Misericordiae Vultus
BULA YA KUZINDUA JUBILEI YA PEKEE YA HURUMA
FRANSISKO
ASKOFU WA ROMA
MTUMISHI WA WATUMISHI
WA MUNGU
KWA WOTE WATAKAOISOMA BARUA HII
NEEMA, HURUMA, NA AMANI
1. Yesu Kristo ni uso wa huruma ya Baba. Katika neno hili upo ufupisho sahihi wa fumbo zima la imani ya kikristo. Huruma imepata kuwa hai na yenye kuonekana katika Yesu Mnazareti, na hata ikafikia kilele chake katika Yeye. Baba “aliye mwingi wa rehema” (Efe 2:4), baada ya kumfunulia Musa jina lake kuwa ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6), hakuwahi kuacha hata mara moja kuonyesha hali yake ya kimungu katika nafasi zote za historia. “Ulipowadia utimilifu wa wakati” (Gal 4:4), kila kitu kilipokuwa kimepangwa kadiri ya utaratibu wake wa ukombozi, alimtuma duniani Mwanae pekee ili kutufunulia upendo wake katika ukamilifu wake. Aliyemwona Yeye, amemwona Baba (Rej. Yn 14:9). Yesu Mnazareti, kwa neno lake, matendo yake na kwa nafsi yake yote [1] anaifunua huruma ya Mungu.
2. Tunahitaji kulitafakari tena na tena fumbo la huruma. Ni chemchemi ya furaha, ya utulivu na ya amani. Ni sharti la wokovu wetu. Huruma ni neno linalotufunulia Utatu Mtakatifu wenyewe. Huruma ni tendo la juu na kuu kabisa ambalo kwa njia yake Mungu anatujia sisi. Huruma ni sheria ya msingi ambayo ipo katika moyo wa kila mtu anayemwangalia kwa unyofu wa macho ndugu anayemkuta katika safari ya maisha. Huruma ni njia inayowaunganisha Mungu na binadamu, na kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya hali yetu ya dhambi.
3. Katika nyakati hizi tunaitwa kuitazama kwa makini sana huruma ili tuweze kuwa ishara wazi kabisa ya utendaji wa Baba katika maisha yetu. Kwa sababu hiyo nimeitangaza Jubilei ya Pekee ya Huruma, kama wakati maalum kwa ajili ya Kanisa, ambapo ushuhuda wa waamini unakuwa wenye nguvu zaidi na wenye kuzaa matunda mengi zaidi.
Mwaka Mtakatifu utafunguliwa tarehe 8 mwezi Desemba mwaka huu 2015, sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Sikukuu hii ya kiliturujia inatukumbusha matendo makuu ya Mungu toka mwanzoni mwa historia yetu. Baada ya dhambi ya Adam na Eva, Mungu hakutaka kuwaacha binadamu peke yao katika maovu. Kwa sababu hiyo alimtazama Maria Mtakatifu na akamfikiria kwa upendo, na akataka awe Mama wa Mkombozi wa wanadamu. Mbele ya ukubwa wa dhambi, Mungu anajibu kwa msamaha kamili. Huruma itakuwa daima kubwa kuliko dhambi yoyote, na hakuna awezaye kuuwekea mipaka upendo wa Mungu anayesamehe daima. Nitafurahi kufungua Mlango Mtakatifu katika sherehe hiyo ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili. Siku hiyo Mlango Mtakatifu utakuwa Mlango wa Huruma, ambao kwa njia yake yeyote aingiaye ataonja mapendo ya Mungu anayefariji, anayesamehe, na anayetupatia tumaini.
Dominika itakayofuata, ya tatu ya Majilio, Mlango Mtakatifu wa Kanisa la kiaskofu la Roma, yaani Basilika ya kipapa la Mtakatifu Yohane wa Laterani, utafunguliwa. Baadaye milango (mitakatifu) ya mabasilika mengine ya kipapa itafunguliwa. Dominika hiyohiyo nitatangaza kuwa katika kila kanisa mahalia, katika kanisa la kiaskofu au makanisa mengine yenye umuhimu mkubwa, Mlango wa Huruma utafunguliwa na kuwa wazi Mwaka wote Mtakatifu. Kwa busara ya mamlaka ya Kanisa mahalia milango mingine yenye hadhi maalum pia itafunguliwa katika sehemu za hija, ambako mahujaji wengi huenda. Hii ni kwa sababu sehemu hizo zimejaa neema, kwani huko watu hutambua kuwa wapo katika njia ya wongofu. Kwa hiyo, kila Kanisa mahalia litakuwa linashiriki kikamilifu kuuishi Mwaka huu Mtakatifu, kama wakati wa pekee wa neema na wa upyaisho wa kiroho. Na hivi Jubilei hiyo itaadhimishwa Roma na pia katika makanisa mahalia, kama ishara inayoonekana ya umoja wa Kanisa lote.
4. Nimechagua tarehe 8 mwezi Desemba kwa sababu ya umaana wake katika miaka ya karibuni ya historia ya Kanisa. Kwa kweli, nitaufungua Mlango Mtakatifu siku tunapoadhimisha miaka hamsini tangu kuhitimishwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano. Kanisa linahitaji kulikumbuka daima tukio hilo. Kwa Mtaguso huo Kanisa liliingia katika upeo mpya wa historia. Mababa wa Mtaguso walitambua kwa dhati kwamba ni pumzi ya kweli ya Roho Mtakatifu hitaji la kumwongokea Mungu kwa binadamu (wake kwa waume) wa nyakati hizi kwa njia ya wazi zaidi. Kuta ambazo kwa muda mrefu zililifanya Kanisa liwe kama ngome ziliangushwa chini, na wakati ulifika wa kutangaza Injili kwa mtazamo mpya. Ni njia mpya ya uinjilishaji uleule uliokuwepo tangu mwanzo. Lilikuwa ni jukumu jipya kwa wakristo wote kutoa ushuhuda wa imani yao kwa ujasiri mkubwa zaidi na kwa msimamo zaidi. Kanisa lilipata kuwa makini zaidi kwamba kazi yake ni kuonyesha kwa dhati zaidi upendo wa Baba ulimwenguni.
