabii Nathani, unaomwahidia Daudi “nyumba”, yaani ukoo wa kifalme, “ulio imara milele” (2Sam 7:12-16), hukumbushwa mara nyingi (2Sam 23:5; 1Nya 17:11-14), hasa katika nyakati za taabu (Zab 89:20-38), wala si pasipo mabadiliko yenye maana, nao huendelezwa na maaguzi mengine (Zab 2:7-8; 110:1.4; Amo 9:11; Isa 7:13-14; Yer 23:5-6; n.k.), ambayo baadhi yake hutangaza kurejeshwa kwa ufalme wa Daudi mwenyewe (Hos 3:5; Yer 30:9; Eze 34:24; 37:24-25; taz. Mk 11:10). Ufalme ulioahidiwa ukawa ufalme wa watu wote jumla (Zab 2:8; Dan 2:25.44; 7:14; taz. Mt 28:18). Hutimiza kikamilifu mwito wa binadamu (Mwa 1:28; Zab 8:6-9; Hek 9:2-3; 10:2). Uaguzi wa Yeremia kuhusu miaka sabini ya adhabu waliyostahili Yerusalemu na Yuda (Yer 25:11-12; 29:10) umekumbushwa katika 2Nya 25:20-23, panapohakikisha utekelezaji; lakini hupata maendelezo zaidi, baada ya muda mrefu, na mwandishi wa kitabu cha Danieli, akiwa na hakika kuwa neno hilo la Mungu linashika bado maana iliyofichwa, inayopaswa kuangaza hali ya sasa (Dan 9:24-27). Tamko la kimsingi la haki ya Mungu katika kutoa thawabu, ambaye anawajazi wema na kuwaadhibu wabaya (Zab 1:1-6; 112:1-10; Law 26:3-33; n.k.), linagongana na mang’amuzi tunayokuta ambayo mara nyingi hayapatani nalo. Basi, Maandiko yanaachia kujitokeza kwa nguvu mateto na upinzani (Zab 44; Ayu 10:1-7; 13:3-28; 23-24) na kuendelea kuchunguza kina cha fumbo hilo (Zab 37; Ayu 38-42; Isa 53; Hek 3-5). 2. Mahusiano baina ya Agano la Kale na Agano Jipya Mahusiano kati ya matini za Biblia yanaongezeka sana katika maandiko ya Agano Jipya, ambayo yamejaa madokezo ya Agano la Kale, na pia nukuu wazi. Waandishi wa Agano Jipya wanatambua kuwa Agano la Kale lina hadhi ya ufunuo wa kimungu. Wanatangaza kuwa ufunuo huo umepata utekelezaji wake katika maisha, mafundisho na hasa katika kufa na kufufuka kwake Yesu, aliye asili ya msamaha na ya uzima wa milele. “Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko; na (...) alizikwa. Na (...) alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko; na alimtokea Kefa... ” (1Kor 15:3-5): hiki ndicho kiini kamili cha mahubiri ya mitume (1Kor 15:11). Jinsi ilivyo daima, baina ya Maandiko na matukio yanayoyatimiza, mahusiano sio ya ulinganifu yakinifu (material correspondence), bali ya kumulikana hayo kwa hayo, na ya maendeleo ya kiupembuzi (dialectical): yawezekana kutambua kwa wakati mmoja kuwa Maandiko hufunulia maana ya matukio, na matukio hufunulia maana ya Maandiko, yaani yanashurutisha kukataa mambo fulani ya ufasiri uliopokelewa, na kuchukua ufasiri mwingine mpya. Tangu wakati wa utume wake hadharani, Yesu alichukua msimamo wa pekee, mbali na ufasiri wa wakati wake, uliokuwa ule “wa Mafarisayo na waandishi” (Mt 5:20). Kuna shuhuda nyingi: tabaini (antithesis) za mafundisho ya mlimani (Mt 5:21-48), uhuru mkuu wake Yesu katika kushika sheria ya sabato (Mk 2:27-28 na nd.), jinsi yake ya kupunguza ukali wa kanuni za usafi wa kiibada (Mk 7:1-23 na nd.); na, kinyume chake, madai yake ya lazima katika mada nyingine (Mt 10:2-12; 10:17-27 na nd.), na hasa msimamo wake wa kuwakaribisha “watoza ushuru na wakosefu” (Mk 2:15-17 na nd.). Nia yake haikuwa shauri la ubishi, bali, la uaminifu kamili kwa mapenzi ya Mungu yalivyodhihirishwa katika Maandiko (rej. Mt 5:17; 9:13; Mk 7:8-13 na nd.; 10:5-9 na nd.). Kifo na ufufuko wake Yesu vilisukuma hadi mwisho maendeleo ya ufasiri aliyoanza, na kusababisha, katika mambo kadhaa, utengano kamili, na, wakati huohuo, ufunguzi usiotarajiwa. Kifo cha Masiya, “mfalme wa Wayahudi” (Mk 15:26 na nd.), kilisababisha mabadiliko katika ufasiri wa kidunia wa zaburi za kifalme na wa maaguzi ya kimasiya. Ufufuko wake na kutukuzwa kwake mbinguni kama Mwana wa Mungu, vilitilia matini hizohizo utimilifu wa maana usioweza kudhaniwa kabla. Semi fulani zilizoonekana za chuku (hyperbole), sasa zilipaswa kuchukuliwa jinsi zilivyo. Ikaonekana kwamba ziliandaliwa na Mungu ili kutambulisha utukufu wa Kristo Yesu, kwa sababu Yesu ni kweli “Bwana” (Zab 110:1) kwa nguvu kamili ya neno (Mdo 2:36; Flp 2:10-11; Ebr 1:10-12); yeye ni Mwana wa Mungu (Zab 2:7; Mk 14:62; Rum 1:3-4), Mungu pamoja na Mungu (Zab 45:7; Ebr 1:8; Yn 1:1; 20:28); “Ufalme wake hautakuwa na mwisho” (Lk 1:32-33; rej. 1Nya 17:11-14; Zab 45:7; Ebr 1:8); na hapohapo yeye ndiye “kuhani wa milele” (Zab 110:2; Ebr 5:6-10; 7:23-24). Kwenye mwanga wa matukio ya Pasaka waandishi wa Agano Jipya walisoma upya Agano la Kale. Roho Mtakatifu aliyepelekwa na Kristo mtukufu (rej. Yn 15:26; 16:7) aliwafunulia maana yake ya kiroho. Hivyo walipaswa kukiri kwa nguvu thamani ya kinabii ya Agano la Kale, lakini pia kupunguza sana thamani yake ya kuwa asasi ya kuleta wokovu. Mtazamo huo wa pili, ambao huonekana tayari katika Injili (taz. Mt 11:11-13 na nd.; 12:41-42 na nd.; Yn 4:12-14; 5:37; 6:32), unajionyesha kwa nguvu yake yote katika nyaraka kadhaa za Paulo na katika waraka kwa Waebrania. Paulo na mwandishi wa waraka kwa Waebrania hudhihirisha kuwa Torati, kwa jinsi ilivyo ufunuo, hutangaza yenyewe mwisho wake wa kuwa mfumo wa kisheria (taz. Gal 2:15-5:1; Rum 3:20-21; 6:14; Ebr 7:11-19; 10:8-9). Hutokana kwamba wapagani wanaomwamini Kristo hawapaswi kuwa chini ya amri zote za mfumo wa sheria wa kibiblia, ambao kwa ujumla, umegeuzwa kuwa asasi ya kisheria kwa taifa maalum, lakini wanapaswa kulishwa na Agano la Kale kama Neno la Mungu, linalowezesha kugundua vizuri zaidi upeo wote wa fumbo la kipasaka wanaloishi kwalo (taz. Lk 24:25-27.44-45; Rum 1:1-2). Ndani ya Biblia ya kikristo, mahusiano baina ya Agano Jipya na Agano la Kale hayakosi magumu. Kuhusu namna ya kutumia matini maalum, waandishi wa Agano Jipya hakika walitumia ujuzi na njia za ufasiri za wakati wao. Kuwadai wawe wametumia mbinu za kisayansi za leo kungekuwa kutozingatia utofauti wa nyakati. Badala yake, mfafanuzi lazima ajipatie ujuzi wa mbinu za kale ili kufasiri kisahihi matumizi yake. Ni kweli, lakini, kuwa mfafanuzi hatakiwi kutilia tunu kamilifu kwa mambo ambayo hutokana na ujuzi pungufu wa kibinadamu. Hatimaye yafaa kuongeza kwamba ndani ya Agano Jipya, kama ilivyokuwa pia kwa Agano la Kale, hugundulika kupangiliwa pamoja mitazamo tofauti, na mara nyingine yenye mvutano kati yao, kwa mfano kuhusu hali ya Yesu (Yn 8:29; 16:32 na Mk 15:34), au kuhusu tunu ya sheria ya Musa (Mt 5:17-19 na Rum 6:14), au kuhusu ulazima wa matendo ili kuhesabiwa haki (Yak 2:24 na Rum 3:28; Efe 2:8-9). Moja ya sifa bainifu za Biblia, kweli, ni kukosa tabia ya kuratibu, bali kuwemo mivutano ya kimkikimkiki. Biblia imepokea aina mbalimbali za kufasiri matukio yaleyale, au ya kutazama masuala yaleyale, na hivyo hualika kukataa kurahisisha mno (excessive simplification), na ufinyu wa roho. Kutokana na yale tuliyosema tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa Biblia inashika maelekezo na maonyo mengi kuhusu usanii wa kuifasiri. Naam, Biblia, toka mwanzo, ndiyo yenyewe ufasiri. Matini zake zimetambuliwa na jumuiya za Agano la Kale na za wakati wa mitume kama uonyesho na thibitisho halisi ya imani yao. Ni kadiri ya ufasiri wa jumuiya hizo na kuhusiana nao kwamba matini hizo zilikubaliwa kama Maandiko Matakatifu (ndivyo ilivyo, k.m., kwa Wimbo ulio Bora uliokubaliwa kama Maandiko Matakatifu kwa kuutazama uhusiano kati ya Mungu na Israeli). Wakati wa utungaji wa Biblia, maandiko yaliyomo mara nyingi yametengenezwa upya, na kufasiriwa upya, ili kuambatana na hali mpya, zisizojulikana kwanza. Namna ya kufasiri matini, inayoonekana katika Maandiko Matakatifu, inadokeza maonyo yafuatayo: Kwa kuwa Maandiko Matakatifu yalikuja kupatikana kwa msingi wa ukubaliano kamili wa jumuiya za waamini zilizotambua katika matini yake uonyesho wa imani iliyofunuliwa, ufasiri wake lazima uwe, kwa imani hai ya jumuiya za kikanisa, chemchemi ya ukubaliano katika mambo ya lazima. Kwa vile uonyesho wa imani, jinsi ulivyokuwa ulionekana katika Maandiko Matakatifu yaliyokubaliwa na wote, ulipaswa daima kutengenezwa upya ili upate kukabili hali mpya – ndiyo sababu ya “kusoma upya” matini nyingi za Biblia – ufasiri wa Biblia lazima upate kuwa na ubunifu fulani na kuyakabili masuala mapya yanayojitokeza, ili kuyajadili kwa kuanzia na Biblia. Kwa kuwa matini za Maandiko Matakatifu mara nyingine zina mvutano kati yao, ufasiri unapaswa kuwa wa namna nyingi mbalimbali. Hakuna ufasiri mmoja pekee unaoweza kutimiza maana ya matini kwa ujumla, iliyo daima kama sinfonia ya sauti nyingi. Ufasiri wa matini maalumu unapaswa kuepa kujidai kuwa ule mmoja peke yake. Maandiko Matakatifu yana mazungumzo na jumuiya za waamini: yalitokana na mapokeo yao ya imani. Matini zake zimekua katika mahusiano na mapokeo hayo na kuchangia, wao kwa wao, kwa ukuzaji wake. Hutokea kwamba ufasiri wa Maandiko hufanyika ndani ya Kanisa katika uwingi wake na katika umoja wake, na katika mapokeo yake ya imani. Mapokeo mbalimbali ya imani yalijenga mazingira hai, ambamo ndani yake ilipatikana amali ya kifasihi ya waandishi wa Maandiko Matakatifu. Hali hiyo ya kuwemo ndani yake ilihusu pia ushiriki katika maisha ya kiliturujia, na katika kazi ya nje ya jumuiya, katika ulimwengu wao wa kiroho, utamaduni wao, na matatizo ya safari yao kihistoria. Ufasiri wa Maandiko Matakatifu, kwa namna sawia, hudai ushiriki wa wafafanuzi katika maisha yote na imani yote ya jumuiya ya waamini ya wakati wao. Mazungumzo na Maandiko Matakatifu kwa ujumla, na