Kiti Kitakatifu
WARAKA WA KITUME
MISERICORDIA ET MISERA
(MHURUMIVU NA MHURUMIWA)
KATIKA KUFUNGA
MWAKA WA JUBILEI YA PEKEE
YA HURUMA
FRANSISKO
kwa watakaosoma Waraka huu wa Kitume pawepo
huruma na amani
Mhurumivu na mhurumiwa (Misericordia et misera) ni usemi uliotumika na mtakatifu Augustino kwa kusimulia mkutano wa Yesu na mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi (taz. Yn 8:1-11). Hakuweza kupata usemi mzuri zaidi na wa kufaa kuliko huo ili kuelezea fumbo la upendo wa Mungu anapokuja kukutana na mwenye dhambi: “Walibaki hao wawili tu: mhurumiwa na mhurumivu”.[1] Jinsi ilivyo kubwa huruma na haki ya Mungu ing’aayo katika simulizi hili! Mafundisho yake yaja kuangaza hitimisho la Jubilei ya Pekee ya Huruma, wakati inaonyesha njia ambayo twaitwa kuifuata katika siku za mbele.
1. Ukurasa huu wa Injili waweza kuchukuliwa kwa haki kama ikona ya lile tuliloadhimisha katika Mwaka Mtakatifu, ambao ulikuwa muda muafaka uliojaa huruma, ambayo yenyewe inaomba kuadhimishwa na kuishwa tena katika jumuiya zetu. Maana, huruma haiwezi kuwa tu sehemu ya nyongeza katika maisha ya Kanisa, bali ni kiini cha uwepo wake, nayo inadhihirisha na kuonjesha ukweli halisi wa Injili. Yote hufunuliwa katika huruma; yote huhitimishwa katika upendo wenye huruma wa Mungu Baba.
Mwanamke na Yesu walikutana. Mwanamke alikuwa mzinzi na, kadiri ya Torati, alihukumiwa afe kwa kupigwa mawe. Na Yesu, ambaye kwa mahubiri yake na kwa kujitoa kabisa sadaka, hadi msalabani, alirejesha sheria ya Musa kwenye lengo lake halisi la awali. Kiini chake si sheria au haki ya kisheria, bali kiini chake ni upendo wa Mungu, ambaye anajua kusoma moyoni mwa kila mtu, na kugundua hamu iliyofichama ndani kabisa, ambayo lazima itangulie juu ya yote. Katika simulizi hili la Injili, lakini, hazikutani dhambi na hukumu kinadharia, bali hukutana mwanamke mdhambi na Bwana Mwokozi. Yesu alitazama mwanamke huyo machoni na kusoma moyoni mwake: na humo alikuta hamu ya kueleweka, kusamehewa na kuokolewa. Dhambi yenye hitaji la kuhurumiwa ilivikwa huruma ya upendo. Yesu hakutoa hukumu yoyote, ila ile iliyotokana na huruma na rehema kwa hali ya yule mwanamke mkosefu. Yesu aliwajibu wale waliotaka kumshtaki na kumhukumu auawe, kwanza kwa kubaki kimya kwa muda mrefu, akitaka kuruhusu sauti ya Mungu izuke kwenye dhamiri zao, ya mwanamke na ya wale waliomshtaki. Nao waliacha mawe walioshika mkononi yaanguke chini, na mmoja mmoja wakatoka, wakaenda zao (taz. Yn 8:9). Na baada ya kubaki kimya hivi, Yesu alisema: “Mwanamke, wako wapi? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? ... Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (a. 10-11). Kwa kufanya hivyo, Yesu alimsaidia kutazama mbele kwa tumaini na kuwa tayari kuanza upya maisha yake; Kuanzia hapo, akipenda, ataweza “kuenenda katika upendo” (taz. Efe 5:2). Mara unapovikwa huruma, hata kama inaendelea kuwepo ile hali ya udhaifu unaotokana na dhambi, hiyo hufunikwa na kushindwa na upendo unaowezesha kutazama mbele zaidi na kuishi tofauti.
2. Na kwa kweli Yesu alikuwa ameshafundisha wazi hayo, pale ambapo, akiwa amealikwa chakulani na mfarisayo mmoja, alikaribiwa na mwanamke mmoja aliyefahamika kwa wote kama mwenye dhambi (taz. Lk 7:36-50). Naye alipaka miguu yake Yesu marhamu, akamdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake (taz. a. 37-38). Na mfarisayo alipokwazika, Yesu alimjibu, akisema: “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo." (a. 47).
Msamaha ni ishara iliyo dhahiri kabisa ya upendo wa Mungu Baba, ambao Yesu alitaka kufunua katika maisha yake yote. Hakuna ukurasa wa Injili unaoweza kuhesabiwa kuwa hauhusiki na amri hii ya upendo unaofikia hadi kusamehe. Hata katika dakika za mwisho za maisha yake hapa duniani, aliposulubiwa msalabani, Yesu alitamka maneno ya msamaha: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Lk 23:34).
Hakuna chochote ambacho mwenye dhambi aliyetubu akikiweka mbele ya huruma ya Mungu, kinabaki hivihivi pasipo kupokea kumbatio la msamaha wake. Ndiyo sababu hakuna mtu anayeweza kuweka masharti kwa huruma; yenyewe inadumu kuwa daima tendo la ukarimu wa bure wa Baba wa mbinguni, upendo usio na masharti na tusioweza kuustahili. Kwa hiyo, tusijiweke kwenye hatari ya kupingana na uhuru kamili wa upendo ambao kwao Mungu anataka kuingia katika maisha ya kila mtu.
Huruma ni tendo hili hai la upendo, ambalo, kwa kusamehe, hugeuza na kubadili maisha. Ndivyo linavyofunuliwa fumbo lake la kimungu. Mungu ni mwingi wa huruma (taz. Kut 34:6), na huruma zake ni za milele (taz. Zab 136), kizazi baada ya kizazi anamkumbatia kila mtu anayemtumainia, na kumgeuza kwa kumkirimia uzima wake mwenyewe.
3. Furaha kubwa kiasi gani imeingia moyoni mwa wanawake hao wawili, yule mzinzi na yule mwenye dhambi! Msamaha umewafanya wajisikie hatimaye wamekombolewa na kufurahi kama hawajawahi kabla. Machozi ya aibu na uchungu vimegeuka kuwa tabasamu la mwenye kujua kwamba anapendwa. Huruma husababisha furaha, kwa sababu moyo hufunguliwa kupokea tumaini la maisha mapya. Furaha ya kusamehewa haiwezi kusemeka, ila inajionyesha yenyewe katika nafsi zetu kila mara tunapoing’amua. Asili yake ni upendo wa Mungu anayekuja kwetu, akivunja duru ya umimi unaotuzungusha, ili kutufanya na sisi tuwe vyombo vya huruma.