Yanatujia tena akilini mwetu yale maneno mazito ya mtangulizi wetu Mtakatifu Yohane XXIII, alipokuwa anaufungua Mtaguso, ambapo alionyesha njia ya kufuata, akisema: “Kwa wakati huu Mchumba wa Kristo anapendezwa kutumia dawa ya huruma kuliko ukali, ... Kanisa Katoliki, likiwa linainua juu mwanga wa ukweli wa kidini katika Mtaguso huu mkuu, linapenda kujionyesha kuwa ni Mama mpendwa sana wa wote, mi pendevu, lenye uvumilivu, linalowaka moto wa mapendo kwa watoto wake waliojitenga”. [2] Mwenyeheri Paulo VI alisema kwa moyo huohuo alipofunga Mtaguso: “Tunapenda zaidi kuonyesha namna gani upendo umekuwa ni msingi wa kidini katika Mtaguso wetu ... masimulizi ya zamani ya Msamaria Mwema yamekuwa ni mfano na kanuni iliyoongoza madhumuni ya kiroho ya Mtaguso wetu. ... Mtaguso ulichukua matazamio na matamanio ya watu wa nyakati zetu. Makosa yalilaaniwa kama vile upendo na ukweli wenyewe ulivyodai; lakini watu wenyewe walialikwa wazingatie daima heshima, upendo, na walitahadharishwa kuhusu makosa. Hivyo, Mtaguso umeupatia ulimwengu wa sasa ujumbe wa kutia moyo badala ya ule unaokatisha tamaa, badala ya utabiri wa kutisha, ujumbe wa matumaini. Desturi za ulimwengu wa sasa siyo tu zilivumiliwa, bali pia ziliheshimika na kuthaminiwa, juhudi zake ziliungwa mkono, matazamio yake yaliboreshwa na kupata baraka ... Suala jingine tunalopasa kulikazia ni hili: mafundisho yote haya yenye utajiri mkubwa namna hii yanaelekezwa upande mmoja, yaani huduma kwa mwanadamu wa kila hali, katika mapungufu yote na mahitaji yake yote”. [3]
Tukiwa na moyo wa shukrani kwa lile ambalo Kanisa limepokea, na tukiwa tayari kutimiza wajibu ambao unatungoja, tutaingia kupitia Mlango Mtakatifu kwa matumaini makubwa kwamba nguvu ya Bwana mfufuka, anayetutia shime daima katika hija yetu, itatuimarisha. Roho Mtakatifu, anayewaongoza waamini kwenye kushiriki kazi ya wokovu iliyoasisiwa na Kristo atuonyeshe njia na alitie shime taifa la Mungu, ili lifikie kuuona uso wa huruma. [4]
5. Mwaka wa Jubilei utahitimishwa kwa sherehe ya kiliturujia ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu, tarehe 20 mwezi Novemba mwaka 2016. Siku hiyo tutakapoufunga Mlango Mtakatifu tutajawa na moyo wa shukrani kwa namna ya pekee kwa Utatu Mtakatifu sana, kwa kutupatia wakati huu wa pekee na wa neema. Tutamkabidhi Kristo Bwana maisha ya Kanisa, watu wote na ulimwengu mzima, tukimwomba atumiminie neema yake kama umande wa asubuhi, ili kila mmoja aweze kushiriki na wengine katika kufanya kazi ya kuuboresha mustakabali wetu. Ningetamani sana kwamba mwaka huo uwe umejaa huruma ili tuweze kuwaendea watu wote, wake kwa waume, tukiwapelekea wema na upole wa Mungu. Harufu nzuri ya huruma iwafikie wote, waamini na walio mbali, kama ishara ya Ufalme wa Mungu ambao upo tayari kati yetu!
6. “Ni kawaida ya Mungu kutenda yote kwa huruma na anaonyesha enzi yake hasa katika huruma hiyo”. [5] Maneno haya ya mtakatifu Tomaso wa Akwino yanaonyesha kuwa namna gani huruma ya Mungu ni ishara ya enzi yake na siyo ya udhaifu wake. Kwa sababu hiyo liturujia katika moja ya sala zake za zamani sana inatuongoza kusali: “Ee Mungu, unayedhihirisha uweza wako hasa kwa kusamehe na kuhurumia ...” [6] Katika historia nzima ya binadamu, Mungu atakuwa daima aliyepo, aliye karibu, mpaji, mtakatifu na mwenye huruma.
“Mvumilivu na mwingi wa huruma”, ni maneno mawili yanayopatikana mara nyingi pamoja katika Agano la Kale wakati wa kueleza hali ya Mungu. Huruma yake inadhihirishwa na matendo mengi katika historia nzima ya wokovu, na wema wake unazishinda adhabu na uharibifu. Kwa namna ya pekee Zaburi zinaonyesha ukuu wa matendo ya Mungu yenye huruma: “Anakusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema” (Zab 103:3-4). Zaburi nyingine inadhihirisha kwa namna wazi kabisa ishara ya huruma yake: “Bwana huwafanyia hukumu walioonewa, , huwapa wenye njaa chakula. Bwana huwafungua waliofungwa, Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama, Bwana huwapenda wenye haki; Bwana huwahifadhi wageni, huwategemeza yatima na mjane; bali njia ya wasio haki huipotosha” (Zab 146:7-9). Halafu kuna misemo mingine ya mzaburi: “Yeye huwaponya waliopondeka moyo, na kuziganga jeraha zao ... Bwana huwategemeza wenye upole, , huwaangusha chini wenye jeuri” (Zab 147:3.6). Kwa hiyo, huruma ya Mungu si kitu cha kinadharia tu, bali ni hali ya kuonekana na kugusika, ambayo anaitumia kutufunulia upendo wake, kama ule wa baba au mama anayeguswa sana na upendo kwa mwanae. Ni halali kabisa kusema kuwa ni upendo wa ndani. Unatoka ndani kabisa ya nafsi, umejaa upole na huruma, rehema na neema.
7. “Kwa maana fadhili zake ni za milele.” Hiki ni kiitikio kinachorudia baada ya kila aya katika zaburi ya 136 inayoelezea historia ya ufunuo wa Mungu. Kwa tendo la fadhili na huruma, matukio yote ya Agano la Kale yamejaa wokovu. Huruma inaainisha kuwa historia ya Mungu na Israeli ni historia ya wokovu. Kurudia kila mara “Huruma yake inadumu milele,” kama zaburi inavyofanya, inaelekea kupenya katika upeo wa mahali na nyakati, na kuingiza kila kitu katika umilele wa fumbo la upendo. Ni kama kusema kwamba si tu katika historia, lakini katika umilele wote, mtu atakuwa daima chini ya uangalizi wa huruma wa Baba. Si kwa bahati kwamba Waisraeli walitaka kuiingiza zaburi hii – “Halel, au Aleluya, Kuu” kama inavyoitwa – katika sikukuu zake muhimu za kiliturujia.
Kabla ya mateso yake, Yesu alisali kwa kutumia zaburi hii ya huruma. Matayo anathibitisha hili katika Injili yake anaposema kwamba “baada ya kuimba wimbo” (26:30), Yesu na mitume wake walitoka kwenda kwenye Mlima wa Mizeituni. Alipokuwa akisimika Ekaristi kama ukumbusho wake wa milele na sadaka yake ya Pasaka, aliweka hili tendo kuu la ufunuo kama alama ya huruma yake. Ndani ya kifungu hikihiki cha huruma, Yesu aliingia katika mateso na kifo chake, kwa kudhamiria lile fumbo kuu la upendo ambalo angelikamilisha msalabani. Kwa kujua kwamba Yesu mwenyewe aliisali zaburi hii, inaipa umuhimu zaidi hata kwetu sisi kama Wakristo, ikituhimiza kutumia kiitikio hiki katika maisha yetu ya kila siku kwa kusali maneno haya ya kusifu: “Kwa maana fadhili zake, huruma yake, ni za milele.”
8. Macho yetu yakiwa yamemkazia Yesu anayetutazama kwa huruma, tunaonja upendo wa Utatu Mtakatifu. Utume ambao Yesu ameupokea kwa Baba ni ule wa kudhihirisha fumbo la pendo tukufu katika utimilifu wake. “Mungu ni Upendo” (1Yoh 4:8,16), Yohane anasisitiza kwa mara ya kwanza na mara hiyo tu katika Maandiko yote Matakatifu. Upendo huu umewekwa wazi na wa kushikika katika maisha yote ya Yesu. Ubinadamu wake si kitu kingine ila upendo, upendo uliotolewa huria. Mahusiano anayoyajenga kati yake na wale watu wanaomwendea yanaonyesha jambo la kipekee na lisiloweza kujirudia. Ishara anazozifanya hasa kwa wenye dhambi, maskini, wale walioko pembezoni, wagonjwa na wanaoteseka, yote ni kwa ajili ya kufundisha huruma. Kila kitu ndani yake kinaongelea huruma. Hakuna chochote kwake kinachopungukiwa na huruma.