hivyo pia ufahamu wa imani iliyo pekee ya kila zama zilizotangulia, hupaswa kuandamana na mazungumzo na kizazi cha sasa. Hayo yadai kujiunga na uhusiano wa mfulizo, lakini pia kutambua tofauti zilizopo. Hutokana kwamba ufasiri wa Maandiko unapaswa kufanya kazi ya kuhakikisha na kuchambua; unadumu katika mfulizo na mapokeo ya kifafanuzi yaliyotangulia. ambayo hutunza mambo yake mengi na kuyafanya kuwa yake; lakini kuhusu mengine unajitenga, ili upate kuendelea. B. Ufasiri katika mapokeo ya Kanisa Kanisa, taifa la Mungu, linatambua kuwa linasaidiwa na Roho Mtakatifu katika kuelewa na kufasiri Maandiko. Wanafunzi wa kwanza wa Yesu walijua kwamba hawakuwa na uwezo wa kufahamu mara katika sura zake zote utimilifu waliopokea. Kwa kadiri walivyodumu katika maisha yao kama jumuiya, wao walikuwa wanang’amua kuongezewa zaidi na zaidi ufahamu na dhihirisho vya kina vya ufunuo waliopokea. Katika hayo walikuwa wakitambua athari na kazi za “Roho wa kweli”, ambaye Kristo aliahidi kupeleka ili kuwaongoza awatie katika kweli yote (Yn 16:12-13). Ndivyo Kanisa linavyoendelea katika safari yake, likitegemezwa na ahadi ya Kristo: “Huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yn 14:26). Likiongozwa na Roho Mtakatifu na katika mwanga wa mapokeo hai liliyopokea, Kanisa lilitambua maandiko yanayopaswa kukubaliwa kama Maandiko Matakatifu, yaani yale ya [vitabu vile] ambavyo “kwa vile viliandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, Mungu mwenyewe ndiye mtunzi wake; na katika hali hiyo vimekabidhiwa kwa Kanisa lenyewe” (Dei Verbum, 11) na yanashika “ukweli ambao Mungu alitaka ukabidhiwe kwa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya wokovu wetu” (ibid.). Kuthibitisha “kanoni” ya Maandiko Matakatifu kumekuwa hatima ya mchakato mrefu. Jumuiya za Agano la Kale (toka vikundi maalum, kama duru za kimanabii, au mazingira ya makuhani, hadi taifa kwa ujumla) zilitambua katika matini kadhaa Neno la Mungu lililoamsha imani yao na kuwaongoza katika maisha yao; wakapokea matini hizo kama urithi wa kutunzwa na kupokezwa. Hivyo matini hizo ziliacha kuwa ishara ya kariha ya waandishi binafsi, na kuwa mali jamii ya taifa la Mungu. Agano Jipya linashuhudia heshima yake kwa matini hizo takatifu, lilizopokea kama urithi wa thamani kubwa uliopokelewa kutoka kwa taifa la Waebrania. Linayatambua kama “Maandiko Matakatifu” (Rum 1:2), “yenye pumzi” la Roho wa Mungu (2Tim 3:16; rej. 2Pet 1:20-21), ambayo “hayawezi kutanguliwa” (Yn 10:35). Kwa matini hizo ziundazo “Agano la Kale” (taz. 2Kor 3:14), Kanisa liliunganisha maandiko ambamo lilitambua, kwa upande mmoja, ushuhuda halisi utokao kwa mitume (taz. Lk 1:2; 1Yoh 1:1-3) na kudhaminiwa na Roho Mtakatifu (taz. 1Pet 1:12), kuhusu “mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha” (Mdo 1:1); na, kwa upande mwingine, mafundisho ya mitume wenyewe na wanafunzi wengine, ili kusimika jumuiya ya waamini. Safu hizi mbili za maandiko zimepata baadaye jina la “Agano Jipya”. Katika mchakato huo yaliingia mambo mengi: uhakika wa kuwa Yesu – na mitume pamoja naye – walitambua Agano la Kale kama Maandiko yenye pumzi la Mungu, na kuwa fumbo la Pasaka la Yesu lilikuwa utimilifu wake; imani ya kuwa maandiko ya Agano Jipya yanatokana kwa namna halisi na mafundisho ya mitume (lakini bila kudai kuwa yalitungwa yote na mitume wenyewe); kutambua utumiaji wake katika liturujia ya kikristo, na ulinganifu na mwongozo wa imani; hatimaye, mang’amuzi ya uafikiano wake na maisha ya kikanisa ya jumuiya na uwezo wake wa kulisha maisha hayo. Kwa kuthibitisha kanoni (orodha rasmi) ya Maandiko, Kanisa lilithibitisha pia na kutambulisha tabia yake lenyewe, na hivyo Maandiko sasa ni kama kioo ambamo Kanisa daima linaweza kujigundua upya na kupima, karne hadi karne, jinsi linavyoitikia daima Injili, na kujiweka lenyewe kuwa chombo cha upokezaji (taz. Dei Verbum, 7). Hayo yatilia maandiko ya kikanoni tunu ya kuleta wokovu na tunu ya kitheolojia mbali kabisa na maandiko mengine ya kale. Na ikiwa hayo ya mwisho yanaweza kutupia mwanga kwenye asili ya imani, hayawezi kuchukua kamwe nafasi ya mamlaka ya maandiko yaliyohesabiwa kuwa ya kikanoni (=rasmi), na hivyo ya msingi kwa ufahamu wa imani ya Kikristo. Toka zama za mwanzoni kulikuwa na uhakika thabiti kuwa Roho Mtakatifu mwenyewe, aliyewasukuma waandishi wa Agano Jipya kutilia kwenye maandishi ujumbe wa wokovu (taz. Dei Verbum 7; 18), hulipa pia Kanisa usaidizi wa daima kwa kufasiri maandiko yake yaliyovuviwa (taz. Ireneo, Adv. Haer. 3.24.1; taz. 3.1.1; 4.33.8; Orijene, De Princ., 2.7.2; Tertuliani, De Praescr.; 22). Mababa wa Kanisa, waliokuwa na dhima muhimu katika mchakato wa uundaji wa kanoni, vilevile walikuwa na dhima ya waanzilishi kuhusu mapokeo hai yanayosindikiza bila kukoma na kuliongoza Kanisa katika kusoma na kufasiri Maandiko (taz. Providentissimus Deus, EB 110-111; Divino afflante Spiritu, 28-30: EB 554; Dei Verbum, 23; TKB, Instr. de Evang histor., 1). Katika mkondo wa Mapokeo makuu, mchango wa pekee wa ufafanuzi wa Mababa umekuwa hivi: umetokeza kutoka kwa Maandiko kwa ujumla maelekeo ya msingi yaliyounda mapokeo ya kimafundisho ya Kanisa, na kuleta utajiri wa mafundisho ya kitheolojia kwa ajili ya kuwafundisha waamini na kuwalisha kiroho. Kwao Mababa wa Kanisa, kusoma Maandiko na kuyafasiri huchukua nafasi muhimu. Ushuhuda hutolewa hasa na kazi zao zilizounganika moja kwa moja na ufahamu wa Maandiko, yaani homilia na mafasiri (commentaries); lakini pia kazi za mabishano na za theolojia, ambamo marejeo ya Maandiko ni hoja muhimu. Mahali pa kawaida pa kusoma Biblia ilikuwa kanisani, wakati wa Liturujia. Ndiyo sababu, ufasiri wanaotoa ni daima wenye tabia ya kitheolojia na ya kiuchungaji, wenye kugusa uhusiano na Mungu, kwa huduma ya jumuiya na ya waamini binafsi. Mababa wanatazama Biblia awali ya yote kama Kitabu cha Mungu, kazi moja ya Mtunzi mmoja; lakini sio kwamba wanawadhania waandishi binadamu kama vyombo vitupu tu; wanakitia kila kitabu, kimoja kimoja, lengo pekee. Lakini taratibu yao hutoa uangalifu haba kwa ukuaji kihistoria wa ufunuo. Mababa wengi wa Kanisa wanamwonyesha Logos, Neno wa Mungu, kama mtunzi wa Agano la Kale, na kusisitiza, hivyo, kuwa Maandiko yote yanaongelea Kristo. Mbali na wafafanuzi wachache wa shule ya Antiokia (kwa namna ya pekee Theodori wa Mopsuestia), Mababa wanajiona kuwa na mamlaka ya kuchukua sentensi moja nje ya muktadha wake na kutambua humo ukweli mmoja uliofunuliwa na Mungu. Katika mabishano na Wayahudi au yale ya kidogma na wanatheolojia wengine, hawasiti kutegemea fasiri za aina hiyo. Wakisukumwa hasa na jitihada ya kuishi Biblia katika ushirika na ndugu zao, Mababa mara nyingi waliridhika kutumia matini ile ya Biblia ambayo huwa ilitumika katika maeneo yao. Orijene, katika kufanya juhudi kuiangalia Biblia ya Kiebrania, alisukumwa hasa na bidii ya kutafuta hoja kwa kupinga Wayahudi, kutokana na matini wanazokubali pia wao. Yeronimo, akitukuza ukweli wa Kiebrania (veritas ebraica), anachukua msimamo wa pembezoni. Mababa wanatumia, zaidi au pungufu, mbinu ya kiistiari, kwa nia ya kutupilia mbali kwazo ambalo wangeweza kulipata Wakristo fulani na pia wapinzani wapagani wa Ukristo katika kusoma sehemu hii au ile ya Biblia. Lakini mara chache sana wanaachana na maana sisisi na tabia ya kihistoria ya matini. Matumizi ya istiari kwa upande wa Mababa, lazima yaeleweke tofauti sana na kawaida ya waandishi wapagani ya kutumia mbinu ya istiari. Matumizi ya istiari hutokana pia na uhakika kuwa Biblia, kitabu cha Mungu, kimetolewa naye kwa taifa lake, yaani Kanisa. Kwa kawaida, hakuna kitu kinachopaswa kuachwa kama kitu kilichopita, au kimeharibika kabisa. Katika kueleza Biblia, Mababa wanachanganya na kushona fasiri za ufananisho (typological) na za kiistiari kwa namna isiyoweza kutengana, daima kwa lengo la kiuchungaji na kimalezi; [wakiamini kuwa] “yote yaliyoandikwa, yameandikwa kwa kutufundisha sisi (taz. 1Kor 10:11). Huku wakiwa na hakika kuwa Biblia ni Kitabu cha Mungu, kwa hiyo kisicho na kina, Mababa wanaamini kuweza kufasiri dondoo fulani kadiri ya utaratibu maalum wa kiistiari; lakini wanadhani kuwa kila mmoja anaweza kutokeza kitu tofauti, ilimradi azingatie ulinganifu wa imani. Ufasiri wa kiistiari wa Maandiko ulio tabia bainifu ya ufafanuzi wa Mababa, una hatari ya kuyumbisha mtu wa leo; lakini mang’amuzi ya Kanisa yaliyodokezwa na ufafanuzi huo yanatoa mchango wenye manufaa daima (taz. Divino afflante Spiritu, 31-32; Dei Verbum, 23). Mababa wafundisha kusoma Biblia kitheolojia ndani ya Mapokeo hai, kwa roho ya kikristo halisi. 