Bado yana maana sana yale maneno ya zamani yaliyowaongoza wakristo wa kwanza: “Ujivike furaha ambayo daima humpendeza Mungu na kumridhisha. Yeye naye anaifurahia. Kila mtu mwenye furaha hutenda mema, huwaza mema na kudharau huzuni. [...] Wataishi katika Mungu wale wanaoondokana na huzuni na kuvalishwa kwa kila furaha”. [2] Kuonja huruma kunaleta furaha. Tusiruhusu mateso na mahangaiko mbalimbali yatunyang’anye furaha. Iweze kubaki imejikita moyoni mwetu na kutufanya tuyatazame daima kwa amani maisha ya kila siku.
Katika utamaduni ambao mara nyingi hutawaliwa na teknolojia, aina za huzuni na upweke zaonekana kuongezeka kwa watu, na hata kwa vijana wengi. Mustakabali unaonekana kuwa mateka ya wasiwasi usioruhusu kuishi maisha thabiti. Ndiyo sababu mara nyingi zinazuka hisia za uchungu, huzuni na wasiwasi, ambazo polepole zaweza kutupeleka kwenye kukata tamaa. Kuna haja sana ya mashahidi wa tumaini na furaha ya kweli, ili kufukuza watangazaji wa uongo wanaoahidi furaha iliyo rahisi katika paradisi za kubuniwa tu. Utupu moyoni walio nao wengi huweza kujazwa na tumaini tulilo nalo, na furaha inayotokana nalo. Kuna hitaji kubwa la kugundua furaha inayojifunua katika moyo ulioguswa na huruma. Kwa hiyo, tutunze kama hazina yetu maneno haya ya Mtume Paulo: “Furahini katika Bwana sikuzote” (Flp 4:4; taz. 1The 5:16).
4. Tumeadhimisha Mwaka wenye matukio mengi, ambamo tumejaliwa kwa wingi neema ya huruma. Kama upepo uletao wokovu uvumao kwa kasi, wema na huruma vya Bwana vilimiminwa juu ya ulimwengu mzima. Na hatuwezi kubaki hivihivi bila kujali, mbele ya mtazamo huu wa Mungu wenye upendo, ambao kwa muda mrefu wote huo ulituelekea, kwa sababu mtazamo huo hugeuza maisha.
Na, kabla ya yote, twapaswa kumshukuru Bwana Mungu na kumwambia: “Bwana, umeiridhia nchi yako, [...]. Umeusamehe uovu wa watu wako” (Zab 85:1-2). Ndivyo ilivyo: Mungu aliyakanyaga maovu yetu na kuzitupa dhambi zetu zote katika vilindi vya bahari (taz. Mik 7:19); hazikumbuki tena, kwa maana umezitupa zote nyuma yake (taz. Isa 38:17); kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali naye (taz. Zab 103:12).
Katika Mwaka huu Mtakatifu, Kanisa limejua kutega masikio na kuonja kwa ari uwepo na ukaribu wa Mungu Baba, ambaye kwa kazi ya Roho Mtakatifu amelidhihirishia kwa wazi zaidi kipawa na utume wa Yesu Kristo kuhusu msamaha. Ulikuwa kweli ujio mpya wa Bwana kati yetu. Tumesikia roho yake kupuliza juu ya Kanisa na, kwa mara nyingine tena, maneno yake yametuonyesha utume: “Pokeeni Roho Mtakatifu: Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yn 20:22-23).
5. Sasa, ikiisha kutimia Jubilei hii, ni wakati wa kuangalia mbele na kufahamu jinsi tunavyoweza kuendelea kwa uaminifu, furaha na ari katika kutumia utajiri wa huruma ya Mungu. Jumuiya zetu zitaweza kudumu hai na tendaji katika kazi ya uinjilishaji mpya kadiri “wongofu wa kichungaji” tunaoitwa kuuishi [3] utaundwa kila siku na nguvu ya huruma inayofanya upya mambo yote. Tusiweke mipaka kwenye utendaji wake, tusimhuzunishe Roho Mtakatifu anayetuonyesha sikuzote njia mpya za kuendea ili kupeleka Injili ya wokovu kwa watu wote.
Kwanza kabisa, tunaitwa kuadhimisha huruma. Kuna utajiri gani katika sala ya Kanisa kila linapomwomba Mungu kama Baba mwingi wa huruma! Katika liturujia, si tu kwamba huruma hutajwa mara nyingi, ila tunaipokea na kuiishi kihalisia. Tangu mwanzo hadi hitimisho la adhimisho la Ekaristi Takatifu, huruma hurudia mara nyingi katika majibizano baina ya kusanyiko linalosali na moyo wa Mungu Baba, anayefurahi kila awezapo kumimina upendo wake wenye huruma. Baada ya kuomba msamaha mwanzoni mwa Misa kwa kusali “Bwana, utuhurumie”, tunahakikishwa mara: “Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.” Kwa tumaini hili jumuiya ya kikristo hukusanyika mbele ya Bwana, hasa siku takatifu ya ufufuko. Sala nyingi za “kolekta” zina lengo la kukumbusha zawadi kubwa ya huruma. Kwa mfano, katika kipindi cha Kwaresima, twasali tukisema: “Ee Mungu, uliye asili ya rehema zote na mema yote, ulionyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kutoa sadaka. Uwe radhi kutazama ungamo hili la unyonge wetu, ili, maadamu tunanyenyekeshwa na dhamiri zetu, tuinuliwe daima na rehema yako.” [4] Halafu tunatoswa katika Sala kuu ya Ekaristi kwa njia ya Utangulizi unaotangaza: “Kwa maana Wewe jinsi hii uliupenda ulimwengu hata, kwa kutuhurumia, ukamtoa kwetu Mkombozi. Ulitaka aishi sawa na sisi, lakini bila dhambi”. [5] Zaidi ya hayo, Sala ya Ekaristi ya nne ni utenzi wa huruma ya Mungu: “Kwa huruma yako ulikuja kuwasaidia watu wote, ili wanaokutafuta wakupate”. “Utuhurumie sisi sote”, [6] ni ombi ambalo kuhani anakazia kutoa katika Sala ya Ekaristi ili kumsihi Mungu atujalie ushirika na uzima wa milele. Baada ya sala ya Baba yetu, kuhani anaongeza sala kwa kuomba amani na kuopolewa na dhambi “kwa msaada wa huruma yako”. Na kabla ya ishara ya amani, tunayopeana kama alama ya udugu na upendano katika mwanga wa msamaha tuliopokea, yeye anasali tena, akisema: “Usizitazame dhambi zetu, ila tu imani ya Kanisa lako”. [7] Kwa maneno haya, kwa matumaini na unyenyekevu tunaliombea Mama Kanisa takatifu zawadi ya umoja na amani. Adhimisho la huruma ya Mungu linafikia kilele chake katika sadaka ya Ekaristi, iliyo ukumbusho wa fumbo la kipasaka la Kristo, ambamo wokovu wa kila mwanadamu, wa historia na wa ulimwengu mzima, hububujikia humo. Kwa kifupi, kila sehemu ya adhimisho la Ekaristi inarejea kwenye huruma ya Mungu.