Yesu, kwa kuyaona yale makundi ya watu waliomfuata aligundua kwamba walikuwa wamechoka na kuishiwa nguvu, wamepotea na bila kiongozi, na akasikia huruma sana kwa ajili yao (rej. Mt 9:39). Ni katika upendo huu uliojaa huruma aliwaponya wagonjwa walioletwa kwake (rej. Mt 14:14) na kwa mikate michache tu na samaki alilishibisha kundi lile kubwa (rej. Mt 15:37). Kilichomsukuma Yesu katika mazingira haya yote si kingine ila huruma, iliyomwezesha kuisoma mioyo ya wale aliokutana nao na kuwatimizia mahitaji yao ya kina. Alipokutana na mama mjane wa Naini akienda kumzika mwanae aliona huruma nyingi kwa ajili ya mateso makali ya huyu mama mwenye majonzi na akamrudishia mwanae kwa kumfufua kutoka wafu (rej. Lk 7:15). Baada ya kumweka huru yule aliyepagawa wa nchi ya Wagerasi, Yesu alimwaminishia utume huu: “Nenda nyumbani kwa marafiki zako, na uwaambie ni jinsi gani Bwana alivyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma” (rej. Mk 5:19). Kuitwa kwa Matayo kumefanyika pia katika mazingira ya huruma. Akipitia kitengo cha mtoza ushuru, Yesu alimkazia Matayo macho. Ulikuwa mtazamo uliojaa huruma, uliosamehe dhambi za yule mtu, mdhambi na mtoza ushuru ambaye Yesu alimchagua – kinyume cha wasiwasi wa wanafunzi wengine – kuwa mmojawapo wa wale kumi na wawili. Mtakatifu Beda Mtukuka, akizungumzia kifungu hiki cha Injili, ameandika kuwa Yesu alimtazama Matayo kwa upendo wa huruma na akamchagua: miserando atque eligendo. [7] Mtazamo huu umenigusa sana ndiyo maana nikauchagua kama kaulimbiu yangu ya kichungaji.
9. Katika mifano inayohusishwa na huruma, Yesu anafunua hali ya Mungu kama Baba asiyekata tamaa mpaka akishasamehe maovu na kwa huruma kushinda kukataliwa. Tunaijua hii mifano vema, hasa mitatu: kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea, na baba na wanae wawili rej. Lk 15:1-32). Katika mifano hii, Mungu anaonyeshwa daima mwenye furaha, hasa anaposamehe. Ndani yake tunapata kiini cha Injili na cha imani yetu kwa sababu huruma imeonyeshwa kama nguvu inayoshinda kila kitu, ikiujaza moyo mapendo na kuleta faraja kwa njia ya msamaha.
Kutoka kwenye mfano mwingine, tunapata fundisho muhimu kwa maisha yetu ya Kikristo. Kwa kujibu swali la Petro kuhusu mara ngapi ni lazima kusamehe, Yesu anasema: “Sisemi mara saba bali sabini mara saba,” (rej. Mt 18:22). Baadaye anaendelea kuelezea mfano wa “mtumwa katili” aliyeitwa na bwana wake kulipa deni kubwa, akamsihi magotini amhurumie. Bwana wake akafuta lile deni. Baadaye anakutana na mtumwa mwenzake ambaye anamwia senti chache naye pia akamsihi magotini amhurumie lakini huyu mtumwa wa kwanza anamkatalia ombi lake na kumtupa jela. Bwana yule anaposikia kuhusu hilo jambo anaghadhibika, akamwita yule mtumwa wa kwanza na kumwuliza, “Hukupaswa kuwa na huruma kwa mtumwa mwenzako kama nilivyokuwa na huruma kwako?” (rej. Mt 18:33). Yesu anahitimisha, “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake” (rej. Mt 18:35).
Mfano huu una mafundisho ya thamani kwetu sote. Yesu anasisitiza kwamba huruma si tendo la Baba peke yake, bali inakuwa kipimo cha kuthibitisha nani kweli ni watoto wake. Kwa kifupi, tumeitwa kuonyesha huruma kwa sababu huruma imeonyeshwa kwetu kwanza. Kusamehe makosa inakuwa kitendo dhahiri cha upendo wenye huruma na kwa sisi Wakristo ni wajibu ambao hatuwezi kuukwepa. Wakati mwingine, ni jinsi gani ilivyo vigumu kasamehe! Na bado msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono yetu dhaifu kutupatia moyo mkunjufu. Kuachilia mbali hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ni jambo muhimu ili kuishi kwa furaha. Kwa hiyo basi, tutilie maanani ushauri wa Mtume “Jua lisichwe juu ya hasira yako” (rej. Efe 4:26). Zaidi ya hayo, tusikilize maneno ya Yesu aliyeifanya huruma kuwa kielelezo cha maisha na kipimo cha thamani ya imani yetu: “Heri wenye huruma kwa kuwa watahurumiwa” (rej. Mt 5:7): heri ambayo tunapaswa kuiwania kwa namna ya pekee Mwaka huu Mtakatifu.
Kama tunavyoweza kuona katika Maandiko Matakatifu, huruma ni neno la msingi linaloashiria kazi ya Mungu kwetu sisi. Haishii tu kukazia upendo wake, bali kuuweka wazi na wa kushikika. Upendo, baada ya yote, hauwezi kwa vyovyote kuwa wazo tu. Kwa mwonekano wake unaonyesha kitu cha kushikika: nia, mitazamo na tabia zinazoonyeshwa katika maisha ya kila siku. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwetu. Anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba anatamani tuwe wenye afya njema, anataka kutuona wenye furaha, wenye kujaa furaha na amani. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma wa Wakristo unapaswa pia kuenenda. Kama Baba apendavyo, vivyo hivyo na watoto wake. Kama vile alivyo na huruma, ndivyo tunavyoitwa kuwa na huruma kila mmoja kwa mwenzake.
10. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonyesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonyesha huruma na upendo. Kanisa “lina hamu isiyo na kikomo katika kuonyesha huruma.” [8] Huenda tumejisahau kwa muda mrefu jinsi ya kuonyesha na kuiishi huruma. Kishawishi, kwa upande mmoja, cha kulengea tu haki, kimetufanya tusahau kwamba hii ndiyo hatua ya kwanza tu, ya muhimu na isiyokwepeka. Lakini Kanisa linahitaji kwenda mbele zaidi na kuwania lengo la juu na la maana zaidi. Kwa upande mwingine, nasikitika kusema, tunapaswa kukubali kuwa tendo la huruma linafifia zaidi na zaidi katika utamaduni wetu. Mara nyingi, neno hili linaonekana kutokomea kimatumizi. Hata hivyo, bila ushuhuda wa huruma, maisha yanakuwa bila matunda na tasa, kana kwamba imetengwa jangwani. Wakati umewadia kwa Kanisa kuitikia kwa mara nyingine huu wito wa furaha wa huruma na msamaha. Ni wakati wa kurudi kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya kaka na dada zetu. Huruma ni msukumo unaotuamsha kwa maisha mapya na kututia ujasiri wa kuangalia wakati ujao kwa matumaini.