3. Dhima ya viungo mbalimbali vya Kanisa katika ufasiri Kwa vile Maandiko yalitolewa kwa Kanisa, basi, ni hazina jamii ya mwili wote na waamini: “Mapokeo Matakatifu na Maandiko Matakatifu yanaunda hazina moja takatifu ya Neno la Mungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Taifa lote takatifu, pamoja na wachungaji wake, likishikamana na hazina hiyo, linadumu daima aminifu katika mafundisho ya Mitume...” (Dei Verbum, 10; taz. pia 21). Ni kweli kuwa uzoefu wa waamini wa kusoma Maandiko ulikuwa mkubwa zaidi katika zama fulani za historia ya Kanisa kuliko zama nyingine. Lakini Maandiko yalichukua nafasi ya mbele katika nyakati muhimu zote za upyaisho wa maisha ya Kanisa, toka uamsho wa kimonaki wa karne za kwanza, hadi zama za siku hizi za Mtaguso wa Vatikano II. Mtaguso huuhuu unafundisha kuwa wabatizwa wote, wanaposhiriki, katika imani kwa Kristo, maadhimisho ya Ekaristi, wanatambua kuwemo kwa Kristo pia katika Neno lake, “kwa sababu ni yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Kanisa” (Sacrosanctum Concilium, 7). Wanakuja kusikiliza neno hilo kwa “utambuzi wa kiimani” (sensum fidei) iliyo sifa pekee ya taifa lote la Mungu. “Kwa sababu ya utambuzi huo wa imani, ulioamshwa na kutegemezwa na Roho wa ukweli, taifa la Mungu, chini ya uongozi wa Majisterio takatifu, linayoifuata kwa uaminifu, lapokea si neno la kibinadamu, bali kwa hakika neno la Mungu (taz. 1The 2:13). Tena, laishika daima imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu (Yda 3), na kwa hukumu iliyo nyofu laipenya kwa undani zaidi na kuitia kikamilifu katika maisha yake” (Lumen Gentium, 12). Hivyo, basi, wanakanisa wote wana dhima yao katika ufasiri wa Maandiko. Katika utekelezaji wa huduma yao ya kiuchungaji, maaskofu, wakiwa waandamizi wa mitume, ni mashahidi wa kwanza na wadhamini wa mapokeo hai ambamo Maandiko yanafasiriwa katika kila zama. “Hao, wakiangazwa na Roho wa ukweli, kwa njia ya kuhubiri kwao, wanapaswa kuhifadhi kiaminifu Neno la Mungu, kulifasiri na kulieneza” (Dei Verbum, 9; taz. Lumen Gentium, 25). Wakiwa wasaidizi wa maaskofu, mapadre wana wajibu wao wa kwanza wa kutangaza Neno (taz. Presbyterorum Ordinis, 4). Nao wana karama pekee ya kufasiri Maandiko, pale wanapolinganisha kweli za milele za Injili na hali halisi ya maisha (ibid.), huku wakitoa siyo maoni yao binafsi, bali Neno la Mungu. Ni wajibu ya mapadre na mashemasi, hasa wanapoadhimisha sakramenti, kudhihirisha wazi umoja wa Neno na sakramenti katika huduma ya Kanisa. Wakiwa viongozi wa jumuiya ya kiekaristi na walezi wa imani. wahudumu wa Neno wana kama wajibu wao muhimu sio tu kutoa mafundisho, bali kusaidia waamini kufahamu na kupambanua Neno linasema nini moyoni mwao wanaposikiliza na kutafakari Maandiko. Hivyo Kanisa mahalia lote, kadiri ya mfano wa Israeli, taifa la Mungu (Kut 19:5-6), linakuwa jumuiya inayojua kuwa Mungu anaongea nayo (taz. Yn 6:45), nalo hufanya juu chini ili kumsikiliza kwa imani, upendo na utiifu kwa Neno (Kum 6:4-6). Jumuiya hizo, wanaosikiliza kweli, wanakuwa, katika mazingira yao – ilimradi zadumu zimeungana na Kanisa lote katika imani na mapendo – moto unaowaka wa uinjilishaji na dialogia, pia watendaji wa mabadiliko kijamii (taz. Evangelii Nuntiandi, 57-58; CDF, Mafundisho kuhusu uhuru wa kikristo na ukombozi, 69-70). Roho ametolewa, hakika, hata kwa wakristo mmoja mmoja ili mioyo yao iweze kuwa “imewaka moto” (taz. Lk 24:32), wanaposali na kuchunguza Maandiko kisala katika mazingira ya maisha yao binafsi. Kwa sababu hiyo Mtaguso wa Vatikano II umetaka kwa nguvu kuwafungulia wazi Maandiko kwa kila namna iwezekanayo (taz. Dei Verbum, 22; 25). Yafaa kusisitiza kwamba aina hii ya kusoma si ya binafsi hata kidogo, kwa sababu mwamini husoma na kufasiri daima Maandiko katika imani ya Kanisa, na halafu huiletea jumuiya matunda ya kusoma kwake, ili kutajirisha imani jamii. Mapokeo yote ya kibiblia na, kwa namna ya pekee, mafundisho ya Yesu katika Injili, yadhihirisha kwamba wasikilizaji wapendelevu wa Neno la Mungu ni wale ambao ulimwengu huwadhania kuwa watu wa hali duni. Yesu alitambua kuwa mambo mengine yalifichwa kwa wenye akili na hekima, na kufunuliwa wadogo (Mt 11:25; Lk 10:21), na kwamba Ufalme wa Mungu ni wao walio kama watoto wadogo (Mk 10:14 na nd.). Hali kadhalika, Yesu alisema: “Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu” (Lk 6:21; taz. Mt 5:3). Kati ya ishara za nyakati za kimasiya linapatikana tangazo la habari njema kwa maskini (Lk 4:18; 7:22; Mt 11:5; taz. CDF, Mafundisho kuhusu uhuru wa kikristo na ukombozi, 47-48). Wale ambao, kwa kukosa nguvu na kukosa vifaa vya kibinadamu, wanasukumwa kuweka matumaini yao kwa Mungu pekee na katika haki yake, wanao uwezo wa kusikiliza na kufasiri Neno la Mungu unaopaswa kuchukuliwa maanani na Kanisa zima, pamoja na kudai pia jawabu kijamii. Kwa kutambua vipaji na wadhifa mbalimbali ambazo Roho huweka kwa huduma ya jumuiya, na hasa kipaji cha kufundisha (1Kor 12:28-30; Rum 12:6-7; Efe 4:11-16), Kanisa linawapa heshima yake wale wanaoonyesha uwezo wa pekee wa kusaidia kujenga Mwili wa Kristo kwa umilisi wao katika ufasiri wa Maandiko (taz. Divino afflante Spiritu, 46-48, EB 564-565; Dei Verbum, 23; TKB, Fundisho kuhusu tabia ya kihistoria ya Injili, Utangulizi). Ijapo chunguzi zao hazikupata daima pongezi wanazopokea siku hizi, wafafanuzi (exegetes) wanaotumikia Kanisa kwa ujuzi wao wanajikuta kuwa katika utajiri wa mapokeo yanayoenea toka karne za mwanzoni, pamoja na Orijene na Yeronimo, hadi nyakati za karibuni, pamoja na padre Lagrange na wengine, na kuendelea hadi siku hizi. Hasa, utafiti wa maana sisisi ya Maandiko, ambayo leo hukaziwa sana, hutaka jitihada jamii ya wale walio na umilisi wa lugha za kale, wa historia na utamaduni, wa uhakiki wa matini na wa uchanganuzi wa fani za kifasihi, na ambao wanajua kutumia mbinu za uhakiki wa kisayansi. Licha ya kujali matini katika muktadha wake wa asili kihistoria, Kanisa linawategemea wafafanuzi wanaosukumwa na Roho yuleyule aliyevuvia Maandiko, ili kuhakikisha kuwa “watumishi wa Neno, kwa wingi uwezekanavyo, waweze kweli kuwaandalia taifa la Mungu lishe ya Maandiko” (Divino afflante Spiritu, 24; 53-55; EB 551, 567; Dei Verbum, 23; Paulo VI, Sedula Cura, 1971). Sababu ya kuridhika imetolewa, katika nyakati zetu, na idadi inayoongezeka ya wanawake wafafanuzi, wanaotoa mara nyingi, katika ufasiri wa Maandiko, mitazamo mipya na ya kina, na kutilia nuru mandhari zilizokuwa zimesahauliwa. Ikiwa Maandiko, tulivyokumbusha hapo juu, ni hazina ya Kanisa zima na sehemu ya “urithi wa imani” ambao wote, wachungaji kwa waamini, “wanatunza, wanaungama na kutekeleza kwa jitihada jamii”, lakini ni kweli kuwa “jukumu la kutoa ufasiri halisi wa Neno la Mungu lililoandikwa au kupokewa umekabidhiwa tu kwa Majisterio hai ya Kanisa, ambayo mamlaka yake inatekelezwa kwa jina la Yesu Kristo” (Dei Verbum, 10). Basi, mwishowe, ni jukumu la Majisterio kuhakikisha uhalisi wa ufasiri na kuonyesha, ikitakiwa, kuwa ufasiri huu ama huo haupatani na uhalisi wa Injili. Hutekeleza jukumu hilo ndani ya koinonia (ushirika) ya Mwili, kwa kukiri rasmi imani ya Kanisa kwa ajili ya kutumikia Kanisa; kwa lengo hilo, huhoji wanatheolojia, wafafanuzi na wataalamu wengine, ambao inatambua haki ya uhuru wao, na pamoja nao imo katika muungano kwa lengo la pamoja la “kulinda taifa la Mungu katika ukweli unaofanya huru” (CDF, Mafundisho kuhusu wito wa mwanatheolojia katika Kanisa, 21). Jukumu la mfafanuzi mkatoliki lina dhima nyingi. Ni jukumu la kikanisa, kwa sababu ni kuchunguza na kueleza Maandiko Matakatifu kwa jinsi ya kuweka utajiri wake wote kwa matumizi ya wachungaji na waamini. Lakini, wakati huohuo, ni jukumu la kisayansi, linalomweka mfafanuzi mkatoliki kuhusiana na wasomi wenzake wasio wakatoliki na katika sekta nyingi za utafiti wa kisayansi. Kwa upande mwingine, jukumu hilo linashika wakati huohuo kazi ya utafiti na ya ufundishaji. Zote mbili kwa kawaida hupeleka kwenye kuandika makala na vitabu. Wakijitahidi katika jukumu lao, wafafanuzi wakatoliki wanapaswa kuchukua mtazamo nyeti wa tabia ya kihistoria ya ufunuo wa kibiblia. Maana, Maagano yote mawili yanatokeza kwa maneno ya kibinadamu, yanayobeba alama za nyakati zao, ufunuo wa kihistoria aliofanya Mungu, kwa namna nyingi, kuhusu Yeye mwenyewe na kuhusu mpango wake wa wokovu. Kwa hiyo, wafafanuzi lazima watumie mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, lakini bila kutaka kuitumia pekee (exclusivity). Mbinu zote zinazohusu ufasiri wa matini zinaruhusiwa kuleta mchango wao kwa ufafanuzi wa Biblia. Katika kazi yao ya kufasiri, wafafanuzi wakatoliki wasisahau kamwe kwamba wanachofasiri ni Neno la Mungu. Jukumu lao haliishi baada ya kubainisha machimbuko, kuainisha fani au kueleza taratibu za kifasihi. Lengo la kazi yao litakuwa limetimia pale tu wanapodhihirisha wazi maana ya matini ya Biblia kama Neno la Mungu kwa siku za leo. Kwa hiyo, lazima watilie maanani mitazamo mbalimbali ya kihemenetiki inayosaidia kudaka nguvu kwa leo ya ujumbe wa Biblia na kuuwezesha kuitikia mahitaji ya wasomaji wa siku hizi wa Maandiko. Jukumu la wafafanuzi ni pia kueleza maana ya kikristolojia, ya kikanoni, na ya kikanisa, ya Maandiko ya Biblia. Maana ya kikristolojia ya matini za Biblia si dhahiri kila mara; lazima kuiweka nuruni kila inapowezekana. Ijapo Kristo alifunga Agano Jipya katika damu yake, vitabu vya Agano la Kwanza havikupoteza thamani yao. Kwa vile vimechukuliwa katika tangazo la Injili, vinapata na kuonyesha maana yake kamili katika “fumbo la Kristo” (Efe 3:4), kwa kuangaza mandhari zake mbalimbali, na, wakati huohuo, kwa kuangazwa nalo. Kwani, vitabu hiyo vilitayarisha taifa la Mungu kwa ujio wake (taz. Dei Verbum, 14-16). Kila kitabu cha Biblia, ijapo kimeandikwa kwa lengo maalum na kuwa na maana yake pekee, hujionyesha kuleta maana ya ziada kinapokuwa kimeingizwa katika jumla ya kanoni rasmi ya vitabu vitakatifu. Jukumu la wafafanuzi linahusu pia kuonyesha ukweli wa usemi wa Mt. Augustino: “Novum Testamentum in Vetere latet, et in Novo Vetus patet” (“Agano Jipya hufichika katika Agano la Kale, na katika Agano Jipya hudhihirika la