Katika maisha yote ya kisakramenti, huruma inatolewa kwetu kwa wingi. Si bila sababu kwamba Kanisa liliona vema kuitaja wazi huruma katika fomula za sakramenti mbili tunazoziita “za uponyaji”, yaani Kitubio au Upatanisho, na Mpako wa wagonjwa. Fomula ya ondoleo la dhambi husema: “Mungu, Baba mwenye huruma, aliupatanisha ulimwengu na nafsi yake, kwa kifo na ufufuko wa Mwanawe; akatushushia Roho Mtakatifu, tupate kuondolewa dhambi. Yeye mwenyewe akusamehe na kukupa amani kwa huduma ya Kanisa”, [8] na ile ya Mpako wa wagonjwa husema: “Kwa Mpako huu mtakatifu na kwa huruma yake kuu, Bwana akusaidie wewe kwa neema ya Roho Mtakatifu”. [9] Kwa hiyo, katika sala ya Kanisa marejeo ya huruma, mbali na kuwa tu suala la uhimizaji, ni uwezo utendao kazi, maana yake, tunapoomba huruma kwa imani, tunajaliwa, na tunapoiungama kuwa hai na halisi, inatugeuza kwelikweli. Huu ndio ukweli wa msingi wa imani yetu, ambao twapaswa kuushika katika uhalisia wake wote: kabla ya kufunuliwa dhambi, tulifunuliwa upendo ambao kwao Mungu aliuumba ulimwengu na binadamu. Upendo ni tendo la kwanza la Mungu ambalo kwalo yeye anajitambulisha kwetu na kutujia. Kwa hiyo, tufungue mioyo na tuamini kwamba Mungu anatupenda. Upendo wake unatutangulia daima, unatusindikiza na kubaki karibu nasi, licha ya dhambi zetu.
6. Katika muktadha huu, kusikiliza Neno la Mungu pia kunapata maana mahsusi. Kila Dominika, Neno la Mungu latangazwa katika jumuiya ya kikristo ili siku ya Bwana iangazwe kwa nuru inayotokana na fumbo la kipasaka. [10] Katika adhimisho la Ekaristi tunahudhuria kwenye mazungumzano kati ya Mungu na watu wake. Maana, katika tangazo la Masomo kutoka Biblia, tunarudia kukumbushwa historia ya wokovu wetu kwa njia ya kazi isiyokoma ya huruma tunayotangaziwa. Mungu anasema tena leo na sisi kama kwa marafiki, “anashinda” pamoja nasi [11] ili kutujalia umoja naye na njia ya uzima. Neno lake linafasiri na kutambua maombi yetu na wasiwasi zetu, na kuwa jibu lizaalo ili tuweze kung’amua kweli kwamba Yeye yupo karibu. Homilia inakuwa na umuhimu mkubwa kweli, na nafasi ambamo “ukweli unaambatana na uzuri na wema”,[12] ili kuishtua mioyo ya waamini mbele ya wingi wa huruma! Ninasihi sana kuandaa vema homilia na kuwa makini katika kuhubiri. Nayo italeta matunda zaidi, kadiri kuhani atakavyozidi kung’amua katika nafsi yake wema na huruma ya Bwana. Kushirikisha uhakika wa kwamba Mungu anatupenda si suala la ufasaha, bali ni sharti ili kuaminika katika ukuhani wake. Kwa hiyo, kuishi huruma ni njia kuu ili kuifanya huruma iwe tangazo la kweli la faraja na wongofu katika maisha ya kichungaji. Homilia, kama vile katekesi pia, huhitaji kutegemezwa daima na moyo huu ulio hai wa maisha ya kikristo.
7. Biblia ndiyo kitabu kikuu kinachosimulia maajabu ya huruma ya Mungu. Kila ukurasa wake umejaa upendo wa Mungu Baba ambaye tangu kuumbwa kwa ulimwengu alipenda kuweka katika viumbe vyote alama za upendo wake. Roho Mtakatifu, kwa kupitia maneno ya manabii na maandiko ya kihekima, aliongoza historia ya Israeli katika kutambua upendo na ukaribu wa Mungu, licha ya watu wake kukosa uaminifu. Maisha ya Yesu na mahubiri yake yanaongoza tangu msingi historia ya jumuiya ya kikristo, ambayo imegundua utume wake kutokana na agizo la Kristo la kuwa chombo cha kudumu cha huruma yake na msamaha wake (taz. Yn 20:23). Kwa njia ya Maandiko Matakatifu, yakitunzwa hai na imani ya Kanisa, Bwana anaendelea kusema kwa Bibi harusi wake na kumwonyesha njia ya kuiendea, kusudi Injili ya wokovu iwafikie watu wote. Ni hamu yangu kubwa sana kwamba Neno la Mungu liadhimishwe zaidi na zaidi, kufahamika na kuenezwa, ili kwa njia yake lieleweke zaidi lile fumbo la upendo linalobubujika katika chemchemi ile ya wokovu. Analikumbusha waziwazi Mtume Paulo, kwa kuandika: “Kila Andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza na kwa kuwaadibisha katika haki” (2Tim 3:16).
Ingefaa kwamba kila jumuiya, katika Dominika moja ya Mwaka wa kiliturujia, ingeweka upya azimio la kueneza, kufahamu na kutafakari Maandiko Matakatifu: Dominika nzima moja iliyowekwa kwa heshima ya Neno la Mungu, ili kufahamu utajiri usio na mipaka unaotokana na mazungumzano ya mara kwa mara ya Mungu na watu wake. Hakutakosekana ubunifu, kusudi fursa hii itajirishwe kwa mipango itakayowachochea waamini kuwa vyombo hai vya kupeleka Neno kwa watu. Bila shaka, miongoni mwa miradi hii kutakuwepo uenezaji mpana zaidi wa lectio divina (Somo la kimungu), kusudi, kwa njia ya usomaji wa kusali wa kitabu kitakatifu, maisha ya kiroho yapate kutegemezwa na kukuzwa. Lectio divina juu ya mada zinazohusiana na huruma itasaidia kugusa kwa mkono kiasi gani cha uzaaji kinatoka katika kitabu kitakatifu, cha kusomwa katika mwanga wa mapokeo yote ya kiroho ya Kanisa, ambao lazima utatimia katika kazi na matendo ya upendo. [13]
8. Adhimisho la huruma linafanyika kwa namna mahususi kabisa katika Sakramenti ya Upatanisho. Hii ndiyo nafasi muafaka tunapoona utamu wa kukumbatiwa na Mungu Baba, ambaye anakuja kutulaki ili kuturudishia neema ya kuwa tena watoto wake. Sisi ni wenye dhambi, na tunabeba ndani yetu uzito wa upinzani baina ya yale tunayotaka kutenda na yale ambayo, kinyume chake, tunayatenda kimatendo (taz. Rum 7:14-21); lakini, neema inatutangulia daima, nayo inakuwa na sura ya huruma yenye uwezo wa kutenda upatanisho na msamaha. Mungu anatujulisha upeo wa upendo wake mbele ya hali yetu ya wenye dhambi. Neema ina nguvu zaidi, inashinda kila upinzani tunaoweza kufanya, kwa sababu upendo hushinda yote (taz. 1Kor 13:7). Katika Sakramenti ya Msamaha, Mungu anatuonyesha njia ya wongofu kumwelekea Yeye, na anatualika kung’amua tena ukaribu wake. Ni msamaha unaopatikana kwa kuanza, kabla ya yote, kuyaishi mapendo. Anatukumbusha pia Mtume Petro, kwa kuandika kwamba “Upendano husitiri wingi wa dhambi” (1Pet 4:8). Mungu peke yake huondoa dhambi, lakini anatuagiza hata sisi kuwa tayari kuwasamehe wengine, hivyo kama Yeye anavyosamehe dhambi zetu: “Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea” (Mt 6:12). Ni huzuni kiasi gani tunapojifungia binafsi na hatuwezi kusamehe! Kinyongo, hasira na kisasi hutushinda, na kufanya maisha yetu yasiwe na furaha, kwa kubatilisha juhudi furahifu za kutenda huruma.