11. Tusisahau mafundisho makuu yaliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Ensiklika yake ya pili, Dives in Misericordia, ambayo kwa wakati ule imekuja bila kutazamiwa, dhamira yake ikigusa wengi kwa mshangao. Kuna ibara mbili hasa ambazo ningependa kuzitilia mkazo. Kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II amekazia ukweli kwamba tumeisahau dhamira ya huruma katika utamaduni wa leo: “Fikra za wakati wa sasa, bila shaka zaidi kuliko kwa watu wa kipindi cha nyuma, zinaonekana kupingana na Mungu wa huruma, na kwa hakika huelekea kutoliingiza katika maisha na kuliondoa katika moyo wa binadamu wazo asilia la huruma. Neno na wazo la ‘huruma’ vinaonekana kuleta mtafaruku kwa binadamu ambaye, kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, ambazo hazikuwa zimejulikana kihistoria, amekuwa mkuu wa ulimwengu na ameutiisha na kuutawala (rej. Mwa 1:28). Huku kuutawala ulimwengu, mara nyingine kwa kuueleweka upande mmoja na juujuu, kunaelekea kukosa nafasi ya huruma ... na hii ndiyo sababu, katika hali ya Kanisa na ya ulimwengu leo, watu wengi mmoja mmoja na makundi wakiongozwa na imani hai wanageuka, naweza kusema kwa hiari kwenye huruma ya Mungu.”[9]
Zaidi ya hayo, Mtakatifu Yohane Paulo II amehimiza uinjilishaji wa haraka zaidi wa kuishuhudia huruma kwa ulimwengu wa leo: Inadaiwa na upendo kwa binadamu, kwa kila kilicho cha kibinadamu na ambao kadiri ya mang’amuzi ya wenzetu wengi unatishiwa kwa hatari kubwa. Fumbo la Kristo... linanihimiza kuihubiri huruma kama upendo wa Mungu, upendo wenye huruma na fadhili, uliodhihirishwa katika fumbo lilelile la Kristo. Vivyo hivyo, linanihimiza kuichukulia uzito huruma hiyo na kuiomba katika kipindi hiki kigumu, msimu wa changamoto katika historia ya Kanisa, na ya ulimwengu.” [10] Fundisho hili linahusiana sana na wakati wa sasa, na linastahili kutumiwa kwa mara nyingine tena Mwaka huu Mtakatifu. Tusikilize tena maneno yake: “Kanisa linaishi maisha mema linapoiungama na kuihubiri huruma – iliyo sifa kuu na yenye kustaajabisha ya Muumba na Mkombozi – na linapowaleta watu karibu na chimbuko la huruma ya Mwokozi, likiwa kweli mdhamini na mpaji wa hiyo huruma.” [11]
12. Kanisa limeagizwa kutangaza huruma ya Mungu, moyo wa Injili unaodunda, ambao kwa namna yake unapaswa kupenya katika moyo na akili ya binadamu. Mchumba wa Kristo anapaswa kujenga tabia yake ifanane na ile ya Mwana wa Mungu aliyemwendea kila mmoja bila kubagua. Kwa siku ya leo, kama Kanisa linavyojishughulisha na jukumu la uenezaji mpya wa Injili, dhamira ya huruma inabidi ipendekezwe mara kwa mara kwa juhudi mpya na utendaji mpya wa kiuchungaji. Ni muhimu kabisa kwa Kanisa na kwa ukweli wa ujumbe wake kwamba lenyewe liiishi na kuishuhudia huruma. Lugha yake na mtazamo wake vinapaswa kutangaza huruma, ili kuigusa mioyo ya watu wote na kuwahamasisha kwa mara nyingine tena ili kuiona njia inayoelekeza kwa Baba.
Ukweli wa kwanza kabisa wa Kanisa ni upendo wa Kristo. Kanisa linajifanya mtumishi wa upendo huu na kuushirikisha kwa watu wote: upendo unaojionyesha katika kusamehe na kujitolea kwa ajili ya wengine. Matokeo yake, popote Kanisa lilipo, huruma ya Baba inapaswa kuonekana. Katika maparokia yetu, jumuiya, vyama na makundi, kwa neno moja, popote walipo Wakristo, kila mmoja anapaswa kuonyeshwa chemchemi ya huruma.
13. Tunapenda kuuishi Mwaka huu wa Jubilei katika mwanga wa maneno ya Bwana: Wenye huruma kama Baba. Mwinjili anatukumbusha juu ya mafundisho ya Yesu anayesema, “Iweni na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma” (Lk 6:36). Ni mpango wa maisha unaodai juhudi, na uletao furaha na amani. Amri ya Yesu inamlenga yeyote aliye radhi kusikia sauti yake (rej. Lk 6:27). Kwa hiyo, ili kuweza kuwa na huruma, tunapaswa kwanza ya yote kujiweka tayari kusikiliza Neno la Mungu. Hii ina maana kutambua upya thamani ya ukimya ili kutafakari juu ya Neno linalokuja kwetu. Kwa njia hii, itawezekana kutafakari juu ya huruma ya Mungu na kuiishi kama mtindo wetu wa maisha.
14. Uzoefu wa hija una nafasi ya pekee katika Mwaka Mtakatifu, kwa sababu unawakilisha safari ambayo kila mmoja wetu anafanya katika maisha haya. Maisha yenyewe ni hija, na binadamu ni msafiri, mhujaji anayesafiri njiani, akielekea pale alipopatamani kama mwisho wa safari yake. Vivyo hivyo, ili kuufikia Mlango Mtakatifu huko Roma au mahali pengine popote duniani, kila mmoja kuendana na uwezo wake, atapaswa kufanya hija. Hii itakuwa dalili kwamba huruma pia ni lengo la kufikiwa na inahitaji majitoleo na sadaka. Hija iwe nyenzo ya wongofu: kwa kuvuka kizingiti cha Mlango Mtakatifu, tutapata nguvu ya kushikamana na huruma ya Mungu na kujitolea kuwa wenye huruma kwa wengine kama Mungu alivyokuwa kwetu.
Bwana Yesu anatuonyesha hatua za hija ili tufikie lengo letu: “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; sameheni, nanyi mtasamehewa; toeni, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho kitakachowekwa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kilekile mpimacho ndicho mtakachopimiwa” (Lk 6:37-38). Bwana anatuambia juu ya yote tusihukumu na wala tusilaumu. Iwapo mtu anataka kuepuka hukumu ya Mungu, hapaswi kujifanya hakimu wa ndugu zake. Binadamu kila wanapohukumu huangalia juujuu, bali Baba anaangalia ndani kabisa ya nafsi. Ni jinsi gani maneno yanavyodhuru yanapochochewa na wivu na kijicho! Kuwasema wengine kunawaweka kwenye hali mbaya, kunadhoofisha heshima yao na kuwaweka katika hatari ya masengenyo. Kuepuka kuhukumu na kulaumu kunamaanisha, kwa upande mzuri, kujua jinsi ya kuupokea utu wema wa kila mtu na kumwepusha na mateso ambayo yangeweza kusababishwa na hukumu yetu ya juujuu, na dhana yetu kwamba tunajua kila kitu juu yake. Lakini hii bado haitoshi kuonyesha huruma. Yesu anatuambia pia tusamehe na kutoa. Kuwa vyombo vya huruma kwa kuwa sisi tumekuwa wa kwanza kupokea huruma toka kwa Mungu. Kuwa wakarimu kwa wengine, tukitambua kwamba Mungu anatujalia mema yake kwa ukarimu mkubwa.
Wenye huruma kama Baba, ndiyo basi “kaulimbiu” ya Mwaka huu Mtakatifu. Katika huruma, tunapata uthibitisho ni jinsi gani Mungu anavyotupenda. Daima anajitoa nafsi yake yote kwa ukarimu bila kudai kurudishiwa kitu. Anakuja kutusaidia kila tunapomwita. Ni jambo zuri kiasi gani Kanisa linapoanza sala zake za kila siku kwa maneno, “Ee Mungu, uniokoe. Ee Bwana, unisaidie hima” (Zab 70:1)! Msaada tunaoomba tayari ni hatua ya kwanza ya huruma ya Mungu kwetu sisi. Anakuja kutusaidia katika udhaifu wetu. Na msaada wake ni wa kutusaidia sisi tukubali uwepo wake na kwamba yu karibu nasi. Siku baada ya siku, tukiguswa na huruma yake, tunaweza pia kuwa na huruma kwa wengine.
15. Katika Mwaka huu Mtakatifu, tunatazamia zoezi la kufungua mioyo yetu kwa wale wanaoishi pembezoni mwa jamii: pembezoni ambako jamii ya kisasa ndiyo inaitengeneza. Kuna namna nyingi kiasi gani za kutoeleweka na za uchungu duniani leo! Ni majeraha mangapi ya wale wasio na sauti kwa sababu kilio chao kimezibwa na kufunikwa kwa kutojali kwa matajiri! Wakati wa Jubilei hii, Kanisa litaalikwa hata zaidi kuponya majeraha haya, kuyapoozesha kwa mafuta ya faraja, kuyafunga kwa huruma, na kuyaponya kwa mshikamano na uangalifu. Tujihadhari na fedheha ya kutojali au mazoea ya kujirudiarudia yatakayotuzuia kugundua mambo mapya! Tujiepushe na dhana potofu! Tufungue macho yetu tuone machungu ya ulimwengu, majeraha ya ndugu zetu wanaonyimwa hadhi yao, na tutambue kwamba tunahimizwa kusikia kilio chao cha kuomba msaada! Tuwaendee na kuwasaidia ili waweze kuonja joto la uwepo wetu, urafiki wetu na udugu wetu. Kilio chao kiwe chetu, na kwa pamoja tubomoe vizuizi vya kutojali ambavyo mara kwa mara vinatawala na kufunika unafiki na majigambo yetu.