Kale”; taz. Mt. Augustino, Quaest. in Hept., 2:73: CSEL 28, III, 3, p. 141). Wafafanuzi wanapaswa pia kueleza uhusiano uliopo kati ya Biblia na Kanisa. Biblia imezaliwa katika jumuiya za waamini. Hudhihirisha imani ya Israeli, na halafu imani ya jumuiya za kikristo za mwanzoni. Ikiunganika na Mapokeo hai yaliyoitangulia, yanayoisindikiza na yanayolishwa nayo (taz. Dei Verbum, 21), Biblia ni chombo kiteule, ambacho Mungu anakitumia kwa kuongoza, hata sasa, ujenzi na ukuzaji wa Kanisa kama taifa la Mungu. Kisichotengana na eneo la kikanisa ni mtazamo wazi wa kiekumeni. Maadamu Biblia hudhihirisha zawadi ya wokovu ambayo Mungu anawatolea watu wote, jukumu la wafafanuzi linaendana na tabia ya kujali wote na yote, inayodai kuzingatia dini nyingine na matazamio ya ulimwengu wa leo. Jukumu la ufafanuzi ni pana mno, lisitimilizwe vema na mtu mmoja tu. Hakuna budi kugawanya kazi, hasa kuhusu utafiti, unaodai wataalamu kwa kila uwanja. Matatizo yatokanayo na kuwa na utaalamu wa aina moja tu yataepukana kwa njia ya juhudi za kuhusiana kati ya wataalamu wa fani mbalimbali. Ni muhimu sana kwa manufaa ya Kanisa zima na kwa uwezo wake wa kuuathiri ulimwengu wa leo kuwa idadi tosha ya watu waliotayarishwa vizuri wajishughulishe kwenye utafiti katika sekta mbalimbali za sayansi ya ufafanuzi. Wakijali mahitaji ya haraka ya huduma, maaskofu na wakuu wa mashirika ya kitawa, mara nyingi hushawishiwa wasitilie maanani sana wajibu unaowaangukia wa kushughulikia hitaji hilo la msingi. Lakini upungufu katika jambo hilo hulihatarisha sana Kanisa, kwa sababu wachungaji na waamini wangeweza kuelekea kwenye sayansi ya kiufafanuzi iliyo ngeni kwa Kanisa, na isiyo na mahusiano na maisha ya kiimani. Kwa kukiri kuwa “mtaala wa Maandiko Matakatifu” lazima uwe “kama roho ya theolojia” (Dei Verbum, 24), Mtaguso wa Vatikano II ulionyesha umuhimu wote wa utafiti wa kiufafanuzi, na wakati huohuo, ulitaka kuwakumbusha pia wafafanuzi wakatoliki kuwa utafiti wao una uhusiano muhimu na theolojia, ambao wanapaswa kuutambua. Tamko la Mtaguso hutufahamisha dhima ya msingi ya ufundishaji wa ufafanuzi katika vyuo vya theolojia, katika seminari, na katika shule za watawa. Ni wazi kuwa kiwango cha mitaala hakitakuwa kilekile katika taasisi hizo mbalimbali. Ni matumaini kuwa mafunzo ya ufafanuzi yatolewe na wanaume na wanawake. Yatakuwa ya kina zaidi kisayansi katika vyuo, ila yatashika mwelekeo moja kwa moja wa kiuchungaji katika seminari; lakini hayataweza kamwe kukosa eneo pana kielimu. Kufanya tofauti itakuwa kukosa heshima kwa Neno la Mungu. Maprofesa wa ufafanuzi lazima watilie kwenye wanafunzi staha ya kina kwa Maandiko Matakatifu, wakionyesha kuwa yanastahili somo angalifu na thabiti, linalowezesha kutambua vizuri zaidi thamani yake ya kifasihi, kihistoria, kijamii na kitheolojia. Hawawezi kuridhika kutoa jumla ya taarifa za kupokea hivihivi, bali wanapaswa kuwazoesha wanafunzi kuhusu mbinu za ufafanuzi, kwa kueleza hatua zake maalum, ili kuwawezesha kujimudu kutoa uamuzi wenyewe. Kwa sababu muda haumtoshi, yafaa mwalimu atumie kwa kubadilibadili mifumo miwili ya kufundishia: kwa upande mmoja, kwa njia ya maelezo ya usanisi kuwaingiza katika somo la vitabu vizima kadhaa vya Biblia bila kuacha pembeni sekta yoyote muhimu ya Agano la Kale, na ya Agano Jipya; kwa upande mwingine, kwa njia ya uchanganuzi wa kina wa matini zilizochaguliwa kwa makini, ambazo zitakuwa nafasi za kuwaingiza wanafunzi kwenye mazoezi ya ufafanuzi. Kwa njia hizo zote mbili, lazima kujitahadhari kutoegemea upande mmoja, yaani kutazama tu maelezo ya kiroho bila ya msingi ya kihistoria-kiuhakiki, wala maelezo ya kihistoria-kiuhakiki bila mafundisho ya kiroho (taz. Divino afflante Spiritu, EB 551-552; TKB, De Sacra Scrittura recte docenda, EB 598). Mafundisho yaonyeshe, kwa wakati mmoja, misingi ya kihistoria ya Maandiko ya Biblia, hali yake ya kuwa neno binafsi la Baba wa mbinguni anayewaelekea wanae kwa upendo (taz. Dei Verbum, 21), na dhima yake ya lazima katika huduma ya kiuchungaji (taz. 2Tim 3:16). 4. Machapisho (Makala na Vitabu) Kama tunda la utafiti na kikomo cha mafundisho, machapisho yana dhima muhimu sana kwa maendeleo na uenezi wa ufafanuzi. Siku zetu hizi machapisho yanatolewa, si tu kwa njia ya karatasi iliyochapwa, lakini pia kwa njia nyingine, za haraka zaidi na zenye nguvu zaidi (redio, televisheni, na vyombo vya kielektroniki), ambazo inafaa kujifunza kuzitumia. Maandishi ya hali ya juu kisayansi ni chombo muhimu kuliko vyote kwa ajili ya dialogia, majadiliano na ushirikiano kati ya wachunguzi. Kwa njia yake, ufafanuzi wa kikatoliki unaweza kujiweka kwenye uhusiano na shule nyingine ya utafiti wa kiufafanuzi, kama vile na ulimwengu wa kisayansi kwa ujumla. Kuna na machapisho mengine ambayo hutoa huduma kubwa sana, kwa kulingana na tabaka mbalimbali za wasomaji, kuanzia wasomaji wasomi hadi watoto wa katekisimu, kwa kupitia katika vikundi vya Biblia, vyama vya kitume na mashirika ya kitawa. Wafafanuzi wenye uwezo wa kutekeleza uenezaji sahihi wanafanya kazi ya kufaa sana na ya faida, kazi iliyo ya lazima ili kuihakikishia mitaala ya kiufafanuzi uwezo wa kuathiri inaopaswa kuwa nao. Katika sekta hiyo, hitaji la kutimiliza ujumbe wa Biblia kwa wakati huu (actualisation) hutambulika kwa nguvu. Nalo linadai kwamba wafafanuzi watilie maanani mahitaji halali ya wasomi na wataalamu wa nyakati zetu na kupambanua wazi kwa ajili yao yale yasiyo muhimu kwa vile yanavyokwenda na nyakati, na yale yanayopaswa kueleweka kama lugha ya kisasili, na hatimaye yale yanayopaswa kutambulika kama maana halisi, ya kihistoria na ya kuvuviwa. Maandiko ya Biblia hayakutungwa katika lugha ya leo, wala katika mtindo wa karne ya ishirini. Fani za usemi na tanzu za fasihi zinazotumika katika matini za Kiebrania, Kiaramayo au Kigiriki lazima zitafsiriwe kwa namna ya kufahamika kwa wanaume na wanawake wa leo, ambao, pasipo hivyo, wangeshawishiwa ama kutojali Biblia ama kuifasiri kwa namna duni: iwe ya kiherufi, au ya ubunifu. Katika jukumu lake lenye dhima nyingi, mfafanuzi Mkatoliki hana lengo lingine ila kulihudumia Neno la Mungu. Fahari yake si kuweka matokeo ya kazi yake mahali pa matini za Biblia, iwe ni kutengeneza hati za kale zilizotumiwa na waandishi waliovuviwa, ama kuelezea kisasa mahitimisho ya mwisho ya sayansi ya ufafanuzi. Kinyume chake, fahari yake ni kuzitilia nuru zaidi matini zenyewe za Biblia, kwa kusaidia kuzithamini zaidi na kuzifahamu kwa hakika zaidi kihistoria na kwa kina zaidi kiroho. D. Mahusiano na fani nyingine za kitheolojia Ufafanuzi, ukiwa wenyewe fani ya kitheolojia, “fides quaerens intellectum” (imani inayotafuta ufahamu), una mahusiano na fani nyingine za kitheolojia, yaliyo ya makini na uchangamano. Naam, kwa upande mmoja theolojia mpangilio inaathiri ufahamu tangulizi (pre-comprehension) ambao kwao wafafanuzi hukaribia matini za Biblia. Lakini, kwa upande mwingine, ufafanuzi unazipa fani nyingine za kitheolojia data zilizo za msingi kwazo. Basi, kati ya ufafanuzi na fani nyingine hujengwa mahusiano ya dialogia, kwa kuheshimiana katika upekee wa kila moja. 1. Theolojia na ufahamu tangulizi wa matini za Biblia Wanapochunguza matini za Biblia, wafafanuzi bila shaka wanakuwa na ufahamu tangulizi. Kwa upande wa ufafanuzi wa kikatoliki, ni ufahamu tangulizi unaotegemea hakika za imani: Biblia ni maandiko yaliyovuviwa na Mungu na kukabidhiwa kwa Kanisa ili kuamsha imani na kuongoza maisha ya kikristo. Hakika hizo za imani haziwafikii wafafanuzi katika hali ghafi, bali baada ya kufasiriwa katika jumuiya ya kikanisa na utafakari wa kitheolojia. Wafafanuzi, basi, wanaelekezwa katika utafiti wao na utafakari wa wanatheolojia wa kidogma kuhusu uvuvio wa Maandiko na kuhusu dhima yake katika maisha ya kikanisa. Lakini, kwa kupeana, kazi ya wafafanuzi juu ya matini zilizovuviwa huwapatia mang’amuzi ambayo wanatheolojia wa kidogma wanapaswa kujali ili kudhihirisha zaidi theolojia ya uvuvio wa Maandiko na ya ufasiri wa kikanisa wa Biblia. Ufafanuzi huamsha, kwa namna ya pekee, dhamiri hai zaidi na sahihi zaidi kuhusu tabia ya kihistoria ya uvuvio wa Biblia. Huonyesha kuwa mchakato wa uvuvio ni wa kihistoria si tu kwa sababu ulikuwako katika historia ya Israeli na ya Kanisa la awali, lakini pia kwa sababu umetekelezwa kwa njia ya wanadamu walioguswa na zama yao, na ambao, wakiongozwa na Roho, walikuwa na dhima kiutendaji katika maisha ya taifa la Mungu. Aidha, tamko la kitheolojia la kuwepo uhusiano makini kati ya Maandiko yaliyovuviwa na Mapokeo ya Kanisa lilihakikishwa na kukamilishwa kwa njia ya ukuaji wa mitaala ya kiufafanuzi, ambao uliwapa wafafanuzi nafasi ya kuzingatia zaidi na zaidi uwezo wa kuathiri wa mazingira hai ambamo matini zilitengenezwa (“Sitz im Leben”). 