9. Tukio la neema ambalo Kanisa limeishi kwa manufaa kwelikweli katika Mwaka huu wa Jubilei bila shaka lilikuwa lile tendo la huduma ya Wamisionari wa Huruma. Utendaji wao wa kichungaji ulitaka kudhihirisha kwamba Mungu haweki mipaka yoyote mbele ya wale wanaomtafuta kwa moyo uliojuta, kwa sababu mwenyewe anawaendea wote kama Baba. Nilipokea mashuhuda mengi yenye furaha kwa ajili ya kukutana tena na Bwana katika Sakramenti ya Kitubio. Tusipoteze fursa ya kuishi imani yetu pia kama mang’amuzi ya upatanisho. “Mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:20) ni mwaliko ambao, kwa mara nyingine tena katika siku zetu hizi, Mtume anatoa ili kumfahamisha kila mwamini uweza wa upendo ambao unatufanya kuwa “kiumbe kipya” (2Kor 5:17).
Nataka nitoe shukrani zangu kwa kila Mmisionari wa Huruma kwa ajili ya huduma hiyo muhimu sana iliyotolewa kwa ajili ya kuifanyiza kazi neema ya msamaha. Huduma hiyo isiyo ya kawaida, lakini, haitakwisha kwa kufungwa Mlango Mtakatifu. Maana, ninataka iendelee kutolewa, hadi agizo jipya litakapotolewa, kama ishara wazi kwamba neema ya Jubilei inaendelea kuwa hai na tendaji katika sehemu mbalimbali za dunia. Itakuwa jukumu la Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kusimamia katika kipindi hiki Wamisionari wa Huruma, kama dhihirisho la moja kwa moja la juhudi zangu na ukaribu wangu katika kutafuta namna zinazofaa zaidi za kutekeleza huduma hiyo muhimu.
10. Ninawahimiza kwa mara nyingine tena makuhani kujiandaa kwa makini kwa huduma ya Kitubio, ambayo ndiyo utume halisi wa kikuhani. Ninawashukuruni sana kwa utumishi wenu na ninawaomba mwakaribishe wote; mwe mashahidi wa upendo mtamu wa kibaba, licha ya uzito wa dhambi; wenye juhudi katika kusaidia kutafakari juu ya maovu yaliyotendeka; mwe wazi katika kusisitiza kanuni msingi za kimaadili; mwe tayari kuwasindikiza waamini katika safari ya toba, mkitembea nao hatua kwa hatua kwa uvumilivu; mwe na busara katika kupambanua kila tatizo la kila mmoja; mwe wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Kama Yesu mbele ya mwanamke mzinzi alivyochagua kubaki kimya ili kumwokoa katika hukumu ya kifo, vivyo hivyo na kuhani katika pakuungamia awe mnyenyekevu wa moyo, akijua kwamba kila mtubuji anamkumbushia pia yeye mwenyewe alivyo: mwenye dhambi, lakini mhudumu wa huruma.
11. Ningependa wote tutafakari maneno ya Mtume, aliyoyaandika mwishoni mwa maisha yake, alipokiri kwa Timotheo kwamba yeye alikuwa wa kwanza wa wenye dhambi, “lakini kwa ajili hii alipata rehema” (1Tim 1:16). Maneno yake, kwa jinsi yalivyo yenye nguvu, yanatusukuma hata sisi kutafakari kuhusu maisha yetu ili kuona namna huruma ya Mungu inavyofanya kazi katika kubadilisha, kuongoa, na kugeuza moyo wetu. “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri; lakini nalipata rehema” (1Tim 1:12-13).
Tukumbuke, basi, maneno ya Mtume kwa juhudi za kichungaji zinazofanywa mpya kila wakati: “Mungu alitupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho” (2Kor 5:18). Sisi ambao tulisamehewa kwanza kwa kutazamia huduma hii, tukafanywa mashahidi katika nafsi yetu wa msamaha kwa ajili ya wote. Hakuna sheria au amri inayoweza kumzuia Mungu asimkumbatie mwanae anayemrudia akitambua kuwa amekosa, lakini akidhamiria kuanza upya. Kujikita tu katika sheria ni sawa na kubatilisha imani na huruma ya Mungu. Kuna thamani ya uongozi katika sheria (taz. Gal 3:24) ambayo mwisho wake ni upendo (taz. 1Tim 1:5). Lakini, mkristo anaitwa kuishi hali mpya ya Injili, “sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu” (Rum 8:2). Hata kwenye shida kubwa zaidi, ambapo kungeweza kuwepo kishawishi cha kutanguliza haki inayoendana na maagizo tu, inapasa kuiamini nguvu inayotokana na neema ya Mungu.
Sisi waungamishaji tunajua vizuri ni watu wangapi wanaodhihirisha wongofu wao wakiwa mbele ya macho yetu. Kwa hiyo, tujitahidi kutumia vitendo na maneno ambavyo vitaweza kumgusa mtimani mwa moyo mtubuji, kusudi agundue jinsi alivyo karibu naye kwa upendo Mungu Baba mwenye kusamehe. Tusibatilishe nafasi hizi kwa vitendo ambavyo vinaweza kupinga hamu ya kupewa huruma. Badala yake, tusaidie kuangaza dhamira ya kila mmoja kwa mwanga wa upendo wa Mungu usio na mipaka (taz. 1Yoh 3:20).
Sakramenti ya Upatanisho inahitaji kupewa nafasi yake katika kiini cha maisha ya kikristo; ndiyo maana inadai wawepo makuhani wanaoweka maisha yao tayari kwa kuitumikia “huduma ya upatanisho” (2Kor 5:18), kwa namna ya kwamba, pamoja na kutowazuia yeyote, mwenye majuto ya dhati, asiujongee upendo wa Mungu Baba anayesubiri kurudi kwake, wote wajaliwe nafasi na uwezo wa kuonja nguvu zenye kuokoa za msamaha.
Fursa muafaka huweza kuwa adhimisho la “masaa ishirini na nne kwa Bwana” mnamo Dominika ya nne ya Kwaresima, ambalo limeshakubaliwa katika Majimbo kadhaa na ambalo linadumu kuwa mwito wa kichungaji wenye nguvu ili kuishi kwa ari Sakramenti ya Kitubio.