Ni hamu yangu kubwa kwamba wakati huu wa Jubilei, Wakristo wazingatie matendo ya huruma kimwili na kiroho. Itakuwa njia ya kuamsha tena dhamira zetu, ambazo mara nyingi zimefifia mbele ya janga la umaskini. Na tuingie ndani zaidi katika kiini cha Injili pale ambapo maskini wanaonja kwa namna ya pekee huruma ya Mungu. Yesu anatuingiza kwenye kazi hizi za huruma katika mahubiri yake ili tuweze kujua kama tunaishi kama wafuasi wake au la. Hebu tuzigundue upya hizi matendo ya huruma ya kimwili: kulisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuzika wafu. Na tusizisahau matendo ya huruma kiroho: kuwashauri walio mashakani, kuwafunza wajinga, kuwaonya wadhambi, kuwafariji waliojeruhiwa, kusamehe maovu, kuchukuliana kwa saburi na wale wanaotutendea maovu, na kuwaombea walio hai na wafu.
Hatuwezi kuepuka maneno ya Bwana kwetu, na kadiri ya hayo tutahukumiwa: ikiwa tumewalisha wenye njaa, na kuwanywesha wenye kiu, kuwakaribisha wageni na kuwavika walio uchi au kuwatembelea wagonjwa na wale walio kifungoni (rej. Mt 25:31-45). Zaidi ya hayo, tutaulizwa kama tumewasaidia wengine kuepuka wasiwasi unaowafanya wakate tamaa na ambao ndio chanzo cha upweke; kama tumesaidia kuushinda ujinga ambao mamilioni ya watu wanauishi, hasa watoto ambao wamenyimwa mambo muhimu ya kuwatoa katika vifungo vya umaskini; kama tumekuwa karibu na walio pweke na waliodhulumiwa; kama tumewasamehe wale waliotukosea na kama tumekataa aina zote za hasira na chuki zinazosababisha ukatili; kama tumekuwa na ule uvumilivu ambao Mungu anauonyesha, ambaye anatuvumilia sana; na kama tumewakabidhi ndugu zetu kwa Mungu katika sala. Ndani ya kila mmoja wa hawa “wadogo,” Kristo mwenyewe yu hai. Mwili wake unadhihirika ndani ya wale waliojeruhiwa, waliopondwa, waliokandamizwa, wenye utapiamlo, na walio uhamishoni... upate kutambulika, kuguswa, na kutunzwa na sisi. Tusiyasahau maneno ya Mtakatifu Yohane wa Msalaba: “Tunapojiandaa kuyaacha maisha haya, tutahukumiwa kwa kigezo cha upendo.” [12]
16. Katika Injili ya Luka, tunaona suala jingine muhimu kwa ajili ya kuiishi kwa imani Jubilei. Mwinjili anasimulia kuwa Yesu sabato moja, alirudi Nazareti na, kama ilivyokuwa kawaida, aliingia katika sinagogi. Walimwita kusoma Maandiko na kuyatafakari. Ilikuwa ni ile sehemu ya Isaya iliyoandikwa: “Roho ya Bwana i juu yangu; kwa sababu hiyo amenitia mafuta na amenituma niwapelekee habari njema maskini, niwatangazie ukombozi wafungwa na vipofu kuona; kuwaweka huru waliokandamizwa, kutangaza mwaka wa huruma ya Bwana” (rej. Isa 61:1-2). “Mwaka wa huruma”: ndio ule uliotangazwa na Bwana, nasi tunatamani kuuishi. Mwaka huu Mtakatifu unatuletea utajiri mkubwa wa utume wa Yesu unaoakisiwa katika maneno ya Nabii: kupeleka neno na tendo la faraja kwa maskini, kuwatangazia ukombozi waliofungwa katika aina mpya za utumwa wa jamii ya kisasa, kumrudishia uwezo wa kuona yule ambaye anashindwa kuona kwa sababu amepinda, kuwarudishia hadhi waliodhalilishwa. Mahubiri ya Yesu yanaonekana katika majibu ya imani ambayo ushuhuda wa wakristo unaitwa kutoa. Yatusindikize maneno ya Mtume: “Anayetenda matendo ya huruma, ayafanye kwa furaha (Rum 12:8)
17. Kwaresima ya Mwaka huu wa Jubilei tuiishi kwa uzito zaidi kama muda mahsusi kwa kuadhimisha na kuonja huruma ya Mungu. Ni kurasa ngapi za Maandiko Matakatifu, zinaweza kutafakariwa katika majuma ya Kwaresima kwa lengo la kutusaidia kuugundua tena uso wa huruma wa Baba! Tunaweza kurudia maneno ya nabii Mika na kuyafanya yetu: Wewe, Ee Bwana, ni Mungu unayefuta uovu na unayesamehe dhambi, usiyetunza hasira kwa milele, unayependa kuhurumia. Wewe, Bwana, utarudi kwetu na kuwahurumia watu wako. Utayakanyaga makosa yetu na utazitupa kilindini mwa bahari dhambi zetu zote (rej. 7:18-19).
Kurasa za nabii Isaya zitaweza kutafakariwa kwa uhalisia zaidi katika kipindi hiki cha kusali, kufunga na kutenda matendo ya huruma: “Je saumu niliyoichagua siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa na kwamba mvunje kila nira? Je, siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kawaleta maskini waliotupwa nje nyumbani mwako? Kumvika aliye uchi bila kuwasahau ndugu zako? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara, na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuatia nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia naye atasema, “Mimi hapa!” Kama utaondoa kati yako uonevu, kunyosha kidole na kunena maovu, kama utamfungulia moyo wako mwenye njaa, na kuishibisha nafsi iliyoteswa, ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani, na kiza chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui” (58:6-11).
Mpango mkakati “Masaa 24 kwa ajili ya Bwana”, ambao utaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Dominika ya Nne ya Kwaresima, unatakiwa usisitizwe katika kila Jimbo. Watu wengi wakiwemo vijana wanarudi kwenye Sakramenti ya Upatanisho, ambao kwa njia hii wanaigundua tena safari ya kumrudia Bwana ili waiishi sala kwa uzito zaidi na kutambua tena maana ya maisha yao. Tunaweka tena kama kiini kwa uhakika sakramenti ya Upatanisho, kwa sababu inamfanya mtu aguse kwa mkono wake ukubwa wa huruma. Kwa kila mfanya toba hii itakuwa chimbuko la Amani ya ndani.
Sitachoka kamwe kusisitiza kuwa waungamishi wawe ishara halisi ya huruma ya Baba. Hatuwi waungamishi ghafla. Tunafanyika waungamishi wazuri, kama kwanza kabisa sisi wenyewe tunakuwa wafanya toba tunaotafuta msamaha. Tusisahau kwamba kuwa waungamishi ni kushiriki utume uleule wa Yesu na kuwa ishara halisi ya mwendelezo wa upendo wa kimungu unaosamehe na kuokoa. Kila mmoja wetu amepokea zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ondoleo la dhambi, katika hili tunawajibika. Hakuna mmoja aliye mmiliki wa Sakramenti, ila mtumishi mwaminifu wa msamaha wa Mungu. Kila muungamishi anatakiwa kuwapokea waamini kama baba katika mfano wa mwana mpotevu: baba anayemkimbilia mtoto hata kama alitapanya mali zake.