2. Ufafanuzi na theolojia ya kidogma Maandiko Matakatifu, bila kuwa locus theologicus (= chimbuko la theolojia) pekee, yamekuwa msingi ulio bora zaidi wa mitaala ya kitheolojia. Ili kufasiri Maandiko kwa usahihi wa kisayansi na kwa uhakika, wanatheolojia wanahitaji kazi ya wafafanuzi. Kwa upande wao, wafafanuzi sharti waelekeze utafiti wao jinsi kwamba “mtaala wa Maandiko Matakatifu” uweze kweli kuwa “kama roho ya theolojia” (Dei Verbum, 24). Kwa hiyo lazima kutilia mkazo pekee maudhui ya kidini ya maandishi ya Biblia. Wafafanuzi wanaweza kuwasaidia wanatheolojia kuepa hatari mbili: kwa upande mmoja, thania (dualism), inayotenga kabisa ukweli mmoja wa kimafundisho na usemi wake kisarufi, unaodhaniwa usio na maana; kwa upande mwingine, ufundamentalisti, ambao, kwa kuchanganya kilicho cha kibinadamu na kilicho cha kimungu, hudhania kuwa ni ukweli uliofunuliwa hata zile mbinu zilizo za kupita za usemi wa kibinadamu. Kwa ajili ya kuepa hatari hizo mbili, lazima kubainisha bila kutenganisha, na kukubali, basi, mvutano unaodumu. Neno la Mungu lilijidhihirisha kwa njia ya waandishi wanadamu. Fikra na semi ziko wakati huohuo za Mungu na za binadamu; kwa hiyo yote katika Biblia hutoka kwa Mungu na kwa mwandishi aliyevuviwa, kwa wakati mmoja. Lakini, si kusema kuwa Mungu aliitia tunu kamilifu kwa athari ya kihistoria juu ya ujumbe wake. Maana, huo ujumbe uko tayari kufasiriwa na kuhusishwa kisasa, yaani kutengwa, walau kwa kiasi fulani, na taathira ya kihistoria ya zamani ili upandikizwe katika taathira ya kihistoria ya sasa. Mfafanuzi huweka misingi ya shughuli hiyo, ambayo mwanatheolojia wa kidogma anaendeleza, akizingatia loci theologici nyingine zinazochangia ukuaji wa dogma. 3. Ufafanuzi na theolojia ya maadili Maoni kama hayo yanaweza kutolewa pia kuhusu mahusiano kati ya ufafanuzi na theolojia ya maadili. Biblia huunganisha barabara masimulizi ya historia ya wokovu na maonyo kadhaa kuhusu mwenendo unaopasika: k. v. amri, makatalio, maagizo ya kisheria, maonyo na ole za manabii, mashauri ya wenye hekima. Jukumu mojawapo la ufafanuzi ni kuhakikisha uzito wa mambo mengi hayo na hivyo kuandaa kazi ya wanatheolojia ya maadili. Jukumu hilo si rahisi, kwa sababu matini za Biblia, hazishughulikii kupambanua kati ya amri za maadili zilizo za wote, na miongozo ya usafi kiibada, na taratibu maalum za kisheria. Yote yamechanganyika pamoja. Tena, Biblia huonyesha maendeleo ya kimaadili makubwa sana, yanayopata utimilifu wake katika Agano Jipya. Basi, haitoshi kuwa msimamo fulani katika maadili ushuhudiwe katika Agano la Kale (k. m. matumizi ya utumwa, au ya talaka, au ya mauaji halaiki katika vita) ili uhesabiwe kuwa halali bado. Ni lazima kuwepo upambanuzi unaozingatia maendeleo yaliyotokea ya dhamiri ya kimaadili. Maandishi ya Agano la Kale yanayo ndani yake mambo “ambayo hayajakamilishwa na ya muda” (Dei Verbum, 15), ambayo utaratibu wa malezi ya Mungu haukuweza kuyafuta mara moja. Agano Jipya lenyewe si rahisi la kufasiriwa katika uwanja wa maadili, kwa vile linatumia mara nyingi semi za mifano au za mafumbo (paradoxical), au hata za kuchokoza; na uhusiano wa wakristo na sheria ya kiyahudi ni hoja yenye mabishano makali. Wanatheolojia ya maadili wana sababu tosha za kuwawekea wafafanuzi maswali mengi na muhimu, yatakayochochea utafiti wao. Mara nyingine inawezekana kupata jibu la kuwa haiko matini inayojadili kwa wazi suala lililoulizwa. Lakini hata hapo ushuhuda wa Biblia, ukichukuliwa katika mkikimkiki wake wa jumla wenye nguvu, hautakosa kusaidia kuhakikisha mwelekeo mmoja wa kina. Kuhusu mambo muhimu zaidi, ni ya msingi maadili ya amri kumi za Mungu. Agano la Kale hushika tayari ndani yake kanuni za msingi na tunu zinazoongoza kutenda kikamilifu kulingana na hadhi ya mwanadamu, aliyeumbwa “kwa mfano wa Mungu” (Mwa 1:27). Agano Jipya linazitilia nuru zaidi kanuni na tunu hizo, kutokana na ufunuo wa upendo wa Mungu katika Kristo. 4. Mitazamo tofauti na ulazima wa kuathiriana Katika hati yake ya 1988 kuhusu ufasiri wa dogma, Tume ya Kitheolojia ya Kimataifa ilikumbusha kuwa, katika nyakati zetu, yamelipuka mapambano kati ya ufafanuzi na theolojia ya kidogma; halafu inatazama michango mizuri ya ufafanuzi wa leo kwa ajili ya theolojia mpangilio (Ufasiri wa dogma; 1988, C, I, 2). Kwa usahihi zaidi inafaa kuongeza kwamba mapambano yalisababishwa na ufafanuzi huria (liberal exegesis). Baina ya ufafanuzi wa kikatoliki na theolojia ya kidogma hayakuwako mapambano ya jumla, bali mvutano wa wakati fulani. Ni kweli, lakini, kwamba mvutano unaweza kugeukia mapambano ikiwa toka upande huu ama huo, hukazika tofauti halali za mitazamo, hadi kuzigeuza kuwa sababu ya upinzani mkali. Naam, mitazamo ni tofauti, ya ndivyo inavyopasika kuwa. Jukumu la kwanza la ufafanuzi ni kupambanua kikamilifu maana ya matini za Biblia katika muktadha wake wenyewe, yaani katika muktadha wake maalum wa kifasihi na kihistoria, halafu katika muktadha wa kanoni ya Maandiko. Kwa kutekeleza jukumu hilo, mfafanuzi hutilia nuru maana ya kitheolojia ya matini, zinapokuwa na uzito wa aina hii. Hivyo, uhusiano wa kudumu unawezekana kati ya ufafanuzi na tafakari ya kitheolojia ya baadaye. Lakini mtazamo sio uleule, kwa sababu kazi ya mfafanuzi ni hasa ya kihistoria na ya kutoa maelezo, na hubaki kwenye ufasiri wa Biblia. Mwanatheolojia ya kidogma, kumbe, anafanya kazi ya kidhana (speculative) na ya kimpangilio (systematic), hasa. Kwa sababu hiyo anashughulikia hasa matini kadhaa na mandhari fulani za Biblia na, tena, hushughulikia data nyingine nyingi zisizo za kibiblia – k.v., maandishi ya Mababa, matamko ya Mitaguso, hati nyingine za Majisterio, liturujia –, na pia mifumo ya kifalsafa, na hali ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa ya leo. Kazi yake si ile ya kufasiri Biblia tu, bali ya kuelekea kwenye ufahamu wa dhati kabisa ya imani ya kikristo, katika maeneo yake yote, na hasa katika mahusiano katakata na maisha ya kibinadamu. Kwa sababu ya maelekeo yake ya kidhana na kimpangilio, theolojia mara nyingi imeangukia kwenye kishawishi cha kuona Biblia kama akiba ya dicta probantia (= semi zinazothibitisha) kwa ajili ya kuthibitisha hoja za kimafundisho. Siku hizi zetu wanatheolojia ya kidogma wamejipatia ufahamu mkali zaidi wa umuhimu wa muktadha wa kifasihi na wa kihistoria kwa ajili ya ufasiri sahihi wa matini za kale, na kukimbilia zaidi kutaka msaada wa wafafanuzi. Kwa vile ni Neno la Mungu liliotiwa kimaandishi, Biblia ina utajiri wa maana usioweza kudakwa kikamilifu, wala kufungwa katika theolojia ya kimpangilio yoyote ile. Moja ya dhima muhimu za Biblia ni kuitupia changamoto mifumo ya kitheolojia na kukumbusha daima kuwemo kwa mambo ya ufunuo wa kimungu na ya hali halisi ya wanadamu, ambayo mara nyingine yalisahauliwa au kupuuzwa kwenye juhudi za utafakari wa kimpangilio. Upyaisho wa mbinu za ufafanuzi unaweza kuchangia kuja kutambua zaidi. Na kwa upande wake, ufafanuzi hauna budi kukubali kuangazwa na utafiti wa kitheolojia. Utafiti huo utauchochea kutilia matini maswali muhimu na kufunua kwa wazi zaidi nguvu zake zote na utajiri wake. Uchunguzi wa kisayansi wa Biblia hauwezi kuepa utafiti wa kitheolojia, wala mang’amuzi ya kiroho na upambanuzi wa Kanisa. Ufafanuzi huzaa matunda bora unapotekelezwa katika mazingira ya imani hai ya jumuiya ya kikristo, inayotazamia wokovu wa ulimwengu mzima. IV. UFASIRI WA BIBLIA Ufasiri wa Biblia, ijapokuwa ni jukumu la pekee la wafafanuzi, lakini si ukiritimba wao, kwa sababu unahusu, katika Kanisa, vipengere ambavyo vyapita uchanganuzi wa kisayansi wa matini. Naam, Kanisa halitazami tu Biblia kama jumla ya hati za kihistoria kuhusu asili yake; linaipokea kama Neno la Mungu linaloelekezwa kwake, na kwa ulimwengu wote, katika siku za leo. Hakika hiyo ya imani ina matokeo yake katika juhudi za kuuhusisha na kuutamadunisha ujumbe wa Biblia, kama vile kuyaratibu matumizi mbalimbali ya matini zilizovuviwa, katika liturujia, katika “lectio divina”, katika huduma ya kiuchungaji, na katika harakati ya ekumeni. Tayari ndani ya Biblia yenyewe – kama tulivyodokeza katika sura iliyotangulia – tunaweza kuona matumizi ya uhusisho. Yaani, matini za kale zaidi zimesomwa upya kwenye nuru ya mazingira mapya, na kulinganishwa na hali ya sasa ya taifa la Mungu. Uhusisho, uliosimama kwenye dhanio ileile, hauna budi kuendelea kutekelezwa katika jumuiya za waamini. Kanuni za msingi za matumizi ya uhusisho ni hizi zifuatazo: Uhusisho unawezekana, kwa sababu matini ya Biblia, kwa ajili ya utimilifu wake wa tunu na wa maana, unafaa kwa zama zote na tamaduni zote (taz. Isa 40:8; 66:18-21; Mt 28:19-20). Ujumbe wa Biblia unaweza kwa wakati mmoja kupunguza (relativize) na kutajirisha mifumo ya tunu na kanuni za mwenendo za kila kizazi. Uhusisho ni wa lazima, kwa sababu, ijapo ujumbe wa Biblia una thamani ya kudumu, matini zake zilihaririwa kwa kuendana na hali za mazingira za kale na katika lugha za nyakati zile. Ili kuonyesha uzito zilio nao kwa wanaume na wanawake wa leo, ni lazima kuambatisha ujumbe wake na hali ya leo, na kuuweka katika lugha inayolingana na wakati uliopo. Hayo yanadai juhudi ya kihemenetiki inayotazamia kuzipambanua, ndani ya hali yake ya kihistoria, pointi muhimu za pekee za ujumbe. Uhusisho lazima uzingatie daima mahusiano changamano yaliyomo, katika Biblia ya kikristo, kati ya Agano Jipya na Agano la Kale, kwa vile Agano Jipya linavyojionyesha kama utimilifu wa Agano la Kale, na wenye kulipita. Uhusisho hutendeka kulingana na umoja wa kimkikimkiki ulioundwa hivyo. Uhusisho hutekelezwa kwa njia ya mkikimkiki wa mapokeo hai ya jumuiya ya imani. Hayo huwekwa wazi katika mwendelezo wa jumuiya zile zilizoyazaa Maandiko Matakatifu, zilizoyatunza na kuyapokeza. Katika kutekeleza uhusisho, mapokeo yatimiza dhima za aina mbili: kwa upande mmoja, yanalinda dhidi ya ufasiri haramu, na kwa upande mwingine, yanahakikisha kwamba mkikimkiki wa asili uendelee kupokezwa. Uhusisho, basi, haumaanishi kuvuruga matini. Si shauri la kutupia