12. Kwa sababu ya hitaji hilo, kusudi kizuio chochote kisiwepo kati ya ombi la kupatanishwa na msamaha wa Mungu, ninawapa kuanzia sasa makuhani wote, kwa nguvu ya huduma yao, kibali cha kuwaondolea dhambi wale waliosababisha kutoa mimba. Idhini niliyotoa kwa muda tu wa mwaka wa Jubilei [14] sasa inaongezewa muda wa kuwa na nguvu, licha ya chochote kilicho kinyume chake. Ninataka kusisitiza kwa nguvu zangu zote kwamba kutoa mimba ni dhambi kubwa, kwa sababu inakomesha uhai wa asiye na kosa. Lakini, kwa nguvu zilezile, ninaweza na kupaswa kutamka wazi kwamba hakuna dhambi yoyote ambayo huruma ya Mungu haiwezi kuifikia na kuiangamiza, pale inapoukuta moyo uliojuta unaoomba kupatanishwa na Mungu. Kwa hiyo, kila kuhani ajifanye kuwa kiongozi, mtegemezi na mfariji katika kuwasindikiza watubuji katika safari hii ya upatanisho maalumu.
Katika mwaka wa Jubilei nilitoa ruhusa kwa waamini ambao kwa sababu mbalimbali wanayahudhuria makanisa wanakohudumia makuhani wa Udugu wa Mtakatifu Pius X ya kupokea kihalali na kisheria ondoleo la kisakramenti kwa dhambi zao. [15] Kwa manufaa ya kiroho ya waamini hao, na kwa kutumaini kwamba makuhani wao watakuwa na mapenzi mema ili kuweza kurudia, kwa msaada wa Mungu, katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki, ninaagiza kwa uamuzi wangu binafsi kwamba ruhusa hiyo iwe na nguvu hata baada ya muda wa Jubilei, hadi pale ambapo maelekezo mengine yatatolewa, kusudi asiwepo yeyote ambaye anakosa ishara ya kisakramenti ya upatanisho kwa njia ya msamaha wa Kanisa.
13. Huruma ina pia uso wa faraja. “Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu” (Isa 40:1) ndiyo maneno yatokayo moyoni mwa nabii na kusikika hadi leo, kusudi neno la tumaini liwafikie wale waliokaa katika mateso na huzuni. Tusiruhusu kamwe tuibiwe tumaini linalotokana na imani kwa Bwana mfufuka. Ni kweli kwamba mara nyingi tunajaribiwa vikali, lakini tunapaswa tusipoteze kamwe uhakika wa kwamba Bwana anatupenda. Huruma yake inaonekana pia katika ukaribu, upendo na msaada ambao ndugu wengi kaka na dada wanaweza kutupatia zinapokuja siku za huzuni na mateso. Kupangusa machozi ni tendo hai linalovunja duru ya upweke ambamo mara nyingi tunafungwamo.
Wote tunahitaji kufarijiwa kwa sababu hakuna asiyepatwa na maumivu, mateso na upweke wa kutoeleweka. Huzuni gani huweza kusababishwa na neno la chuki, lililo tunda la kijicho, wivu na hasira! Mateso gani husababishwa na usaliti, ujeuri na utelekezwaji; uchungu gani mbele ya kifo cha wapendwa wetu! Lakini, Mungu si mbali kamwe tunapopatwa na misiba hiyo. Neno moja lenye kutupa moyo, kumbatio ambalo linakufanya ujisikie hauko upweke, kitendo kimoja cha ukarimu kinachofanya uonje upendo, sala inayokufanya kuwa imara zaidi, ...: hayo yote ni ishara ya kwamba Mungu yupo karibu nasi kwa kupitia faraja tunayopewa na ndugu.
Mara nyingine, hata ukimya unaweza kuwa msaada mkubwa; kwa sababu mara nyingine hakuna maneno yanayoweza kutoa jibu kwa maswali ya mwenye kuteswa. Lakini, yakikosekana maneno, huweza kusaidia huruma ya waliopo karibu, wenye kupenda na kutoa mkono. Si kweli kwamba kubaki kimya ni dalili ya kukata tamaa, kinyume chake, ni nafasi ya nguvu na upendo. Pia ukimya ni sehemu ya lugha yetu ya kuleta faraja, kwa sababu unageuka kuwa tendo hai la ushirikiano na mshikamano katika mateso ya ndugu yetu.
14. Katika kipindi cha pekee kama ulivyo wakati wetu huu, ambacho kinaona kati ya migogoro mingi hata ule wa familia, ni muhimu kwamba neno moja lenye nguvu ya kufariji lizifikie familia zetu. Paji la ndoa ni wito mkubwa ambao, kwa neema ya Kristo, twapaswa kuitikia kwa upendo na ukarimu, kwa uaminifu na uvumilivu. Uzuri wa familia unabaki ulivyo, licha ya viwuli vingi vinavyoutilia giza, na miungano ya mbadala. “Furaha ya upendo ambayo watu wanaiishi katika familia ni furaha ya Kanisa pia." [16] Safari ya maisha inayopeleka mwanamume na mwanamke kukutana, kupendana na, mbele ya Mungu, kuahidiana uaminifu kwa daima, mara nyingi inakwama kwa sababu ya mateso, usaliti na upweke. Furaha ya kujaliwa zawadi ya kupata watoto mara nyingi inaendana na wasiwasi wa wazazi kuhusu makuzi na malezi yao, kuhusu mustakabali unaostahili kuuishi kwa ari.
Neema ya Sakramenti ya Ndoa si tu kwamba inaipa familia nguvu ili iwe mahali maalumu pa kuiishi huruma, lakini pia inaipa jumuiya ya kikristo wajibu, na hata utendaji wote wa kichungaji uwajibike, ili thamani kubwa na hai ya familia iibuke wazi. Lakini, Mwaka huu wa Jubilei, hauwezi kuficha msukosuko wa hali ya familia ya siku hizi. Kuwa wazoefu wa huruma kunatuwezesha kutazama magumu yote ya kibinadamu kwa moyo unaojaa upendo wa Mungu, ambaye hachoki kupokea na kusindikiza [watu wote]. [17]
Hatuwezi kusahau kwamba kila mtu anasheheni utajiri na uzito wa maisha yake, ambayo yanamfanya kuwa wa pekee miongoni mwa watu wote. Maisha yetu, pamoja na furaha na huzuni zake, ni kitu cha pekee na kisichorudia, yenye mwendo wake chini ya mtazamo wa huruma ya Mungu. Hayo yote yanadai, hasa kwa upande wa padre, upambanuzi wa kiroho unaofanywa kwa makini, wa kina na wenye kutazama mbele, ili kila mmoja, pasipo kumbagua yeyote, akiwa na hali yoyote ile ya maisha, aweze kujisikia kwamba Mungu kweli anampokea, naye anaweza kushiriki hai katika maisha ya kijumuiya na kuwa miongoni mwa Watu wa Mungu ambao, bila kuchoka, hutembea kuelekea utimilifu wa ufalme wa Mungu, ulio ufalme wa haki, wa upendo, wa msamaha na wa huruma.