Waungamishi wanatakiwa kumkumbatia yule mtoto aliyejuta na anayerudi nyumbani na waonyeshe furaha ya kumpata tena. Tusichoke pia kumwendea hata yule mtoto mwingine aliyebaki nje na asiyeweza kufurahi na kumweleza kwamba hukumu yake kali dhidi ya ndugu yake si ya haki, na haina maana mbele ya huruma ya Baba isiyo na mipaka. Waungamishi wasiulize maswali yasiyofaa, badala yake wawe kama baba wa kwenye mfano; wakatishe maelezo yaliyoandaliwa na mwana mpotevu, kwani watatambua kilio cha msaada cha mfanya toba na ombi la msamaha. Kwa ujumla waungamishi wanaitwa kuwa daima, mahali pote, katika kila hali, pamoja na yote, ishara ya ukuu wa huruma.
18. Katika Kwaresima ya Mwaka huu Mtakatifu ninayo nia ya kuwatuma Wamisionari wa Huruma. Watakuwa ishara ya hamasa ya kimama ya Kanisa kwa Taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika utajiri wa fumbo hili msingi kwa Imani. Watakuwa ni mapadre ambao watapewa mamlaka ya kuondolea hata dhambi ambazo kwa kawaida huondolewa na Kiti cha Kitume pekee, ili upana wa utume wao uonekane wazi. Watakuwa, hasa, ishara hai ya namna Baba anavyowapokea wale wanaotafuta msamaha wake. Watakuwa wamisonari wa huruma kwa sababu watakuwa wawezeshaji kwa wote wa mkutano uliojaa ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo na kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Katika utume wao wataongozwa na maneno ya Mtume: “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rum 11:32). Wote kwa kweli, bila kumtoa hata mmoja, wanaitwa kuupokea mwito wa huruma. Wamisionari wauishi mwito huu wakijua kwamba wanaweza kumkazia macho Yesu, “kuhani mkuu mwenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu” (Ebr 2:17).
Ninawaomba ndugu zangu Maaskofu kuwaalika na kuwapokea wamisionari hawa ili kwamba wawe, kabla ya yote, wahubiri washawishi wa huruma. Majimbo yapange “utume kwa watu”, ili Wamisionari hawa wawe watangazaji wa furaha ya msamaha. Maaskofu wenyewe wanaombwa kuadhimisha sakramenti ya Upatanisho kwa ajili ya watu, ili kipindi cha neema kilichotolewa katika Mwaka wa Jubilei kiwasaidie watoto wa Mungu wengi walio mbali kurudi nyumbani kwa Baba. Wachungaji, hasa katika kipindi kizito cha Kwaresima, wahamasike kuwaalika waamini “kukikaribia kiti cha neema ili kupokea huruma na kupata neema” (rej. Ebr 4:16)
19. Neno la msamaha liwafikie watu wote na wito wa huruma usimwache yeyote bila kuguswa nao. Ninaelekeza kwa msisitizo zaidi wito wangu wa wongofu kwa walio mbali na neema ya Mungu kwa mtindo wao wa maisha. Ninawafikiria kwa namna ya pekee akina baba na akina mama walio katika kikundi fulani kiovu, chochote kile kiwacho. Kwa faida yenu, ninawaomba mbadilishe maisha. Ninawaomba kwa jina la Mwana wa Mungu, ambaye pamoja na kupambana dhidi ya dhambi, kamwe hajamkataa mdhambi. Msitumbukie kwenye mtego hatari wa kufikiri kwamba maisha yanategemea fedha na kwamba mbele yake kila kitu kinakuwa hakina thamani wala hadhi. Ni kujidanganya tu. Huko mbinguni hatuendi na fedha. Fedha haitupi furaha ya kweli. Ukatili unaotumika katika kujilimbikizia fedha zinazovuja damu hazitufanyi wenye nguvu wala hazituzuii kufa. Kwa wote, mara au baadaye, inatujia hukumu ya Mungu ambayo hakuna anayeweza kuikimbia.
Wito huu uwaendee pia wanaofanya na wanaoshiriki rushwa au ufisadi. Donda hili la jamii linalonuka ni dhambi kubwa inayozililia mbingu, kwa sababu inaiathiri misingi yenyewe ya maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Rushwa inazuia kuwa na mtazamo wa mbele wenye matumaini kwa sababu inaharibu mipango ya wanyonge na inawakandamiza walio maskini zaidi. Ni uovu unaojichanganya kwenye shughuli za kila siku hata kufikia kuwa kashfa za kijamii. Rushwa ni ung’ang’anizi kwenye dhambi, inayotaka kubadili nafasi ya Mungu na udanganyifu wa fedha kama aina fulani ya uweza. Ni kazi ya giza, inayosaidiwa na mashaka na udanganyifu. Corruptio optimi pessima, mtakatifu Gregori Mkuu alisema vizuri, akimaanisha kuwa katika hili hakuna mwenye kinga inayomzuia kuingia kwenye jaribu hili. Ili kuondoa rushwa katika maisha binafsi na jamii kwa ujumla inahitajika busara, uangalifu, unyofu na uwazi, vikiunganishwa na ujasiri wa kuishutumu inapotokea. Tusipoipiga vita waziwazi, hata kama si sasa, baadaye itatufanya washiriki na kuharibu maisha yetu.
Huu ni wakati mwafaka wa kubadili maisha yetu! Huu ni muda ambapo kila mmoja anatakiwa aguswe moyoni. Mbele ya uovu uliotendwa, hata uhalifu mkubwa, ni wakati wa kusikiliza kilio cha watu wasio na hatia wanaodhulumiwa na kunyimwa mali zao, hadhi yao, mapendo, hata na maisha yenyewe. Kubaki katika njia ya uovu ni chemchemi ya kudanganyika na uchungu. Maisha ya kweli ni mengine. Mungu hachoki kunyosha mkono. Yupo tayari daima kusikiliza, hata mimi niko hivyo, kama ilivyo kwa ndugu zangu maaskofu na mapadre. Inatosha kupokea mwito wa wongofu na kwenda mbele ya haki huku Kanisa likitoa msamaha.
20. Haitakuwa si sahihi katika mazingira haya kuhusianisha haki na huruma. Si mambo mawili yanayokinzana, bali pande mbili za kitu kilekile kinachokua taratibu hadi kufikia kilele cha utimilifu wa mapendo. Haki ni wazo msingi, wakati ambapo kwa kawaida, tunaurejea mfumo wa kimahakama unaotumia sheria. Haki, inamaanisha pia kwamba kila mmoja apate kile anachopaswa kupata. Katika Biblia mara nyingi tunakutana na haki ya kimungu na Mungu kama hakimu. Kwa kawaida inamaanisha kufuata sheria kwa uaminifu na tabia njema ya kila muMwisraeli inayoendana na sheria zilizotolewa na Mungu. Mtazamo huu, hata hivyo, si mara chache umetufanya tufuate sheria bila kutafuta thamani ya kina ambayo haki inayo. Ili kwenda mbele zaidi ya sheria, ni lazima kukumbuka kuwa katika Maandiko Matakatifu haki inatafsiriwa kama kujikabidhi kwa matumaini kwa mapenzi ya Mungu.
Yesu kwa upande wake, anazungumzia mara nyingi umuhimu wa imani, badala ya kuzingatia sheria. Ni kwa mtindo huu ndiyo tunatakiwa tuyaelewe maneno yake, akiwa mezani pamoja na Matayo na watoza ushuru wengine na wadhambi, anawaambia mafarisayo waliokuwa wanampinga: “Nendeni mkajifunze maana yake maneno haya: Nataka rehema, wala si sadaka. Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, ila wenye dhambi” (Mt 9:13). Mbele ya mtazamo unaozingatia sheria tu, unaohukumu ukiwagawanya watu kati ya wema na wadhambi, Yesu anaonyesha zawadi kubwa ya rehema inayowatafuta wadhambi ili iwasamehe na kuwapa wokovu. Tunaelewa kwa nini kwa mtazamo wake huu tofauti unaookoa na ulio chemchemi ya upyaisho, Yesu alikataliwa na mafarisayo na walimu wa sheria. Hawa ili wawe waaminifu kwa sheria waliwatwisha mizigo watu mabegani, wakibatilisha hivyo huruma ya Baba. Kufuata sheria hakuwezi kuzuia umakini kwa mahitaji yanayogusa hadhi ya watu.