kwenye maandishi ya Biblia, maoni au itikadi mpya, bali ni kutafuta, kwa unyofu, mwanga yanaoshika ndani yake kwa ajili ya wakati wa leo. Matini ya Biblia ina mamlaka kwa nyakati zote juu ya Kanisa la kikristo na, ijapo zimepita karne nyingi tangu utungaji wake, unaendelea kushika wadhifa wake wa mwongozo mkuu usioweza kuvurugwa. Majisterio ya Kanisa “haiko juu ya Neno la Mungu, bali hulitumikia, ikifundisha yale tu iliyoyarithi. Kwani, kwa amri ya Mungu na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hulisikiliza Neno kwa uchaji, kulihifadhi kitakatifu, na kulieleza kiaminifu” (Dei Verbum, 10). Kutokana na kanuni hizo, inawezekana kutumia mbinu anuwai za uhusisho. Uhusisho, uliofanyika hata ndani ya Biblia, uliendelea katika Mapokeo ya kiyahudi kwa njia ya mbinu zinazopatikana katika Targumim na katika Midrashim: kutafuta madondoo yaliyo sambamba (gezerah shawah), kubadili namna ya kusoma matini (‘al tiqrey), kuchukua maana ya pili (tartey mishma’), n.k. Kwa upande wao, Mababa wa Kanisa walitumia ufananisho (typology) na istiari ili kuhusisha matini za Biblia kusudi ziifae hali ya Wakristo wa wakati wao. Wakati wetu, uhusisho lazima uangalie mabadiliko ya fikara na ukuaji wa mbinu za ufasiri. Uhusisho hudai kuanzia na ufafanuzi sahihi wa matini, wenye kupambanua maana yake sisisi. Ikiwa mwenye kujishughulisha katika kazi hiyo ya uhusisho hana utaalamu wa ufafanuzi, lazima ajipatie usaidizi wa miongozo ya kufaa kwa usomaji wake wa Biblia, inayoweza kumwelekeza vizuri katika ufasiri. Ili kutekeleza vema uhusisho, ufasiri wa Maandiko kwa njia ya Maandiko ni mbinu iliyo salama zaidi na ya kufaa sana, hasa kuhusu matini za Agano la Kale ambazo zilisomwa upya katika Agano la Kale lenyewe (k. m. “mana” ya Kut 16 katika Hek 16:20-29) na/au katika Agano Jipya (Yn 6). Uhusisho wa matini fulani ya Biblia katika maisha ya Kikristo hauwezi kutekelezwa kisahihi yakikosekana mahusiano na fumbo la Kristo na la Kanisa. Isingekuwa sahihi, kwa mfano, kuwawekea Wakristo, kama vielelezo vya mapigano ya kujipatia uhuru, masimulizi tu ya Agano la Kale (Kutoka; 1-2 Makabayo). Mbinu ya kihemenetiki, iliyo na misingi katika falsafa za kihemenetiki, hudai hatua tatu: 1) kusikiliza Neno kuanzia na hali ya kisasa; 2) kupambanua vile vipengele vya hali ya kisasa ambavyo matini ya Biblia huviangaza au kutaka kuvijadili; 3) kuchota katika utimilifu wa maana ya matini ya Biblia mambo yanayoweza kuendeleza hali ya kisasa kwa namna ya kufaa, kadiri ya mapenzi ya Mungu ya kuleta wokovu katika Kristo. Kwa njia ya uhusisho, Biblia huyaangaza masuala mengi ya sasa, kwa mfano: suala la huduma za aina mbalimbali, tabia ya kijumuiya ya Kanisa, uamuzi pendelevu kwa maskini, theolojia ya ukombozi, hali ya wanawake. Uhusisho unaweza pia kuwa makini kwa tunu zilizo nyeti zaidi kwa dhamiri ya leo, kama vile haki za binadamu, kulinda uhai wa binadamu, kuhifadhi mazingira, mvuto kwa amani kwa wote. Ili kuendelea kuafikiana na ukweli wenye kuokoa ulivyo katika Biblia, uhusisho lazima kujali mipaka fulani na kujihadhari na hatari ya kukengeuka. Ijapo kila aina ya usomaji wa Biblia inafanya uteuzi fulani, lazima kuepukana na usomaji wa kiuzushi, yaani ule ambao badala ya kuitii matini, unaitumia kwa malengo yake yenye hitilafu (kama ilivyo kwa uhusisho unaofanywa na madhehebu fulani, kama, k.m., Mashahidi wa Yehova). Uhusisho hupoteza uhalali wote ukifanyika kadiri ya kanuni za kinadharia zisizopatana na maelekeo ya kimsingi ya Biblia, kama k. m., urazini ulio kinyume na imani, au uyakinifu wenye kukana Mungu. Ni wazi kuwa ya kulaumiwa kila uhusisho unaoelekea kinyume cha haki na upendo wa kiinjili: kwa mfano ule unaotaka kusimika kwenye matini za Biblia ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Wayahudi, au ubaguzi wa kijinsia, iwe wa wanaume au wa wanawake. Uangalifu wa pekee ni wa lazima, kadiri ya roho ya Mtaguso wa Vatikano II (Nostra Aetate, 4), ili kuepa kabisa kuzihusisha matini kadhaa za Agano Jipya kwa maana ambayo ingeweza kuamsha au kutilia nguvu mitazamo hasi dhidi ya Waebrania. Kinyume chake, matukio ya kutisha ya wakati uliopita yanapaswa kusukuma kukumbusha bila kuchoka kuwa, kadiri ya Agano Jipya, Waebrania bado “wamekuwa wapenzi” wa Mungu “kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake” (Rum 11:28-29). Mikengeuko itaepushwa ikiwa uhusisho utaanzia katika ufasiri sahihi wa matini na kuendelea katika mkondo wa Mapokeo hai, chini ya uongozi wa Majisterio ya Kanisa. Kwa vyovyote, kuwepo hatari za kukengeuka hakuwezi kuwa upinzani halali dhidi ya utekelezaji wa jukumu la lazima la kufiki-sha ujumbe wa Biblia hadi masikioni na moyoni mwa vizazi vyetu. Kwa juhudi za uhusisho, unaowezesha Biblia kulinda ufanisi wake hata kati ya mabadiliko ya nyakati, hulingana, kadiri ya tofauti za mahali, juhudi za utamadunisho unaohakikisha kutia mizizi kwa ujumbe wa Biblia katika nchi zilizo tofauti. Utofauti ambao, lakini, si katika mambo yote kabisa, kamwe. Maana, kila utamaduni halisi huchukua, kwa namna yake, tunu za jumla zilizowekwa na Mungu. Msingi wa kitheolojia wa utamadunisho ni hakika ya imani ya kwamba Neno la Mungu hupita tamaduni zote ambamo limetungwa, na lina uwezo wa kuenea katika tamaduni nyingine, kwa jinsi ya kuwafikia wanadamu wote katika mazingira ya kiutamaduni wanamoishi. Hakika hiyo hutoka katika Biblia yenyewe, ambayo, tangu Kitabu cha Mwanzo, huchukua mwelekeo kwa wote (Mwa 1:27-28), na kuushika halafu katika baraka kwa watu wote aliyoahidiwa Ibrahimu na uzao wake (Mwa 12:3; 18:18), na kuuthibitisha kikamilifu kwa kueneza kwa “mataifa yote” uinjilishaji wa kikristo (Mt 28:18-20; Rum 4:16-17; Efe 3:6). Hatua ya kwanza ya utamadunisho ni kutafsiri katika lugha nyingine Maandiko yaliyovuviwa. Hatua hii ilianza tangu zama za Agano la Kale, matini ya Kiebrania ya Biblia ilipotafsiriwa kisimulizi katika lugha ya Kiaramayo (Neh 8:8.12) na, baadaye kimaandishi kwa Kigiriki. Maana, utafsiri daima ni zaidi kuliko unukuzi tu wa maandishi ya asili. Kupita toka lugha moja kwenda lugha nyingine kunadai kwa lazima mabadiliko ya muktadha wa kiutamaduni: dhana si sawa, na maana ya viashirio ni tofauti, kwa sababu zinahusiana na mapokeo mengine ya fikra na mitindo mingine ya maisha. Agano Jipya, lililoandikwa kwa Kigiriki, limeathiriwa lote na mkikimkiki wa utamadunisho, kwa sababu linatafsiri katika utamaduni wa Wayahudi wa kiyunani ujumbe wa kipalestina wa Yesu, likionyesha hivyo nia ya kuvuka mipaka ya eneo moja tu la kiutamaduni. Kazi ya kutafsiri matini za Biblia, ni hatua ya kimsingi, ambayo lakini haitoshi ili kuhakikisha utamadunisho wa kweli. Lazima hiyo kazi ifuatwe na ufasiri unaohusianisha kwa wazi zaidi ujumbe wa Biblia na aina za hisia, za fikra, za maisha na za kujieleza zilizo pekee za utamaduni mahalia. Kutoka ufasiri hupigwa hatua nyingine za utamadunisho, ambazo zapeleka kuunda utamaduni mahalia ulio wa kikristo, wenye kuenea katika sekta zote za maisha (sala, kazi, maisha ya kijamii, desturi, muundo wa sheria, sayansi na sanaa, tafakari za kifalsafa na za kitheolojia). Neno la Mungu, basi, ni mbegu ambayo, kutoka kwa ardhi ilipo, inanyonya mambo ya kufaa kwa ukuaji na uzaaji wake (taz. Ad Gentes, 22). Ndiyo sababu, Wakristo wanapaswa kujitahidi kupambanua “utajiri gani Mungu mkarimu aliwajalia mataifa. Wakati huohuo, inawapasa waamini wajaribu kuumulika utajiri huo na nuru ya kiinjili, na pia kuuokoa na kuurejesha kwa utawala wa Mungu Mwokozi” (Ad Gentes, 11). Inavyoonekana, si shauri la mchakato wa njia moja, bali wa “kurutubishana”. Kwa upande mmoja, utajiri uliomo katika tamaduni mbalimbali huliwezesha Neno la Mungu kuzaa matunda mapya na, kwa upande mwingine, mwanga wa Neno la Mungu huwezesha kuchambua yale yanayoletewa na tamaduni, ili kupinga mambo ya hasara na kuhimiza ukuaji wa yaliyo mema. Uaminifu kamili kwa nafsi ya Kristo, kwa mkikimkiki wa fumbo lake la Pasaka na kwa upendo wake kwa Kanisa, husaidia kuepukana na suluhisho za uongo: ile ya “ulinganisho” wa juujuu wa ujumbe, na ile ya fujo ya mchanganyo-dini (syncretism) (taz. Ad Gentes, 22). Katika Ukristo wa Mashariki na wa Magharibi utamadunisho wa Biblia ulitekelezwa tangu karne za mwanzoni na kuonyesha matokeo makuu. Lakini, haiwezekani kamwe kuudhania kama umetimilika; kumbe, sharti ufanyike daima, kuhusiana na mabadiliko endelevu ya tamaduni. Katika nchi zilizopata uinjilishaji nyakati za karibu kuna suala la aina nyingine. Naam, wamisionari hawakosi kuleta Neno la Mungu lilivyotamadunishwa katika nchi zao asilia. Ni lazima Makanisa mapya yajitahidi sana kupita kutoka kwa aina hiyo ngeni ya utamadunisho wa Biblia hadi aina nyingine, inayolingana na utamaduni wa nchi yao wenyewe.