15. Umuhimu wa pekee una kipindi cha kifo. Kanisa limeishi daima kipindi hicho cha msiba katika mwanga wa ufufuko wa Yesu Kristo, ambaye alifungua njia ya uhakika wa maisha yajayo. Tunayo changamoto kubwa mbele yetu, ya kukabiliana nayo, hasa katika utamaduni mamboleo ambao mara nyingi unaelekea kupuuzia kifo hadi kukieleza kama tukio bandia, au kukificha. Kumbe, badala yake, tunapaswa kukikabili kifo na kukiandaa kama mpito wenye uchungu na usioepukika, lakini umejaa maana: ile ya kuwa tendo la mwisho la upendo kwa watu wanaotuacha na kwa Mungu anayeendewa. Katika dini zote, tukio la kifo, kama vile lile la kuzaliwa, linaambatana na hisia za kidini. Sisi twaishi tukio la mazishi kama sala iliyojaa tumaini kwa ajili ya nafsi ya marehemu, pia ili kuwafariji wale waliohuzunishwa kwa kupotewa na mpendwa.
Nina hakika kwamba tunahitaji, katika utendaji wa kichungaji uliohuishwa na imani hai, kuwezesha kugusa kwa mikono jinsi ishara za kiliturujia na sala zetu zinavyokuwa kielelezo cha huruma ya Bwana Mungu. Ni Yeye mwenyewe ambaye anatoa maneno ya tumaini, kwa sababu hakuna kitu wala kiumbe kinachoweza kututenganisha na upendo wake (taz. Rum 8:35). Kuhani kushiriki muda huu ni namna muhimu ya kuwasindikiza wahusika, kwa sababu kunawezesha kuishi ukaribu wa jumuiya ya kikristo wakati wa udhaifu, upweke, wasiwasi na machozi.
16. Mwaka wa Jubilei umekwisha, na Mlango Mtakatifu wa Huruma unafungwa. Lakini mlango wa huruma wa mioyo yetu unaendelea kubaki wazi daima kwa upana wake wote. Tumejifunza kuwa Mungu anatuinamia sisi (taz. Hos 11:4), ili hata sisi tuweze kumwiga Yeye katika kuwainamia ndugu zetu. Hamu ya wengi ya kurudi kwenye nyumba ya Baba, anayesubiri wamjie, inazushwa pia na mashahidi wa kweli na wakarimu katika kuonyesha huruma ya Mungu. Mlango Mtakatifu tuliovuka katika Mwaka huu wa Jubilei umetuingiza katika njia ya mapendo, ambayo twaitwa kuiendea kila siku kwa uaminifu na furaha. Ni njia ya huruma ambayo inatukutanisha na kaka na dada wengi ambao wananyosha mkono ili mtu aweze kuushika na kuwa mwenzi wao njiani.
Hamu ya kuwa karibu na Kristo inatudai kujifanya jirani na ndugu zetu, kwani hakuna jambo linalompendeza zaidi Baba kuliko ishara halisi ya huruma. Kwa asili yake, huruma inaonekana na kugusika katika vitendo halisi na vyenye ari. Pale huruma inapong’amuliwa katika ukweli wake, haiwezekani kurudi nyuma: inakua siku kwa siku na kugeuza maisha. Ni uumbaji mpya kwelikweli, unaounda moyo mpya, uwezao kupenda kikamilifu, na kutakasa macho kusudi yatambue mahitaji yaliyofichama. Ni ya kweli kabisa yale maneno ambayo Kanisa linayatumia katika kusali kwake kwenye Kesha la Pasaka, baada ya kusoma simulizi la uumbaji: “Ee Mungu, ulimwumba mtu kwa namna ya ajabu, ukamkomboa kwa namna ya ajabu zaidi”. [18]
Huruma hufanya upya na kukomboa, kwa sababu ni mkutano wa mioyo miwili: moyo wa Mungu ambao huja kukutana na moyo wa mwanadamu. Huo hupata moto na wa kwanza huuponya: moyo wa jiwe hugeuzwa kuwa moyo wa nyama (taz. Eze 36:26), wenye uwezo wa kupenda, licha ya dhambi zake. Hapo naelewa kuwa mimi ni "kiumbe kipya" kwelikweli (taz. Gal 6:15): napendwa, kwa hiyo naishi; nasamehewa, kwa hiyo nazaliwa katika maisha mapya; nimehurumiwa, kwa hiyo nimekuwa chombo cha huruma.
17. Katika Mwaka huu Mtakatifu, hasa kwenye “Ijumaa za huruma”, niliweza kugusa kwa mkono ulivyo mkubwa wema uliopo ulimwenguni. Mara nyingi haujulikani kwa sababu unatendeka siku kwa siku katika faragha na ukimya. Hata kama hazitangazwi sana, zipo ishara hai nyingi za wema na upendo zinazotendwa kwa ajili ya walio wadogo au wasiojiweza, walio wapweke au wametekelezwa. Wapo kweli mabingwa wa matendo ya huruma ambao wanaonyesha daima mshikamano na walio maskini na wenye huzuni. Tumshukuru Mungu kwa zawadi hizi za thamani ambazo zinatualika kugundua furaha ya kujifanya jirani wa udhaifu wa ubinadamu uliojeruhiwa. Pia nawashukuru kwa dhati wale wengi wanaojitolea, ambao kila siku wanatoa muda wao na nguvu zao ili kudhihirisha uwepo na ukaribu wa Mungu kwa njia ya juhudi zao. Huduma zao ni tendo halisi la huruma, linalowasaidia watu wengi kulijongea Kanisa.
18. Sasa ni wakati wa kufungua ubunifu wa huruma ili kuzaa matendo mapya mengi, yaliyo tunda la neema. Kanisa leo linahitaji kusimulia zile "ishara zingine nyingi" alizozifanya Yesu, "zisizoandikwa" (Yn 20:30), kusudi nazo ziweze kuwa vielelezo wazi vya matunda ya upendo wa Kristo na wa jumuiya inayopata uzima kutoka kwake. Zaidi ya miaka elfu mbili zimepita, lakini matendo ya huruma yaendelea kudhihirisha wema wa Mungu.
Hadi leo watu wengi wanateswa kwa njaa na kiu, na mahangaiko makubwa yasababishwa na picha za watoto ambao hawana cha kujilisha. Umati wa watu waendelea kuhama toka nchi hii hadi nchi nyingine ili kutafuta chakula, kazi, makao na amani. Magonjwa, katika aina zake mbalimbali, ni sababu ya kudumu ya mateso, nayo huomba msaada, faraja na utegemezi. Magereza ni mahali ambamo, mara nyingi, pamoja na adhabu inayozuia uhuru, huongezwa mateso, ambayo mara nyingine ni mazito, kutokana na mazingira ya maisha yasiyo ya kiutu. Kutokujua kusoma na kuandika bado ni shida iliyoenea sana nayo huwazuia watoto wa kiume na wa kike kukua vizuri, hadi kuathirika na namna mpya za utumwa. Utamaduni wa umimi pindukia, hasa kwenye nchi za Magharibi, unapeleka kwenye kupoteza hisia za mshikamano na uwajibikaji na wengine. Mungu mwenyewe anabaki leo kama pembeni, na asiyejulikana kwa wengi; jambo hilo ni umaskini mkubwa sana, pia ni kikwazo kikubwa kwa utambuzi wa hadhi isiyodhurika ya uhai wa binadamu.