Rejea anayofanya Yesu kwenye kitabu cha Hosea – “nataka rehema, wala si sadaka” (6:6) – ni ya maana sana kuhusiana na hili. Yesu anatoa tamko kuwa, kuanzia sasa na kuendelea, maisha ya wafuasi wake yatatakiwa kuweka rehema katika nafasi ya kwanza, kama yeye mwenyewe anavyoshuhudia kwa kula pamoja na wadhambi. Rehema, kwa mara nyingine tena, inafunuliwa kama sehemu muhimu ya utume wa Yesu. Hii ni changamoto ya kweli kwa wale wanaohusiana naye, wale wanaofuata sheria kwa mazoea tu. Yesu, kumbe, anakwenda mbali zaidi ya sheria; kushirikiana kwake na wale ambao sheria iliwahukumu kuwa wadhambi kunatufanya tuelewe ni mpaka wapi rehema yake inafika.
Hata mtume Paulo amepitia njia hiyo. Kabla ya kukutana na Yesu katika njia ya Dameski, maisha yake yalikuwa ni kuitimiza kwa uaminifu haki ya sheria (rej. Flp 3:6). Wongofu wake kwa Kristo kulimfanya abadilishe kabisa mtazamo, kiasi kwamba katika Waraka kwa Wagalatia anasema: “Sisi nasi tumemwamini Yesu Kristo ili tuhesabiwe haki kwa imani na si kwa matendo ya sheria” (2:16). Uelewa wake wa haki unabadilika kabisa. Paulo sasa anaiweka katika nafasi ya kwanza imani na siyo sheria. Si kufuata sheria kunakookoa, ila imani katika Yesu Kristo, ambaye kwa kifo na ufufuko wake analeta wokovu pamoja na rehema inayohesabia haki. Haki ya Mungu inakuwa sasa ukombozi kwa wale waliokandamizwa na utumwa wa dhambi na matokeo yake yote. Haki ya Mungu ni msamaha wake (rej. Zab 51:11-16).
21. Huruma haipingani na haki, bali inaonyesha msimamo wa Mungu dhidi ya mwenye dhambi, yaani Mungu anampa nafasi nyingine ya kujirekebisha, kutubu na kuamini. Yaliyompata nabii Hosea yanatusaidia kwa sababu yanatuonyesha jinsi huruma inavyozidi haki. Kipindi alipoishi nabii huyo ni kati ya vipindi vyenye fujo zaidi katika historia ya Taifa la Wayahudi. Ufalme unakaribia kuangamizwa kabisa, watu wamekosa uaminifu kwa agano, wamemkimbia Mungu na kupoteza imani ya Mababa. Kwa mtazamo wa kibinadamu ni haki Mungu awakatalie watu wasio aminifu: hawakuzingatia yale waliyokubaliana katika agano, hivyo wanastahili adhabu, yaani kupelekwa uhamishoni. Ndivyo anavyoandika nabii: “Hatarudi tena nchi ya Misri, bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake, kwa sababu walikataa kurejea.” (Hos 11:5). Lakini, baada ya maneno hayo yanayotokana na kuzingatia haki, nabii anabadilisha kabisa maneno yake na kuonyesha uso wa kweli wa Mungu: “Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu, kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu, wala sitaingia ndani ya mji.(11:8-9). Mtakatifu Augustino, kama kwa kueleza maneno ya nabii, alisema: “Ni rahisi zaidi Mungu ajizuie kuwa na hasira kuliko kuwa na huruma”. [13] Na ndivyo ilivyo. Hasira ya Mungu inadumu punde tu, bali huruma yake inadumu milele.
Kama Mungu angebaki kuzingatia haki tu asingekuwa Mungu, angekuwa kama wanadamu wale wanaodai sheria ichukue mkondo wake. Haki peke yake haitoshi, na uzoefu unatufundisha kwamba tukitegemea haki tu kuna hatari ya kuiharibu. Kwa sababu hiyo Mungu anaipita haki kwa huruma na msamaha. Hilo halimaanishi kuishusha thamani ya haki au kuipuuza, bali ni kinyume chake. Mwenye kosa lazima atumikie adhabu. Lakini hilo si lengo bali ni mwanzo tu wa toba, ili mtu aonje upole wa msamaha. Mungu hakatai haki. Mungu anaichukua na kuizidi katika tukio la juu ambapo watu wanaonja upendo ulio msingi wa haki ya kweli. Lazima tuyasome kwa makini sana yale yaliyoandikwa na Paulo ili tusianguke katika kosa lile lililosababisha maonyo kwa Wayahudi wa wakati wake: “Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu. Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ila kila aaminiye ahesabiwe haki” (Rum 10:3-4). Haki hii ya Mungu ni huruma iliyogawiwa kwa wote kama neema kutokana na kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Basi, msalaba wa Kristo ni hukumu ya Mungu juu yetu sisi sote na juu ya dunia, kwa sababu inatupa uhakika wa upendo na wa maisha mapya.
22. Tukio la Jubilei linatuelekeza pia katika suala la rehema. Katika Mwaka Mtakatifu wa huruma suala hilo linapewa uzito wa pekee. Msamaha wa Mungu kwa dhambi zetu hauna mipaka. Katika kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, Mungu anadhihirisha wazi upendo wake huo unaofikia hata kufuta kabisa dhambi ya wanadamu. Kupatanishwa na Mungu kunawezekana kwa njia ya fumbo la kipasaka na ushenga wa Kanisa. Hivyo Mungu yu tayari kila wakati kusamehe na kamwe hachoki kutupatia msamaha wake kwa namna mpya na tusiyoitarajia. Sisi sote, lakini, tunatenda dhambi. Tunajua tumeitwa kuwa wakamilifu , lakini uzito wa dhambi unatusonga sana. Tunapohisi nguvu ya neema inayotubadilisha wakati huohuo tunasikia pia nguvu ya dhambi inayotuathiri. Ingawa tumepata msamaha katika maisha yetu tunaibeba migongano iliyosababishwa na dhambi zetu. Katika sakramenti ya Upatanisho Mungu hutusamehe dhambi zetu, na zinafutwa kweli. Hata hivyo, matokeo mabaya ya dhambi zetu, zilizoathiri mienendo yetu na mawazo yetu, hubaki. Huruma ya Mungu lakini ina nguvu zaidi hata kuliko hayo. Huruma yake inakuwa rehema ya Baba ambayo kwa njia ya Bibi arusi ya Kristo inamjia mwenye dhambi aliyesamehewa na inamwondoa yale yote yaliyosababishwa na dhambi na kumpa nguvu ya kutenda kwa upendo, kukua katika upendo kuliko kuanguka tena dhambini.