C. Utumiaji wa Biblia katika Kanisa Tangu mwanzoni mwa Kanisa, usomaji wa Maandiko Matakatifu ulihesabiwa kama sehemu muhimu ya liturujia ya kikristo, iliyorithi kiasi cha liturujia ya sinagogi. Hadi leo Wakristo wanayakaribia Maandiko Matakatifu sanasana kwa njia ya liturujia, hasa katika maadhimisho ya Ekaristi ya Dominika. Kwa ujumla, liturujia, hasa liturujia ya sakramenti, ambazo adhimisho la Ekaristi ni kilele chake, hutekeleza kikamilifu uhusisho wa matini za Biblia, kwa sababu huweka tangazo lake kati ya jumuiya ya waamini waliokusanyika kandokando ya Kristo ili kumkaribia Mungu. Wakati huu Kristo “yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Kanisa” (Sacrosanctum Concilium, 7). Matini iliyoandikwa imekuwa tena Neno hai. Marekebisho ya Liturujia yaliyoamuliwa na Mtaguso wa Vatikano II yalijitahidi kuwaandalia Wakatoliki chakula cha Biblia kwa wingi zaidi. Utaratibu wa miaka mitatu ya masomo katika Misa ya Dominika unaipa Injili mahali pa pekee, kwa lengo la kudhihirisha vizuri fumbo la Kristo kama asili ya wokovu wetu. Kwa kuweka kwa kawaida somo moja la Agano la Kale kulingana na somo la Injili, utaratibu huo hudokeza mara nyingi njia za ufananisho kuwa njia ya kufaa kwa ufasiri wa Maandiko. Hiyo, inavyoeleweka, si njia pekee inayowezekana. Homilia, inayohusisha kwa wazi zaidi Neno la Mungu, ni sehemu halisi na muhimu ya liturujia. Tutairejea zaidi hapo mbele, kuhusu huduma ya kiuchungaji. Kitabu cha Masomo, kilichoandaliwa kutokana na maagizo ya Mtaguso (Sacrosanctum Concilium, 35), kilipaswa kuwezesha kusoma Biblia “kwa wingi zaidi, kutoka sehemu zake mbalimbali na kwa jinsi inavyofaa zaidi”. Kilivyo sasa, kinatekeleza kwa kiasi tu maelekeo hayo. Hata hivyo, kuwepo kwake kumeleta mafanikio kwa ekumeni. Katika nchi kadhaa imesaidia pia kufichua utovu wa mazoea ya Wakatoliki na Maandiko Matakatifu. Liturujia ya Neno imekuwa jambo mkataa katika adhimisho la kila sakramenti ya Kanisa. Si shauri la mfululizo wa masomo tu, bali hudai pia nyakati za ukimya na sala. Liturujia hiyo, hasa Liturujia ya Vipindi, huchota katika kitabu cha Zaburi sala ili kuziwezesha jumuiya za kikristo kusali. Tenzi na maombi zimejaa lugha ya kibiblia na uashiriaji wake. Hayo yote hudhihirisha jinsi ilivyo lazima ushiriki wa liturujia utayarishwe na kusindikizwa na mazoea ya kusoma Biblia. Ikiwa katika masomo “Mungu anasema neno lake kwa watu wake” (Missale Romanum, n. 35), liturujia ya Neno hudai jitihada kubwa katika kutangaza masomo, na pia kwa ufasiri wake. Basi, hutamaniwa kuwa katika malezi ya viongozi wa kesho wa jumuiya na makusanyiko, na pia ya wasaidizi wao, yazingatiwe madai ya Liturujia ya Neno iliyorekebishwa kweli. Hivyo, kutokana na jitihada ya wote, Kanisa litaendeleza utume wake liliokabidhiwa “wa kujilisha mkate wa uzima kutoka katika meza moja ya Neno la Mungu na pia ya Mwili wa Kristo, na kuwapa waamini” (Dei Verbum, 21). Lectio divina ni somo, la binafsi au la kijumuiya, la sehemu ndefu au si ndefu ya Maandiko, yanayopokelewa kama Neno la Mungu, na lenye kukua chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu, katika tafakari, sala na taamuli. Juhudi ya kusoma kwa utaratibu Maandiko, hata kila siku, ni mazoea ya kale ya Kanisa. Kama mazoea ya pamoja, hushuhudiwa katika karne ya tatu, enzi za Orijene; huyu alikuwa akitoa homilia akianzia na matini ya Maandiko, kwa kuisoma mfululizo katika siku za juma. Wakati ule kulikuwepo makusanyiko ya kila siku kwa ajili ya masomo na maelezo ya Maandiko. Desturi hiyo haikupata daima mafanikio makubwa kati ya Wakristo, na baadaye ikaachwa (Taz. Orijene, Hom. Gen., X, 1). Lectio divina kama mazoea hasa ya binafsi, inajulikana katika mazingira ya wamonaki wa mwanzoni. Katika enzi zetu, hati fundisho ya Tume ya Biblia iliyokubaliwa na Papa Pius XII iliipendekeza na kuhimiza kwa mafrateri wote, wa kijimbo na wa kitawa (De Scriptura Sacra, 1950; EB 592). Sisitizo juu ya lectio divina katika tabia zake mbili, ya kijumuiya na ya binafsi, hivyo imekuwa tena ya kawaida. Lengo linalokusudiwa ni kuunda na kulisha “upendo wa kweli na wa kudumu” kwa Maandiko Matakatifu, chemchemi ya uhai wa ndani na wa uzaaji wa kitume (De Scriptura Sacra; na Divino afflante Spiritu; EB 591 na 567), na pia kukuza ufahamu bora wa liturujia, na kuihakikishia Biblia nafasi muhimu katika masomo ya theolojia na katika sala. Hati ya Mtaguso Dei Verbum (n. 25) husisitiza vilevile somo la makini la Maandiko kwa upande wa Mapadre na Watawa. Aidha – na hili ndilo jambo jipya – huwaalika wote “waamini wa Kristo” kujifunza “uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu” (Flp 3:8). Hupendekezwa njia kadha wa kadha. Karibu na somo la binafsi, hushauriwa somo katika kikundi. Hati ya Mtaguso hukazia kuwa somo la Maandiko lazima lisindikizwe na sala, kwa sababu sala ndiyo jibu kwa Neno la Mungu linalopatikana katika Maandiko chini ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Katika taifa la Mungu zimeanzishwa mbinu nyingi kwa ajili ya somo la kijumuiya, na hakuna budi kuhimiza shauku hiyo ya kumjua zaidi Mungu na mpango wake wa wokovu katika Yesu Kristo kwa njia ya Maandiko. 3. Katika huduma ya kiuchungaji Matumizi ya mara kwa mara ya Biblia katika huduma ya kiuchungaji hushauriwa na Dei Verbum (n. 24), nayo huchukua mbinu tofauti kadiri ya aina ya hemenetiki wanayotumia wachungaji na ambayo waamini wanaweza kuielewa. Inawezekana kuona maeneo yake muhimu matatu: katekesi, mahubiri na utume wa kibiblia. Tena, yanaingia mambo mengi, kadiri ya kiwango cha jumla cha maisha ya kikristo. Maelezo ya Neno la Mungu katika katekesi (Sacrosanctun Concilium, 35; Mwongozo wa jumla wa katekesi, 1971,16), chemchemi yake ya kwanza ni Maandiko Matakatifu, ambayo, yakielezwa katika muktadha wa Mapokeo, huwa ni chanzo, msingi na kanuni ya mafundisho ya katekisimu. Ingefaa sana kwamba moja la malengo ya katekesi liwe ni kuingiza kwenye ufahamu sahihi ya Biblia, na usomaji wake uletao matunda, unaowezesha kufumbua ukweli wa kimungu uliomo, na kuamsha jibu, la ukarimu mkuu uwezekanavyo, kwa ujumbe ambao Mungu anawafikishia wanadamu kwa njia ya Neno lake. Katekesi lazima ianze na muktadha wa kihistoria wa ufunuo wa kimungu ili kuonyesha watu na matukio ya Agano la Kale na ya Agano Jipya kwenye mwanga wa mpango wa Mungu. Halafu, ili kupita kutoka kwa matini ya Biblia hadi maana yake ya wokovu kwa wakati wa sasa, hutumika taratibu za kihemenetiki mbalimbali, zinazotokeza maelezo ya aina tofauti. Mafanikio ya katekesi hutegemea ubora wa hemenetiki inayotumika. Kuna hatari ya kubaki kwenye maelezo ya juujuu, yanayotazama matukio na watu wahusika wa Biblia, kuendana na mfululizo wa nyakati tu. Ni wazi kuwa katekesi haiwezi kutumia Biblia yote, isipokuwa sehemu ndogo tu ya matini zake. Kwa kawaida, hutumia hasa masimulizi, katika Agano Jipya na katika Agano la Kale. Husisitiza hasa Amri kumi za Mungu. Lazima iangalie kutumia sawia maaguzi ya manabii, mafundisho ya vitabu vya hekima, na hotuba kuu za Injili, kama Hotuba ya mlimani. Mafundisho kuhusu Injili lazima yapeleke kukutana na Kristo, ambaye huleta ufunguo wa ufunuo wote ya kibiblia, na kuwasilisha mwito wa Mungu, ambao kila mmoja anapaswa kuitika. Neno la manabii na lile la “wahudumu wa neno” (Lk 1:2) halina budi kuonekana kana kwamba limetolewa sasa kwa Wakristo. Maonyo sawia yanafaa kwa huduma ya mahubiri, inayopaswa kutokeza katika matini za kale lishe ya kiroho inayofaa kwa mahitaji ya sasa ya jumuiya ya kikristo. Sasa, huduma hiyo hutekelezwa hasa mwishoni mwa sehemu ya kwanza ya adhimisho la Ekaristi, kwa njia ya homilia inayofuata tangazo la Neno la Mungu. Maelezo yanayotolewa katika homilia juu ya matini za Biblia hayawezi kuingia katika vipengele vingi. Kwa hiyo inafaa kutilia maanani michango muhimu ya matini hizo, ile ambayo huangazia imani na huwa na mvuto kwa maendeleo ya maisha ya kikristo, yawe ya kijumuiya au ya kibinafsi. Kwa kuonyesha michango hiyo, lazima kushughulikia uhusisho na utamadunisho, kadiri tulivyosema hapo juu. Kwa lengo hilo, inafaa kufuata kanuni sahihi za kihemenetiki. Kukosa matayarisho katika fani hiyo, matokeo yake ni kishawishi cha kukataa kuchambua kwa kina katika masomo ya Biblia na kubaki tu kuhubiri maadili au kuongea kuhusu masuala ya kisasa, bila kuyaangaza na Neno la Mungu. Katika nchi mbalimbali yalitolewa machapisho (publications), kwa msaada wa wafafanuzi, ili kusaidia wanaohusika na uchungaji kufasiri kisahihi masomo ya Biblia ya liturujia na kuyahusisha kwa namna ya kufaa. Ni matumaini kuwa juhudi hizo zienee hata zaidi. Wahubiri lazima waepukane na msisitizo wa upande mmoja tu kuhusu wajibu zinazowapasa waamini. Ujumbe wa Biblia sharti udumishiwe tabia yake maalum ya kuwa habari njema ya wokovu uliyotolewa na Mungu. Mahubiri yatakuwa na manufaa na yatalingana zaidi na Biblia yakisaidia kabla ya yote waamini “kujua karama ya Mungu” (Yn 4:10), ilivyofunuliwa katika Maandiko, na kufahamu kwa namna iliyo bora masharti yatokanayo. Utume wa kibiblia una shabaha ya kujulisha Biblia kama Neno la Mungu na chemchemi ya uhai. Kwanza, huhimiza kazi ya kutafsiri Biblia katika lugha mbalimbali, na kusambaza tafsiri hizo. Huamsha na kutegemeza shughuli nyingi: uundaji wa vikundi vya Biblia, mihadhara kuhusu Biblia, “majuma ya Biblia”, uchapishaji wa magazeti na vitabu, n.k. Mchango maalum hutolewa na vyama na harakati za kikanisa zinazoweka katika nafasi ya kwanza somo la Biblia kwa mtazamo wa imani na wa uwajibikaji wa kikristo. “Jumuiya ndogondogo” nyingi zinatia Biblia kama kiini cha mikutano yao na kudhamiria lengo la aina tatu: kujua Biblia, kujenga jumuiya na kuwahudumia watu. Na hapo pia msaada wa wafafanuzi unafaa ili kuepa uhusisho usio na misingi. Lakini, ni sababu ya furaha kuona Biblia mikononi mwa watu wanyonge na maskini, wanaoweza kutilia nuru ya ndani kwa ufasiri na uhusisho wake kisasa, kwa upande wa mtazamo wa kiroho na wa kimaisha, kuliko wale wenye sayansi inayojitegemea yenyewe (taz. Mt 11:25). Umuhimu unaozidi kukua daima wa vyombo vya upashanaji habari (“mass-media”) – vitabu na magazeti, redio, televisheni – hudai kuwa tangazo la Neno la Mungu na ujuzi wa Biblia vienezwe kwa bidii kwa njia ya vyombo hivyo. Dhima maalum sana za vyombo hivyo, na tena, nguvu ya juu ya kuwaathiri watazamaji wengi hudai matayarisho ya pekee kwa ajili ya utumiaji wake ili kuepa ufaraguzi usiopendeza, na pia matokeo ya kushangaza chapwa. Iwe ni katekesi, iwe ni mahubiri au utume wa kibiblia, matini ya Biblia lazima ionyeshwe daima kwa heshima istahilivyo. Ijapo ekumeni kama harakati maalum na iliyoratibishwa si ya siku nyingi sana, wazo la umoja wa taifa la Mungu unaokusudiwa kurudishwa kwa njia ya harakati hiyo lina misingi ya kina katika Maandiko. Lengo hilo lilikuwa juhudi ya daima ya Bwana (Yn 10:16; 17:11.20-33). Inatazamia umoja wa Wakristo katika imani, matumaini na upendo (Efe 4:2-5), katika kuheshimiana (Flp 2:1-5) na katika mshikamano (1Kor 12:14-27; Rum 12:4-5), lakini pia, na hasa, umoja hai na Kristo, kama matawi katika mzabibu (Yn 15:4-5), au viungo vya mwili na kichwa (Efe 1:22-23; 4:12-16). Umoja huo sharti uwe mkamilifu, kwa mfano wa ule wa Baba na Mwana (Yn 17:11-22). Maandiko hueleza msingi wake kitheolojia (Efe 4:4-6; Gal 3:27-28). Jumuiya ya kwanza ya kitume ni mfano wake thabiti na hai (Mdo 2:44; 4:32). Wingi wa masuala ambayo dialogia ya kiekumeni hukabiliana nao una uhusiano na ufasiri wa matini za Biblia. Baadhi ya masuala hayo ni ya kitheolojia: elimu ya mambo ya mwisho, muundo wa Kanisa, mamlaka kuu ya Papa na mamlaka ya pamoja ya Maaskofu, ndoa na talaka, kuwapa daraja la upadre kwa wanawake, n. k. Mengine ni ya taratibu ya kikanuni na kisheria; yanahusu uendeshaji wa Kanisa lote zima na wa makanisa mahalia. Hatimaye, mengine ni ya taratibu hasa ya kibiblia: orodha ya vitabu vya kanoni, masuala kadhaa ya kihemenetiki, n. k. Ufafanuzi wa Biblia, ijapo hauwezi kudai kutatua masuala yote hayo peke yake, hutakiwa kuipa ekumeni mchango muhimu. Maendeleo yenye maana yamekwisha onekana. Kwa sababu ya kutumia mbinu zilezile na malengo ya kiekumeni yanayofanana, wafafanuzi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo walifikia kuelekeana kwa vikubwa katika ufasiri wa Maandiko, zinavyoonyesha matini na tanbihi za tafsiri nyingi za Biblia za kiekumeni, na tena vitabu na makala nyingine pia. Inafaa, tena, kutambua kuwa, kuhusu mambo kadhaa ya pekee, tofauti katika ufasiri wa Maandiko mara nyingi zinatia changamoto na zinaweza kudhihirika kuwa za kutimizana na za kuleta manufaa. Ndivyo ilivyo zinapoonyesha tunu za mapokeo maalum ya jumuiya za Kikristo mbalimbali na hivyo kufafanua sura mbalimbali za fumbo la Kristo. Kwa vile Biblia ilivyo msingi jamii wa kanuni ya imani, sharti la kiekumeni hudai, kwa Wakristo wote, mwito wa ari wa kusoma upya Maandiko yaliyovuviwa, katika utiifu kwa Roho Mtakatifu, katika upendo, katika unyofu na katika unyenyekevu, kuyatafakari na kuyaishi, ili kufikia kwenye toba ya moyoni na utakatifu wa maisha, ambavyo, pamoja na sala kwa kuomba umoja wa Wakristo, ni roho ya harakati yote ya kiekumeni (taz. Unitatis Redintegratio, 8). Ingetakiwa, basi, kufanya kuwe rahisi kwa Wakristo walio wengi iwezekanavyo kujipatia Biblia, pia kuhimiza uandaaji wa tafsiri za kiekumeni – kwani matini moja ileile jamii husaidia usomaji na uelewa wa pamoja –, pia kuchochea vikundi vya sala vya kiekumeni ili kusaidia, kwa njia ya ushuhuda halisi na hai, kutengeneza umoja katika utofauti (taz. Rum 12:4-5).
HITIMISHO Kutokana na yaliyosemwa katika hati hii kwa kirefu – ijapo bado kwa ufupi mno katika pointi nyingi – hitimisho la kwanza litokanalo ni kwamba ufafanuzi wa kibiblia hutekeleza, katika Kanisa na katika ulimwengu, jukumu la lazima kabisa. Kutaka kuepukana nao wakati wa kuifasiri Biblia kungekuwa ndoto ya mchana, na kungeonyesha kukosa heshima kwa Maandiko yaliyovuviwa. Wafundamentalisti, kwa kutaka kuwafanya wafafanuzi kana kwamba wangekuwa watafsiri tu (hivyo wakisahau kuwa kutafsiri Biblia ni tayari kazi ya ufafanuzi) na wakikataa kuwafuata mbele zaidi katika uchunguzi wao, hawaelewi kuwa, kwa ajili ya kero, inayostahili sifa, ya kuwa waaminifu kamili kwa Neno la Mungu, wanashika njia, ambazo kwa kweli, zinawapeleka mbali na maana halisi ya matini za Biblia, na pia mbali na kupokea kikamilifu matokeo ya Umwilisho. Neno la milele lilichukua mwili katika wakati maalum wa historia, katika mazingira ya kijamii na kiutamaduni yanayoeleweka wazi. Anayetaka kulisikiliza, sharti alitafute kwa unyenyekevu pale linapopatikana, akikubali msaada wa lazima wa ujuzi wa kibinadamu. Ili kuongea na wanaume na wanawake, tangu zamani za Agano la Kale, Mungu alitumia kila kifaa cha lugha ya binadamu, lakini, wakati huohuo, alipaswa kuliweka Neno lake chini ya masharti ya lugha hiyo. Heshima ya kweli kwa Maandiko yaliyovuviwa hudai kuwa zitendeke juhudi zote zinazotakiwa ili kuweza kudaka vizuri maana yake. Kweli, haiwezekani kuwa kila Mkristo afanye mwenyewe binafsi kila aina ya utafiti, mpaka awezeshwe kuelewa vizuri zaidi matini za Biblia. Kazi hiyo wanakabidhiwa wafafanuzi, walio wahusika, katika sekta hii, kwa manufaa ya wote. Hitimisho la pili ni kwamba tabia yenyewe ya matini za Biblia hudai kuwa, kwa ajili ya kuzifasiri, uendelee kutumika mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, walau katika hatua zake kuu. Kwa maana, Biblia haijionyeshi kama ufunuo wa moja kwa moja wa kweli zisizohusiana na wakati, bali kama ushuhuda wa kimaandishi wa mfululizo wa matukio ambayo kwayo Mungu hujifunua katika historia ya wanadamu. Mbali na mafundisho matakatifu mengi ya dini nyinginezo, ujumbe wa Biblia umesimikwa imara katika historia. Hutokana na hilo kwamba maandishi ya Biblia hayawezi kueleweka barabara bila utafiti wa taathira zake za kihistoria. Utafiti wa “kidiakronia” hudumu kuwa wa lazima katika ufafanuzi. Njia za “kisinkronia”, kwa vyovyote, haziwezi kuchukua nafasi yake. Ili kuweza kufanya kazi kwa mafanikio, lazima kwanza ziyakubali matokeo ya [utafiti wa kidiakonia], walau kwa ujumla. Lakini, kisha kutimiza sharti hilo, njia za “kisinkronia” (ya kibalagha, ya kisimulizi, ya kisemiotiki, na nyingine) zinaweza kusaidia kufanya upya ufafanuzi, na kutoa mchango wa kufaa sana. Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, kweli, haiwezi kudai ukiritimba, bali inatakiwa kutambua mapungufu yake, na pia hatari zilizomo mbele yake. Ustawi wa siku hizi wa hemenetiki za kifalsafa na, kwa upande mwingine, maoni tuliyotoa kuhusu ufasiri katika mapokeo ya kibiblia na mapokeo ya Kanisa, vilitilia nuru mandhari kadhaa za suala la ufasiri, ambazo mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ilitaka kusahau. Kwani, kwa kutaka kukaza vema maana ya matini kwa kuziweka katika muktadha wao wa kihistoria wa asili, mbinu hiyo huonekana mara nyingine kukosa kuzingatia umkikimkiki wa maana ya matini na uwezekano wa kukua kwake. Isipofikia kuchunguza uhariri wa matini, bali hutazama tu masuala ya machimbuko na utabakishaji (stratification) wa matini, hautimizi kikamilifu jukumu lake la kiufafanuzi. Kwa kuwa aminifu kwa Mapokeo makuu, ambayo Biblia huyashuhudia, ufafanuzi wa kikatoliki lazima uepe – kadiri inavyowezekana – aina hii ya uharibifu kitaaluma na kudumisha tabia yake ya kuwa somo la kitheolojia, ambalo lengo lake muhimu ni kwenda kina katika imani. Hilo halimaanishi bidii pungufu katika utafiti wa kisayansi kamili, wala uharibifu wa mbinu kwa sababu ya juhudi ya utetezi. Kila sekta ya utafiti (uhakiki wa matini, mitaala ya lugha, uchanganuzi wa kifasihi, n.k.) ina sheria zake, zinazopasika kufuatwa kwa uhuru. Lakini hata moja ya sekta hizo maalum ni lengo linalojitosheleza. Katika utaratibu wa jumla wa jukumu la ufafanuzi, mwelekeo kwenye lengo kuu lazima ukubaliwe ili kuepesha nguvu kumwagwa bure. Ufafanuzi wa kikatoliki hauna haki ya kufanana na mkondo wa maji unaopotea katika mchanga wa uchanganuzi wa uhakiki pindukia. Unatekeleza, katika Kanisa na katika ulimwengu, dhima iletayo uhai: yaani, kutoa mchango wake kwa urithishaji halisi zaidi wa maudhui ya Maandiko yaliyovuviwa. Kwa lengo hilo hasa zinaelekea juhudi za ufafanuzi wa kikatoliki, kwa kuungana sana na upyaisho wa fani nyingine za kitheolojia, pia na kazi ya kiuchungaji ya uhusisho na utamadunisho wa neno la Mungu. Kwa kuchunguza masuala ya leo na kudokeza maoni fulani kuhusu masuala hayo, inatumainiwa kuwa hati hii imerahisisha, kwa ajili ya wote, ufahamu dhahiri zaidi wa wajibu wa wafafanuzi Wakatoliki.
Roma, 15 Aprili 1993. [1] Tunaposema “mbinu” (method) ya kiufafanuzi tunamaanisha jumla ya taratibu za kisayansi zinazotumika ili kufasiri matini mbalimbali. Tunaposema “njia” (approach), maana yake ni utafiti unaoongozwa kadiri ya mtazamo wa pekee. [2] Matini ya ibara hii ya mwisho ilipitishwa kwa wingi wa kura 11 juu ya 19; wanne walipinga na wanne hawakupiga kura (abstension). Waliopinga waliomba matokeo ya kura yachapishwe pamoja na matini yenyewe. Tume imekubali. [3] Hemenetiki ya neno iliyoendelezwa na Gerhard Ebeling na Ernst Fuchs ina chanzo chake katika njia nyingine [ya ufasiri] na unatokana na uwanja mwingine wa fikra. Unahusu zaidi theolojia ya kihemenetiki kuliko falsafa ya kihemenetiki. Hata hivyo, Ebeling akubaliana na waandishi kama Bultmann na Ricoeur katika kusema kwamba Neno la Mungu linapata maana yake kamilifu likiunganika tu na wale linaowaelekea.
|
|