Kwa kifupi, matendo ya huruma ya kimwili na ya kiroho yanaendelea hadi siku zetu hizi kuwa hakikisho la mchango mkubwa na chanya wa huruma kama thamani ya kijamii. Maana, huruma inatuhimiza kujiandaa kujibidiisha ili tuwarudishie hadhi mamilioni ya watu walio kaka na dada zetu, ambao pamoja nasi wameitwa kujenga "mji wa kuaminika". [19]
19. Ishara nyingi halisi za huruma zimefanyika wakati wa Mwaka Mtakatifu huu. Jumuiya, familia, na waamini mmoja mmoja wametambua tena furaha ya kushirikiana na uzuri wa kushikamana. Lakini haitoshi. Dunia yetu inaendelea kutengeneza mifumo mipya ya umaskini wa kimwili na kiroho ambayo inashambulia hadhi ya binadamu. Ndiyo sababu, Kanisa lazima liwe macho na tayari kila wakati kubainisha matendo mapya ya huruma na kuyatekeleza kwa ukarimu na kwa ukunjufu wa moyo.
Kwa hiyo, tufanye kila jitihada ili kuyapa mapendo maumbo halisi mbalimbali, na, wakati uleule kufanya matendo ya huruma yawe na busara. Nayo huruma, utendaji wake hujumlisha yote, ndiyo maana kwa kawaida hujieneza kama maji yaliyomwagika, bila kujua mipaka. Na katika maana hiyo tunaitwa kuyatia sura mpya matendo ya huruma tunayoyajua tangu zamani. Kwani huruma inafurika; inazidi kusonga mbele, na kuzaa matunda mengi. Ni sawa na chachu inayoumua unga wa ngano (taz. Mt 13:33), au mbegu ya haradali inayoota na kuwa mti (taz. Lk 13:19).
Kwa kutolea mfano, tufikirie tu juu ya tendo la huruma ya kimwili “kuwavika walio uchi” (taz. Mt 25:36.38.43.44). Latupeleka kukumbuka hapo awali, kwenye bustani la Edeni, ambapo Adamu na Eva waligundua kuwa wa uchi na, wakisikia Bwana Mungu akiwakaribia, wakaona aibu na kujificha (taz. Mwa 3:7-8). Twajua kwamba Bwana Mungu aliwapa adhabu; lakini, Yeye “akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika” (Mwa 3:21). Aibu hufukuzwa, na hadhi kurudishwa.
Tumtazame pia Yesu huko Golgotha. Mwana wa Mungu yuko msalabani uchi; kanzu yake ilipigiwa kura na kuchukuliwa na askari (taz. Yn 19:23-24). Yeye hana kitu tena. Msalabani unafunuliwa kikamilifu ushirikiano wa hali ambao Yesu alishiriki na wale waliopoteza heshima kwa sababu wamenyimwa mahitaji. Kanisa, jinsi linavyoitwa kuwa “kanzu ya Kristo” [20] ili kumvika Bwana wake, vivyo hivyo linawajibika kushikamana na walio uchi wa dunia ili wapate tena heshima ambayo walinyimwa. Kwa hiyo, neno: “Nilikuwa uchi, mkanivika” (Mt 25:36), linatulazimisha tusigeuze macho mbali na aina mpya za umaskini na unyanyapaa zinazozuia watu wasiishi maisha yenye heshima wanayostahili.
Kutokuwa na ajira au kupokea mshahara usiojitosheleza; kutokuwa na nyumba au eneo pa kuishi; kupatwa na mnyanyaso kutokana na imani, rangi au matabaka ya kijamii ...: hayo yote ni baadhi ya mifano michache kati ya mingi ya hali zenye kushambulia hadhi ya kiutu. Utendaji wenye huruma wa wakristo ukikabiliana na hali hizi za mashambulio, unajibu kabla ya yote kwa uangalifu na mshikamano. Kuna mazingira mangapi yaliyopo leo ambamo tunaweza kuwarejeshea watu hadhi yao na kutengeneza uwezekano wa kuishi maisha yaliyo ya kiutu kwelikweli! Tuwafikirie tu watoto wangapi wa kike na kiume wanatendwa ujeuri wa aina nyingi, ambao unawaibia furaha ya kuishi. Nyuso zao zenye huzuni na wasiwasi zimechorwa akilini mwangu; nao waomba msaada wetu ili kuopolewa na utumwa wa aina nyingi wa ulimwengu wa leo. Watoto hao ndio vijana wa kesho; tunawaandalia namna gani kuishi kwa heshima na uwajibikaji? Kwa tumaini gani waweza kukabiliana na wakati wa sasa na ule ujao wa maisha yao?
Tabia ya kijamii ya huruma inadai tusibaki walegevu na kuondoa hali ya kutojali na ile ya unafiki, isije mikakati na mipango yetu ikabaki kwenye karatasi tu. Roho Mtakatifu atusaidie kuwe tayari daima katika kuchangia kiutendaji na pasipo ubinafsi, kusudi haki na maisha yenye hadhi zisiwe maneno matupu, bali ziwe uwajibikaji halisi wa wale wanaonuia kutoa ushuhuda juu ya uwepo wa Ufalme wa Mungu.
20. Tunaitwa kukuza utamaduni wa huruma, uliojengwa katika kutambua upya maana ya kukutana na wengine: utamaduni ambamo hakuna mtu anayemtazama mwingine bila kumjali, au anageukia mbali macho yake asije akayaona mateso ya kaka na dada zake. Matendo ya huruma ni kazi ya “msanii”: hakuna moja lililo sawa na jingine; mikono yetu yaweza kuyafinyanga kwa namna elfu tofauti, na, hata kama Mungu anayetuvuvia kuyabuni ni mmoja na moja ni “kitu” ambacho yametengenezwa nacho, yaani huruma yenyewe, kila moja linapata umbo tofauti.
Maana, matendo ya huruma hugusa maisha yote ya mtu. Ndiyo sababu twaweza kuanzisha mapinduzi halisi ya utamaduni kuanzia tu na urahisi wa vitendo ambavyo vyajua kuufikia mwili na roho, yaani maisha ya watu. Ni wajibu ambao jumuiya ya kikristo huweza kuushika kama wa kwake, katika kutambua kwamba Neno la Bwana linaiita daima kuondokana na hali ya kutojali na umimi ambamo tunashawishiwa kujifungia ili kuishi maisha ya raha na yasiyo na matatizo. “Maskini mnao sikuzote pamoja nanyi” (Yn 12:8), asema Yesu kwa wanafunzi wake. Hakuna udhuru inayoweza kutupa haki ya kutojali tunapojua kwamba Yeye alijitangaza kuwa kitu kimoja na kila mmoja wa hao [maskini].