Kanisa linaishi ushirika wa Watakatifu. Katika Ekaristi ushirika huo, ulio zawadi ya Mungu, unakuwa kama muungano wa kiroho unaotuunganisha sisi waamini na Watakatifu na Wenye Heri ambao idadi yao haihesabiki (rej. Ufu 7:4). Utakatifu wao unausaidia udhaifu wetu; kwa namna hiyo Mama Kanisa linaweza kwa sala yake na maisha yake kuusaidia udhaifu wa wengine kwa nguvu ya utakatifu wa wengine. Basi, kuiishi rehema katika Mwaka Mtakatifu kunamaanisha kuisogea huruma ya Baba tukiwa na uhakika kwamba msamaha wake unaenea juu ya maisha yote ya mwamini. Rehema ni kufahamu na kufaidi na utakatifu wa Kanisa ambalo linawagawia watu wote manufaa ya ukombozi wa Kristo, ili msamaha ufikie mpaka kilele kinachofikiwa na upendo wa Mungu. Tuiishi kwa dhati kabisa Jubilei tukimwomba Baba atujalie msamaha wa dhambi na uenezaji wa rehema yake yenye huruma
23. Huruma ina thamani inayovuka mipaka ya Kanisa. Huruma inatuunganisha na dini ya Kiyahudi na ya Kiislamu, dini hizo zinaitambua huruma kati ya sifa bora zaidi ya Mungu. Waisraeli wamekuwa wa kwanza kuupokea ufunuo huo unaobaki katika historia kama mwanzo wa utajiri usiopimika wa kuwagawia watu wote. Kama tulivyoona, kurasa za Agano la Kale zimejaa huruma, kwa sababu zinasimulia yaliyotendwa na Bwana kwa manufaa ya watu wake katika vipindi vigumu zaidi ya historia yake. Waislamu, kwa upande wao, kati ya majina ya Muumba wameliweka jina la Mwenye Huruma na Mpole. Majina hayo mara nyingi yanatumika na waamini Waislamu ambao hujisikia kama wanasindikizwa na kutegemezwa na huruma katika udhaifu wao wa kila siku. Wao pia wanaamini kwamba huruma ya kimungu haiwezi kuwekwa mipaka na mtu yeyote kwa sababu milango yake daima ni wazi.
Mwaka huo wa Jubilei tukiuishi katika huruma uwe nafasi ya kuzisaidia dini hizo pamoja na mapokeo mengine ya kidini zikutane; tuweze kuwa tayari zaidi kuzungumza ili tufahamiane vizuri zaidi na kuelewana; ufute kila aina ya kiburi na udhalilishaji na uondoe kila aina ya ukatili na ubaguzi.
24. Sasa tunamwelekea Mama wa huruma. Katika Mwaka huo Mtakatifu uso wake mpole utusindikize ili wote tuweze kugundua upya furaha ya upendo wa Mungu. Hakuna mtu aliyeweza kufahamu kina ya fumbo la Mungu aliyejifanya mtu kama Maria. Yote katika maisha yake yametokana na uwepo wa huruma iliyofanyika mwili. Mama wa Msulibiwa Mfufuka ameingia katika hekalu la huruma ya kimungu kwa sababu alishiriki kwa undani kabisa fumbo la upendo wake.
Maria, aliyechaguliwa kuwa Mama wa Mwana wa Mungu , aliandaliwa na upendo wa Baba tangu milele ili awe Sanduku la Agano kati ya Mungu na watu. Aliihifadhi moyoni mwake huruma ya kimungu akiungana kabisa na Mtoto wake Yesu. Wimbo wake wa sifa mlangoni pa nyumba ya Elizabeti uliimbia huruma inayoenea vizazi na vizazi (Lk 1:50). Sisi pia tulikuwepo katika maneno yale ya kinabii ya Bikira Maria. Hilo litakuwa faraja na tegemeo tutakapopita katika Mlango Mtakatifu ili kuonja matunda ya huruma ya kimungu.
Karibu na msalaba, Maria pamoja na Yohane, mwanafunzi wa upendo, ni shahidi wa maneno yenye msamaha yaliyotoka mdomoni mwa Yesu. Msamaha mkuu uliotolewa na Yesu kwa wale waliomsulibisha unaonyesha huruma ya Mungu inaweza kufikia mpaka wapi. Maria anashuhudia kwamba huruma ya Mwana wa Mungu haina mipaka na inawajia wote bila kumwacha hata mmoja. Tumwelekee Maria kwa sala ya zamani lakini mpya daima ya Salamu Malkia, ili asichoke kamwe kutuangalia kwa macho yake yenye huruma na atujalie tustahili kuuona uso wa huruma, yaani Mwana wake Yesu.
Sala yetu iwajumuishe pia Watakatifu na Wenye heri wengi ambao wameichukulia huruma kama utume wa maisha yao. Kwa namna ya pekee tunamfikiria Mtakatifu Faustina Kowalska mtume mkubwa wa huruma. Yeye, aliyeitwa kuingia katika undani wa huruma ya Mungu, atuombee ili tupate kuishi na kutembea daima katika msamaha wa Mungu na katika kuutegemea kabisa upendo wake.
25. Basi, ni Mwaka Mtakatifu wa pekee ili tuweze kuishi katika maisha yetu ya kila siku huruma ile ambayo Baba daima anaieneza kwetu. Katika Jubilei hii tushangazwe na Mungu. Yeye hachoki kamwe kutufungulia mlango wa moyo wake na kurudia kwamba hutupenda na hutaka kutushirikisha maisha yake. Kanisa linasikia kwa nguvu jukumu nyeti la kutangaza huruma ya Mungu. Maisha ya Kanisa yana ukweli na yanaeleweka ikiwa ujumbe wa huruma unatangazwa kwa dhati. Kanisa linajua kwamba jukumu lake la kwanza, hasa katika kipindi chetu hiki kilichojaa matumaini makubwa na migongano mikali, ni kuwaingiza wote katika fumbo kuu la huruma ya Mungu, kwa kuutazama uso wa Kristo. Kanisa linaitwa wa kwanza kuwa shahidi mwaminifu wa huruma, kwa kuitangaza na kuiishi kama kiini cha Ufunuo wa Yesu Kristo. Kutoka moyoni mwa Utatu Mtakatifu, kutoka ndani kabisa ya fumbo la Mungu, unabubujika na kutiririka bila pumziko mto mkubwa wa huruma. Chemchemi hii haiwezi kukauka kamwe, hata wale wanaoijia wawe idadi kubwa kiasi gani. Kila mara kila mmoja atakayehitaji ataweza kuisogea, kwa sababu huruma ya Mungu haina mwisho. Jinsi kina ya fumbo hilo haiwezi kuchunguzika, vivyo hivyo utajiri unaotokana na fumbo hilo hauwezi kumalizika.
Katika mwaka huu wa Jubilei Kanisa liwe mwangwi wa Neno la Mungu unaolia kwa nguvu na ushawishi, kama neno na tendo la msamaha, la kutegemeza, la kusaidia na la upendo. Kanisa lisichoke kamwe kuwa na huruma na daima liwe na uvumilivu katika kufariji na kusamehe. Kanisa liwe sauti ya kila mwanamume na kila mwanamke na kwa imani lirudie bila kukoma “Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, maana zimekuwako tokea zamani” (Zab 25:6)
Imetolewa Roma, katika Kanisa la Mtakatifu Petro, tarehe 11 Aprili, Kesha la Dominika ya Pili ya Pasaka, au Dominika ya Huruma ya Mungu, katika mwaka wa Bwana 2015, wa tatu wa Upapa wangu.
FRANSISKO
[1] Rej. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Konst. ya kidogma Dei Verbum, 4.
[2] Hotuba ya kwenye kuzindua Mtaguso Mkuu wa Vatikano II Gaudet Mater Ecclesia (11 Oktoba 1962), 2-3: AAS 54 (1962), 792-793.
[3] Hotuba ya kuhitimisha Mtaguso Mkuu wa Vatikano II (7 Desemba 1965): AAS 78 (1966), 54-57.
[4] Rej. Mtaguso Mkuu wa Vatikano II, Konst. ya kidogma Lumen gentium, 16; Konst. ya kichung. Gaudium et spes, 15.
[5] Tomaso wa Akwino, Summa Theologiae, II-II, q. 30, a. 4.
[6] Dominika ya 26 kwa mwaka. Kolekta hii ilikuwa ikitumika tayari katika karne ya 8, na inapatikana miongoni mwa sala zilizokusanywa katika gombo la Sacramentarii Gelasiani (mwaka 1198).
[7] Hom. 21: CCL 122, 149-151.
[8] Wosia wa kitume, Evangelii gaudium, 24.
[9] N. 2.
[10] Iohane Paulo II, Waraka Insiklika Dives in misericordia, 15.
[11] Ibid., 13.
[12] Avisos y sentencias, 57.
[13] Enarr. in Ps. 76, 11.
Copyright © Dicastero per la Comunicazione - Libreria Editrice Vaticana