Utamaduni wa huruma unaundwa katika sala ya kudumu, moyo wazi na utayari kwa kazi ya Roho Mtakatifu, uzoefu katika kuyajua maisha ya watakatifu na ujirani halisi kwa maskini. Ni mwaliko wenye ari wa kuelewa bila kuyumba ni wapi ambapo ni lazima kuwajibika. Kishawishi cha kutunga “nadharia ya huruma” kinashindwa kwa kadiri ile tu ambayo yenyewe inakuwa maisha ya kila siku ya ushirikiano na mshikamano. Aidha, hatuna budi kukumbuka daima maneno ya mtume Paulo, aliposimulia kuhusu mkutano wake na Petro, Yakobo na Yohane, baada ya kuongoka kwake, akisisitiza jambo la msingi la utume wake na la maisha ya kikristo kwa ujumla: “Ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya” (Gal 2:10). Hatuwezi kuwasahau maskini: ni mwito unaofaa kabisa hata leo, na inaonyesha dhahiri ulazima wake wa kiinjili.
21. Mang’amuzi tuliyofanya wakati wa Jubilei yapenyeze ndani yetu maneno ya Mtume Petro: “Ninyi kwanza mlikuwa hamkupata rehema, lakini sasa mmepata rehema” (1Pet 2:10). Tusijishikie kwa wivu kile tulichokipata; tujue kukishirikisha na ndugu wanaoteswa, kusudi wategemezwe na nguvu ya huruma ya Mungu Baba. Jumuiya zetu ziwe wazi kuwafikia wote wanaoishi katika eneo lake, kusudi busu la upendo wa Mungu liwafikie wote kwa kupitia ushuhuda wa waamini.
Huu ndio wakati wa huruma. Kila siku ya safari yetu ina alama ya uwepo wa Mungu anayeongoza hatua zetu kwa nguvu za neema ambayo Roho Mtakatifu humimina moyoni mwetu ili kuufinyanga na kuuwezesha kupenda. Ni wakati wa huruma, wa wote na wa kila mmoja, maana, hawezi kuwepo mtu anayedhani kwamba yeye hahusiki na ukaribu wa Mungu na uweza wa upendo wake mtamu. Ni wakati wa huruma, kwa sababu walio dhaifu na wasio na ulinzi, walio mbali na wapweke, waweze kuona uwepo wa kina kaka na kina dada ambao wanawategemeza katika shida. Ni wakati wa huruma kwa ajili ya walio maskini, ili waone kwamba wengine wanawatazama kwa heshima na uangalizi, wakiisha kushinda moyo wa kutojali, na kugundua kilicho muhimu kweli katika maisha. Huu ndio wakati wa huruma, kwani kila mwenye dhambi asichoke kuomba msamaha na kusikia mkono wa Mungu Baba ambaye daima anampokea na kumkumbatia.
Katika mwanga wa “Jubilei ya watu waliotegwa na jamii”, wakati katika kila kanisa kuu la jimbo na katika kila kanisa la hija duniani pote Milango ya Huruma ilikuwa ikifungwa, nilipata wazo kwamba, kama ishara halisi ya nyongeza katika Mwaka huu Mtakatifu wa pekee, ni lazima kuadhimisha katika Kanisa zima, kwenye Dominika ya 33 katika Kipindi kwa Mwaka, Siku ya Maskini Duniani. Itakuwa sehemu bora ya maandalizi ya kuishi sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, ambaye alijifananisha na walio wadogo na maskini na ambaye atatuhukumu juu ya matendo ya huruma (taz. Mt 25:31-46). Itakuwa Siku ambayo itasaidia jumuiya zetu na kila mbatizwa kutafakari jinsi umaskini unavyokaa katika kiini cha Injili na kuhusu suala la kwamba, hadi pale Lazaro atakapoendelea kutupwa chini mlangoni pa nyumba yetu (taz. Lk 16:19-21), hakutaweza kuwepo amani ya kijamii. Siku maalumu hiyo itakuwa pia namna halisi ya uinjilishaji mpya (taz. Mt 11:5), ambao unafanya upya uso wa Kanisa katika mchakato wake wa wongofu wa kichungaji ili kuwa kweli shahidi wa huruma.
22. Juu yetu hudumu kuelekea macho yenye huruma ya Mama Mtakatifu wa Mungu. Yeye ndiye wa kwanza anayefungua njia na kutusindikiza katika kuushuhudia upendo. Mama wa Huruma anatukusanya wote chini ya ulinzi wa joho lake, kama mara nyingi sanamu za wasanii zimependa kumwonyesha. Tunategemea msaada wake wa kimama, na kufuata maelekezo yake ya sikuzote ya kumtazama Yesu, ambaye ndiye uso unaong’aa wa huruma ya Mungu.
Ilitolewa Roma, kwenye kanisa la mtakatifu Petro, tarehe 20 Novemba, Sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu, katika Mwaka wa Bwana 2016, wa nne wa upapa.
FRANSISKO
[1] Juu ya Injili ya Yohane 33,5.
[2] Mchungaji wa Erma, XLII, 1-4.
[3] Taz. Wosia wa Kitume Furaha ya Injili, 27.
[4] Misale ye Kiroma, Dominika ya III ya Kwaresima.
[5] Sawa kama ilivyotangulia, Utangulizi wa 7 wa Dominika za Mwaka.
[6] Sawa kama ilivyotangulia, Sala ya Ekaristi II.
[7] Sawa kama ilivyotangulia, Madhehebu ya Komunyo.
[8] Riti ya Sakramenti ya Upatanisho, na. 46.
[9] Sakramenti ya Mpako na uangalizi wa kichungaji wa wagonjwa, na. 76.
[10] Taz. Mtaguso Mkuu Vatikano II, Konst. Sacrosanctum Concilium, 106.
[11] Sawa kama ilivyotangulia, Konst. ya kidogma, Dei Verbum, 2.
[12] Wosia wa Kitume Furaha ya Injili, 142.
[13] Taz. Benedikto XVI, Wosia wa Kitume wa baada ya Sinodi, Verbum Domini, 86-87.
[14] Taz. Waraka wa kutoa rehema kwa nafasi ya Jubilei ya Huruma, 1 Septemba 2015.
[15] Taz. sawa kama ilivyotangulia.
[16] Wosia wa Kitume wa baada ya Sinodi, Furaha ya upendo, 1.
[17] Taz. sawa kama ilivyotangulia, 291-300.
[18] Misale ya Kiroma, Kesha la Pasaka, Sala baada ya Somo la Kwanza.
[19] Waraka Insiklika, Lumen fidei, 50.
[20] Taz. Sipriano, Umoja wa Kanisa Katoliki, 7.
Matini: © Copyright - Libreria Editrice Vaticana
Tafsiri: © Copyright - Familia za Maamkio Iringa na Libreria Editrice Vaticana
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana